Kuna Aina Ngapi Za Dhulma?

SWALI:

 

assalama alykum

Dhumunio ya email hii ni kutaka kuuliza  je kuna aina ngapi za Dhulm


 

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Tunakushukuru kwa kutuma swali hili ambalo ni muhimu kwani kila Muislamu inampasa ajipushe na dhulma ili aweze kuepukana na hatari yake.

Dhulma inaweza kuwa ni baina ya binaadamu na Mola wake au dhulma baina yake na mwenzake.

Kumfanyia dhulma Allaah سبحانه وتعالى nayo ni kumshirikisha, nayo ni dhulma kubwa kabisa. Ilipoteremshwa aya,    

((الَّذِينَ آمَنُواْ وَلَمْ يَلْبِسُواْ إِيمَانَهُم بِظُلْمٍ أُوْلَئِكَ لَهُمُ الأَمْنُ وَهُم مُّهْتَدُون))

((Wale ambao wameamini, na hawakuchanganya imani yao na dhulma,  hao ndio watakaopata amani na wao ndio walioongoka)) [Al-An'aam 6:82]

Iliwaingiza shaka Maswahaba wakamuuliza Mtume صلى الله عليه وآله وسلم "Ewe Mjumbe wa Allah, nani katika sisi asiyejidhulumu?" Akasema: ((Sivyo hivyo mlivyofahamu, hamkusikia mja mwema (Luqmaan) alivyosema:

 ((يَا بُنَيَّ لَا تُشْرِكْ بِاللَّهِ إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ))

((Ewe mwanangu! Usimshirikishe Allaah. Kwani hakika ushirikina bila ya shaka ni dhulma iliyo kubwa)) [Luqmaan 31:13]

Kwa hiyo kumshirikisha Allaah سبحانه وتعالى ni dhulma kubwa ambayo inampasa kila Muislamu ajiepueshe na hatari yake kwani Allaah سبحانه وتعالى Humsamehe binaadamu madhambi yote ila yenye kumshirikisha:

((إِنَّ اللّهَ لاَ يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَلِكَ لِمَن يَشَاء وَمَن يُشْرِكْ بِاللّهِ فَقَدِ افْتَرَى إِثْمًا عَظِيمًا))

((Hakika Allaah Hasamehe kushirikishwa, na husamehe yaliyo duni ya hilo kwa Amtakaye. Na anayemshirikisha Allaah basi hakika amezua dhambi kubwa)) An-Nisaa:48

Dhulma baina ya binaadamu ni kuoneana, kuchukuliana haki ya kila aina ikiwa ni mali au inayomhusu mtu kama kumvunjia heshima yake na kadhalika, kama tunavyopata mafundisho katika Hadiyth hizi ziufatazo:

Hadiythi ya kwanza:

  ‏ ‏عن ‏ ‏أبي هريرة رضي الله عنه ‏ ‏أن رسول الله ‏ ‏صلى الله عليه وسلم ‏ ‏قال ‏‏)) أتدرون ما المفلس قالوا المفلس فينا يا رسول الله من لا درهم له ولا متاع قال رسول الله ‏ ‏صلى الله عليه وسلم ‏‏ المفلس من أمتي من يأتي يوم القيامة بصلاته وصيامه وزكاته ويأتي قد شتم هذا ‏ ‏وقذف ‏ ‏هذا وأكل مال هذا وسفك دم هذا وضرب هذا فيقعد ‏ ‏فيقتص ‏ ‏هذا من حسناته وهذا من حسناته فإن فنيت حسناته قبل أن ‏ ‏يقتص ‏ ‏ما عليه من الخطايا أخذ من خطاياهم فطرح عليه ثم طرح في النار)) ألترمذي

Imetoka kwa Abu Hurayrah رضي الله عنه kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema: ((Mnamjua nani aliyefilisika?)) Wakasema (Maswahaba): Aliyefilisika ni yule miongoni mwetu asiyekuwa na diraham au mali. Mtume صلى الله عليه وآله وسلم akasema: ((Aliyefilisika katika umma wangu ni yule atakayekuja siku ya Qiyaamah na Swalah zake, Swawm zake na Zakah zake, lakini atakuja akiwa amemtukana huyu, amemtuhumu huyu, amekula mali ya huyu, amemwaga damu ya huyu na amempiga huyu, yatachukuliwa mema yake na kulipwa wale aliowadhulumu. Yatakapomalizika mema yake kabla ya kufidia madhambi aliyowakosea wenzake, zitachukuliwa dhambi za wale aliowakosea kisha atajaliziwa yeye na mwishowe atakuwa ni wa kutupwa motoni)) [At-Tirmidhiy]    

Hadiyth ya pili:

 : عن أبي هُريرةَ رضي اللهُ عنه قال: قال رسوُل الله صلى الله عليه وسلم ))لا تَحَاسَدُوا، ولا تَنَاجَشُوا، ولا تَباغَضُوا، ولا تَدَابَرُوا، ولا يَبعْ بَعْضُكُمْ على بَيْعِ بَعْضٍ، وكُونُوا عِبادَ اللهِ إخْوَاناً، المُسْلمُ أَخُو المُسْلمِ: لا يَظْلِمُهُ، ولا يَكْذِبُهُ، ولا يَحْقِرُهُ، التَّقْوَى هاهُنا - ويُشِيرُ إلى صَدْرِه ثَلاثَ مَرَّاتٍ - بِحَسْبِ امْرِىءٍ مِنَ الشَّرِّ أن يَحْقِرَ أخاهُ المُسْلِمِ، كُلُّ المُسْلِمِ على الْمسْلِم حَرَامٌ: دَمُهُ ومالُهُ وعِرْضُهُ((رَوَاهُ مُسْلِمٌ     

Kutoka kwa Abu Hurayrah رضي الله عنه   ambaye amesema: Mtume صلى الله عليه وسلم   kasema: ((Msioneane choyo, wala msizidishiane bei (za vitu), wala msichukiane, wala msipigane mapande (msitengane), wala msishindane kwa kupunguza bei. Lakini kuweni ndugu, enyi  waja wa Mwenyeezi Mungu, Muislamu ni ndugu wa Muislamu mwenzake, hamdhulumu wala hamvunji, hamwambii uongo wala hamdharau. Ucha Mungu  uko hapa (huku akiashiria kifuani kwake kwa vidole vyake) mara tatu. Ni uovu wa kutosha kwa mtu kumdharau ndugu yake Muislamu. Muislamu ameharamishiwa kwa Muislamu mwenzake: damu yake, mali yake na heshima yake)) (Yaani haramu kuchukua mali ya mwenzako, kumuua na kumdhalilisha) [Imesimuliwa na Muslim]  

Na Allah Anajua zaidi.

 

 

Share