Anafanya Kitendo Cha Siri Kisha Anatubu Kisha Anarudia Tena, Hadi Anaacha Kuswali, Vipi Aache Maasi Haya

 

SWALI:

 

Assalam Aleykum Enyi ndugu zangu Waislam Kwana kabla sijauliza Swali Langu ningependa Kuwapongeza kwa kufungua Tovuti hii yenye Kuelimisha wanaopenda dini ya Kiislam mi nina Swali ngependa Kuwauliza na nitafurahi mtakavyonjibu

 

NINI ATHARI YA ALIEAPA KWAMBA HATORUDIA JAMBO HALAFU AKALIRUDIA MARA MBILI LAKINI MTU HUYO HUYO BADO ANANIA AONGOKE LAKINI MATAMANIOA YA MWILI HAYAMUACHI? NA ANATAKA MSAMAHA KUTOKA KWA MOLA WAKE.  Mfano mimi huwa nina matamanio sana ya kuingiliana Kimwili na msichana nimejitahidi nimeacha lakini nimeshindwa kuacha Musterbation na niliapa kwamba najuta kwa ninayo fanya ewe Mola Niongoze na sitarudia tena lakini nimerudia mara mbili jee nifanye vp kurudia kwangu hunifanya muda mwingine nisi swali Kabisa Nisaidieni ndugu zangu Lakini nahitaji Maghfira kutoka kwa Mola wangu. Masalaam

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kurudia madhambi mara kwa mara.

Fahamu ndugu yetu kuwa Allaah Aliyetukuka ni Msamehevu sana, Naye Anasamehe kila jambo kama Alivyosema:

Sema: Enyi waja Wangu waliojidhulumu nafsi zao! Msikate tamaa na rehema ya Allaah. Hakika Allaah Husamehe dhambi zote. Hakika Yeye ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu” (Az-Zumar 39: 53).

 

Kwa hiyo, mwanzo usikate tama na ni lazima uwe na azma yenye nguvu. Ukiwa na sifa hizo pamoja na kumuomba Allaah Aliyetukuka basi yatakusaidia kabisa katika kujiondoa na madhambi hayo. Huenda pia una marafiki wabaya ambao wanaokushawishi kuliendea hilo ovu ambalo limekatazwa na Allaah Aliyetukuka. Ikiwa unaweza kutimiza masharti haya, basi msamaha wako kutoka kwa Allaah Aliyetukuka una dhamana:

 

1.     Kujiondoa katika maasiya hayo.

2.     Ajute sana katika kufanya kosa hilo.

3.     Aazimie kutolirudia tena kosa hilo.

 

Uchu huo wa matamanio huenda ukawa unakuja kwa sababu huna mke. Kwa hiyo, unatakiwa ufanye juhudi za kutafuta mke ili uweze kukidhi mahitaji yako ya kimwili kwa njia ya halali. Kisha pia usiwe ni mwenye kuapa apa kila wakati, bali weka nia nzuri kabisa wala usiape kwani kuapa kunahitajia kafara ikiwa hujatekeleza kiapo chako.

 

Ili kupunguza matamanio yako inabidi pia uwe ni mwenye kufunga kama alivyoagiza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kufanya hivyo kutafanya matamanio yako yapungue kwa kiasi kikubwa. Na kufanya kosa la kujichua isikupelekee kuacha Swalah kwa hali yoyote ile. Shikamana na Swalah kwa hali zote na huku unamnyenyekea Allaah Aliyetukuka ili Akuondolee tatizo hilo.

 

Yaonyesha kuwa yamini uliyoweka si ya upuuzi bali ni ya kweli kweli. Kwa ajili hiyo kuonyesha kuwa kweli unataka kurudi kwa Allaah Aliyetukuka inatakiwa na inafaa utoe kafara iliyolezewa katika Aayah iliyo chini. Allaah Aliyetukuka Anasema:

Allaah Hatakushikeni kwa viapo vyenu vya upuuzi, lakini Atakushikeni kwa mnavyoapa kweli kweli kwa makusudio. Basi kafara yake ni kuwalisha masikini kumi kwa chakula cha wastani mnachowalisha ahli zenu, au kuwavisha, au kumkomboa mtumwa. Asiyepata hayo, basi afunge siku tatu. Hii ndiyo kafara ya viapo vyenu mnapoapa. Na hifadhini yamini zenu. Namna hivyo Allaah Anakubainishieni Aayah Zake ili mpate kushukuru” (Al-Maaidah 5: 89).

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share