Je, Unamshukuru Allaah سبحانه وتعالى Ipasavyo Kwa Neema Zake Nyingi Zisizohesabika?

Anasema Allaah سبحانه وتعالى:

   وَآتَاكُم مِّن كُلِّ مَا سَأَلْتُمُوهُ وَإِن تَعُدُّواْ نِعْمَتَ اللّهِ لاَ تُحْصُوهَا إِنَّ الإِنسَانَ لَظَلُومٌ كَفَّارٌ

((Na Akakupeni kila mlichomuomba. Na mkihisabu neema za Allaah hamtaweza kuzihesabu. Hakika mwanaadamu ni dhaalimu mkubwa, mwenye kuzikufuru neema)) [Ibraahiym: 34] 

Tukizingatia sana tutaona kwamba hakika neema za Allaahسبحانه وتعالى  hatuwezi kuzihesabu. Tukianza kuangaza neema zilizo katika ulimwengu, kuanzia ardhi jinsi Alivyoitandaza ikatulia, Akaweka ndani yake mito, milima, mimea, Akateremsha mvua ya kustawisha hiyo miti na mimea na bustani za kupendeza. Kisha tukitazama jua linalotupatia mwanga na mwezi kuweza kujua idadi ya hesabu za miaka, miezi na siku,  na mwanga wa kusafiria. Kisha Alivyotuumbia wanyama wa kunufaika nao kwa kila aina na wala hatuwezi kuhesabu mengi mema Aliyoyajaza katika huu ulimwengu kwa manufaa yetu.

Vile vile kama Anavyosema Mwenyewe سبحانه وتعالى:

  وَفِي أَنفُسِكُمْ أَفَلَا تُبْصِرُونَ    

((Na pia katika nafsi zenu, Je! Hamwoni?)) [Adh-Dhaariyaat: 21]

Anasema Allaah سبحانه وتعالى  kuhusu umbo letu:

  لَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ فِي أَحْسَنِ تَقْوِيمٍ 

((Bila ya shaka Tumemuumba mtu kwa umbo lilio bora kabisa)) [At-Tiyn: 4]

Basi inatupasa tumshukuru Allaah سبحانه وتعالى  kila mara kwa kadiri tunavyoweza, na kila tunapomshukuru Yeye Hutuzidishia hizo neema kama Anavyosema:

 وَإِذْ تَأَذَّنَ رَبُّكُمْ لَئِن شَكَرْتُمْ لأَزِيدَنَّكُمْ

((Na Alipotangaza Mola wenu Mkishukuru Nitakuzidishieni)) [Ibraahiym: 7]

Na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ametufundisha katika nyiradi za kila siku kwamba utakapoomba du'aa hii ifuatayo asubuhi utakuwa umetekeleza  shukurani ya siku nzima, na ukiisoma jioni utakuwa umetekeleza shukurani ya usiku mzima:

اللّهُـمَّ ما  أَصْبَـَحَ بي مِـنْ نِعْـمَةٍ أَو بِأَحَـدٍ مِـنْ خَلْـقِك ، فَمِـنْكَ وَحْـدَكَ لا شريكَ لَـك، فَلَـكَ الْحَمْـدُ وَلَـكَ الشُّكْـر

 

Allaahumma maa aswbaha biy min ni’matin au biahadin min Khalqika, Faminka Wahdaka, laa shariyka Laka, Falakal-Hamdu wa Lakas-shukr

“Ee Allaah  sikuamka na neema yoyote au kati ya kiumbe Chako chochote, na neema ila inatoka Kwako hali ya kuwa Peke Yako Huna mshirika, ni Zako  sifa njema na ni Zako shukurani”

Vile vile usimulizi huu kutoka kwa ibn 'Umar kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  amesema:

 ((إن عبدًا من عباد الله قال: يا رب، لك الحمد كما ينبغي  لجلال وجهك وعظيم سلطانك، فعضلت بالملكين فلم يدريا كيف يكتبانها، فصعدا إلى السماء فقالا يا رب، إن عبدا قد قال مقالة لا ندري كيف نكتبها، قال الله -وهو أعلم بما قال عبده-: ماذا قال عبدي؟ قالا يا رب إنه قد قال: يا رب لك الحمد كما ينبغي لجلال وجهك وعظيم سلطانك. فقال الله لهما: اكتباها كما قال عبدي حتى يلقاني فأجزيه بها))  إبن ماجه

((Mja katika waja wa Allaah alisema: Ee, Mola wangu! Zako wewe tu sifa zote njema Unayestahiki kushukuriwa kama inavyopasa Utukufu Wako na nguvu Zako kubwa kabisa. Malaika wawili walibabaika hawakujua vipi waandike maneno hayo (jinsi alivyomtukuza utukufu wa Mola wake) Wakaenda kwa Allaah wakasema: Ee Mola wetu! Hakika mja wako kasema aliyoyasema na wala hatujui vipi tuyaandike. Akasema Allaah سبحانه وتعالى Kwani kasema nini mja wangu? (Na Allaah سبحانه وتعالى  Anajua aliyoyasema mja Wake bila ya malaika kumwelezea) Wakasema amesema: Ee Mola wangu! Zako Wewe tu sifa zote njema Unayestahiki kushukuriwa kama inavyopasa Utukufu Wako na nguvu Zako kubwa kabisa. Allaah سبحانه وتعالى akasema: Yaandikeni kama alivyosema mja Wangu mpaka atakaponikuta (siku ya malipo) basi nitampa jazaa yake kwa hayo (aliyoyasema) )) [Ibn Maajah 2:1249]

 Adhkaar nyingi za kumshukuru Allaah zimo katika mafunzo ya Qur-aan na Sunnah, hivyo basi tusiache daima kumshukuru Allaah, kwa kukiri neema Zake moyoni, kumshukuru kwa ndimi zetu, na kwa vitendo vyetu.

 

 

 

Share