Mashairi 2: Karibu Wetu Mgeni, Mtukufu Ramadhani

 

 

Mashairi 2:  Karibu Wetu Mgeni, Mtukufu Ramadhani

 

            ‘Abdallaah Bin Eifan (Rahimahu-Allaah)

 

 Alhidaaya.com

 

 

Salam zangu natuma, mijini na vijijini,

Habari imeshavuma, amewasili mgeni,
Leo mwezi kuandama, ni yetu matumaini,
Karibu wetu mgeni, mtukufu Ramadhani.

 

 

 

Mwezi huu wa fadhila, na mwezi wa ihsani,
Sio mwezi wa chakula, kushindilia tumboni,
Au mwezi wa kulala, kukoroma kitandani,
Karibu wetu mgeni, mtukufu Ramadhani.

 

 

 

Mwezi huu wa ibada, na kusoma Qur-aani,
Ni mwezi wenye faida, nyingi ziso na kifani,
Si mwezi wa kawaida, ni mwezi wenye thamani,
Karibu wetu mgeni, mtukufu Ramadhani.

 

 

 

Imo siku ya Kudura, kwenye kumi za mwishoni,
Hiyo siku ndio bora, kuliko zote yakini,
Ni siku yenye kung'ara, Jibrili ni mgeni,
Karibu wetu mgeni, mtukufu Ramadhani.

 

 

 

Mwezi huu mashetani, wana pingu mikononi,
Minyororo ya shingoni, wametiwa huwaoni,
Ona vipi Rahmani, mwezi Anauthamini!
Karibu wetu mgeni, mtukufu Ramadhani.

 

 

 

Mwezi huu Qur-aani, ilishuka ardhini,
Kwa wahyi toka mbinguni, ni maneno ya Manani,
Isomwe kila makani, itunawiri moyoni,
Karibu wetu mgeni, mtukufu Ramadhani.

 

 

 

Mwezi huu tarawihi. ni Swalah za Ramadhani,
Usikose kuziwahi, ziswali msikitini,

Mwenyewe utafurahi, utakuwa burudani,
Karibu wetu mgeni, mtukufu Ramadhani.

 

 

 

Mwezi huu mafakiri, pamoja na masikini,
Uwaalike futari, wakaribishe nyumbani,

Wape maneno mazuri, na sadaka mkononi,
Karibu wetu mgeni, mtukufu Ramadhani.

 

 

 

Mwezi huu wa kufunga, kila kitu mdomoni,
Sio mwezi wa kuringa, kujivuna mitaani,
Ni mwezi wa kujikinga, na maasi duniani,
Karibu wetu mgeni, mtukufu Ramadhani.

 

 

 

Mwezi huu kujishika, kujizuia mwilini,
Usiyavuke mipaka, yalokatazwa na dini,
Na ibada shughulika, asubuhi na jioni,
Karibu wetu mgeni, mtukufu Ramadhani.

 

 

 

Mwezi huu kula daku, mama aende jikoni,
Ukiingia usiku, kula unavyotamani,
Mchana ni marufuku, ila uwe safarini,
Karibu wetu mgeni, mtukufu Ramadhani.

 

 

 

Mwezi huu inafungwa, milango yote motoni,
Hapo inafunguliwa, milango yote peponi,
Dua zinakubaliwa, ombeni ndugu ombeni
Karibu wetu mgeni, mtukufu Ramadhani.

 

 

 

Mwezi huu wa kutubu, uyafute ya zamani,
Uzikusanye thawabu, uombe na samahani,
Uzungmze kwa adabu, na ndugu na majirani,
Karibu wetu mgeni, mtukufu Ramadhani.

 

 

 

Mwezi huu tenda mema, uchoyo weka pembeni,
Tena uwe na huruma, kwa wale walioduni,
Kama Mola kawanyima, huo ndio mtihani,
Karibu wetu mgeni, mtukufu Ramadhani.

 

 

 

Mwezi huu wa baraka, wa amani na imani,
Tumuombe Mtukuka, pepo iwe maskani,
Ni mwisho wa kuandika, nimefika kikomoni

Karibu wetu mgeni, mtukufu Ramadhani.
 

 

 

 

         

 

 

Share