Skip to main content

Tangulizi Za Suwrah Za Qur-aan032-As-Sajdah: Utangulizi Wa Suwrah

032-As-Sajdah: Utangulizi Wa Suwrah

Alhidaaya.com

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

Idadi Za Aayah: 30

Jina La Suwrah: As-Sajdah

Suwrah imeitwa As-Sajdah (Sijda), na inayodalilisha ni kutajwa katika Hadiyth iliyonukuliwa chini katika Fadhila.  

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

1-Ubainisho wa uhakika wa viumbe, na hali za watu duniani na Aakhirah. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

2-Kubainisha Utukufu wa Allaah (سبحانه وتعالى) na Sifa Zake Kamilifu, na Uwezo Wake katika Kuumba, Kudabiri mambo, Kufufua na malipo.

3-Kuinua utajo wa Qur-aan, kwani hiyo ndio iliyokusanya kila aina ya uongofu.

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

1-Suwrah imefunguliwa kwa herufi zinazojulikana kama الحروف المقطعة  (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah), ambazo hakuna ajuaye maana zake isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Al-Baqarah (2:1). Kisha imetukuzwa Qur-aan kwamba haina shaka ndani yake, na kwamba imeteremshwa na Rabb wa ulimwengu, na kuwapinga washirikina wanaodai kuwa imetungwa.

2-Imetajwa kuwa Allaah (سبحانه وتعالى) Ndiye Aliyeumba mbingu na ardhi na kubainisha baadhi ya mambo yanayoonyesha Uwezo Wake.

3-Imeweka wazi baadhi ya hoja za makafiri katika kupinga kwao kufufuliwa pamoja na kuwaraddi kwenye hilo.

4-Imetajwa baadhi ya mambo ya Siku ya Qiyaamah hasa kwa watu waovu wakiwa mbele ya Allaah (سبحانه وتعالى) .

5-Imetajwa baadhi ya sifa za Waumini, na waliyoahidiwa na Allaah (سبحانه وتعالى) Peponi katika Neema Zake. 

6-Imetajwa kuwa Waumini hawako sawa na mafasiki na ikatajwa malipo yao; Waumini watapata Jannaat na makazi mazuri na takrima humo. Mafasiki makazi yao yatakuwa ni motoni.

7-Imetajwa kuhusu Nabiy Muwsaa (عليه السلام), na Neema aliyopewa na Allaah (سبحانه وتعالى) ya kupewa Tawraat.

8-Da’wah kwa washirikina kutakiwa waizingatie na kutafakari Qur-aan.

9-Simulizi za baadhi ya ujinga wa washirikina.

10-Suwrah imekhitimishwa kwa kuamrishwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kuwapuuza washirikina na kujitenga nao.

Fadhila Za Suwrah:   

Ni Sunnah kuisoma Suwrah As-Sajdha katika Swalaah ya Alfajiri siku ya Ijumaa:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ ـ رضى الله عنه ـ قَالَ كَانَ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم يَقْرَأُ فِي الْجُمُعَةِ فِي صَلاَةِ الْفَجْرِ ‏ الم * تَنْزِيلُ‏  السَّجْدَةَ  وَ هَلْ أَتَى عَلَى الإِنْسَانِ‏

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akisoma katika Swalaah ya Alfsjiri siku ya Ijumaa:

الم ﴿١﴾ تَنزِيلُ

As-Sajdah (32) na

هَلْ أَتَىٰ عَلَى الْإِنسَانِ

Suwrah Al-Insaan (76). [Al-Bukhaariy, Muslim na wengineo]