19-Swabrun Jamiyl: Subira Za Maswahaba - Ka'ab bin Maalik (Radhwiya Allaahu 'Anhu)

 

Swabrun Jamilyl (Subira njema)

 

19 - Subira Za Maswahaba – Ka’ab Bin Maalik (Radhwiya Allaahu ‘Anhu)

 

 

 

 

Subira yake ilihusiana na Maswahaba watatu (Radhwiya Allaahu ‘anhum) waliofanya makosa ya kutokwenda kupigana vita vya Tabuwk bila ya sababu pamoja na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Vilikuwa ni vita ambavyo kwa mara ya kwanza jeshi la Waislam lilijitayarisha kupambana na jeshi kubwa la Warumi katika mwaka wa 9 Hijriyyah wakati wa joto kali sana. Vita hivyo vilivyojulikana kama ni ‘Vita vya Dhiki’. Wanafiki takriban themanini hawakushiriki na wakatoa visingizio mbali mbali. Lakini Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akateremsha Aayah kadhaa za Qur-aan katika Suwratut-Tawbah kuhusu unafiki wao.

 

 

Ka’ab bin Maalik (Radhwiya Allaahu 'anhu) alikuwa mwenye taqwa na mapenzi ya Allaah na Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Alikwishashiriki katika vita vyote pamoja na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) isipokuwa vita vya Badr. Na katika vita vya Uhud alimhami Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kubadilishana naye nguo ili maadui wasipate kumuandama na kumuua Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), na kwa hivyo, Ka’ab alipata majeraha kumi na moja.

 

 

Kisa chake kuhusu vita vya Tabuwk ni fundisho kubwa kwa Waislamu kujifunza subira katika kutafuta radhi za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) pamoja na kujifunza namna gani Maswahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) walikuwa watiifu kwa kiongozi wao na kipenzi chao Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Maswahaba watatu hao (Radhwiya Allaahu ‘anhum) walivumilia sana katika subira yao wakawa katika dhiki ya nafsi mpaka walihisi kuwa ardhi imewabana kutokana na dhiki. Walitambua kuwa hapana pa kukimbilia isipokuwa Kwake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Kisa chake amekielezea mwenyewe kama alivyokirekodi Imaam Al-Bukhaariy.

 

Anasema Ka’ab (Radhwiya Allaahu 'anhu):

“Sikupata kuwa katika hali nzuri kwa hali na mali kama nilivyokuwa wakati watu wakijitayarisha na vita hivyo. Wa-Allaahi sikupata kukusanya wanyama wawili wa kunipeleka vitani isipokuwa katika vita hivyo. Na ilikuwa kawaida ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anapotaka kupigana vita vyovyote hutoa ishara kama kwamba anataka kupigana vita vingine, (Isipokuwa katika vita hivi hakufanya hivyo kwa sababu ya umbali wa safari na ukali wa joto), mpaka ulipowadia wakati wa vita hivyo vilivyokuwa katika joto kali sana, safari ndefu, pamoja na maadui wengi sana.

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa katika hali ya kujitayarisha, na Waislam pia wakawa katika hali hiyo, na watu walikuwa wengi sana. Nikasema: “Kesho mimi nitajitayarisha nijiunge nao.” Nikawa nakwenda nikirudi bila ya kufanya chochote, huku nikijisemesha nafsini mwangu: “Wakati wowote ninapotaka nitaweza kujitayarisha nijiunge nao.”

 

Nikaendelea na hali hiyo mpaka mambo yalipoanza kupamba moto, na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipoamua kuondoka asubuhi ya siku ya pili yake pamoja na Waislam, na mimi bado sikuwa nimejitayarisha kwa chochote. Nikasema: “Nitajitayarisha siku ifuatayo baada ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuondoka, au hata baada ya siku mbili kisha nitakutana nao njiani kabla ya wao kuwasili Tabuwk.”

 

Nikatoka asubuhi ya siku ya pili ili nianze kujitayarisha na kununua mahitajio yangu ya vitani, hatimae nikarudi nyumbani bila kufanya chochote. Nikawa katika hali hiyo mpaka zikatufikia habari kuwa Waislam wamekwishawasili Tabuwk na kwamba vita vishaanza, ndipo iliponipitikia niondoke ili niwawahi. Laiti ningefanya hivyo. Lakini sikujaaliwa. Nikawa kila ninapotoka nje ya nyumba yangu na kuonana na watu, ninahuzunika sana na kuona uchungu kwa sababu sikuwa nikimuona mtu yeyote aliye kufu yangu (aliyelingana nami). Sikuwa nikiwaona isipokuwa wale watu waliokuwa wakijulikana kuwa ni wanafiki, au wale waliokuwa na udhuru wa kutokwenda vitani kwa sababu ya umasikini, udhaifu wa hali zao au maradhi.

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakuuuliza juu yangu mpaka walipowasili Tabuwk, akasema huku akiwa amekaa pamoja na watu: ((Amefanya nini Ka’ab?)) Mmoja katika watu wa Bani Salamah akasema: "Limemzuia tandiko lake na kuwatazama awapendao." Mu’aadh bin Jabal (Radhwiya Allaahu 'anhu) akasema: "Maneno mabaya yaliyoje uliyosema! Wa-Allaahi ee Rasuli wa Allaah, sisi tunavyomjua ni mtu anayependa kheri tu." Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akanyamza.

 

 

Niliposikia kuwa misafara inaanza kurudi nikaanza kujisemesha huku nikifikiri uongo upi niuseme hata Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) (anisadiki na) asighadhibike nami? Nikawaendea jamaa zangu wale wenye hekima kutaka ushauri wao. Wakati Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipowasili Madiynah, mimi nilikuwa nishafikia uamuzi kuwa sina budi kumwambia ukweli, na kwamba nikisema uongo sitoweza kuokoka nao. Nikaamua kuwa lazima niseme kweli tu. Asubuhi iliyofuata Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliwasili, na ilikuwa kawaida yake anapowasili kwanza huenda Msikitini kuswali rakaa mbili, kisha hukaa hapo muda kidogo kwa ajili ya kusikiliza matatizo ya watu. Wale waliobaki Madiynah wasiende vitani wakaanza kumuendea huku wakimtolea (kila aina ya) udhuru, na walikuwa kiasi cha watu themanini na kidogo hivi. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliwakubalia wote udhuru wao na kuwaombea maghfirah na kumuachia Rabb wao ukweli wa udhuru walioutoa. Nilipomsogelea mimi na kumsalimia alitabasamu huku akionyesha dalili ya kughadhibika nami, kisha akaniambia: ((Njoo)) Nikamuendea mpaka nikakaa mbele yake. Akaniuliza: ((Nini kilichokufanya ubaki nyuma, si ulikuwa ushajitolea kupigana?)) Nikamwambia: "Ndiyo, wa-Allaahi ningeulizwa suali hili na mwengine asiyekuwa wewe katika watu wa dunia ningeweza kusalimika kwa kutoa udhuru wowote ule. Lakini nilijishauri sana nikaona kuwa ikiwa nitakutolea udhuru wowote wa uongo leo ukaridhika nami, Allaah Atakujulisha na utakuja kunichukia. Na iwapo nitakuambia ukweli, ukaujua ukweli juu yangu, mimi nategemea msamaha wa Allaah. Wa-Allaahi sikuwa na udhuru wowote, wa-Allaahi sikupata kuwa na nguvu na uwezo wa kifedha kuliko siku niliyokuacha na kubaki nyuma.” Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaniambia: ((Ama huyu amesema kweli. Inuka na ungoje mpaka Allaah Atakapotoa uamuzi wake juu yako)).

 

Nikainuka na kuondoka hapo, na watu wa kabila la Bani Salamah wakainuka kunifuata, wakaniambia: "Wa-Allaahi sisi tunavyokujuwa ni kuwa hujapata kufanya kosa kabla ya hili, kwa nini umeshindwa kutoa udhuru (wowote) kama walivyofanya wengine? Ingelitosha kufuta dhambi yako kwa maghfirah atakayokuombea Rasuli kwa Allaah.” Wakawa wanaendelea kunilaumu mpaka nikafikiria nirudi tena kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kutoa udhuru wowote na kujidanganya nafsi yangu. Kisha nikawaambia: "Yuko mwengine aliyekuwa kama mimi?" Wakasema: "Wawili, wamesema kama ulivyosema na wakaambiwa kama ulivyoambiwa." Nikauliza: "Nani hao?" Wakaniambia: "Muraarah bin Rabiy’ Al-‘Amriy na Hilaal bin Umayyah Al-Waaqifiyy." Hawa ni watu wawili wenye taqwa waliopigana vita vya Badr na walijulikana kuwa ni wenye mfano mwema.

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaamrisha sote watatu tusisemeshwe na mtu.

 

Tukawa tunawaepuka watu na wao wanatuepuka. Haukupita muda watu wakaanza kutubadilikia hata nikaichukia ardhi ikawa kama nisiyoijua. Tukaendelea katika hali hiyo muda wa siku hamsini. Wenzangu walijikalia majumbani mwao wakilizana, lakini mimi nilikuwa kijana zaidi kupita wao na mwenye ustahamilivu zaidi. Nikawa natoka na kuswali Msikitini pamoja na Waislam, huku nikitembea sokoni, lakini hakuna mtu anayenisemesha. Nilikuwa nikimkabili Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kumsalimia akiwa amekaa mahali pake baada ya Swalaah, kisha hujiuliza nafsini mwangu: “Mdomo wake ulitikisika kuijibu salamu au haukutikisika?” Mara nyingi huswali karibu yake, na baada ya Swalaah, humtizama kwa kuibiaibia huku nikijishughulisha na du’aa baada ya Swalaah, na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa mara nyingine akiniangalia, lakini ninapomuangalia mimi, yeye huugeuza uso wake.

 

Dhiki ya kupigwa pande ilipozidi nikaamua siku moja kwenda nyumbani kwa Abuu Qataadah ambaye ni mtoto wa ‘ammi yangu, na nilikuwa nikimpenda sana. Nikaparamia ukuta, nikaingia uani na kugonga mlango wa nyumba yake, nikaingia ndani na kumsalimia. Wa-Allaahi hakuijibu salamu yangu. Nikamuambia: "Abu Qataadah! Unavyonijua mimi je, simpendi Allaah na Rasuli Wake?" Akanyamaza asinijibu kitu. Nikamuuliza tena suala hilo hilo, akanijibu: “Allaah na Rasuli Wake ndio wanaojua.” Machozi yakanitoka. Nikaondoka na kuruka ukuta nikatoka nje.

 

Siku moja nilipokuwa nikitembea sokoni nikamsikia mmoja katika watu wa Shaam aliyekuja kufanya biashara ya vyakula akisema: “Nani atakayenipeleka kwa Ka’ab bin Maalik?” Watu wakamuelekeza kwangu. Akanijia na kunipa barua iliyotoka kwa mfalme Ghassaan iliyoandikwa yafuatayo: “Nimepata habari kuwa sahibu yako amekupiga pande, na Rabb wako amekufanya usiwe na raha, kwa hivyo njoo kwetu tutakuliwaza.” Nikasema moyoni mwangu: “Huu pia ni mtihani mwengine.” Nikaitumbukiza barua ile ndani ya tanuri la moto na kuiunguza, na ilipofika siku ya arubaini katika zile siku hamsini, mjumbe kutoka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alinijia na kuniambia: "Kwa hakika Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anakuamrisha usimkaribie mkeo”.

Nikamuuliza: “Nimtaliki au nifanyeje?” Akaniambia: “Bali uwe mbali naye na usimkaribie.” Na wenzangu wale wawili wakapewa amri kama niliyopewa mimi. Nikamuambia mke wangu: “Nenda kwa wazee wako na ubaki kwao mpaka Allaah Atakapotoa amri Yake.” Mke wa Hilaal bin Umayyah alikwenda kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kumuambia: “Ee Rasuli wa Allaah, kwa hakika mume wangu Hilaal ni mtu mzima asiyeweza kujitumikia mwenyewe na hana mfanyakazi wa kumsaidia, utachukizwa iwapo nitabaki kwake na kumhudumia?” Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamuambia: ((Hapana [sitochukizwa] lakini asikukaribie)). Akasema: “Wa-Allaahi yeye hana haja ya kufanya jambo lolote. Tokea yalipotokea yaliyotokea, mpaka leo hana isipokuwa kulia tu.”

 

Baadhi ya watu wangu wakaniambia: “Na wewe ungelimuomba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amruhusu mkeo akutumikie kama alivyomruhusu mke wa Hilaal bin Umayyah.” Nikawaambia: “Wa-Allaahi mimi sitomuomba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), sijui atanijibu nini nitakapomuomba, kwa sababu mimi ni kijana bado.” Nikaendelea katika hali hiyo kwa muda wa siku kumi nyingine, mpaka zikakamilika siku hamsini tokea Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipowataka watu wasitusemeshe.

 

Baada ya kuswali Swalaah ya Alfajiri ya siku ya hamsini, nikapanda juu ya dari la mojawapo ya nyumba zetu na kukaa. Na wakati nilipokuwa katika hali ile Aliyoisema Allaah kuwa: ((mpaka ardhi ikadhikika kwao juu ya kuwa ni pana)) [At-Tawbah 9: 118] Nikasikia sauti kali ikitokea juu ya jabali ikisema: “Ee Ka’ab pokea bishara njema!” Pale pale nilipo nikaporomoka na kusujudu, nikajua kuwa faraja imekwishawasili. Baada ya Swalaah ya Alfajiri Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliwatangazia watu juu ya kusamehewa kwetu na Allaah, na watu wakatoka na kuanza kutupa bishara njema hizo.

 

Wengine wakaja kwangu na wengine wakaenda kwa sahibu zangu. Walikuja wakiwa wamepanda wanyama wao na wengine kwa miguu kwa ajili ya kutupongeza. Na aliponijia yule niliyeisikia sauti yake akinipa bishara njema pale mwanzo, nilimvisha guo langu kama ni zawadi yake. Wa-Allaahi sikuwa nikimiliki isipokuwa nguo hiyo tu, na mimi nikaazima nguo nyingine za kuvaa, kisha nikaelekea Msikitini kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) huku watu wakinijia makundi kwa makundi wakinipongeza na kuniambia: “Tunakupongeza kwa tawbah iliyokuja kutoka kwa Allaah!”   Nilipoingia Msikitini, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa amekaa akiwa amezungukwa na watu, na Twalhah bin ‘Ubaydillaah alikuwa wa mwanzo kunijia mbio na kunipa mkono na kunipongeza. Hakusimama na kunipongeza katika Muhaajiriyn mahali pale isipokuwa Twalhah, sitomsahau kwa tendo lake hilo.

 

Nilipomsalimia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) huku uso wake ukiwa unang'ara kwa furaha, na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anapofurahi, uso wake huwa unang'ara mfano wa kipande cha mwezi, akaniambia: ((Pokea bishara njema za kufikiwa na siku bora kupita siku zote tokea ulipozaliwa)) Nikamuuliza: “Msamaha huu umetoka kwako ee Rasuli wa Allaah, au kutoka kwa Allaah?” Akanijibu: ((Bali kutoka kwa Allaah)).  Nikiwa bado nimekaa mbele yake nikamuambia: “Ee Rasuli wa Allaah, kwa ajili ya kutubiwa kwangu huku, nataka kutoa mali yangu yote sadaka kwa ajili ya Allaah.”  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaniambia: ((Zuia mali yako, kwani hiyo ni kheri yako)). Nikamuambia: “Mimi nitazuia sehemu yangu ya Khaybar.”

 

Nikawa kila siku naiambia nafsi yangu: “Allaah Ameniokoa kwa ajili ya kusema ukweli. Kwa ajili hiyo katika maisha yangu sitotamka isipokuwa ukweli tu. Kwani Wa-Allaahi simjui Muislam yeyote aliyepata mtihani mkubwa kutoka kwa Allaah kwa ajili ya kusema ukweli tokea siku niliyozungumza na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) mpaka leo hii, kuliko mtihani nilioupata mimi. Na mimi namuomba Allaah Anihifadhi katika siku zangu zilizobaki." Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akateremsha Aayah zifuatazo:

 

لَّقَد تَّابَ اللَّـهُ عَلَى النَّبِيِّ وَالْمُهَاجِرِينَ وَالْأَنصَارِ الَّذِينَ اتَّبَعُوهُ فِي سَاعَةِ الْعُسْرَةِ مِن بَعْدِ مَا كَادَ يَزِيغُ قُلُوبُ فَرِيقٍ مِّنْهُمْ ثُمَّ تَابَ عَلَيْهِمْ ۚ إِنَّهُ بِهِمْ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ﴿١١٧﴾

 

Kwa yakini Allaah Amepokea tawbah ya Nabiy na Muhajirina na Answaar ambao wamemfuata (Nabiy صلى الله عليه وآله وسلم) katika saa ya dhiki baada ya nyoyo za kundi miongoni mwao zilikaribia   kuelemea mbali na haki Akapokea tawbah yao. Hakika Yeye kwao ni Mwenye huruma mno, Mwenye kurehemu.

 

وَعَلَى الثَّلَاثَةِ الَّذِينَ خُلِّفُوا حَتَّىٰ إِذَا ضَاقَتْ عَلَيْهِمُ الْأَرْضُ بِمَا رَحُبَتْ وَضَاقَتْ عَلَيْهِمْ أَنفُسُهُمْ وَظَنُّوا أَن لَّا مَلْجَأَ مِنَ اللَّـهِ إِلَّا إِلَيْهِ ثُمَّ تَابَ عَلَيْهِمْ لِيَتُوبُوا ۚ إِنَّ اللَّـهَ هُوَ التَّوَّابُ الرَّحِيمُ﴿١١٨﴾

 

Na (Akapokea tawbah) ya wale watatu waliobaki nyuma (wakajuta mno) mpaka ardhi ikadhikika kwao juu ya kuwa ni pana na zikadhikika nafsi zao, na wakatambua kwamba hakuna pa kumkimbia Allaah isipokuwa kuelekea Kwake; kisha (Allaah) Akapokea tawbah yao, ili watubie. Hakika Allaah Yeye Ndiye Mwingi wa kupokea tawbah, Mwenye kurehemu.

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَكُونُوا مَعَ الصَّادِقِينَ﴿١١٩﴾

 

Enyi walioamini! Mcheni Allaah na kuweni pamoja na wakweli. [At-Tawbah: 117-119]

 

 

Naapa kwa Allaah! Mbali ya (neema) kuwa Allaah Amenihidi katika Uislamu, Hajapata kuniteremshia neema kama neema ya ukweli wangu kuwa sikusema uongo kwa Rasuli wa Allaah, jambo ambalo lingeliniangamiza kama walivyoangamia waliosema uongo, kwani Allaah Amewataja waliosema uongo kwa sifa mbaya kabisa Hajapatapo kumpa sifa hiyo yeyote mwengine, Aliposema:

 

سَيَحْلِفُونَ بِاللَّـهِ لَكُمْ إِذَا انقَلَبْتُمْ إِلَيْهِمْ لِتُعْرِضُوا عَنْهُمْ ۖ فَأَعْرِضُوا عَنْهُمْ ۖ إِنَّهُمْ رِجْسٌ ۖ وَمَأْوَاهُمْ جَهَنَّمُ جَزَاءً بِمَا كَانُوا يَكْسِبُونَ﴿٩٥﴾

 

Watakuapieni kwa Allaah, mtakaporudi kwao ili muwapuuze. Basi wapuuzeni; hakika wao ni najsi, na makazi yao ni Jahannam. Ni jazaa kwa yale waliyokuwa wakiyachuma.

 

يَحْلِفُونَ لَكُمْ لِتَرْضَوْا عَنْهُمْ ۖ فَإِن تَرْضَوْا عَنْهُمْ فَإِنَّ اللَّـهَ لَا يَرْضَىٰ عَنِ الْقَوْمِ الْفَاسِقِينَ﴿٩٦﴾

 

Watakuapieni ili muwaridhie. Mkiwaridhia, basi hakika Allaah Haridhii watu mafasiki. [At-Tawbah:  95-96]

 

 

Ka’ab akaendelea kusema: “Hali ya sisi watatu ni tofauti na ambao visingizio vyao alivipokea Rasuli wa Allaah walipomuapia. Akafungamana nao kiapo cha utiifu, na akamuomba Allaah Awasamehe. Lakini Rasuli wa Allaah aliacha kesi yetu ibakie kungoja uamuzi mpaka Allaah Alipoitolea hukmu Yake. Na kwa hiyo Akasema Allaah:

((Na [Akapokea tawbah ya] wale watatu walioachwa nyuma [wakajua makosa yao]...))

 

Aliyoyasema Allaah katika Aayah hii haidhihirishi kushindwa kwetu kushiriki vita, ila inahusu kuakhirishwa maamuzi ya Rasuli kuhusu kesi yetu. Ni tofauti na kesi ya waliofungamana naye kiapo akawasamehe kwa kupokea visingizio vyao”.

 

Share