Kisomo Cha Arubaini Baada Ya Maiti Kufa Ni Sunnah Au Bid'ah?
SWALI:
Imezoeleka maiti anapozikwa baada ya siku tatu watu hufanya kisomo, wengine hufanya AROBAINI je hiki kisomo haswa kinahitajika kifanyike lini? na hii AROBAINI inabidi iwe imesomwa kabla au baada ya kupita siku AROBAINI tangu kupita mazishi?
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani ndugu yetu kwa swali lako hilo. Hakika ni kuwa jambo hili la kufanya kisomo baada ya siku tatu au kufanya arobaini na watu kula mpunga kama katika karamu ni mambo yaliyozoeleka sana. Zipo sehemu nyingine wanakusanyikana Msikitini kwa ajili ya kisomo kwa siku tatu mfululizo. Lakini kwa kuwa uchumi umezorota huwa siku hizi inafanywa siku moja peke yake na thawabu ya kisomo anapatiwa maiti.
Hakika jambo hili halikuthubutu kabisa kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Maswahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema. Hakika ni kuwa kisomo hicho thawabu zake hazimfikii maiti.
Ifahamike kuwa katika Uislamu hakuna kabisa mas-ala ya siku arobaini. Arobaini kawaida ni siku ambazo anakaa mwanamke aliyezaa akiwa anatokwa na damu. Wakati huu mwanamke huyo huwa ana udhuru hivyo haruhusiwi kisheria kuswali wala kufunga. Sasa bila msingi wowote imechukuliwa kuwa baada ya mtu kufa watu wanakusanyikana katika nyumba ya marehemu na hapo kuandaliwa chakula aina kadhaa ili watu wale pamoja na kumkumbuka marehemu. Hakika jambo hili la arobaini halipo kabisa na hivyo ni uzushi. Inabidi sisi tuachane na jambo hilo na tuangalie mambo ambayo yanaweza kumfaa maiti kaburini. Yapo mambo mengi lau yatafanywa na watu wa marehemu basi yeye anapata thawabu japokuwa keshafariki. Miongoni mwa mambo hayo ni:
1. Kuombewa Du’aa na mtoto wake mwema.
2. Kulipiwa madeni anayodaiwa.
3. Kufanyiwa Hajj au ‘Umrah ikiwa hakuwahi kufanya.
4. Kutolewa sadaka wakati wowote ule na sio baada ya siku arobaini au siku tatu.
5. Kumlipia nadhiri zake.
6. Waislamu kwa jumla kumuombea Du’aa.
Hayo ni mambo yatakayomsaidia sana kuliko mkusanyiko wa mara moja na watu kusoma, kula na kuondoka.
Na Allaah Anajua zaidi
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha


