Skip navigation.
Home kabah

Kisa Cha Aswhaabul-Kahf (Watu Wa Pangoni) Sehemu ya 3


Imeandikwa na Alhidaaya.com

 


 

وَكَذَلِكَ أَعْثَرْنَا عَلَيْهِمْ لِيَعْلَمُوا أَنَّ وَعْدَ اللَّهِ حَقٌّ وَأَنَّ السَّاعَةَ لَا رَيْبَ فِيهَا إِذْ يَتَنَازَعُونَ بَيْنَهُمْ أَمْرَهُمْ فَقَالُوا ابْنُوا عَلَيْهِم بُنْيَانًا رَّبُّهُمْ أَعْلَمُ بِهِمْ قَالَ الَّذِينَ غَلَبُوا عَلَى أَمْرِهِمْ لَنَتَّخِذَنَّ عَلَيْهِم مَّسْجِدًا  

 

{{Na namna hivi Tuliwajuulisha kwa watu wapate kujua ya kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli, na kwamba Saa haina shaka. Walipokuwa wakigombania jambo lao wao kwa wao walisema: Jengeni jengo juu yao. Mola wao Mlezi Anawajua vyema. Wakasema walioshinda katika shauri yao: Bila ya shaka tutawajengea msikiti juu yao}}.

 

}} سَيَقُولُونَ ثَلَاثَةٌ رَّابِعُهُمْ كَلْبُهُمْ وَيَقُولُونَ خَمْسَةٌ سَادِسُهُمْ كَلْبُهُمْ رَجْمًا بِالْغَيْبِ وَيَقُولُونَ سَبْعَةٌ وَثَامِنُهُمْ كَلْبُهُمْ قُل رَّبِّي أَعْلَمُ بِعِدَّتِهِم مَّا يَعْلَمُهُمْ إِلَّا قَلِيلٌ فَلَا تُمَارِ فِيهِمْ إِلَّا مِرَاء ظَاهِرًا وَلَا تَسْتَفْتِ فِيهِم مِّنْهُمْ أَحَدًا  {{

 {{Watasema: Walikuwa watatu, wa nne wao ni mbwa wao. Na wanasema: Walikuwa watano, wa sita wao ni mbwa wao. Wanavurumisha ovyo. Na wanasema: Walikuwa saba, na wa nane wao ni mbwa wao. Sema: Mola wangu Mlezi Ndiye Anayejua sawa sawa hisabu yao. Hawawajui ila wachache tu. Basi usibishane juu yao ila kwa mabishano ya juu juu tu hivi. Wala usiulize khabari zao kwa yeyote yule}}

 Al-Kahf: 21:22

 

JINSI WATU WA MJI WALIVYOWAJUA NA WAKAJENGA JENGO KATIKA PANGO LAO

 

}}وَكَذَلِكَ أَعْثَرْنَا عَلَيْهِمْ لِيَعْلَمُوا أَنَّ وَعْدَ اللَّهِ حَقٌّ وَأَنَّ السَّاعَةَ لَا رَيْبَ فِيهَا إِذْ يَتَنَازَعُونَ بَيْنَهُمْ أَمْرَهُمْ فَقَالُوا ابْنُوا عَلَيْهِم بُنْيَانًا رَّبُّهُمْ أَعْلَمُ بِهِمْ قَالَ الَّذِينَ غَلَبُوا عَلَى أَمْرِهِمْ لَنَتَّخِذَنَّ عَلَيْهِم مَّسْجِدًا{{ 

{{Na namna hivi Tuliwajuulisha kwa watu wapate kujua ya kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli, na kwamba Saa haina shaka. Walipo kuwa wakigombania jambo lao wao kwa wao walisema: Jengeni jengo juu yao. Mola wao Mlezi Anawajua vyema. Wakasema walioshinda katika shauri yao: Bila ya shaka tutawajengea msikiti juu yao}} [Al-Kahf:21]

 

Wanachuoni wengi wamesema kwamba watu wakati huo walikuwa wana shaka kuhusu kufufuliwa kwao. 

Ikrimah  kasema:  Kulikuwa na kundi lililosema kuwa  roho zao ndio zilizofufuliwa na si miili yao, kwa hiyo Allaah Kawafufua watu wa pango wakaenda sokoni na kujulikana na watu ili iwe uthibitisho wa  kufufuliwa kwao kikamili; yaani kiroho na kimwili.  [At-Taariykh At-Twabariy 2:9]

 

Wametaja kuwa walipomtuma mmoja wao kwenda mjini kununua chakula, alijibadilisha shakili yake na akatumia njia nyingine kabisa mpaka akafika mji wa Daqsus. Akafikiri kuwa si muda mrefu tokea walipoondoka, na hali kumbe ni karne baada ya karne, kizazi baada ya kizazi, umma baada ya umma zimepita na nchi pamoja na watu wake wamebadilika wote. Hakuona alama zozote za mji alizozitambua na wala hakumtambua hata mtu mmoja.

Akaanza kuzungukwa na akili na  kusema peke yake.  "Labda nina wazimu au nimehadaika?  Au ninaota?" Kisha akasema: "Wallaahi mimi sio lolote katika hayo (yaani kuwa na wazimu au kuota), niliyoyaona usiku wa jana (hapo mwanzoni walipokuwa kabla ya kulala katika pango miaka yote hiyo) ni tofauti kabisa na haya ninayoyaona sasa".  Kisha akasema: "Bora nitoke nikimbie". Akatoka kwenda kwa muuzaji mmoja aliyekuwa anauza chakula, akampa zile pesa alizokuwa nazo, na kumuomba amuuzie chakula.  Yule mtu alipoziona zile pesa hakuzitambua kwa hiyo akampa jirani yake (muuzaji mwenziwe) naye pia hakuzitambua, zikawa zinazunguka kwa wenye maduka kila mmoja hazitambui. Mmoja wao akasema "labda huyu mtu kapata hazina". Wakaanza kumuuliza kutaka kujua nani yeye na wapi kazipata zile pesa.  Je, kapata bahati ya kupata hazina?   Wakamuuliza nani wewe?  Akasema: "mimi ni mtu wa mji huu huu, nimeishi hapa jana na Decianus ndio alikuwa mfalme". Wakamhukumu kuwa ni mwendazimu na wakamchukuwa kumpelekea kwa mkuu wa serikali (gavana) ambaye alimuuliza  maswali mbali mbali kuhusu hali yake kutaka kujua vizuri vipi anazo pesa za karne na vipi anasema kuwa jana tu aliishi na mfalme Decianus?

Yule mkuu wa serikali alishangazwa na akachanganyikiwa na akili. Alipowaambia kuhusu wenzake walio pangoni, yule mfalme na baadhi ya watu wakaenda katika lile pango. 

Yule kijana alimwambia mfalme: "Acha nianze kuingia mimi kwanza ili niwajulishe wenzangu". Kisha waliingia katika pango na mfalme akawasalimia na kuwakumbatia kwani kumbe yeye alikuwa ni Muislamu na jina lake aliitwa Tedosis. Wakafurahi kuonana naye na wakakaa kuzungumza naye, kisha wakaagana, walipoondoka wakarudi zao kulala na hapa tena Allaah akawafisha.   [Tarikh At-Twabariy 2:9]

Na Allaah ndiye anayejua. 

}}وَكَذَلِكَ أَعْثَرْنَا عَلَيْهِمْ{{

 {{Na namna hivi Tuliwajulisha kwa watu}}

 

Kama vile Tulivyowafanya walale na kuamka na kiwiliwili chao kizima, Tumekifanya kisa chao kijulikane kwa watu waliokuwapo wakati ule

 

}}لِيَعْلَمُوا أَنَّ وَعْدَ اللَّهِ حَقٌّ وَأَنَّ السَّاعَةَ لَا رَيْبَ فِيهَا إِذْ يَتَنَازَعُونَ بَيْنَهُمْ أَمْرَهُمْ{{

{{Wapate kujua ya kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli, na kwamba Saa haina shaka. Walipokuwa  wakigombania jambo lao wao kwa wao}} 

Maana ya kuhusu kufufuliwa kwao: Wengine waliamini kisa chao, na wengine walikikanusha, kwa hiyo Allaah Aliwafanya watu wa pango watambulike kama ni uthibitisho, aidha kwa mapendeleo yao au dhidi yao. 

}}فَقَالُوا ابْنُوا عَلَيْهِم بُنْيَانًا رَّبُّهُمْ أَعْلَمُ بِهِمْ{{

{{Jengeni jengo juu yao. Mola wao Mlezi Anawajua vyema}}

 

Yaani, zibeni  mlango wa pango wabakie humo tuwaache kama walivyo.

}}قَالَ الَّذِينَ غَلَبُوا عَلَى أَمْرِهِمْ لَنَتَّخِذَنَّ عَلَيْهِم مَّسْجِدًا{{  

{{Wakasema walioshinda katika shauri lao: Bila ya shaka tutawajengea msikiti juu yao}}

Hawa waliosema hivi ni wale watu waliokuwa na  ukubwa na nguvu wenye cheo fulani. Lakini je, walikuwa watu wema au wabaya?   Kuna majadiliano kuhusu jambo hili kwani Mtume صلى الله عليه وسلم    alisema:

 ((لَعَنَ اللَّهُ الْيَهُودَ وَالنَّصاَرَى اتَّخَذُوا قُبُورَ أَنْبِيَائِهِمْ وَصَالِحِهِمْ مَسَاجِدَ))

((Allaah Kawalaani Mayahudi na Manaswaara, wamefanya makaburi ya mitume yao kuwa ni misikiti))   [Fath- Al-Baariy 1:634] 

Ni onyo kutoka kwa Allaah kwa walivyofanya kwani ni moja ya shirk kubwa kufanya makaburi misikiti.

 

Idadi ya  watu wa pangoni

 

}} سَيَقُولُونَ ثَلَاثَةٌ رَّابِعُهُمْ كَلْبُهُمْ وَيَقُولُونَ خَمْسَةٌ سَادِسُهُمْ كَلْبُهُمْ رَجْمًا بِالْغَيْبِ وَيَقُولُونَ سَبْعَةٌ وَثَامِنُهُمْ كَلْبُهُمْ قُل رَّبِّي أَعْلَمُ بِعِدَّتِهِم مَّا يَعْلَمُهُمْ إِلَّا قَلِيلٌ فَلَا تُمَارِ فِيهِمْ إِلَّا مِرَاء ظَاهِرًا وَلَا تَسْتَفْتِ فِيهِم مِّنْهُمْ أَحَدًا{{  

{{Watasema: Walikuwa watatu, wa nne wao ni mbwa wao. Na wanasema: Walikuwa watano, wa sita wao ni mbwa wao. Wanavurumisha ovyo. Na wanasema: Walikuwa saba, na wa nane wao ni mbwa wao. Sema: Mola wangu Mlezi Ndiye Anayejua sawa sawa hisabu yao. Hawawajui ila wachache tu. Basi usibishane juu yao ila kwa mabishano ya juu juu tu hivi. Wala usiulize khabari zao kwa yeyote yule}}

 

 }} سَيَقُولُونَ ثَلَاثَةٌ رَّابِعُهُمْ كَلْبُهُمْ وَيَقُولُونَ خَمْسَةٌ سَادِسُهُمْ كَلْبُهُمْ رَجْمًا بِالْغَيْبِ{{

 {{Watasema: Walikuwa watatu, wa nne wao ni mbwa wao. Na wanasema: Walikuwa watano, wa sita wao ni mbwa wao. Wanavurumisha ovyo}} 

Allaah Anatuelezea kuwa kulikuweko na mgogoro kuhusu idadi ya vijana hao waliokuwako pangoni.  Aya inatuonyesha kuwa ni rai tatu na hakuna ya nne.  Na Allaah Anatuonyesha kuwa rai mbili za mwanzo sio za kweli kwani kasema,

}}رَجْمًا بِالْغَيْبِ{{

  {{Wanavurumisha ovyo}} 

Maana; wanasema bila kuwa na elimu yoyote, kama vile mtu anayerusha mshale bila ya kuwa na shabaha fulani, huwa hawezi kufikia (kudunga) panapostahiki kufikiwa, na akifikia basi itakua ni bahati tu sio kusudio. 

Kisha Allaah Anataja rai ya tatu na wala Hakutaja kuwa ni kweli au sio kweli.

 

}} وَيَقُولُونَ سَبْعَةٌ وَثَامِنُهُمْ كَلْبُهُمْ{{

{{Na wanasema: Walikuwa saba, na wa nane wao ni mbwa wao}}

}}قُل رَّبِّي أَعْلَمُ بِعِدَّتِهِم{{

{{Sema: Mola wangu Mlezi Ndiye Anayejua sawa sawa hisabu yao}}

 

Kwamba ni bora zaidi wakati kuna shaka kama hizi kurudisha katika elimu ya  Allaah.  Sio sawa kutaka kuingilia mambo bila ya kuwa na elimu.Tukipewa elimu kuhusu jambo tulieleze, ikiwa haikutufikia elimu basi tuepuke kueleza jambo tusilolijua. 

}}مَّا يَعْلَمُهُمْ إِلَّا قَلِيل{{

{{Hawawajui ila wachache tu}}

Qataadah kasema kwamba Ibn 'Abbaas kasema:  "Mimi ni mmoja wa wachache waliotajwa katika aya hii. Idadi yao walikuwa ni watu saba" [At-Twabariy 17:642]

  

}}فَلَا تُمَارِ فِيهِمْ إِلَّا مِرَاء ظَاهِرًا{{

{{Basi usibishane juu yao ila kwa mabishano ya juu juu tu hivi}}

Maana; kwa upole,  kwani  sio jambo kubwa na la kuwa muhimu kulijua. 

}}وَلَا تَسْتَفْتِ فِيهِم مِّنْهُمْ أَحَدًا{{

{{Wala usiulize khabari zao kwa yeyote yule}}

Maana; hawana elimu kuhusu hilo isipokuwa tu wanabahatisha tu kwa yale yasiyoonekana. Hawana ushahidi kutoka kwenye chanzo cha uhakika.  Lakini Allaah Amekuleta wewe ewe Muhammad na  ukweli (haki) ambao hauna shaka au kubabaisha. Ukweli ambao unatakiwa uwekwe mbele ya vitabu vyote vya nyuma.  

Mafunzo na uongofu tunaopata: [Shaykh Abubakar Al-Jazaairy]

 

1)     Kuthibitisha kufufuliwa na malipo ambayo wameyakanusha  watu Wa Makkah.

2)      Kusadikisha kauli ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم :  ((Allaah Kawalaani Mayahudi na Manaswaara, wamefanya makaburi ya mitume yao kuwa ni misikiti)) na  kauli yake ((Hakika hao anapokuweko mtu mwema na anapokufa humjengea katika kaburi lake msikiti na wakaweka picha yake (sanamu lake), hao ni viumbe wa shari (wabaya kabisa) siku ya Qiyaamah" [Al-Bukhari na Muslim]

 

3)      Kusadikisha kauli ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم   ((Mtafuata nyendo za watu wa kabla yenu shibiri baada ya shibiri, dhira'a baada ya dhira'a))

Na hii imethibitika kutokana na Waislamu waliowajengea Awliyaa wao (Wapenzi wao) na waja wema misikiti karibu na makaburi yao.

4)     Kudhihirisha ikhtilaaf ya Ahlul-Kitaab na kutokuwa na uhakika wao kwa matukio ya historia.

5)      Kudhihirisha idadi ya vijana wa pangoni kwamba ni saba na wanane wao ni mbwa wao.


Kisa kitaendelea....../4