Nyama Ya Halaal Uchinjaji Wake

 

SWALI:

Asalam Alaykum
Kwa jina la Mwenyezi Mungu mwingi rehma mwenye kuneemesha neema ndogo ndogo na mwenye kuneemesha neema kubwa kubwa.  Swala na salamu zimfikie kipenzi chetu Mtume Muhammad (SAW) na Swahaba zake (RA) na watangu wema mpaka siku ya Kiama. Swala langu ni kama lifuatavyo, na litahusiana na ulaji wa nyama halali huku nchi za Magharibi.


Ni kawaida yangu, kununua nyama moja kwa moja toka katika machinjio, ambayo nyama ile inakua imechinjwa katika misingi na taratibu za kiislam kama ilivyoamrishwa na Mwenyezi Mungu na kuwekwa wazi katika hadith za Mtume Muhammad (SAW). Kikawaida ninaweka oda wiki moja au siku tatu kabla ya kwenda kuchukua ile nyama, au kwa upande mmoja au mwingine kama ni mwenye kubahatika unaweza kupita pale machinjioni ukakuta nyama halal.

Sasa hii jana, nimekwenda kule buchani kuchukua nyama ambayo tayari nimeshaiwekea oda,  kwa bahati mbaya au nzuri, nyama halal ilikua haipo kwa wakati ule.  Sasa yule mwenye bucha ni Mzungu mkatoliki alinichukua mpaka ndani ya kwenye machinjio, na kufika kule nikapewa kisu nimchinje yule kondoo, kwa kipindi kile bila ya mimi mwenyewe kufahamu kuwa nililoitiwa mule ndani ni nini, kwa kweli nilishtuka kidogo, na mshituko wangu una sababu moja kuu, nayo kwamba mimi binafsi sijawahi kuchinja mnyama kama kondoo, sasa kwangu mimi ilikua ni mtihani kidogo.  Sasa yule Mzungu, anauzoefu wa siku nyingi na ameona waislam wengu ambao wanananua nyama kwake na jinsi ya uchinjaji wake bila ya kumtesa yule mnyama, kwa kumaanisha kile kisu kinapitishwa sehemu gani hasa, kuondoa utesaji wa mnyama wakati wa kutoa roho.

Sasa swala ni kama ifuatavyo, je yule Mzungu Mkatoliki, anaweza kunichinjia yule mnyama hali yakuwa mimi mwenyewe nipo, kwa kusoma bismillah, na kutaja jina la Mwenyezi Mungu ? Naomba munichambulie kutokana na Hadiyth na maamrisho ya Mwenyezi Mungu.
Maasalam

 


 

 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Tunamshukuru Allaah Aliyetukuka pamoja na ndugu zetu ambao wamekuwa wakituombea katika kuwafikisha kazi hii nzito na pia wenye kutuuliza maswali tofauti ambayo yanatupatia sisi fursa ya kurejea vitabu na kuongeza elimu yetu zaidi.

Inaeleweka kuwa Waarabu wapagani walikuwa wakichinja wanavyotaka, bila kutaja jina la Allaah Aliyetukuka na kutumia kifaa chochote wanachotaka. Uislamu ukaweka kanuni ya kumchinja mnyama bila kumsumbua au kumtesa. Ukaweka pia ulazima wa kutaja jina la Allaah Aliyetukuka wakati wa kuchinja. Katika kanuni zake ukafanya vyakula vya watu waliopewa Vitabu kuwa ni halali ikiwa ni nyama halali au punje punje. Allaah Aliyetukuka anasema: “Na chakula cha wale waliopewa Kitabu ni halali kwenu” (5: 5).

Hii ni ayah iliyokusanya jamii ya vyakula vyao vya kuchinjwa na vyenginevyo. Hivyo vyote ni halali maadamu chakula chenyewe si haramu kwetu sisi Waislamu kama mfu, damu, nguruwe na kadhalika.

Sasa tukirudi kwa swali lako wewe mwenyewe ulimuona mnyama akichinjwa na ukasema Bismillahi pamoja na kisu kuwa kikali. Ikiwa hayo yamefanyika basi nyama hiyo inakuwa halali bila wasiwasi aina yoyote. Masharti haya yako wazi katika machimbuko ya sheria. Allaah Aliyetukuka Anasema: “Basi kuleni katika wale waliosemewa jina la Allaah, ikiwa nyinyi mnaziamini aya zake” (6: 118). Na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Kilichochinjwa kwa kumwagwa damu yake na kutajwa jina la Allaah juu yake kuleni” (al-Bukhaariy).

Pia maagizo ya Uislamu ni kuwa unapotaka kumchinja mnyama basi kinoe kisu chako ili umuondolee usumbufu mnyama. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakika Allaah Ameamrisha kufanya wema katika kila jambo, basi mkiua ueni vizuri, na mkichinja chinjeni vyema, na atie makali kisu chake aanayetaka kuchinja na amuondoshee adhabu dhabihu wake” (Muslim, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy, an-Nasaa’iy, Ibn Maajah na ad-Daarimiy).

Si hayo, bali mnyama anatakiwa afanyiwe ihsani zaidi kuliko hivyo, kwani Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) amesimulia Hadiyth kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: “Akichinja mmoja wenu mnyama basi amalize upesi upesi” (Ibn Maajah). Hii ina maana mtu anafaa anowe kisu barabara, amlishe, ampatie maji mnyama na ampapase kabla ya kumchinja.

Ibn ‘Abbaas anasimulia kuwa wakati mmoja Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuona mtu akinoa kisu baada ya kumlaza kondoo chini kwa ajili ya kuchinjwa. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimrekebisha kwa kumwambia: “Unataka kumuua mara mbili? Kwa nini hukunowa kisu chako kabla ya kumlaza chini?” (al-Haakim).

Ikiwa hayo yametimia basi mnyama aliyechinjwa anakuwa halali. Tunatoa nasaha kwa ndugu zetu sote tuwe ni wenye kuondoa uoga katika kuchinja ili tuweze kufanya wenyewe hata bila ya kusaidiwa na wengine kwani huenda siku moja ukawa ni wewe peke yako na mtarajiwa kuwa unaweza tekeleza shughuli hiyo. Tujiandae, InshaAllaah.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share