Je Kuna Malipo Kama Hukumnyonyesha Mtoto?

SWALI

ASALAM ALYKUM MIMI NAULIZA NI MUDA GANI WA KUMYONYESHA MTOTO HALAFU KAMAHAUKUTIMIA IMETOKEA BAHATI MBAYA UNAWEZA KUMLIPA  YULE MTOTO?

 


JIBU:

BismiLLaah wa AlhamduliLLaah was-Swalaatu wa Salaamu ‘alaa Muhammad wa ‘alaa  aalihi wa Aswhaabihil Kiraam, wa Ba’ad:

Muda wa kunyonyesha ni miaka miwili na hakuna fidia ya kumlipa mtoto ikiwa hutomnyonyesha mtoto wako. Mas-ala yote haya yamekusanyika dalili zake katika kauli ya Allaah سبحانه وتعالى  ifuatayo: 

((وَالْوَالِدَاتُ يُرْضِعْنَ أَوْلاَدَهُنَّ حَوْلَيْنِ كَامِلَيْنِ لِمَنْ أَرَادَ أَن يُتِمَّ الرَّضَاعَةَ وَعلَى الْمَوْلُودِ لَهُ رِزْقُهُنَّ وَكِسْوَتُهُنَّ بِالْمَعْرُوفِ لاَ تُكَلَّفُ نَفْسٌ إِلاَّ وُسْعَهَا لاَ تُضَآرَّ وَالِدَةٌ بِوَلَدِهَا وَلاَ مَوْلُودٌ لَّهُ بِوَلَدِهِ وَعَلَى الْوَارِثِ مِثْلُ ذَلِكَ فَإِنْ أَرَادَا فِصَالاً عَن تَرَاضٍ مِّنْهُمَا وَتَشَاوُرٍ فَلاَ جُنَاحَ عَلَيْهِمَا وَإِنْ أَرَدتُّمْ أَن تَسْتَرْضِعُواْ أَوْلاَدَكُمْ فَلاَ جُنَاحَ عَلَيْكُمْ إِذَا سَلَّمْتُم مَّآ آتَيْتُم بِالْمَعْرُوفِ وَاتَّقُواْ اللّهَ وَاعْلَمُواْ أَنَّ اللّهَ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِير))

((Na wazazi wanawake wawanyonyeshe watoto wao miaka miwili kamili kwa anayetaka kutimiza kunyonyesha. Na juu ya baba yake chakula cha kina mama, na nguo zao kwa mujibu wa ada. Wala halazimishwi mtu ila kwa kadiri ya uwezo wake. Mama asitiwe tabuni kwa ajili ya mwanawe, wala baba kwa ajili ya mwanawe. Na juu ya mrithi mfano wa hivyo. Na kama wote wawili wakitaka kumwachisha ziwa kwa kuridhiana na kushauriana, basi si vibaya kwao. Na mkitaka kuwapatia watoto wenu mama wa kuwanyonyesha basi hapana ubaya kwenu mkitoa mlichoahidi kwa mujibu wa ada. Na mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni kwamba Mwenyezi Mungu Anayaona yote mnayoyatenda)) [Al-Baqarah: 233]

Lakini, mama anafaa atambue kuwe kumnyonyesha mtoto ni jambo lenye kumpatia faida nyingi mtoto pamoja na mama yake, kwani ni jambo la kitabia Alilojaaliya Allaah سبحانه وتعالى  na kwa Rahma Yake kubwa na Hikma Yake na bila shaka faida zake hakuna asiyezikubali, kwani hata madaktari wametambua faida nyingi baada ya utafiti. Baadhi ya hizo faida tunazitaja hapa:

Faida kwa mtoto mwenyewe

1.   Mtoto analindika na maradhi mengi ya kila aina.

2. Imepatikana asilimia ndogo ya vifo vya watoto wanaonyonyeshwa  vifuani.

3. Asilimia kubwa imeonekana kuwa watoto wanaonyonyeshwa huwa ni wenye akili kubwa (mahodari) na wenye utulivu zaidi.

4. Maziwa ya mama ni chakula kamili anachokihitaji mtoto katika miezi yake ya mwanzo.

5. Maziwa ya mama yako tayari wakati wowote na yako katika hali ya joto linalomfaa mtoto.

6. Huenda maziwa ya kutengenezwa yakamfanyia mtoto mzio (allergy), ama maziwa ya kifuani hayana matatizo kama hayo.

7. Hupata hamu ya kupenda kula zaidi (appetite).      

 

Faida kwa mzazi

1.   Mama atapata himaya kutokana na maradhi ya saratani (cancer)

2.  Fuko la uzazi hurudi katika hali yake ya kawaida baada ya kunyonyesha.

3.  Mwili wa mama hupunguka uzito uliomzidi.     

4. Ni njia ya kupunguza masarifu ya hela kwa kununua badala yake maziwa ya sinai  (ya kutengenezwa) na pia kuepukana na malipo ya hospitali kutokana na utafiti ulioonekana kwamba asilimia kubwa ya watoto wasionyonyeshwa hupata maradhi mara kwa mara.

5. Kujipunguzia kazi za kutengeneza maziwa ya sinai (ya kutengenezwa) na kupata faida ya wakati zaidi, kwani ya kifuani yako tayari hayahitaji wakati wa kutengeneza, mbali pia kujiepusha na kazi za kukosha chupa na vifaa vya maziwa ya sinai.

6. Wakati wowote, mahali popote yako tayari hana haja mama ya kubeba chupa za maziwa anapotoka nje au anapokuwa safarini.

Faida baina ya mama na mtoto

1.  Mtoto na mama wote kupata utulivu na kutulia nafsi.

2.  Huathiri mapenzi baina yao yakawa makubwa zaidi.

3. Mama huridhika kuwa ameitumia Rahma na neema ya Allah (Subhaana wa Ta'aalah) na hutosheka kuwa ametimiza wajibu wake kwa mwanawe kwani wengi wanaoacha kunyonyesha huja kujuta baadaye. 

Baada ya kutambua faida hizo hatudhani kama mama yeyote atapenda kuacha kumnyonyesha mtoto wake, kwani hii ni Rahma na neema mojawapo kubwa kutoka kwa Mola Mtukufu Aliyemjaalia mja Wake, kwa hivyo kwa nini mama asiitumie neema hii?

Na Allah Anajua zaidi.

 

Share