Dawa Gani Za Kurudisha Ubikra

SWALI:

 

Nimesoma nakala yenu, nimevutiwa sana na ushauri wenu. lakini kama ilivyo kwa wanaume zipo dawa za kienyeji za kuongeza uume ambazo hazina madhara. sasa naomba kuuliza hakuna dawa  za kienyeji za kuweza kurudisha bikira ambazo  hazina madhara? Tafadhali naomba unijibu kwenye email  yangu. asanteni   sana


 

 JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa dada yetu muuliza swali.

Tunataka kuuliza kwa nini mwanamke wa Kiislamu anataka kurudisha ubikira? Hii ni njia ya udanganyifu inayotumiwa na wasichana wanaoolewa hasa kwa siku hizi katika mwambao wa Tanzania na Kenya. Kwa nini wanafanya hivyo?

Bila shaka wengi wao wanafanya hivyo ili kuwadanganya ma-bwana harusi kwa ule usiku wa mwanzo kuwa wao bado ni watwahirifu na wamejihifadhi kutokana na zinaa.

 

Wenye kufanya hayo aghalabu huwa wamezunguka na wanaume wengine kabla ya ndoa katika kitendo cha zinaa. Mume anadhania kwa usiku huo wa mwanzo kuwa mkewe ni bikira naye ni wa mwanzo kufungua kizibo ilhali si hivyo.

 

 

Kadhaalika, hata ikiwa kuna dawa za kuukuza uume, vilevile hazifai kutumia kwani ni katika kubadili maumbile mtu aliyopewa na Allaah na vilevile kuna madhara mengine yanayopatikana kwa kufanya hilo kama kudhoofisha nguvu za uume.

Lililo bora ni mtu kubaki na maumbile yake yalivyo kama ni mwanamme na kama ni mwanamke ni kujihifadhi na kulinda utupu wake hadi kwa lililo la halali yake (mume wake). Na kurejesha ubikira wa bandia ili aje kuonekana na atakayemuoa kuwa ni msafi, aliyejitunza, mwaminifu... huo utakuwa ni uongo na haufai katika Dini. Isitoshe atakayekuoa akibainikiwa na hilo mbeleni, hatokuwa na imani na wewe na huenda ndoa ikavunjika.

 

Tutahadharini hayo kwani Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Mwenye kutughushi sisi (kutudanganya) si katika sisi" (Muslim).

 

Na tufahamu kuwa udanganyifu ni alama moja ya unafiki.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share