Baba Na Mama Waliotengana Anaweza Kumwandikia Mama Mali Kabla Ya Kufa Kama Zawadi?

SWALI:

 

Assalam aleykum,

Naomba kuuliza haki ya mirathi kwa Baba na Mama wazazi walikwisha tengana muda mrefu, Baba ana nyumba yake na ameshasema hata akifa Mama hana haki, mimi mtoto nikifa Baba na Mama kila mmoja ana haki kiasi gani kurithi vyangu iwapo mimi nitatangulia kabla yao.

Na Je kama sheria ya dini yeu inampa kipaumbele Baba hata kama wameshatengana, nataka kumsaidia Mama, naweza kumsadia vipi? Je sahihi kwa mimi kuandisha mali zangu kama kumpa zawadi Mama bado sijafa ili hata ikitokea ziwe mali yake?

Najitahidi kutafuta kumsaidia Mama bila kuvunja sheria za dini yangu, Sheria ikimpa zaid Mama nikitangulia Mama atabakia anahangaika hana nyumba na ni yatima, na yeye hasa ndio aliyenijali kuliko Baba. Asanteni


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mirathi kwa wazazi.

Uislamu ambayo ni Dini ya kimaumbile inaweka shari'ah ya kila mtu na kila mtu anapewa haki yake. Kuhusiana na mirathi ni kuwa pindi wazazi (mume na mke) wanapoachana na eda ikamalizika ya mama yako hawatoweza kurithiana kishari'ah kwa sababu mafungamano yao yamekwisha.

 

Ama kuhusu mali yako, Allaah Aliyetukuka tayari Amegawanya kila mmoja katika wazazi kupata haki yake kulingana na mambo kadhaa. Mfano kama umeoa, au una watoto na ndugu au wazazi wako ndio warithi wa pekee n.k. 

Allaah Aliyetukuka Anasema:

Na wazazi wake wawili, kila mmoja wao apate sudusi ya alichokiacha, ikiwa anaye mtoto. Akiwa hana mtoto, na wazazi wake wawili wamekuwa ndio warithi wake, basi mama yake atapata thuluthi moja. Na akiwa anao ndugu, basi mama yake atapata sudusi” (an-Nisaa’ [4]: 11).

 

Kwa hiyo, kulingana na Aayah ya hapo juu ni kuwa:

1.     Ukiwa na watoto, kila mzazi wako (baba na mama) atapata sudusi (1/6).

2.     Ikiwa wazazi ni warithi peke yake, baba atapata thuluthi mbili na mama thuluthi.

3.     Ikiwa una ndugu waliobakia nawe basi mama atapata sudusi.

 

Ama kumsaidia mama yako ni jambo zuri na la thawabu kubwa sana hapa duniani na Kesho Akhera. Mtazame kwa hali na mali kwa kumuweka katika nyumba yako, umlishe, umvishe, na kumpatia zawadi na bila kumsahau baba yako mzazi katika wema.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share