Malaika Wanaoandika Mema Na Maovu Ya Mja Wanajua Siri Za Allaah?

SWALI:

 

Asasalm alykum.

Naomba tusaidiane juu ya suala hili.

Tunaamini kua Allah subhanahu wa taala, yeye ndie anaejua mazuri yetu na mabaya yetu, sasa ni hivi, hawa malaika wanaoandika mema na mabaya yetu huwa wao wanajuaje na hii siri ni ya allah subhanahu wa taala peke yake, kwa sababu Mashekh wanatufundisha kua chochote ufanyacho Allah subhanahu wa taala yeye ndie anaejua. Je na hawa malaika wawili na wao huwa wanajua kuhusu jambo hili la thawabu na dhambi juu yetu sisi wanaadam na majini. NAOMBA RADHI KAMA NITAKUA SIJAFAHAMIKA VIZURI. NAOMBA JIBU

INSHAALLAH


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu Malaika wanaoandika mema na maovu.

Malaika ni viumbe kama viumbe vingine ambao wameumbwa na Allaah Aliyetukuka. Ghaibu inajulikana na Allaah Aliyetukuka peke Yake. Hata hivyo, tufahamu kuwa Malaika umbile lao ni tofauti nao wameumbwa kutekeleza maagizo ya Allaah Aliyetukuka peke Yake. Allaah Aliyetukuka Anasema yafuatayo kuhusu sifa za Malaika:

Enyi mlioamini! Jilindeni nafsi zenu na ahali zenu na Moto ambao kuni zake ni watu na mawe. Wanausimamia Malaika wakali, wenye nguvu, hawamuasi Allaah kwa Anayowaamrisha, na wanatenda wanayoamrishwa(At-Tahriym [66]: 6).

 

Kwa kuwa Malaika wote wana zile sifa za kutomuasi Allaah Aliyetukuka na wanatenda wanayoamrishwa, basi yao wanayoyafanya yanakwenda sambamba na Anayotaka Allaah, Muumba wa kila kitu. Tukifahamu hilo basi hakutakuwa na utata kwa yale wanayoandika Malaika hao wawili ambao Allaah Aliyetukuka Amewataja:

Hatamki neno ila karibu yake yupo mwangalizi tayari(Qaaf [50]: 18).

Kwa hiyo, Malaika hawa wanarekodi maneno hata minong’ono na matendo ya mja. Na wao wanaweza kufanya hayo kwa kuwa hiyo ni kazi waliopatiwa na Allaah Aliyetukuka, hivyo, wamepatiwa uwezo wa kuweza kutekeleza hilo bila tatizo lolote.

 

Na kwa kuwa Malaika waliopatiwa kazi hii tayari wamepatiwa maelekezo ya jambo ambalo ni thawabu au dhambi kunakuwa hakuna shida. Na kwa hiyo Malaika wanatekeleza kazi zao bila ya shida wala utata wowote.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share