Zakaah Ikiwa Mtaji Unaongezeka Itolewa Vipi?

 

SWALI  

Asalaam Aleikum, Ikiwa mtaji unaongezeka kila mwezi, Je zakah yake itatolewa vipi. Wabillahi tawfik. Asalaam aleikum warahmatuhu llahi.

Asalaam aleikum warahmatuhullahi, Kwa kuweka sawa suali nililouliza kuhusu vipi kutolewa zakah kwa mali inayozidi kila mwezi nimekusudia tayari imeshaanza kutolewa zaka ya mwaka, lakini pato linaongezeka kila mwezi. Je miaka unayofuatia itatolewa vipi?


 

JIBU

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Llaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako hilo. Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Atupatie tawfiki ya kuweza kutekeleza Ibadah Zake zote kwa kiasi tunachoweza na Atufishe tukiwa katika Imani na Uislamu, Amiin.

Ama kuhusu swali lako la Zakaah ambayo ni nguzo ya Uislamu na Ibaadah kubwa yenye thawabu nyingi kwa mwenye kutekeleza ina masharti. Hili si ngeni kwa Zakaah peke yake kwani hata Ibaadah nyingine kama Swalah, funga, Hijjah pia nazo zina masharti yake. Miongoni mwa masharti ya mtu kutoa Zakaah ni:

1.       Kufikisha kiwango cha chini kwa mtu kutoa Zakaah (Niswaab). Hicho kinakuwa kiwango cha pesa sawa na thamani ya gramu 82½ za dhahabu.

2.     Kiwango hicho ni lazima kipitwe na Hawl (mwaka katika kalenda ya Kiislamu).

Ikiwa masharti hayo mawili yatatimia basi Muislamu anafaa atoe asili mia 2½ (2.5%). Ikiwa kiwango chako uichonacho kimefika Niswaab na kikapitiwa na mwaka huku kinaongezeka basi itabidi mwaka unapofika utazame una pesa ngapi, na hizo ndizo utazitolea Zakaah.

Mfano tuseme kuwa 1000 ndio Niswaab na katika miezi kumi na miwili inayofuatia kikawa kinaongezeka mpaka mwisho wa Hawl kikafika 1500. Itabidi utolee Zakah kiwango hicho cha mwisho ulichofikia cha 1500. Hivyo itakuwa ni 1500 x 2½% = 37.5 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share