Mfugaji Wanyama – Vipi Achinje Idadi Kubwa Ya Wanyama Kama Kuku?

SWALI:

 

ASSALAM ALAYKUM

MIMI NI MFUGAJI WA KUKU WA KIZUNGU NAOMBA NIFAHAMISWE TARATIBU ZA KISHERIA ZA KUCHINJA KUKU IDADI NYINGI KAMA ZAIDI YA 200 NIMEAMBIWA NISIPOOSHA KISU KWA MAJI BAADA YA KILA KUKU, KUKU HAO WATAKUWA NI HARAMU KUWALA, VIPI PIA KUHUSU KUKU  KUWAKUSANYA PAMOJA WAKATI WA KUWACHINJA?


 

JIBU:

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako zuri kuhusu kuchinja kuku idadi kubwa.

 

Hakika hatujapata chochote kuhusu kuosha kisu baada ya kuchinja kuku mmoja na kabla ya kumchinja mwingine. Kile ambacho kinahitajika katika Sunnah ni kukinoa kisu ili uondoe usumbufu kwa mnyama. Hii ni kwa mujibu wa kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Hakika Allaah Ameamrisha ihsani (wema) kwa kila kitu. Kwa hivyo, mkiua ueni vizuri, na mkichinja chinjeni vizuri. Kila mmoja wenu na akitie makali kisu chake na akipunguzie uchungu kichinjwa chake” (Muslim, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy, an-Nasaa’iy, Ibn Maajah na ad-Daarimiy).

 

Kuchinja vizuri ni kwa kutumia ala ya kuchinjia yenye makali na kumchinja mnyama upesi upesi. Haifai mnyama kupigwa ovyo kabla ya kuchinjwa wala kumburuza. Achinjaye aseme BismiLlaahi, amuelekeze Qiblah, amkate gorombo (koo) na mishipa miwili ya damu (jugular veins) ili afe upesi na damu yote itoke. Pia ni vyema kuwa wanyama (kuku kwa kesi yako) wawe hawapo sehemu moja ya kuchinjwa.

 

 

Kuwakusanya pamoja kuku wote pamoja na wakawa wanaona wenzao wanaochinjwa haipendezi, ni bora kuwaweka sehemu na ukamtoa mmoja mmojabila wengine kuona. Likiwa haliwezekani hilo na ikawa inabidi lazima wawe pamoja, hapo ni masuala ya dharura na haitokatazwa kwa dharura hiyo, lakini kama inawezekana ni bora kutokufanya hivyo.

 

Bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi

 

Nyama Ya Halaal Uchinjaji Wake

 

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share