07-Sifa Kumi Na Fadhila Zake: Watoao Sadaka Wanaume Na Wanawake

 

Sifa Kumi Na Fadhila Zake

 

07- Watoao Sadaka Wanaume Na Wanawake

 

 

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

إِنَّ الْمُسْلِمِينَ وَالْمُسْلِمَاتِ وَالْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ وَالْقَانِتِينَ وَالْقَانِتَاتِ وَالصَّادِقِينَ وَالصَّادِقَاتِ وَالصَّابِرِينَ وَالصَّابِرَاتِ وَالْخَاشِعِينَ وَالْخَاشِعَاتِ وَالْمُتَصَدِّقِينَ وَالْمُتَصَدِّقَاتِ

Hakika Waislamu wanaume na wanawake, na Waumini wanaume na wanawake, na watiifu wanaume na wanawake, na wasemao kweli wanaume na wanawake, na wanaosubiri wanaume na wanawake, na wanyenyekevu wanaume na wanawake, na watoao swadaqah wanaume na wanawake, [Al-Ahzaab: 35]

 

 

Sadaka ni kufanya wema kwa watu wenye kuhitaji na ambao ni dhaifu na wasiokuwa na uwezo kuwatoshelezea mahitaji yao.

 

Kutoa sadaka ni ‘amali njema ya kumtii Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Aliyoyaamrisha katika Qur-aan na kutafuta radhi Zake:

 

 

وَمَا تُنفِقُوا مِنْ خَيْرٍ فَلِأَنفُسِكُمْ ۚ وَمَا تُنفِقُونَ إِلَّا ابْتِغَاءَ وَجْهِ اللَّـهِۚ وَمَا تُنفِقُوا مِنْ خَيْرٍ يُوَفَّ إِلَيْكُمْ وَأَنتُمْ لَا تُظْلَمُونَ ﴿٢٧٢﴾

Na chochote cha kheri mtoacho basi ni kwa ajili ya nafsi zenu. Na hamtoi ila kutaka Wajhi wa Allaah. Na chochote mtoacho katika kheri mtalipwa kamilifu nanyi hamtodhulumiwa [Al-Baqarah: 272]

 

 

Al-Hasan Al-Basri amesema: "Kila Muumini anapotumia (sadaka) pamoja na matumizi yake mwenyewe hutafuta radhi za Allaah [Ibn Haatim 3:1115].

Abubakar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alijulikana kuwa na sifa hiyo ya ukarimu wa kutoa sadaka na ndio maana zilipoteremka Aayah:

وَسَيُجَنَّبُهَا الْأَتْقَى ﴿١٧﴾

Na ataepushwa nao mwenye taqwa kabisa.

 

 

الَّذِي يُؤْتِي مَالَهُ يَتَزَكَّىٰ ﴿١٨﴾

Ambaye anatoa mali yake kujitakasa.

 

 

وَمَا لِأَحَدٍ عِندَهُ مِن نِّعْمَةٍ تُجْزَىٰ ﴿١٩﴾

Na hali hakuna mmoja yeyote aliyemfanyia fadhila yoyote hata amlipe.

 

 

إِلَّا ابْتِغَاءَ وَجْهِ رَبِّهِ الْأَعْلَىٰ ﴿٢٠﴾

Isipokuwa kutaka Wajihi wa Rabb wake Aliyetukuka.

 

وَلَسَوْفَ يَرْضَىٰ ﴿٢١﴾

Na bila shaka atakuja kuridhika. [Al-Layl: 17-21]

 

 

Wafasiri wa Qur-aan wametaja kuwa Aayah hizo zinamhusu Abuu Bakar As-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwa sababu   yeye ni mwenye kustahiki kupewa sifa hizo pamoja na sifa nyingine nyingi njema. Hakika yeye alikuwa ni mkweli, mwenye taqwa ya hali ya juu, mkarimu aliyekuwa akitoa daima mali yake kwa wanaohitajia na alimsaidia sana Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kutoa mali yake katika njia ya Allaah.

 

Muislam anapotoa sadaka kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), basi thawabu zake zitakuwa zimeshafika kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) hata kama sadaka yake imemfikia asiyestahiki akaja kutambua baadaye kwa dalili:

 

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَة رضي الله عنه قَالَ : قَالَ رَسُول اللَّه - صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ (( قَالَ رَجُل "لَأَتَصَدَّقَنَّ اللَّيْلَة بِصَدَقَةٍ" فَخَرَجَ بِصَدَقَتِهِ فَوَضَعَهَا فِي يَد زَانِيَةٍ فَأَصْبَحَ النَّاس يَتَحَدَّثُونَ  "تُصُدِّقَ عَلَى زَانِيَة" فَقَالَ : "اللَّهُمَّ لَك الْحَمْد عَلَى زَانِيَة لَأَتَصَدَّقَنَّ اللَّيْلَة بِصَدَقَةٍ" فَوَضَعَهَا فِي يَد غَنِيّ فَأَصْبَحُوا يَتَحَدَّثُونَ "تُصُدِّقَ اللَّيْلَة عَلَى غَنِيّ" قَالَ : "اللَّهُمَّ لَك الْحَمْد عَلَى غَنِيّ لَأَتَصَدَّقَنَّ اللَّيْلَة بِصَدَقَةٍ" فَخَرَجَ فَوَضَعَهَا فِي يَد سَارِق فَأَصْبَحُوا يَتَحَدَّثُونَ "تُصُدِّقَ اللَّيْلَة عَلَى سَارِق" فَقَالَ : "اللَّهُمَّ لَك الْحَمْد عَلَى زَانِيَة وَعَلَى غَنِيّ وَعَلَى سَارِق" فَأُتِيَ فَقِيلَ لَهُ "أَمَّا صَدَقَتك فَقَدْ قُبِلَتْ وَأَمَّا الزَّانِيَة فَلَعَلَّهَا أَنْ تَسْتَعِفَّ بِهَا عَنْ زِنًا وَلَعَلَّ الْغَنِيّ يَعْتَبِر فَيُنْفِق مِمَّا أَعْطَاهُ اللَّه وَلَعَلَّ السَّارِق أَنْ يَسْتَعِفَّ بِهَا عَنْ سَرِقَته")). البخاري و مسلم

Imetoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mtu mmoja alisema: "Leo nitatoa sadaka." Akatoka na sadaka yake na (bila ya kujua) akampa mzinifu. Asubuhi ya pili watu wakasema: "Sadaka imetolewa kwa mzinifu." Yule mtu akasema: "Yaa Allaah! Himdi ni Zako (Nimetoa sadaka yangu) kwa mzinifu. Usiku wa leo nitatoa sadaka tena." Akatoka na sadaka yake na (bila ya kujua) akampa tajiri. Siku ya pili (watu) wakasema: "Usiku wa jana tajiri kapewa sadaka." Akasema: "Yaa Allaah! Himdi ni Zako. (Nimetoka sadaka) kwa tajiri. Usiku wa leo nitatoa sadaka tena." Akatoka na sadaka yake na (bila ya kujua) akampa mwizi. Asubuhi ya pili (watu) wakasema: "Usiku wa jana mwizi alipewa sadaka." Akasema: "Yaa Allaah! Himdi ni Zako (nimetoa sadaka) kwa mzinifu, tajiri na mwizi." Akaja mtu na kumwambia: "Sadaka uliyoitoa imekubaliwa. Kwani mzinifu, huenda sadaka ikamzuia kufanya uzinifu. Ama tajiri, huenda ikampa fundisho naye atoe (sadaka) mali yake aliyopewa na Allaah. Ama mwizi, huenda ikamzuia kuiba.")) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Aayah nyingi na Hadiyth zimetaja kuhusu fadhila za kutoa sadaka. Na Muislamu anapotoa sadaka Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Humlipa duniani marudufu na Akhera pia hupata ujira wake. Na jambo la kutia moyo katika kutoa sadaka ni kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Ametuhakikishia kuwa tunapotoa basi ni kama mkopo tunaomkopesha Yeye kama Anavyosema: 

 

مَّن ذَا الَّذِي يُقْرِضُ اللَّـهَ قَرْضًا حَسَنًا فَيُضَاعِفَهُ لَهُ وَلَهُ أَجْرٌ كَرِيمٌ ﴿١١﴾

Nani ambaye atamkopesha Allaah karadha nzuri kisha (Allaah) Amuongezee maradufu na apate ujira mtukufu. [Al-Hadiyd: 11]

 

Na Muislamu asidharau kutoa japo iwe ni kitu kidogo mno kadiri ya tendo moja.

 

وعَن عَدِيِّ بنِ حاتم رضي اللَّه عنه أَن رسول اللَّه صَلّى اللهُ عَلَيْهِ وسَلَّم قال :  (( اتَّقُوا النَّارَ وَلَوْ بِشِقِّ تَمَرةٍ)) متفقٌ عليه

Imetoka kwa 'Adiyyi bin Haatim (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Jikingeni na moto hata kwa kipande cha tende)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Kisa Cha Aliyetoa  Sadaka Kutoka Katika Shamba Lake:

 

   

عن أبي هريرة رضي الله عنه عن النبي صَلّى اللهُ عَلَيْهِ وسَلَّم قال  ((بيْنَما رَجُلٌ يَمشِي بِفَلاةٍ مِن الأَرض ، فَسَمِعَ صَوتاً في سَحَابَةٍ : اسقِ حَدِيقَةَ فُلانٍ ، فَتَنَحَّى ذلكَ السَّحَابُ فَأَفْرَغَ مَاءَهُ في حَرَّةٍ ، فإِذا شرجة من تِلْكَ الشِّراجِ قَدِ اسْتَوعَبَتْ ذلِكَ الماءَ كُلَّهُ فَتَتَبَّعَ الماءَ ، فإِذا رَجُلٌ قَائِمٌ في حَدِيقَتِهِ يُحَوِّلُ المَاءَ بمِسحَاتِهِ ، فقال له : يا عَبْدَ اللَّهِ ما اسْمُكَ قال : فُلانٌ، للاسْمِ الَّذِي سَمِعَ في السَّحَابَةِ ، فقال له : يَا عَبْدَ اللَّهِ لِمَ تَسْأَلُنِي عَنِ اسْمِي ؟ فَقَال : إني سَمِعْتُ صَوتاً في السَّحَابِ الذي هذَا مَاؤُهُ يقُولُ : اسقِ حَدِيقَةَ فُلانٍ لإسمِكَ ، فما تَصْنَعُ فِيها ؟ فقال : أَما إِذْ قُلْتَ هَذَا ، فَإني أَنْظُرُ إِلى ما يَخْرُجُ مِنها ، فَأَتَّصَدَّقُ بثُلُثِه ، وآكُلُ أَنا وعِيالي ثُلُثاً ، وأَردُّ فِيها ثُلثَهُ)) . رواه مسلم

 

Imetoka kwa Abuu Hurayra (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Wakati mtu mmoja alikuwa anatembea njiani katika ardhi ya ukame ambayo haina alama ya maji, alisikia  sauti inatoka kutoka katika mawingu ikisema: "Mwagia maji shamba la fulani!" Mawingu yakaelekea upande fulani na kuanza kumwaga maji juu ya miamba tambarare. Mchiriziko ukatiririka katika mfereji mkubwa. Mtu huyo akaufuata mfereji huo hadi ukafika katika shamba na akamuona mwenye kumiliki shamba amesimama katikati yake akiyatandaza maji kwa sepeto (huku anabadilisha njia ya maji yaelekee katika sehemu nyingine ya shamba lake). Akamuuliza: "Ee mja wa Allaah! Jina lako nani?" Akamwambia jina lake ambalo ni lile lile alilolisikia kutoka katika mawingu. Mwenye shamba akamuuliza: "Ee mja wa Allaah! Kwa nini umeniuliza jina langu?" Akamjibu: "Nimesikia sauti kutoka katika mawingu yaliyomwaga maji ikisema: "Mwagia maji shamba la fulani." Basi nataka kujua huwa unaifanyia jambo gani?" Akasema: "Kwa vile umeniuliza nitakuambia: Hupima mapato ya shamba na kugawa thuluthi moja katika sadaka, na thuluthi moja natumia mwenyewe na familia yangu, na thuluthi moja nairudisha katika (kuizalisha) shamba")) [Muslim]

 

Muumini anapotoa Sadaka basi ni ahadi ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kumzidishia fadhila Zake mbali mbali. Ama asiyependa kutoa sadaka juu ya kuwa na uwezo basi ni tahadharisho kwake kuombewa du’aa na Malaika apate khasara katika mali yake kama ilivyothibiti katika Hadiyth:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه)  أَنَّ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((مَا مِنْ يَوْمٍ يُصْبِحُ الْعِبَادُ فِيهِ إلاَّ مَلَكَانِ يَنْزِلاَنِ فَيَقُولُ أَحَدُهُمَا: اللَّهُمَّ أَعْطِ مُنْفِقًا خَلَفًا. وَيَقُولُ الأَخَرُ: اللَّهُمَّ أَعْطِ مُمْسِكًا تَلَفًا)) متفق عليه

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu)   kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  amesema: ((Kila siku inayowapambaukia watu kuna Malaika wawili wanateremka, mmoja wao akiomba: Ee Allaah! Mwenye kutoa [sadaka] mlipe zaidi. Na mwengine huomba: Ee Allaah! Mwenye kuzuia mpe hasara)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Na kisa katika Qur-aan kinachothibitisha khasara ya wanaozuia kutoka sadaka:

 

 

Alikuweko mtu mmoja ambaye alikuwa ana mashamba ambayo yakitoa mazao na matunda mbali mbali, na kila anapochuma mazao alikuwa akigawa sehemu tatu; sehemu moja akiirudisha katika kuzalisha tena mazao, sehemu ya pili akila yeye pamoja na watoto wake, na inayozidi alikuwa akitoa sadaka. Alipofariki na watoto wake waliporithi shamba hilo, hawakutaka kufanya kama alivyokuwa akifanya baba yao. Walisema: "Hakika baba yetu alikuwa mpumbavu kutoa mazao ya shamba kuwapa masikini. Tukizuia sisi tusiwape, basi tutakuwa na mazao mengi yetu wenyewe!" Usiku mmoja wakapanga mpango na wakaapa kuwa wakiamka asubuhi yake watakwenda kuchuma mazao yote ili masikini watakapokuja kuomba hawatotambua wamefanya hivyo. Na wala hawakusema "In Shaa Allaah!" Lakini Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Alitaka kuvunja kiapo chao na Akawapa mtihani kwa kuwaangamizia shamba lao usiku huo. Akalifanya shamba likauke kabisa na lipige weusi kama vile limeungua au kama mfano lilokwishavunwa kisha likawa kavu kabisa.

 

Walipoamka asubuhi, wakaitana ili waende shambani kuchuma mazao kama walivyopanga na kuapa. Wakaondoka huku wakinongo'nezana ili mtu yeyote asiwasikie.

 

Wakaenda, lakini walipofika walidhani kuwa wamepotea maana hawakulitambua shamba lao kabisa.  Hapo tena ndio wakatambua kuwa hakika shamba lao ni hilo ambalo limeangamia!  Wakakosa kila kitu, wakaanza kulaumiana wenyewe kwa wenyewe na majuto yakawa  makubwa!

 

 

Kisha tena wakakiri makosa yao na kujirudi nafsi zao wakaomba kwa Rabb wao  Awaghufurie na mwishowe wakawa watu wema.

 

 

Baadhi ya Salaf wamesema kuwa watu hao walikuwa ni watu kutoka Yemen.  Sa'iyd bin Jubayr amesema kuwa: "Ni watu kutoka katika kijiji kilichoitwa Darawaan ambacho kilikuwa ni maili sita kutoka Sanaa."

 

Imesemekena vile vile kuwa ni miongoni mwa Ahlul-Kitaab kutoka Ethiopia. Na Allaah Anajua zaidi [Tafsiyr ya Ibn Kathiyr] 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Ameelezea kisa hichi katika Suwratul-Qalam kama ifuatavyo:

 

إِنَّا بَلَوْنَاهُمْ كَمَا بَلَوْنَا أَصْحَابَ الْجَنَّةِ إِذْ أَقْسَمُوا لَيَصْرِمُنَّهَا مُصْبِحِينَ﴿١٧﴾

Hakika sisi Tumewajaribu (Maquraysh) kama Tulivyowajaribu watu wa shamba, pale walipoapa kuwa bila shaka watayavuna (mazao yake) watakapopambaukiwa asubuhi.

 

وَلَا يَسْتَثْنُونَ﴿١٨﴾

Na wala hawakusema In-Shaa Allaah.  

 

فَطَافَ عَلَيْهَا طَائِفٌ مِّن رَّبِّكَ وَهُمْ نَائِمُونَ﴿١٩﴾

Basi (shamba lao) likazungukwa na chenye kuzunga (moto) kutoka kwa Rabb wako na hali wao wamelala.

 

 

فَأَصْبَحَتْ كَالصَّرِيمِ﴿٢٠﴾

Likawa kama lilovunwa ikabakishwa majivu meusi.

 

فَتَنَادَوْا مُصْبِحِينَ﴿٢١﴾

Wakaitana, walipopambaukiwa asubuhi.

 

 

أَنِ اغْدُوا عَلَىٰ حَرْثِكُمْ إِن كُنتُمْ صَارِمِينَ﴿٢٢﴾

Kwamba nendeni asubuhi mapema shambani mwenu, mkiwa mnataka kuvuna.

 

 

فَانطَلَقُوا وَهُمْ يَتَخَافَتُونَ﴿٢٣﴾

Wakatoka na huku wanakwenda kimya kimya wakinong’onezana.

 

 

أَن لَّا يَدْخُلَنَّهَا الْيَوْمَ عَلَيْكُم مِّسْكِينٌ﴿٢٤﴾

Kwamba: “Asikuingilieni humo kwa hali yoyote leo masikini.”

 

 

وَغَدَوْا عَلَىٰ حَرْدٍ قَادِرِينَ﴿٢٥﴾

Wakatoka asubuhi mapema kwa kusudio la nguvu, wakidhani wana uwezo (wa kuwazuia maskini).

 

 

فَلَمَّا رَأَوْهَا قَالُوا إِنَّا لَضَالُّونَ﴿٢٦﴾

Basi walipoliona wakasema: “Hakika sisi bila shaka Tumepotea.”

 

 

بَلْ نَحْنُ مَحْرُومُونَ﴿٢٧﴾

 (Walivyotanabahi!): “Bali sisi tumenyimwa!”

 

 

قَالَ أَوْسَطُهُمْ أَلَمْ أَقُل لَّكُمْ لَوْلَا تُسَبِّحُونَ﴿٢٨﴾

Mbora wao akasema: “Je, sikukuambieni kwanini hamumsabbih (Allaah?)”

 

 

قَالُوا سُبْحَانَ رَبِّنَا إِنَّا كُنَّا ظَالِمِينَ﴿٢٩﴾

Wakasema: “Ametakasika Rabb wetu! Hakika Sisi tulikuwa madhalimu.”

 

 

فَأَقْبَلَ بَعْضُهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ يَتَلَاوَمُونَ﴿٣٠﴾

Wakakabiliana wenyewe kwa wenyewe wakilaumiana.

 

 

قَالُوا يَا وَيْلَنَا إِنَّا كُنَّا طَاغِينَ﴿٣١﴾

Wakasema: “Ole wetu! Hakika sisi tumekuwa warukao mipaka.”

 

 

عَسَىٰ رَبُّنَا أَن يُبْدِلَنَا خَيْرًا مِّنْهَا إِنَّا إِلَىٰ رَبِّنَا رَاغِبُونَ﴿٣٢﴾

 “Asaa Rabb wetu Akatubadilishia lililo bora kuliko hilo hakika sisi kwa Rabb wetu ni wenye raghba.”

 

 

كَذَٰلِكَ الْعَذَابُ ۖ وَلَعَذَابُ الْآخِرَةِ أَكْبَرُ ۚ لَوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ﴿٣٣﴾

Hivyo ndivyo adhabu, na bila shaka adhabu ya Aakhirah ni kubwa zaidi lau wangelikuwa wanajua. [Al-Qalam: 17-33]

 

 

Tunataraji kuwa mafunzo haya na visa hivyo vitakuwa ni mafunzo kwetu ambayo yatatukinaisha na kutuzidishia iymaan zetu tupende kutoa sadaka kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kuwapa masikini, ndugu, jamaa na wenye kuhitaji, mayatima, na kutoa katika njia ya Allaah.    

 

 

Share