03-Buluwgh Al-Maraam: Kitabu Cha Nikaah: Mlango Wa Mahari

 

بُلُوغُ الْمَرام

Buluwgh Al-Maraam

 

كِتَابُ اَلنِّكَاحِ

Kitabu cha Nikaah (Ndoa)

 

بَابُ اَلصَّدَاقِ

03-Mlango Wa Mahari

 

 

 

 

879.

عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ، عَنِ اَلنَّبِيِّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ {أَنَّهُ أَعْتَقَ صَفِيَّةَ، وَجَعَلَ عِتْقَهَا صَدَاقَهَا} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

Kutoka kwa Anas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ): “alimuacha huru Swafiyyah[1] na akafanya kumuacha huru kwake ndio mahari yake.”[2] [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

880.

وَعَنْ أَبِي سَلَمَةَ بْنِ عَبْدِ اَلرَّحْمَنِ، رَضِيَ اللهُ عَنْهُ  أَنَّهُ قَالَ: {سَأَلْتُ عَائِشَةَ زَوْجَ اَلنَّبِيِّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ  كَمْ كَانَ صَدَاقُ رَسُولِ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ  قَالَتْ: كَانَ صَدَاقُهُ لِأَزْوَاجِهِ ثِنْتَيْ عَشْرَةَ أُوقِيَّةً وَنَشًّا. قَالَتْ: أَتَدْرِي مَا اَلنَّشُّ ؟ قَالَ: قُلْتُ: لَا. قَالَتْ: نِصْفُ أُوقِيَّةٍ. فَتِلْكَ خَمْسُمِائَةِ دِرْهَمٍ، فَهَذَا صَدَاقُ رَسُولِ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ  لِأَزْوَاجِهِ} رَوَاهُ مُسْلِمٌ

Kutoka kwa Abuu Salamah bin ‘Abdir-Rahmaan[3] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Nilimuuliza ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) mahari ya Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) ilikuwa kiasi gani?[4] Akasema: Mahari ya wakeze yalikuwa ni wakia kumi na mbili na An-Nash. Akasema: Unajua ni nini An-Nash? Akasema Hapana. Akasema: ni nusu wakia. Kwa hivyo hizo ni dirhamu mia tano (500) haya ndiyo mahari ya Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) kwa wakeze.” [Imetolewa na Muslim]

 

 

 

881.

وَعَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ : {لَمَّا تَزَوَّجَ عَلِيٌّ فَاطِمَةَ عَلَيْهِمَا اَلسَّلَامُ . قَالَ لَهُ رَسُولُ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ  " أَعْطِهَا شَيْئًا " ، قَالَ: مَا عِنْدِي شَيْءٌ . قَالَ:" فَأَيْنَ دِرْعُكَ الحُطَمِيَّةُ ؟} رَوَاهُ أَبُو دَاوُدَ، وَالنَّسَائِيُّ، وَصَحَّحَهُ اَلْحَاكِمُ 

Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema: “’Aliy alipomuoa Faatwimah عَلَيْهِمَا اَلسَّلَامُ, Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alimuambia: Mpe kitu (kama mahari yake), ‘Aliy akasema: Sina kitu, Rasuli wa Allaah akasema: Iko wapi ile deraya yako ya Al-Hutwamiyyah?.”[5] [Imetolewa na Abuu Daawuwd na An-Nasaaiy na akaisahihisha Al-Haakim]

 

 

 

882.

وَعَنْ عَمْرِو بْنِ شُعَيْبٍ، عَنْ أَبِيهِ، عَنْ جَدِّهِ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ {أَيُّمَا اِمْرَأَةٍ نَكَحَتْ عَلَى صَدَاقٍ، أَوْ حِبَاءٍ، أَوْ عِدَةٍ، قَبْلَ عِصْمَةِ اَلنِّكَاحِ، فَهُوَ لَهَا، وَمَا كَانَ بَعْدَ عِصْمَةِ اَلنِّكَاحِ، فَهُوَ لِمَنْ أُعْطِيَهُ، وَأَحَقُّ مَا أُكْرِمَ اَلرَّجُلُ عَلَيْهِ اِبْنَتُهُ، أَوْ أُخْتُهُ} رَوَاهُ أَحْمَدُ، وَالْأَرْبَعَةُ إِلَّا اَلتِّرْمِذِيَّ

Kutoka kwa ‘Amr bin Shu’ayb kutoka kwa baba yake naye kutoka kwa babu yake amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Mwanamke yeyote anayeolewa kwa mahari, zawadi au kwa ahadi ya kupewa zawadi kabla ya kifungo cha ndoa, basi kitu hicho ni chake.[6] Na kinachotolewa baada ya kifungo cha ndoa hicho ni cha aliyepewa. Na kilicho haki zaidi mtu kukirimiwa kwa sababu yake ni binti yake au dada yake.” [Imetolewa na Ahmad na Al-Arba’ah (An-Nasaaiy, Abuu Daawuwd, Ibn Maajah) isipokuwa At-Tirmidhiy.

 

 

 

883.

وَعَنْ عَلْقَمَةَ، عَنِ ابْنِ مَسْعُودٍ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ { أَنَّهُ سُئِلَ عَنْ رَجُلٍ تَزَوَّجَ اِمْرَأَةً، وَلَمْ يَفْرِضْ لَهَا صَدَاقًا، وَلَمْ يَدْخُلْ بِهَا حَتَّى مَاتَ، فَقَالَ اِبْنُ مَسْعُودٍ: لَهَا مِثْلُ صَدَاقِ نِسَائِهَا، لَا وَكْسَ، وَلَا شَطَطَ، وَعَلَيْهَا اَلْعِدَّةُ، وَلَهَا اَلْمِيرَاثُ، فَقَامَ مَعْقِلُ بْنُ سِنَانٍ الْأَشْجَعِيُّ فَقَالَ: قَضَى رَسُولُ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ  فِي بِرْوَعَ بِنْتِ وَاشِقٍ  اِمْرَأَةٍ مِنَّا  مِثْلَ مَا قَضَيْتَ، فَفَرِحَ بِهَا اِبْنُ مَسْعُودٍ} رَوَاهُ أَحْمَدُ، وَالْأَرْبَعَةُ، وَصَحَّحَهُ اَلتِّرْمِذِيُّ وَالْجَمَاعَةُ

Kutoka kwa ‘Alqamah[7] naye kutoka kwa Ibn Mas ‘uwd (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) aliulizwa: “kuhusu mtu aliyeoa mke, hakumkadiria mahari, wala hakumuingilia hadi akafa. Ibn Mas‘uwd akasema: ana mfano wa mahari ya wanawake wake, hakuna kupunguza wala kuzidisha, naye (mwanamke) itamlazimu akae eda na pia anastahiki kupata mirathi. Ma’qil bin Sinaan Al-Ashja’iyy akasimama na akasema: Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alihukumu kwa Birwa’[8] bint Waashiq ni mwanamke miongoni mwetu kama hivyo ulivyo hukumu wewe. Ibn Mas-‘uwd akafurahi kwa ushahidi huu.” [Imetolewa na Ahmad na Al-Arba’ah (At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, Abuu Daawuwd, Ibn Maajah) na akaisahihisha At-Tirmidhiy na ‘Ulamaa

 

 

 

884.

وَعَنْ جَابِرِ بْنِ عَبْدِ اَللَّهِ  رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا أَنَّ اَلنَّبِيَّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ  قَالَ: { مَنْ أَعْطَى فِي صَدَاقِ اِمْرَأَةٍ سَوِيقًا، أَوْ تَمْرًا، فَقَدْ اِسْتَحَلَّ} أَخْرَجَهُ أَبُو دَاوُدَ، وَأَشَارَ إِلَى تَرْجِيحِ وَقْفِهِ

Kutoka kwa Jaabir bin ‘Abdillaah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema kuwa Nabiy   (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Mwenye kutoa Sawiyq[9] au tende katika mahari ya mwanamke basi amekuwa halaal kwake mwanamke huyo.” [Imetolewa na Abuu Daawuwd]

 

 

 

885.

وَعَنْ عَبْدِ اَللَّهِ بْنِ عَامِرِ بْنِ رَبِيعَةَرَضِيَ اللهُ عَنْهُ  ، عَنْ أَبِيهِ {أَنَّ اَلنَّبِيَّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ  أَجَازَ نِكَاحَ اِمْرَأَةٍ عَلَى نَعْلَيْنِ} أَخْرَجَهُ اَلتِّرْمِذِيُّ وَصَحَّحَهُ، وَخُولِفَ فِي ذَلِكَ 

Kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Aamir bin Rabiy’ah[10] kutoka kwa baba yake (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) Ameruhusu mwanamke kuolewa kwa (mahari ya) viatu.” [Imetolewa na At-Tirmidhiy na akaisahihisha na amekhalifiwa katika hilo (la kufanya Hadiyth kuwa ni sahihi)

 

 

 

886.

وَعَنْ سَهْلِ بْنِ سَعْدٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ قَالَ: {زَوَّجَ اَلنَّبِيُّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ  رَجُلاً اِمْرَأَةً بِخَاتَمٍ مِنْ حَدِيدٍ} أَخْرَجَهُ اَلْحَاكِمُ.

وَهُوَ طَرَفٌ مِنَ الْحَدِيثِ اَلطَّوِيلِ اَلْمُتَقَدِّمِ فِي أَوَائِلِ اَلنِّكَاحِ 

Kutoka kwa Sahl bin Sa’d (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alimuoza mtu mwanamke kwa (mahari ya) pete ya chuma.” [Imetolewa na Al-Haakim nayo ni sehemu katika Hadiyth ndefu iliyotangulia mwanzo wa Mlango wa Ndoa][11]

 

 

 

887.

وَعَنْ عَلَيٍّ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ  قَالَ: {لَا يَكُونُ اَلْمَهْرُ أَقَلَّ مِنْ عَشَرَةِ دَرَاهِمَ} أَخْرَجَهُ اَلدَّارَقُطْنِيُّ مَوْقُوفًا، وَفِي سَنَدِهِ مَقَالٌ 

Kutoka kwa ‘Aliy (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Mahari haiwi chini ya dirhamu kumi.” [Imetolewa na Ad-Daaraqutwniyy  ikiwa ni Mawquwf na katika Isnaad yake kuna maelezo]

 

 

 

888.

وَعَنْ عُقْبَةَ بْنِ عَامِرٍ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ {خَيْرُ اَلصَّدَاقِ أَيْسَرُهُ} أَخْرَجَهُ أَبُو دَاوُدَ، وَصَحَّحَهُ اَلْحَاكِمُ 

Kutoka kwa ‘Uqbah bin ‘Aamir (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Mahari yalio na kheri ni yalio mepesi.” [Imetolewa na Abuu Daawuwd na akaisahihisha Al-Haakim]

 

 

 

889.

وَعَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا {أَنَّ عَمْرَةَ بِنْتَ اَلْجَوْنِ تَعَوَّذَتْ مِنْ رَسُولِ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ  حِينَ أُدْخِلَتْ عَلَيْهِ تَعْنِي: لَمَّا تَزَوَّجَهَا فَقَالَ: "لَقَدْ عُذْتِ بِمَعَاذٍ"، فَطَلَّقَهَا، وَأَمَرَ أُسَامَةَ فَمَتَّعَهَا بِثَلَاثَةِ أَثْوَابٍ} أَخْرَجَهُ اِبْنُ مَاجَهْ، وَفِي إِسْنَادِهِ رَاوٍ مَتْرُوكٌ

وَأَصْلُ اَلْقِصَّةِ فِي "اَلصَّحِيحِ" مِنْ حَدِيثِ أَبِي أُسَيْدٍ اَلسَّاعِدِيِّ

Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema: “’Amrah bint Al-Jawn alijilinda dhidi ya Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) wakati alipoingia kwake (siku aliyomuoa). Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akasema: Kwa hakika umejilinda kwa kinga. Akamtaliki na akamuamrisha Usaamah ampe (mwanamke yule) nguo tatu.”  [Imetolewa na Ibn Maajah na katika Isnaad yake kuna mpokezi anayeachwa. Asili ya kisa chenyewe kimo katika Swahiyh Al-Bukhaariy kutoka katika Hadiyth ya Abuu Usayd As-Saa’idiy]

 

 

 

[1] Huyu ni Mama wa Waumini Swafiyyah bint Huyai bin Al-Akhtwab, ni kutoka katika kizazi cha Nabiy Haaruwn. Mwanzoni alikuwa ameolewa na Kinaanah bin Abdil-Huqaiq ambaye aliuwawa katika vita vya Khaybar. Swafiyyah alitekwa, kisha Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alimchagua kuwa mke wake na akasilimu. Aliachwa huru na uhuru wake ndiyo iliyokuwa mahari yake. Alifariki mwaka 50 Hijriyyah na alizikwa katika makaburi ya Baqi’

 

[2] Hii ina maana mahari inaweza kuwa kitu kisichokuwa fedha.

[3] Huyu ni Abuu Salamah bin ‘Abdir-Rahmaan bin ‘Awf Az-Zuhri Al-Qurayshiy. Huyu ni mmoja katika Mafuqahaa saba wakubwa katika mji wa Madiynah na ni miongoni mwa Taabii’ wakubwa. Ni madhubuti na amepokea Hadiyth nyingi ambazo alizisikia kutoka katika makundi mbalimbali ya Maswahaba na kutoka kwa waliopokea kutoka kwake. Alifariki mwaka 94 au 104 katika mapokezi mengine akiwa na umri wa miaka 70.

 

[4] Hakuna kiwango maalumu cha mahari katika Shariy’ah, hata hivyo kuifanya ndogo zaidi kunapendeza, ili kuifanya ndoa kuwa ni nyepesi kwa watu wengi.

[5] Ni deraya iliyotengenezwa na watu wa kabila la Al-Hutwamah, walikuwa mahodari wa kutengeneza maderaya ya kivita. Hadiyth hii ni dalili kuwa bwana arusi anatakiwa ampe mkewe kitu kabla ya kumuingilia.

[6] Hii ina maana kila kilichoamuliwa kabla ya ndoa ni mahari, na yote yanakuwa ni ya muolewa. Ikiwa zawadi hiyo ni ya fedha, dhahabu, nguo, ardhi, nyumba au kitu kingine chochote, yeye ndiye mmiliki kamili wa kitu  hicho. Ikiwa kuna kitu chochote watakachopewa jamaa za binti baada ya kuolewa kwake, hilo halitazingatiwa kuwa ni mahari, na si milki ya binti. Ni zawadi aliyopewa mtu tu.

 

[7] Huyu ni ‘Alqamah bin Qays Abu Shibl bin Maalik katika kabila la Banu Bakr bin An-Nakha, amepokea Hadiyth nyingi kutoka kwa ‘Umar na Ibn Mas-‘uwd. Alikuwa ni Taabi’ mkubwa, alikuwa maarufu kwa Hadiyth ya Abdullaah bin Mas‘uwd na kuwa na usuluba naye, alikuwa ni mjomba wa Al-Aswad bin An-Nakahi alifariki mwaka 61 Hijriyyah.

 

[8] Jina hili la Birwa’ lina ikhtilafu kwa Wanazuoni wa lugha ambao wao humuita Barwa’ na Wanazuoni wa Hadiyth humuita Birwa’

 

[9] Sawiyq ni unga wa mtama au wa mahindi au wa shayiri uliokaangwa.

[10] Huyu ni Abuu ‘Imraan ‘Abdillaah bin ‘Aamir bin Rabiy’ah Al-Anzi. Alikuwa ni mwenye umri wa miaka minne au mitano pindi Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alipofariki. Alifariki mwaka wa 85 Hijriyyah.

[11] Tazama Hadiyth ya 832.

Share