Duaa Gani Kuomba Ya Kujiokoa Na Zinaa

SWALI:

Ni dua gani mtu anaweza kusoma ili apate mchumba mwema (mwanamuke awo mwanawume). Ni duwa gani mtu mzinifu anaweza kusoma ili Mwenyezi mungu amnusuru na zina?


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa ndugu yetu muulizaji swali. Hakika ni kuwa katika jamii ambayo tunaishi ndani hivi leo ni kuwa maasiya yamezidi maradufu mpaka mema yanaonekana kuwa ni mabaya na maovu kuwa mema.

Zinaa katika jamii zetu za leo inaonekana kuwa ni jambo la sawasawa tu mbali na kuwa Allaah Aliyetukuka Anatufahamisha:

Wala msikaribie uzinzi. Hakika huo ni uchafu na njia mbaya ().

Hapa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anatupatia muongozo kuwa dawa ya zinaa ni kujiepusha na mambo ambayo yanaweza kukupeleka huko. Hayo ni kama kusalimiana na msichana asiyekuwa maharimu yako kwa kumpa mkono, kukaa faragha na msichana, kuangalia filamu na picha chafu, kwenda disco, kuwa katika hafla za mchanganyiko baina ya wanaume na wanawake na mengineyo.

Pia inafaa uwe na marafiki ambao ni wema wanaoweza kukuelekeza katika mambo ya kheri. Kushikamana na Ibadah tofauti kwani Ibadah zote zinatuepusha na machafu. Kwa mfano, Swalah, Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anatueleza:

SOMA uliyofunuliwa katika Kitabu, na ushike Swalah. Hakika Swalah inazuilia mambo machafu na maovu. Na kwa yakini kumdhukuru Allaah ndilo jambo kubwa kabisa. Na Allaah Anayajua mnayoyatenda (29: 45).

Pia kujilazimisha kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) mchana na usiku kwa nyiradi mbali mbali.

Hali kadhalika kuweza kutafakari juu ya yule ambaye utazini naye. Ima huyo atakuwa ni mama, dada, binti, shangazi, halati wa mtu. Swali ni kuwa je, wewe utakubali au kuridhika mamako au dadako au binti yako azini na mtu. Ikiwa hupendelei jamaa zako wafanyiwe kitendo hicho kwa nini unataka kufanya na dada au mama au shangazi za wengine?

Ukitafakari hayo basi yatakuepusha na zinaa isipokuwa akili yako iwe kama ya hayawani.

Njia bora ya kuweza kujiepusha na zinaa ni kutafuta msichana mwenye Dini na maadili mema ufunge naye ndoa na ikiwa hujaweza hilo kwa sababu moja au nyingine fanya bidii ufunge. Funga ni kinga kama alivyotuambia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Ama kujiepusha huko hakuna du’aa fulani ambayo unaweza kuisoma hasa kwa suala hilo. Bali ni juu yako umuombe Allaah Aliyetukuka Akuepushe na jambo hilo hasa unapoinuka katika Swalah ya usiku.

Pia hakuna du’aa maalumu ya kupata mchumba bali inafaa ufanye juhudi ya kutafuta msichana ambaye ana sifa zilizopendekezwa na Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama Dini na maadili mema. Unaweza pia kutuma jamaa zako wa karibu kukutafutia.

Baada ya kupatikana na kabla ya kupeleka posa inafaa uswali Swalah ya Istikhaarah kumtaka shauri Allaah Akiyetukuka.

Tunakuombea kwa Allaah Aliyetukuka Akuepushe na zinaa pamoja na kukupatia msichana mwema mwenye Dini mtakayesikilizana kwa njia nzuri.

Na Allaah Anajua zaidi

Share