Wakati Wa Swalah Ya Tahajjud Na Vipi Kuswali
SWALI:
Swala ya Tahajjud inaswaliwa vipi? Na wakati gani?
Je unaweza kutumia saa yake ikuamshe ili upate kuswali au mpaka uamke mwenyewe?
JIBU:
AlhamduliLLah, Waswalaatu Was-salaam 'alaa Rasuli-Llah صلى الله عليه وآله وسلم Amma ba'ad,
Swalah ya Tahajjud ni Swalah inayoswaliwa usiku ambayo pia kwa jina lengine ni Qiyaamul-Layl (kusimama kuswali usiku). Nayo huswaliwa wakati wowote baada ya Swalah ya 'Ishaa mpaka karibu na Alfajiri.
Ama ikiwa mtu anataka kupata fadhila zilizotajwa kuswali katika thuluthi ya usiku
((Imetoka kwa Abu Hurayra رضي الله عنه kwamba Mtume صلى الله عليه وسلم amesema: Allaah سبحانه وتعالى Huteremka kila siku katika mbingu ya dunia (mbingu ya kwanza) inapobakia thuluthi ya mwisho ya usiku na Husema: Nani ananiomba nimtakabalie? Nani Ana shida nimtekelezee? Nani ananiomba maghfira nimghufurie? ))
basi wakati huu wa Thuluthi ya mwisho ni kugawa sehemu tatu wakati tokea Swalah ya Magharibi mpaka Swalah ya Alfajiri. Sehemu ya tatu ndio wakati unaitwa Thuluthiy-Llayl ya mwisho (thuluthi ya usiku )
Na huswaliwa ifuatavyo:
a) Idadi ya Swalah za Sunnah za usiku
Jumla ya Swalah za usiku za Sunnah ni Raka'ah kumi na moja kutokana na Hadiythi ya Bibi 'Aishah ضي الله عنها
((Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa akiswali usiku Raka'ah kumi na akitoa salam baada ya kila Raka'ah mbili kisha akiswali Witr Raka'ah moja)) Muslim
Na akasema vile vile ((Hajapata Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kuzidisha katika Ramadhaan wala miezi mingine zaidi ya Raka'ah kumi na moja, akiswali nne, wala usiulize uzuri wake na urefu wake, kisha akiswali nne wala usiulize uzuri wake na urefu wake, kisha akiswali tatu)) Al-Bukhariy na Muslim
b) Namna zinavyoswaliwa Swalah za usiku
Unatoa salam kila baada ya Raka'ah mbili
((Swalah ya usiku ni (raka’ah) mbili mbili na ukiogopa kukukuta asubuhi basi Swali Witr [Raka'ah] moja)) Al-Bukhariy
c) Sura za kusoma katika Swalah ya usiku
Hakuna Sura Maaluum ya kusomwa katika Swala za usiku, bali ni vizuri sana kusoma sura ndefu kwani kama hadithi ya Bibi 'Aishah iliyotajwa hapo juu kuwa alisema 'wala usiniulize uzuri wake' akikusudia kuwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa akiswali Swalah kwa utulivu kabisa kwa kusoma mara nyingine sura ndefu, Rukuu ndefu, sujuud ndefu na kadhalika.
Ifuatayo ni Hadiyth inayoonyesha fadhila za kusoma aya nyingi katika Swalah ya usiku:
((Atakayesimama (usiku) na aya kumi hatoandikiwa katika miongoni mwa walioghafilika, na atakayesimama kwa aya mia ataandikiwa ni miongoni mwa wanyenyekevu, na atakayesimama kwa aya Alfu ataandikwa miongoni mwa wenye mirundi)) Abu Dawuud na amesahihisha Albaniy (Maana ya mirundi ni wale walio na mrundi wa thawabu)
Ama katika Raka'ah tatu za mwisho imethibitika kuwa alikuwa akisoma sura hizi
Hadiyth kutoka kwa Bibi 'Aishah رضي الله عنها ambaye amesema ((Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa akisoma katika Raka'ah ya mwanzo ya (Swalah) Witr 'Sabbihisma Rabikal-A'ala' na Raka'ah ya pili 'Qul-Yaa-Ayyuhal-Kaafiruun' na Raka'ah ya tatu 'Qul- Huwa-Allaahu Ahad pamoja na Qul-A'udhu mbili (Al Falaq na An Naas)' At Tirmidhiy
Raka'ah hizi tatu za mwisho vile vile ziswaliwe mbili kwanza kisha umalizie na moja pekee, na katika hiyo raka’ah ya mwisho bada ya kuinuka katika ruku'u usome du'aa ya Qunuut. Au ziswaliwe zote tatu kwa tash-shahud moja tu ya mwisho na kisha kutoa salaam, yaani bila kusoma At-Tahiyaat kwenye raka’a ya pili, na kufanya huku wanasema Ma'ulamaa ni kuitofautisha na Swalah ya Maghrib ambayo unakaa At-Tahiyaat kwenye raka’ah ya pili.
Swali kuhusu kuweka saa au kuamka mwenyewe, jibu ni kwamba hakuna shuruti ya kuweka saa, vyovyote utakavyoamka kuswali ni sawa fadhila zake ni zile zile.
Wa Allaahu A'alam.
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha
