Skip navigation.
Home kabah

Mawasiliano Na Mchumba Baada Kuposa Na Kabla Ya Ndoa


SWALI:

 

INARUHUSIWA KUWASILIANA MARA KWA MARA NA MCHUMBA WAKO? KWA SIMU AMA BARUA AMA E-MAIL?
 

 



JIBU

Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)  Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allahu 'anhum jamiy'an) na watangu wema mpaka Siku ya Qiyaamah.

Ama kuhusu kuwasiliana baina ya mvulana aliyeposa na posa yake kukubaliwa na msichana na walii wake basi hakuna tatizo lolote ikiwa mawasiliano yao ni katika mipaka ya sheria. Hivyo, kumpigia simu hakuna ubaya ikiwa ni katika kuyapanga yale mambo ya ndoa yao na matayarisho yake. Ama ikiwa mawasiliano hayo yatakuwa nje ya misingi hiyo na kupelekea kuzungumza kuhusu mahusiano na mapenzi na mengine yasiyofaa, basi ni vizuri kujiepusha na mawasiliano hayo.

Mara nyingi mawasiliano ya karibu kabla ya ndoa, yameleta uharibifu mkubwa na madhara katika jamii na kusababisha posa nyingi kuharibika na hata vatu kutumbukia katika zinaa.

Mbali na mawasiliano hayo mvulana anaweza kwenda nyumbani kwa mchumba wake bora tu wasikae faragha wao peke yao katika mazungumzo. Inabidi awe pamoja nao maharimu wa msichana. Hii ni kwa sababu Mtume (Swalla Llaahu 'alayhi wa sallam) amesema: “Hakai faragha mwanamume na mwanamke ila wa tatu wao ni shetani. Na hakika shetani hutembea katika mwili wa mwanaadamu kama itembeavyo damu”. Hii ni kuwa bado nyinyi hamjakuwa mume na mke, na mmoja kati yenu anaweza kuvunja ndoa hiyo baada ya kuwa mmekubaliana hapo awali. Mwanamume anaweza kusema basi hataki tena harusi au mwanamke kujibu kuwa hakuna tena harusi.

Ile desturi ya wachumba kuwa wanakwenda pamoja katika mabustani, sinema au kusafiri kabla ya kuoana si desturi ya Kiislamu. Na athari yake mara nyengine inakuwa mbaya kwani wanaweza kutumbukia katika maasi na kisha mwanamume akasema hataki tena harusi na binti huyo. Baada ya hapo wanaume wanakuwa wakimtweza binti kama yule na inakuwa ni vigumu kwake kutakiwa na mume mwengine.

Na Allah Anajua zaidi