Skip navigation.
Home kabah

Inafaa Kufunga Siku 9 Za Dhul-Hijjah?

SWALI:

Assalamu aleikum warhma tullahi wabarakatu......

Jee inapasa ama inafaa kufunga yale masiku kumi ya dhul hajj,. Na vile vile kuna zile saum za siku tatu kabla hajj.

Kwani kuna baadhi wanaosema ni sunna siku kumi ama tatu. Shukran wa jazakallah.

 

 







 JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukran kwa swali lako na huu ni wakati muafaka kwani mwezi wa Dhul Hijjah haupo mbali nasi zikiwa kwa sasa zimebakia siku chache tu.kama

Ni muhimu tujue ya kwamba zile siku 10 za awali za mwezi wa 12 (Dhul Hijjah) katika kalenda ya Kiislamu zina fadhila kubwa. Haifai zikawa siku hizi zitampita mtu bila kufaidika. Zikipita siku hizi bila faida yoyote basi mtu kama huyo atakuwa amekhasirika . Allah Aliyetukuka Anatutajia fadhila za masiku hayo kwa kusema: sana

Naapa kwa Alfajiri. Na kwa masiku kumi” (89: 1-2).

Haya masiku kumi wanazuoni wengi wamesema ni siku kumi za mwanzo za Dhul Hijjah kwani hayo ni masiku bora katika mwaka. Hii imethibiti katika Hadiyth iliyopokewa na al-Bukhaariy: “Hakuna masiku ambayo amali njema zinapendwa na Allah ndani yake kuliko masiku haya – yaani masiku kumi ya Dhul Hijjah”. Akaulizwa: “Hata Jihadi katika njia ya Allah?” Akasema: “Hata Jihadi katika njia ya Allah ila mtu aliyetoka mwenyewe na yake, kisha asirudi na chochote (akafariki shahidi)”. Amali njema ni nyingi zikijumlisha hata funga.mali

Ingawa kuna Hadiyth iliyosimuliwa na mmoja wa wakeze ambaye amesema: “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akifunga masiku tisa ya mwanzo ya Dhul Hijjah, siku ya ‘Ashuuraa, na masiku matatu ya kila mwezi” [Abu Daawuud]

Lakini kutokana na Hadiyth nyingine iliyo sahihi inaonyesha kuwa hakuna uwajibu wa kufunga masiku hayo, na wala si Sunnah iliyojulikana kuwa akiifanya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Anasema mama wa waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anhaa): “Sikumuona Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akifunga masiku kumi (ya Dhul-Hijjah)” [Muslim]

Hivyo, unapoingia mwezi wa Dhul Hijjah mtu anaweza kufunga kuanzia tarehe moja hadi tarehe 9 (ambayo ni siku ya Arafah). Tarehe kumi haifai kufungwa na Muislamu kwani ni siku ya ‘Iyd na Waislamu wanafaa kusherehekea kwa kula. Katika mwezi huu zile siku tatu za funga zinakuwa hazipatikani kwani hizo huwa ni tarehe 13, 14 na 15 ambazo zinajulikana siku nyeupe. Sasa siku ya 13 inakuwa ni Tashriyq ambayo ni siku ya mwisho ya kuchinja kwa mwenye uwezo.kama

 Na kufunga siku hizo 9 unaweza kufunga kwa kadiri ya uwezo wako, ukipenda unaweza kufunga siku zote hizo au moja tu au mbili au tatu n.k. Na wala hakuna kufunga  siku tatu hasa za kabla ya Hajj.

Muhimu zaidi mtu asikose siku ya ‘Arafah kwa sababu ya fadhila zake nyingi na pia kwa kuthibiti kwake ushahidi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Vilevile anatakiwa Muislam ajue kuwa ushahidi wenye nguvu ni kuwa Mtume hakufunga masiku hayo, hivyo pamoja na kuwa Maulamaa wamependekeza kutokana na kheri za masiku hayo na pia inasemekana kuwa baadhi ya wema waliopita walifunga, ila asije Muislam kuitakidi kuwa ni lazima kufunga masiku hayo na hata kuwalazimisha watu au kusumbuana na wengine kwa hilo.

Siku ya ‘Arafah ni ile siku ambayo Mahujaji wamesimama katika wangwa (bonde) la ‘Arafah, tarehe 9 katika kalenda inayofuatwa na Saudia kwani Hijjah inafanywa huko. Hili wameafikiana wanazuoni wote. Mtume (Swalla Llahu ‘Alayhi wa sallam) amesema: “Hajj ni ‘Arafah”. Hii inamaanisha ukikosa kuwepo katika sehemu hiyo basi huna Hijjah ya mwaka huo. Ama kufunga siku hiyo, Abu Qataadah (Radhiya Llahu ‘Anhu) amesema, aliulizwa Mtume wa Allah (Swalla Llahu ‘Alayhi wa sallam) kuhusu kufunga siku ya ‘Arafah, akasema: “Inafuta madhambi ya mwaka uliopita na unaokuja” (Muslim, Abu Daawuud na Ibn Maajah).

Na Allah Anajua zaidi