Wanandoa Wanapoendeana Kinyume Au Kufanya Maasi Wasameheane Au Waachane?

 

SWALI:

 

Assalam aleykum. Shukrani za dhati kwa ndugu zetu katika imani ya kiislam ambao mmejitolea kwa hali na mali katika kutuelimisha na inshALLAH ALLAH akulipeni kheri sisi na nyinyi hapa duniani na akhera. Amma ba'ad. suali langu ni hili:  je kama mke wa mtu au mume wa mtu amezini nje ya ndoa na baadae akatanabahi kosa alilofanya  na akamkabili mkewe au mumewe kumuomba samahani, je huyu mume au mke aloombwa samahani ni lipi bora kwake kumsamehe wakarejeana? Au kutomsamehe wakaachana? Na sio zinaa tu bali pia suala langu linakwenda kwa madhambi makubwa mengine kama shirki, kuuwa, kufitinisha n.k. Wassalam aleykum.

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu wanandoa wanaofanya maasi wachukuliane vipi.

 

Uislamu ni Dini iliyokamilika katika mambo yake yote ya hapa duniani. Toba inatakiwa ifanywe kwa kila dhambi inayofanywa na Muislamu kubwa au dogo. Na mtu yeyote akiomba msamaha hata kwa dhambi kubwa Allaah Aliyetukuka Humsamehe. Hii ni kwa mujibu wa kauli Yake:

Sema: Enyi waja Wangu waliojidhulumu nafsi zao! Msikate tamaa na rehema ya Allaah. Hakika Allaah Husamehe dhambi zote. Hakika Yeye ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu” (Az-Zumar 39: 53).

 

Ili kusamehewa aliyefanya dhambi anahitajika kufanya yafuatayo katika masharti:

 

1.     Kujiondoa katika maasiya hayo.

2.     Ajute sana katika kufanya kosa hilo.

3.     Aazimie kutolirudia tena kosa hilo.

4.     Na kwa kuwa amemdhulumu mwenziwe katika haki yake basi aombe msamaha kutoka kwake.

 

Ikiwa mke au mume aliyefanya kosa amerudi nyuma akajirekebisha na kuomba msamaha basi ni bora kusameheana na kuendelea kuishi pamoja. Allaah Aliyetukuka Anasema:

Shikamana na kusamehe, na amrisha mema, na jitenge na majahili (wajinga)” (Al-A’raaf 7: 199).

 

Na katika Aayah nyingine, Allaah Aliyetukuka Anatuambia:

Na kusamehe ni karibu na uchaji Mungu”.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share