Mambo Muhimu Mwenye Swawm Anapaswa Ayajue Kuhusu Swiyaam

 

 

Mambo Muhimu Mwenye Swawm Anapaswa Ayajue Kuhusu Swiyaam

 

Abuu 'Abdillaah

 

Alhidaaya.com

 

 

بسم الله الرحمن الرحيم

 

 

Yanayobatilisha (Ynayoharibu) Swawm

 

 

1. Kula na kunywa kwa makusudi. Na si kwa kusahau au kwa kulazimishwa, katika mchana wa Swawm.

 

 

2. Kujitapisha kwa makusudi. Kuwe kujitapisha huko kwa kutia kidole mdomoni au kunusa kitu kitachopelekea kutapika.

 

 

3. Mume kumuingilia Mke wake. Na pia kumkumbatia au kumchezea hadi yakamtoka manii.

 

 

4. Kujichua (kuyatoa manii) kwa makusudi ima kwa mkono au kwa kuchezewa na Mkeo au kwa njia yoyote ile. Ama manii hayo yakitoka kwa kuota (ndoto) au kutazama (bila kukusudia) basi haiharibu Swawm.

 

 

5. Kupatwa na Hedhi au Nifasi kwa Mwanamke. Hata kukiwa kutokea huko kuwa ni wakati wa kukaribia kufuturu/kufutari.

 

 

6. Mwenye kutia Niyyah ya kula wakati amefunga, kwa sharti kuwa kaazimia tendo hilo hata kama hakulitekeleza.

 

 

7. Kudhania kuwa jua lishazama Magharibi au bado hakujapambazuka (yaani haujaanza wakati wa kufunga), kisha akala akanywa au akamuingilia mke wake.

 

 

Yasiyobatilisha (Yasiyoharibu) Swawm  

 

1. Kula au kunywa kwa kusahau, kimakosa au kulazimishwa.

 

 

2. Kuingia maji ndani ya matundu ya mwili bila kukusudia, kwa mfano wakati wa kuoga.

 

 

​3. Kudungwa sindano mwilini wakati wa maradhi.

 

 

4. Dawa ya maji idondoshewayo machoni.

 

 

5. Kujipulizia dawa ya asthma mdomoni (puffer au inhaler).

 

 

​6. Kuoga na kujimwagia maji mwilini wakati wa joto kali.

 

 

7. Kuonja chakula kwa mpishi kwa sharti asimeze kile akionjacho.

 

 

8. Kumbusu au kumkumbatia mkeo, kwa sharti awe mtu ana uwezo wa kujizuia na kudhibiti matamanio yake.

 

 

9. Hijaamah (Kupiga chuku, cupping), ikiwa kupiga chuku huko hakutomfanya huyo mtu adhoofike. Ingawa kuna baadhi ya 'Ulamaa wanaona kuwa haifai.

 

 

10. Haitobatilika Swawm ya mtu atakayeamka na janaba au atakayeota mchana wa Swawm akatokwa na manii.

 

 

11.  Kuingia harufu ya manukato au udi puani mwake. Ingawa baadhi ya 'Ulamaa wanasema ni vizuri kujiepusha moshi usiingie hadi kufika tumboni.

 

 

12. Kupiga mswaki, kusukutua au kusafisha pua kwa kutia maji puani bila kuzidisha.

 

 

Du'aa Ya Kufuturu

 

 

Wanachuoni wa Hadiyth wanaeleza kuwa hakuna Hadiyth yoyote iliyo sahihi katika du'aa ya kufuturu.

 

 

Kuanza Kufuturu Kwa Tende Au Maji

 

قال رسول الله صلى الله عليه وسلم: ((من وجد التمر فليفطر عليه ، ومن لم يجد التمر فليفطر على الماء ، فإن الماء طهور)) رواه أحمد وأبو داود والترمذي 

Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Atakayepata tende afuturu kwayo, na asiyepata basi afungue kwa maji, kwani maji ni twahara)) [Imesimuliwa na ma-Imaam Ahmad, Abu Daawuwd na At-Tirmidhiy]

 

 

Watu Walioruhusiwa Kutokufunga 

 

Swawm Za Ramadhwaan ni fardh kwa kila Muislam aliye baaligh, mwenye akili timamu isipokuwa kwa wale kufunga ni shida na itawaletea madhara nao ni wenye udhuru kama huu ufuatao:

 

 

1. Walio katika safari na wagonjwa ambao kufunga kwao kutawafanya wawe wagonjwa zaidi, haipendezwi kwa watu hao kufunga, lakini wakifunga Swawm yao itakubaliwa. Wakichagua au kupenda kuwa wasifunge basi ni lazima walipe siku hizo wasizofunga baada ya Ramadhwaan.

 

 

​2. Wanawake walio katika hedhi na waliotoka kuzaa ambao wako katika damu ya Nifaas hawaruhusiwi kufunga, na wakifunga katika hali hii, basi Swawm yao haitokubaliwa. Nao pia ni lazima walipe kila siku walizoacha baada ya Ramadhwaan.

 

 

​3. Wanawake wajawazito na wanaonyonyesha ikiwa watakhofu kuwa Swawm itawadhuru watoto wao au wenyewe, hao si lazima kufunga. Lakini ikiwa hawatofunga Ramadhwaan basi ni lazima wafunge baada ya Ramadhwaan kulipa siku zao.

 

 

​3. Watu wasioweza kufunga kutokana na umri mkubwa na maradhi yasiyopona hawatakiwi kufunga. Inawatosheleza kulisha maskini mmoja kwa kila siku moja wanayoshindwa kufunga. Na kila wakiweza kulisha mas

kini zaidi ni bora.

 

* Maelezo yote hapo juu ni kutoka katika mkusanyiko wa fatwa mbalimbali za 'Ulamaa.

 

 

Tunawaombea kila la khayr katika Mwezi wa Ramadhwaan. Allaah Aujaalie uwe wa khayr na wenye kutakabaliwa matendo yetu.

 

 

 

Share