Kumnyoa Mtoto Nywele Staili Za Kihuni Na Kumchora Michoro Mwilini

SWALI

 

 

Asalam Alaqum Warahmat llah wabarakat. Swali langu ni hili je inafaa kumnyoa mtoto nywele za mtindo wa pank au kuchorwa michoro mbali mbali kama vile nike na vinginevyo. Naomba ushahidi wa aya na hadithi. Asalam allaiqum.


 

 

JIBU

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kumnyoa mtoto mitindo ya kihuni au kumchora michoro mbali mbali kwenye kichwa. Kuhusu nukta ya kwanza ambayo ni mtindo wa panki ambao Kiislamu unaitwa Qaza‘, nao ni kunyoa baadhi ya nywele na kuacha nyingine. Hii imekatazwa na sheria kwa Hadiyth ya Mtume Wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutoka kwa Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) aliyesema: “Amekataza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kukata baadhi ya nywele za kichwa na kuacha nyingine” (al-Bukhaariy na Muslim).

 

Na amesema tena (Radhiya Allaahu ‘anhuma): Mtume Wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaona watoto ambao wamenyolewa baadhi ya nywele na kuachwa nyingine, akawakataza kufanya hilo. Akasema: “Nyoeni zote, au ziacheni zote” (Abu Daawuud na an-Nasaa’iy).

 

Ama kuchora michoro mbali mbali pia imekatazwa na kuharamishwa katika Dini yetu. Huko ni kubadilisha umbile la Allaah Aliyetukuka Alilomuumba nalo Allaah na kufanya hivyo ni kumfuata Shaytwaan (4: 119). Kisha kufanya hivyo ni kujifananisha na makafiri ambako Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza. Pia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amewalaani wenye kuchanja – kutia chale (tattoo) na mwenye kuchanjwa, mwenye kuchonga meno na mwenye kuchongwa. Na huku kuchanja kunaumbua na kuharibu uso na mikono kwa chale zitiwazo na nakshi mbaya ichorwayo, na wengine wamepindukia kwa kuchora mwili mzima. Pia yapo maumivu na adhabu inayosababishwa katika kuchorwa na sindano na hata kama hakuna maumivu mwilini ni jambo lililokatazwa.

 

Ama kuchora kichwani mchoro wa ‘nike’ au hata kuvaa mavazi ya nembo hiyo ya ‘nike’, kwanza kabla Muislam hajavaa nguo za mitindo au kutumia majina na nembo mbalimbali, ni muhimu sana kwanza ajue jina au nembo hiyo inawakilisha nini? Nembo na jina la ‘nike’, linamaanisha ‘mungu wa kike wa ushindi’ katika miungu ya kigiriki ambao wao walikuwa na miungu ya kila kitu!

 

Kwa maana tu ya jina hilo, basi haifai kabisa Muislam kuvaa majina kama hayo au kutumia nembo zake kwani kwa njia moja au nyingine ni kukubaliana na ushirikina huo.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share