Kwenda Kwa Sheikh Kusomewa Kuondosha Mikosi Na Kutumia Miti Shamba inafaa? Je, Kweli Allaah Kaumba Miti 99 Tujitibu Nayo?

SWALI:

 

 

Asaalam aleykum. Inshaallah kheri kutoka kwa Allah iwe juu yenu.

Nimekuwa nikishawishika sana kutoka kwa jamaa zangu niende kwa masheikh kusomewa duaa ili kuondoshwa mikosi na nuksi kwani mambo yangu hasa ktk ndoa zimekuwa haziwi nimekua nikiwakatalia na kuwaambia madhara yake kwani unaweza kumshirikisha Allah kwani huko hupewa dawa za miti shamba kuogea kwa kutoa mikosi na kuwa na bahati na kunywa maji yaliyosomewa lkn wamekuwa wakiniambia Allah ameumba miti 99 ajili tuweze kujitibu kutokana nayo, sasa sina elimu ya kuweza kuwapinga ninaomba fatwa juu ya hilo niweze kuwaeleza na pia kama si vby ninaweza na mimi kwenda kusomewa niwe na bahati kwani ni kweli ndoa kwangu imekua ni hadithi lkn hata hivo namshkuru Allah kwani kuna mengi kanirudhuku. JAZAAK ALLAHU KHAYRA

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kusomewa na masheikh ili kuondosha mikosi na kutumia miti shamba kwa ajili ya kujitibu.

Matatizo hutokea na kumpata mtu kwa sababu kadhaa. Mara nyingine hayo mnayoyaita ni mikosi huenda ikawa ni mitihani kutoka kwa Allaah Aliyetukuka. Mtihani kukutazama uimara wako wa kuweza kushikilia Uislamu katika wakati tofauti. Mitihani inapokuja inatakiwa Muislamu asiende kwa masheikh wala maustadh wala waalimu wenye kutumia uchawi ili kuondoa mikosi bali kurudi kwa Allaah Aliyetukuka na Mtume Wake (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kufuata maagizo yao na kuacha makatazo yao.

 

Uchawi ni shirki na Muislamu hafai kutumia, bali anafaa awe ni mwenye kusoma Aayah, Surah pamoja na Adhkaar zilizo suniwa. Na hizi hapa chini zinaweza kukusaidia kwa kiasi kikubwa:

 

 

  1. Kusoma Aayah kumi za al-Baqarah (2) ambazo zinaepusha nyumba ya mmoja wetu na mashaytwaan. Nazo ni kuanzia ayah 1-5, 255-257 na 284-286. Hizi Aayah zinatakiwa zisomwe asubuhi na jioni.

 

 

  1. Kusoma Suratul Ikhlaasw, al-Falaq na an-Naas mara tatu tatu, asubuhi na jioni na pia wakati wa kulala.

 

 

 

  1. Na Qur-aan yote ni dawa inatakiwa kila Muislamu awe na ada ya kuisoma na kujua maana yake na kutekeleza yaliyomo ndani yake.

 

 

  1. Usome du’aa ambazo ni kinga unapotoka nyumbani na unapoingia.

 

 

  1. Du’aa ambayo wewe na mumeo mnatakiwa msome wakati wa kitendo cha ndoa ambayo inawalinda na kukilinda na Shaytwaan kitoto kitakachozaliwa kutokana na tendo hilo.

 

 

  1. Adhkaar za baada ya Swalah na pia wakati wa kulala.

 

 

  1. Usome Adhkaar za asubuhi na jioni

 

  1. Adhkaar nyingine ni kama, “Bismillaahi Arqiyk min kulli shay’in yu’dhiyka wa min sharri kulli nafsin aw ‘aynin haasidin. Allaahu yashfiyk Bismillaahi arqiyk” (Muslim, at-Tirmidhiy, an-Nasaa’iy na Ibn Maajah). Kwa du’aa hii mume atamsomea mkewe na kinyume chake. Na du’aa nyingine ya kusomeana mara tatu ni, “Bismillaahi arqiyk Wallaahi yashfiyk min kulli daa’in fiyk wa min kulli an-Naffaathaati fil ‘uqad wa min sharri haasidin idhaa hasad” (al-Haakim na Ibn Abi Shaybah).

 

 

Na hizi adhkaar pamoja na nyingine unaweza kuzipata katika kijitabu ambacho ni muhimu sana nacho ni Hiswn al-Muslim (Kinga ya Muislamu). Pia kinaweza kupatikana katika tovuti ya Al-Hidaaya hapa:

 

Hiswnul Muslim

 

Ama miti ambayo inaweza kutumika katika matibabu inaweza kuzidi 99 au kuwa chini ya idadi hiyo, kwani hakuna dalili yoyote kuhusu idadi hiyo. Inatakiwa ikiwa ni kufanya matibabu basi uende kwa madaktari waliobobea au kwa matabibu mahiri wanaotumia Sunnah katika kutibu kwao bila ya kutumia ushirikina. Tufahamu kuwa hakuna ugonjwa ambao hauna dawa, hiyo ni kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuamuru tutafute dawa tunapokuwa wagonjwa. Na katika kauli yake nyingine akasema:

 

“Allaah Hakuteremsha ugonjwa isipokuwa ameleta na dawa yake basi jitibieni.” (al-Haakim).

 

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Akupe shifaa kwa uliyo nayo na Akuondoshee matatizo hayo kabisa.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share