Skip navigation.
Home kabah

Kisa Cha Aswhaabul-Kahf (Watu Wa Pangoni) Sehemu Ya 2

Kimeandikwa na: Alhidaaya.com

 


وَتَرَى الشَّمْسَ إِذَا طَلَعَت تَّزَاوَرُ عَن كَهْفِهِمْ ذَاتَ الْيَمِينِ وَإِذَا غَرَبَت تَّقْرِضُهُمْ ذَاتَ الشِّمَالِ وَهُمْ فِي فَجْوَةٍ مِّنْهُ ذَلِكَ مِنْ آيَاتِ اللَّهِ مَن يَهْدِ اللَّهُ فَهُوَ الْمُهْتَدِي وَمَن يُضْلِلْ فَلَن تَجِدَ لَهُ وَلِيًّا مُّرْشِدًا  

{{Na unaliona jua linapochomoza linainamia kuliani mwao kutoka hapo pangoni; na linapokuchwa linawakwepa kushotoni, na wao wamo katika uwazi wa pango. Hizo ni katika ishara za Mwenyezi Mungu. Ambaye Mwenyezi Mungu Anamwongoa basi huyo ni mwenye kuongoka. Na Anayemuacha kupotea basi hutampatia mlinzi wala mwongozi}}

}}وَتَحْسَبُهُمْ أَيْقَاظًا وَهُمْ رُقُودٌ وَنُقَلِّبُهُمْ ذَاتَ الْيَمِينِ وَذَاتَ الشِّمَالِ وَكَلْبُهُم بَاسِطٌ ذِرَاعَيْهِ بِالْوَصِيدِ لَوِ اطَّلَعْتَ عَلَيْهِمْ لَوَلَّيْتَ مِنْهُمْ فِرَارًا وَلَمُلِئْتَ مِنْهُمْ رُعْبًا  {{

 {{Nawe utawadhania wamacho, na hali wamelala. Nasi tunawageuza kulia na kushoto. Na mbwa wao amenyoosha miguu yake ya mbele kizingitini. Kama ungeliwatokea hapana shaka ungeligeuka kuwakimbia, nawe umejaa khofu}}

}} وَكَذَلِكَ بَعَثْنَاهُمْ لِيَتَسَاءلُوا بَيْنَهُمْ قَالَ قَائِلٌ مِّنْهُمْ كَمْ لَبِثْتُمْ قَالُوا لَبِثْنَا يَوْمًا أَوْ بَعْضَ يَوْمٍ قَالُوا رَبُّكُمْ أَعْلَمُ بِمَا لَبِثْتُمْ فَابْعَثُوا أَحَدَكُم بِوَرِقِكُمْ هَذِهِ إِلَى الْمَدِينَةِ فَلْيَنظُرْ أَيُّهَا أَزْكَى طَعَامًا فَلْيَأْتِكُم بِرِزْقٍ مِّنْهُ وَلْيَتَلَطَّفْ وَلَا يُشْعِرَنَّ بِكُمْ أَحَدًا  {{

 {{Na kwa namna hii Tuliwainua usingizini wapate kuulizana wao kwa wao. Alisema msemaji katika wao: Mmekaa muda gani? Wakasema: Tumekaa siku moja au sehemu ya siku. Wakasema: Mola wenu Mlezi Anajua zaidi muda mliokaa. Hebu mtumeni mmoja wenu na hizi fedha zenu ende mjini, akatazame chakula chake kipi kilicho bora kabisa akuleteeni cha kukila. Naye afanye mambo hayo kwa busara, wala asikutajeni kabisa kwa yeyote}}

}} إِنَّهُمْ إِن يَظْهَرُوا عَلَيْكُمْ يَرْجُمُوكُمْ أَوْ يُعِيدُوكُمْ فِي مِلَّتِهِمْ وَلَن تُفْلِحُوا إِذًا أَبَدًا{{

{{Kwani wao wakikutambueni watakupigeni mawe, au watakurudisheni katika dini yao; na hapo hamtafanikiwa kabisa}}  Al-Kahf :17-20

 

Tunaendelea na Kisa cha Asw-habul-Kahf, baada ya kukimbilia pangoni vijana hao, na kulala humo kuwa muda wa miaka zaidi ya mia tatu, bila ya kujulikana na watu, nako ni kwa Rahma na uwezo wa  Allaah سبحانه وتعالى.

}}وَتَرَى الشَّمْسَ إِذَا طَلَعَت تَّزَاوَرُ عَن كَهْفِهِمْ ذَاتَ الْيَمِينِ وَإِذَا غَرَبَت تَّقْرِضُهُمْ ذَاتَ الشِّمَالِ وَهُمْ فِي فَجْوَةٍ مِّنْهُ ذَلِكَ مِنْ آيَاتِ اللَّهِ مَن يَهْدِ اللَّهُ فَهُوَ الْمُهْتَدِي وَمَن يُضْلِلْ فَلَن تَجِدَ لَهُ وَلِيًّا مُّرْشِدًا {{

{{Na unaliona jua linapochomoza linainamia kuliani mwao kutoka hapo pangoni; na linapokuchwa linawakwepa kushotoni, na wao wamo katika uwazi wa pango. Hizo ni katika ishara za Mwenyezi Mungu. Ambaye Mwenyezi Mungu Anamwongoa basi huyo ni mwenye kuongoka. Na Anayemuacha kupotea basi hutampatia mlinzi wala mwongozi}}

 

Sehemu lililokuwepo pango:

Hapa inaonyesha kwamba mlango wa pango hilo ulielelekea upande wa Kaskazini kwa sababu Allaah سبحانه وتعالى   Anatuambia kwamba jua lilipokuwa linachomoza, mwangaza ulikuwa unaingia katika pango. 

}}ذات اليمين{{

{{kuliani mwao}}

}}وَتَرَى الشَّمْسَ إِذَا طَلَعَت تَّزَاوَرُ عَن كَهْفِهِمْ ذَاتَ الْيَمِينِ{{

{{Na unaliona jua linapochomoza linainamia kuliani mwao kutoka hapo pangoni}}

Maana: Kivuli kilipungua upande wa kulia kama alivyosema Ibn 'Abbaas, Sa'iyd Bin Jubayr na Qataadah.

}}وَإِذَا غَرَبَت تَّقْرِضُهُمْ ذَاتَ الشِّمَالِ{{ 

 {{na linapokuchwa linawakwepa kushotoni}}

Maana: Jua liliingia katika pango lao kutoka upande wa kushoto wa mlango wa pango,  ina maana kutoka upande wa Magharibi.  

Ibn 'Abbaas, Mujaahid na Qataadah wamesema kwamba:

}} تَّقْرِضُهُمْ{{

{{Linawakwepa}}

Yaani Jua lilikuwa likiwaangazia kisha likiwaondokea.  [At-Twabariy 17:621,622]

Allaah سبحانه وتعالى Ametuambia haya na Ametaka tufahamu na tutafakari maana yake, lakini Hakutuambia sehemu iliokuwepo hilo pango, yaani nchi gani, kwa sababu hakuna faida kwetu kujua hilo na haipatikani lengo la sheria ndani yake. Na kama ingelikuwa inapatikana maslahi ya kiroho au ya kidini basi Allaah سبحانه وتعالى  na Mtume Wake wangelitufundisha kwa kutupa maelezo yake kama alivyosema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم :

(( والذي نفسي بيده ما تركت شيئا يقربكم من الجنة ويباعدكم عن النار إلا أمرتكم به، وما تركت شيئا يقربكم من النار، ويباعدكم عن الجنة إلا نهيتكم عنه   ((صحيح  الألباني رحمه الله

((Naapa Kwa Yule Ambaye nafsi yangu iko katika mikono Yake, sikuacha jambo la  kukukurubisheni  na Pepo na la kukuwekeni mbali na moto ila nimekwisha kukuamrisheni nalo.  Wala sikuacha jambo la kukukurubisheni na moto na kukuwekeni mbali na Pepo ila nimekwisha kukukatazeni nalo))  [Katika Sahihi  Shaykh Al -Albaaniy   رحمه الله ]

 Ibn 'Abbaas anatafsiri kuhusu:

}}تَّزَاوَرُ عَن كَهْفِهِمْ ذَاتَ الْيَمِينِ وَإِذَا غَرَبَت تَّقْرِضُهُمْ ذَاتَ الشِّمَالِ وَهُمْ فِي فَجْوَةٍ مِّنْهُ{{

{{linainamia kuliani mwao kutoka hapo pangoni; na linapokuchwa linawakwepa kushotoni, na wao wamo katika uwazi wa pango}}

Maana, jua liliingia katika pango bila ya kuwagusa, kwa sababu lingeliwagusa, lingeliwaunguza miili yao na nguo zao.  [At-Twabariy 17:620]

}}ذَلِكَ مِنْ آيَاتِ اللَّهِ{{

{{Hizo ni katika ishara za Mwenyezi Mungu}}

Ni ishara ya Allaah سبحانه وتعالى Kuwaongoza katika pango na Kuwajaalia kuwa hai, na jua na upepo ukipita katika pango kuwahifadhi miili yao

Kisha Allaah سبحانه وتعالى Anasema:

}}مَن يَهْدِ اللَّهُ فَهُوَ الْمُهْتَدِي وَمَن يُضْلِلْ فَلَن تَجِدَ لَهُ وَلِيًّا مُّرْشِدًا{{

{{Ambaye Mwenyezi Mungu Anamwongoa basi huyo ni mwenye kuongoka. Na Anayemuacha kupotea basi hutampatia mlinzi wala mwongozi}}

Yeye Allaah سبحانه وتعالى ndiye Aliyewaongoza hawa vijana katika uongofu wa haki, kwani yule Anayemuongoa hakuna wa kumpotoa na Anayempotoa hakuna wa kumuongoa.

 }}وَتَحْسَبُهُمْ أَيْقَاظًا وَهُمْ رُقُودٌ وَنُقَلِّبُهُمْ ذَاتَ الْيَمِينِ وَذَاتَ الشِّمَالِ وَكَلْبُهُم بَاسِطٌ ذِرَاعَيْهِ بِالْوَصِيدِ لَوِ اطَّلَعْتَ عَلَيْهِمْ لَوَلَّيْتَ مِنْهُمْ فِرَارًا وَلَمُلِئْتَ مِنْهُمْ رُعْبًا{{  

 {{Nawe utawadhania wamacho, na hali wamelala. Nasi Tunawageuza kulia na kushoto. Na mbwa wao amenyoosha miguu yake ya mbele kizingitini. Kama ungeliwatokea hapana shaka ungeligeuka kuwakimbia, nawe umejaa khofu}}

 

Kulala kwao katika pango

Baadhi wa wafasiri wamesema kuwa Allaah سبحانه وتعالى  Alipowafanya walale, kope za macho yao hazikufunga. Kubakia kwa macho yao kuwa wazi ilikuwa ni bora kwa sababu ya kuhifadhi macho yao, kama inavyosemekana kuwa mbwa mwitu akilala anafunga jicho moja na moja huliacha wazi, kisha anabadilisha jicho jingine huku amelala. 

   }} وَتَحْسَبُهُمْ أَيْقَاظًا وَهُمْ رُقُودٌ {{

{{Nawe utawadhania wamacho, na hali wamelala}}

  }}وَنُقَلِّبُهُمْ ذَاتَ الْيَمِينِ وَذَاتَ الشِّمَالِ{{

{{Nasi tunawageuza kulia na kushoto}}

Ibn 'Abbaas kasema: Kama wasingelikuwa wanageuka, ardhi ingeliwafanya waoze.  [At-Twabariy  17:620]

  }}وَكَلْبُهُم بَاسِطٌ ذِرَاعَيْهِ بِالْوَصِيدِ{{

{{Na mbwa wao amenyoosha miguu yake ya mbele kizingitini}}

Ibn 'Abbaas, Mujaahid, Sa'iyd bin Jubayr na Qataadah wamesema:  Wasiyd ina maana kizingiti. Ibn 'Abbaas kasema: pembeni mwa mlango. Pia imesemwa kuwa ni ardhini. Lakini usemi wa rai ya uhakika ni kuwa ni kizingiti cha mlango (wa pango).  [At-Twabariy 17:624-625]

Kama vile katika aya:

}}إِنَّهَا عَلَيْهِم مُّؤْصَدَةٌ{{

{{Hakika huo utafungiwa nao}}

[Al-Humazah:8]

Mbwa wao alilala chini katika mlango, nayo ndio tabia ya mbwa na kazi yake mbwa kulinda kama alivyosema Ibn Jubayr. Na mbwa huyo alikaa nje ya mlango kwa sababu malaika hawaingii nyumba iliyo na mbwa kama ilivyosimuliwa katika Al-Bukhaariy, wala hawaingii katika nyumba iliyo na picha za viumbe zilizochorwa au vinyago. 

Neema hiyo ya kulala ilimfikia mpaka mbwa wao. Na hii ndio faida ya kuambatana na watu wema. Ilisemekana, kwamba  huyo mbwa alikuwa wa mpishi wa mfalme ambaye aliamini rai za dini ya Tawhiyd ya Vijana hao. Na Allaah سبحانه وتعالى Anajua zaidi.

}}لَوِ اطَّلَعْتَ عَلَيْهِمْ لَوَلَّيْتَ مِنْهُمْ فِرَارًا وَلَمُلِئْتَ مِنْهُمْ رُعْبًا{{  

{{Kama ungeliwatokea hapana shaka ungeligeuka kuwakimbia, nawe umejaa khofu}}

Maana yake ni:  Allaah Kawafanya waonekane wanatisha hali yao, hata mtu asiwakaribie kuwagusa na kuwaamsha mpaka muda Alioutaka Allaah سبحانه وتعالى  walale uishe na hii ni kutokana na hikma, uthibitisho wa wazi na Rahma kubwa iliyohusiana na haya. 

Walipoamka wakamtuma mmoja wao sokoni kununua chakula,

}}وَكَذَلِكَ بَعَثْنَاهُمْ لِيَتَسَاءلُوا بَيْنَهُمْ قَالَ قَائِلٌ مِّنْهُمْ كَمْ لَبِثْتُمْ قَالُوا لَبِثْنَا يَوْمًا أَوْ بَعْضَ يَوْمٍ قَالُوا رَبُّكُمْ أَعْلَمُ بِمَا لَبِثْتُمْ فَابْعَثُوا أَحَدَكُم بِوَرِقِكُمْ هَذِهِ إِلَى الْمَدِينَةِ فَلْيَنظُرْ أَيُّهَا أَزْكَى طَعَامًا فَلْيَأْتِكُم بِرِزْقٍ مِّنْهُ وَلْيَتَلَطَّفْ وَلَا يُشْعِرَنَّ بِكُمْ أَحَدًا{{ 

{{Na kwa namna hii tuliwainua usingizini wapate kuulizana wao kwa wao. Alisema msemaji katika wao: Mmekaa muda gani? Wakasema: Tumekaa siku moja au sehemu ya siku. Wakasema: Mola wenu Mlezi Anajua zaidi muda mliokaa. Hebu mtumeni mmoja wenu na hizi fedha zenu ende mjini, akatazame chakula chake kipi kilicho bora kabisa akuleteeni cha kukila. Naye afanye mambo hayo kwa busara, wala asikutajeni kabisa kwa yeyote}}  

Allaah سبحانه وتعالى  Anasema, kama Tulivyowafanya kulala, tumewafufua na miili yao, nywele na  ngozi zao, bila ya kuharibika kiungo chochote cha mwili wao na hakuna kilichopunguka katika kuonekana kwao. Hii ni baada ya miaka 309, ndio maana wakawa wanaulizana,

  }}كَمْ لَبِثْتُمْ{{

{{Mmekaa muda gani?}}

Kwa sababu  walipoingia katika pango ilikuwa mwanzo wa siku na  walipoamka ilikuwa mwisho wa siku ndio maana wakasema, 

}}قَالُوا لَبِثْنَا يَوْمًا أَوْ بَعْضَ يَوْمٍ {{

{{Wakasema: Tumekaa siku moja au sehemu ya siku}}

}}قَالُوا رَبُّكُمْ أَعْلَمُ بِمَا لَبِثْتُمْ{{

{{Wakasema: Mola wenu Mlezi Anajua zaidi muda mliokaa}}

Maana: Allaah Anajua zaidi hali yenu.  Walikuwa hawana hakika muda waliolala. Na Allaah سبحانه وتعالى Ndiye Ajuaye. Wakaelekea kutafuta mahitajio yaliyo muhimu kwao nayo ni chakula na kinywaji, hivyo wakasema:

}}فَابْعَثُوا أَحَدَكُم بِوَرِقِكُمْ هَذِهِ إِلَى الْمَدِينَةِ{{ 

{{Hebu mtumeni mmoja wenu na hizi fedha zenu ende mjini}}

Walikuwa na pesa zao  Dirhams  (aina za fedha za wakati huo)  kutoka kwao, walizitoa baadhi yake katika sadaqa na baadhi waliweka kwa matumizi. Wakamtuma mmoja wao aende mjini (mji wao) ili kutafuta chakula kilicho safi kabisa.

}}فَلْيَنظُرْ أَيُّهَا أَزْكَى طَعَامًا{{

{{akatazame chakula chake kipi kilicho bora kabisa}}

 

Azkaa أَزْكَى hapa inamaanisha iliyotoharika kama ilivyo katika ayah hii,

{{ وَلَوْلَا فَضْلُ اللَّهِ عَلَيْكُمْ وَرَحْمَتُهُ مَا زَكَا مِنكُم مِّنْ أَحَدٍ أَبَدًا}}

{{Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu na rehema Yake juu yenu, asingelitakasika miongoni mwenu kabisa hata mmoja}}

[An-Nuur 21]

}}قَدْ أَفْلَحَ مَن تَزَكَّى{{   

{{Hakika amekwishafanikiwa aliyejitakasa}} [Al A'alaa :14]  

 }}فَلْيَأْتِكُم بِرِزْقٍ مِّنْهُ{{

{{akuleteeni cha kukila}}

}}وَلْيَتَلَطَّفْ{{

{{Naye afanye mambo hayo kwa busara}}

Maana kwamba ajihadhari asije kutambulikana anapokwenda kununua chakula na anaporudi.

}}وَلَا يُشْعِرَنَّ بِكُمْ أَحَدًا{{  

{{wala asikutajeni kabisa kwa yeyote}}

}}إِنَّهُمْ إِن يَظْهَرُوا عَلَيْكُمْ يَرْجُمُوكُمْ أَوْ يُعِيدُوكُمْ فِي مِلَّتِهِمْ وَلَن تُفْلِحُوا إِذًا أَبَدًا   {{

{{Kwani wao wakikutambueni watakupigeni mawe, au watakurudisheni katika dini yao; na hapo hamtafanikiwa kabisa}}

  }} إنّهُمْ إِن يَظْهَرُوا عَلَيْكُمْ{{

{{Kwani wao wakikutambueni}}

 }}يَرْجُمُوكُمْ أَوْ يُعِيدُوكُمْ فِي مِلَّتِهِمْ{{

{{watakupigeni mawe, au watakurudisheni katika dini yao;}}

Walikusudia watu wa ule mji wa Decianus, ambao waliogopa kuwa wakiwajua watawaadhibu kwa kuwatesa kwa kila aina ya mateso ili warudi dini yao ya kuabudu masanamu, au wawatese mpaka wawaue. Na kwao vijana hao, ilikuwa ni bora kwao kufa hivyo kuliko kurudia dini ya ushirikina kwani wamejua kuwa hawatofaulu duniani wala akhera, ndio maana wakasema, 

}}وَلَن تُفْلِحُوا إِذًا أَبَدًا{{

{{na hapo hamtafanikiwa kabisa}}

 

Mafunzo na uongofu tunayopata: [Sh Abubakar Al-Jazaairiy]

1)      Kudhihirisha upole wa Allaah سبحانه وتعالى  kwa Awliyaa (Vipenzi) wake kuwakirimu wanapohama kwa Ajili Yake.

2)     Uongofu  umo katika Mikono ya Allaah سبحانه وتعالى , kwa hiyo aliyeongoka ameongozwa na Allaah سبحانه وتعالى  na aliyepotea amepotezwa na Allaah سبحانه وتعالى . Na inatupasa tumuombe Allaah سبحانه وتعالى uongofu na kujikinga Kwake na upotofu.

3)      Udhihirisho wa maajabu Anayoweza kuyafanya Allaah سبحانه  وتعالى  na kufanya Apendavyo kwa viumbe Vyake, Subhanahu Wa Ta'alah, Mtukufu, Mwenye Kujua, Mwenye Hikma.

4)      Kumpasa mja kutafuta chakula na kinywaji cha halali na mengineyo.

5)      Kufa katika shirki na kufru kunamzuia mtu kupata kufaulu siku ya Qiyaamah.

 

Kisa kitaendelea....../3