Fiqh Ya Swawm Ya Ramadhwaan Kutoka Kitabu 'Al-Wajiyz Fiy Fiqhis-Sunnah Wal-Kitaabil-'Aziyz

 

Fiqh Ya Swawm Ya Ramadhwaan

Kutoka Kitabu 'Al-Wajiyz Fiy Fiqhis-Sunnah Wal-Kitaabil-'Aziyz

 

Alhidaaya.com

 

  

Kufunga mwezi wa Ramadhwaan ni moja katika nguzo za Dini yetu ya Kiislamu na moja katika mambo ya lazima yampasayo kila Muislamu. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Anasema:

 يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ

Enyi walioamini! Mmefaridhishwa Swiyaam kama ilivyofaridhishwa kwa walio kabla yenu mpate kuwa na taqwa. [Al-Baqarah: 183]

 

Baada ya Aayah hii Allaah (Subhaanahu wa Ta´aalaa) Anasema tena:

 

شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِيَ أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَى وَالْفُرْقَانِ فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَى سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ يُرِيدُ اللّهُ بِكُمُ الْيُسْرَ وَلاَ يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْرَ وَلِتُكْمِلُواْ الْعِدَّةَ وَلِتُكَبِّرُواْ اللّهَ عَلَى مَا هَدَاكُمْ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ

Mwezi wa Ramadhwaan ambao imeteremshwa humo Qur-aan ili iwe mwongozo kwa watu na hoja bayana za mwongozo na pambanuo (la haki na batili). Basi atakayeshuhudia miongoni mwenu mwezi na afunge. Na atakayekuwa mgonjwa au safarini, basi (inapaswa kulipa) idadi sawa katika masiku mengineyo. Allaah Anakutakieni mepesi na wala Hakutakieni magumu; na ili mkamilishe idadi na ili mumkabbir Allaah kwa kuwa Amekuongozeni na ili mpate kushukuru. [Al-Baqarah: 185]

 

 

Ibn ´Umar (Radhwiya Allaahu ´anhuma) alimsikia Nabiy (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

 

“Uislaam umejengewa katika (nguzo) tano: Kuthibitisha kidhati kuwa hakuna Rabb apasae kuabudiwa kwa Haqq ila Allaah, na kuthibitisha kidhati kuwa Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa Sallam) ni Rasuli Wake, kusimamisha Swalaah, kutoa Zakaah, kutekeleza ´Ibaadah ya Hajj kwa mwenye uwezo, na kufunga mwezi mtukufu wa Ramadhwaan.” [Imeripotiwa na Al-Al-Bukhaariy na Muslim].

 

Waislamu wote wamekubaliana kuwa kufunga mwezi wa Ramadhwaan ni wajibu wa kila Muislamu na kuwa ni moja katika (nguzo) za Uislaam na ni jambo lenye kujulikana katika Dini yetu kwa kutekelezwa kwake. Yeyote atakayekanusha ´Ibaadah hii ya Kufunga mwezi wa Ramadhwaan kuwa si wajibu kwa kila Muislamu atakuwa amekufuru Kufru ambayo inamtoa katika Uislaam.

 

Uzuri Wa Kutekeleza ´Ibaadah Ya Kufunga Mwezi Wa Ramadhwaan

 

Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ´anhu) alimsikia Nabiy (Swalla Allaahu ´alayhi wa aalihi sallam) akisema:

 

“Yeyote atakayefunga mwezi wa Ramadhwaan kwa Imani na kutarajia malipo kutoka kwa Allaah basi Allaah Atamsamehe madhambi yake yote yaliyopita.” [Imeripotiwa na Al-Al-Bukhaariy na Muslim, An-Nasaaiy na Ibn Maajah].

 

Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ´anhu) amesema tena, alimsikia Nabiy (Swalla Allaahu ´alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

 

“Allaah amesema: “Kila ‘Amali ya mwanaadam ni yake yeye mja Wangu ila Swawm. Ni yangu Mimi na mimi ndiye Nitakayemlipa mja Wangu.”

 

Swawm ni kinga. Itakapofikia siku mmoja wenu amefunga ajiepushe na kufanya kitendo cha jimai na mabishano na watu. Na yeyote atakayetaka kupigana naye basi amwambie “Mimi nimefunga.” Naapa kwa jina la Allaah, Harufu inayotoka katika mdomo wa mwenye kufunga ni nzuri kwa Allaah kuliko harufu ya Misk. Kwa Mwenye kufunga ana furaha mbili: Furaha anapofungua Swawm yake na furaha pale atakapoonana na Rabb Ameridhika kwa kufunga kwake.” [Imeripotiwa na Al-Al-Bukhaariy na Muslim na An-Nasaaiy]

 

Sahl ibn S’ad (Radhwiya Allaahu ´anhu) alimsikia Nabiy (Swalla Allaahu ´alayhi wa Sallam) akisema:

 

‘’Jannah kuna mlango unaitwa Ar-Rayyaan. Wale wenye kufunga wataingia Jannah kupitia lango huu siku ya Qiyaamah na hakuna mwengine atakayepita katika mlango huu ila (wafungaji). Itaambiwa: ‘’Wako wapi waliokuwa wakifunga?” Watasimama na watapita katika mlango huu na watakapomalizika kuingia wote (wafungaji) utafungwa na hakuna mwengine atakayepita hapo tena.“ [Imeripotiwa na Al-Al-Bukhaariy na Muslim, At-At-Tirmidhiy, Ibn Maajah na An-Nasaaiy].

  

Kufunga Mwezi Wa Ramadhwaan Ni Wajibu Pale Mwezi Unapoonekana

 

Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ´anhu) amemsikia Nabiy (Swalla Allaahu ´alayhi wa aalihi sallam) akisema:

“Fungeni kwa kuona au kuandama mwezi wa Ramadhwaan na fungueni (malizeni) kufunga mwezi wa Ramadhwaan kwa kuona mwezi na msipouona mwezi basi timizeni siku thelathini.” [Imeripotiwa na Al-Al-Bukhaariy, Muslim, na An-Nasaaiy].

 

Mwezi Wa Ramadhwaan Unathibitishwaje Kuonekana Kwake?

 

Mwezi wa Ramadhwaan unathibitishwa kuonekana kwake na mtu mmoja mwenye kujulikana kwa ukweli na kumcha kwake Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) au kwa kutimiza siku thelathini za mwezi wa Sha’abaan.

 

Ibn ´Umar amesema watu walikuwa wakitafuta kuandama kwa mwezi. nikamjulisha Nabiy (Swalla Allaahu ´alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa mimi nimeuona mwezi. Nabiy (Swalla Allaahu ´alayhi wa aalihi wa sallam) akafunga na akaamrisha watu wafunge.” [Hadiyth Swahiyh. Angalia Kitaab I’rwa al-Ghaliyl na. 908 na Imeripotiwa na Abu Daawuwd].

 

Ikiwa mwezi haukuandama, kwa sababu ya kufunikwa na mawingu au kwa sababu nyingine basi hapo mwezi wa Sha’abaan utatimizwa kwa siku thelathini kama alivyoripoti Abu Hurayrah katika Hadiyth iliyo hapo juu.

 

Lakini mwezi wa Shawwaal unatangazwa kuonekana kwa mashahidi wawili.’ ´Abdur-Rahmaan bin Zayd bin Al-Khatwaab amesema: “Nilipokuwa nikikhutubia siku ambayo ni ya shaka (kama mwezi wa Ramadhwaan kama umekwisha ama la), nikasema: “Nilikaa na Swahaba zake Nabiy (Swalla Allaahu ´alayhi wa aalihi wa sallam) nikawauliza wao. Wakaniambia mimi kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ´alayhi wa Sallam) alisema:

 

‘’Fungeni kwa kuonekana mwezi na fungueni kwa kuonekana mwezi na tekelezeni ´Ibaadah ya Hajj kwa haki zake. Ikiwa kuna mawingu basi timizeni siku thelathini. Na Ikiwa Waislamu wawili watachukua kiapo kwa kuonekana kwa mwezi basi fungeni na mfungue kwa kushuhudia kwao mwezi.’’ [Hadiyth Swahiyh. Angalia Kitaab cha Shaykh Al-Albaaniy, Swahiyh al-Jamiy’ Asw-Swaghiyr na. 3811. Pia Imeripotiwa na Imaam Ahmad na An-Nasaaiy bila kipande kinachosema ‘’Waislamu wawili.’’].

 

Mtawala wa Makkah, Al-Haarith bin Hatwiyb amesema:

 

“ Nabiy (Swalla Allaahu ´alayhi wa aalihi wa sallam) alituambia sisi tekelezeni ´Ibaadah ya Hajj kwa haki zake munapouona mwezi. Na ikiwa hamkuuona mwezi lakini mashahidi wawili wa kuaminika wakishuhudia kwa kuona mwezi tunatekeleza ´Ibaadah ya Hajj kutokana na ushahidi wao.’’ [Hadiyth Swahiyh angalia Shaykh Al-Albaaniy, Swahiyh Sunan Abiy-Daawuwd, na. 205. Imeripotiwa na Abu Daawuwd].

 

Tukiangalia ripoti mbili hizi,

 

’’Ikiwa waislamu wawili watachukua kiapo kwa kuona mwezi, basi fungeni na fungueni’’ katika Hadiyth ya Abdur-Rahmaan bin Zayd na:

 

‘’Na ikiwa hamkuuona mwezi lakini watu wawili wenye kujulikana kwa ukweli wakasema wameuona mwezi tunatimiza haki za ´Ibaadah ya Hajj kutokana na ushahidi wao.’’ katika Hadiyth ya Al-Haarith wanaonyesha kwa kutilia mkazo, kuwa haifai kuanza kufunga au kumaliza kufunga kutokamana na ushahidi wa mtu mmoja pekee. Juu ya hilo, tangu kuanza kwa kufunga imeondolewa uzito kutokana na ushahidi (uliotolewa hapo juu), inawacha suala la kumaliza kufunga, ambalo halina ushahidi kwamba linatoshelezwa kwa ushahidi wa mtu mmoja pekee. Huu ni ufupi wa mjadala unaopatikana katika Kitabu ‘Tuhfah Al-Ahwadhiy’ [Mjalada wa 3, uk. 373-3749].

 

Tanbihi: Ikiwa mtu atauona mwezi yeye peke yake, hafungi mpaka watu wafunge na hamalizi kufunga mpaka watu wamalize kufunga kama ilivyoripotiwa na Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ´anhu), kwamba amesema Nabiy (Swalla Allaahu ´alayhi wa aalihi wa sallam):

 

‘’Swawm (kufunga) ni siku ambayo watu wanafunga. Na kumaliza kufunga ni siku ambayo watu wanamaliza kufunga. Na kuchinja ni katika siku ambayo watu wanachinja.’’ [Hadiyth Swahiyh. Angalia Swahiyh Al-Jami’ Asw-Swaghiyr, na. 3869]. Imehifadhiwa na Imaam At-At-Tirmidhiy ambaye amesema: ‘’Baadhi ya ‘Ulamaa wanaifasiri Hadiyth hii kwa maana: “Kuanza kufunga na kumaliza kufunga kunatekelezwa na watu wote kwa pamoja na wakati mmoja.”

 

Nani Anawajibika Kufunga

 

‘Ulamaa wamekubaliana kufunga ni wajibu kwa mwenye akili timamu, Baleghe, mwenye afya na mkazi wa mji. Tukiongezea wanawake waliotwaharika na hedhi na nifasi.

 

Kwa wale ambao Swawm si wajibu juu yao ni wale ambao hawana akili timamu, hawajabaleghe.

 

Nabiy (Swalla Allaahu ´alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Kalamu (kurekodiwa ‘amali) imeinuliwa (hairekodi) kwa watu watatu: anayepatwa na usingizi mpaka aamke, mtoto mpaka afike umri wa kubaleghe, na aliorukwa na akili mpaka atakapopata akili timamu.” [Hadiyth imesahihishwa na Shaykh Al-Albaaniy katika Swahiyh Al-Jami´, na. 3513 na Imerikodiwa na Abu Daawuwd].

 

Ama kwa wale wasioweza kufunga  ni kutokamana na maneno Yake Allaah:

 

 فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَى سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ

Basi atakayeshuhudia miongoni mwenu mwezi na afunge. Na atakayekuwa mgonjwa au safarini, basi (inapaswa kulipa) idadi sawa katika masiku mengineyo.  [Al-Baqarah: 185]

 

Ikiwa mgonjwa au msafiri atafunga basi inawatosheleza, ama wakichukua ruhsa ya kula hapo wameondolewa uzito. Ama wakiamua kufunga kwa kuwa wanataka kufunga hapo pia wako sawa.

 

Ni kupi bora: Kutofunga au Kufunga?

 

Ikiwa mgonjwa au msafiri hawatoona tabu yoyote katika kufunga, basi kufunga kunapendekezwa. Ama wakikhofia kupata tabu kutokamana na kufunga, basi hapo kutofunga kunapendekezwa.

 

Abu Sa’iyd al-Khudriy ameelezea:

 

‘’Tulikuwa vitani na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa aalihi wa sallam) wakati wa Ramadhwaan. Wengine katika sisi walikuwa wamefunga na wengine walivunja Swawm zao. Wale waliofunga hawakuwaona waliovunja Swawm zao kuwa wako makosani na waliokula pia hawakuwaona waliofunga kuwa wako na makosa. Waliona wenye uwezo wa kufunga (walifunga) na hilo ni jambo zuri. Na ambao hawakuweza kufunga walivunja Swawm zao kwa udhaifu wa kufunga (hawakufunga) na hili pia ni jambo zuri.’’ [Imesahihishwa na Shaykh Al-Albaaniy katika Swahiyh Sunan At-At-Tirmidhiy na. 574. Pia imerikodiwa na Imaam Muslim].

 

Ushahidi wa wanawake wasio Twahara kuwa hawafungi ni Hadiyth ya Abu Sa´iyd ambayo Nabiy (Swalla Allaahu ´alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

’’Je, si kwa kesi kwamba anapopatwa na damu yake ya mwezi, haswali wala hafungi? huo ni upungufu katika Dini yake.’’ [Imesahihishwa na Shaykh Al-Albaaniy, katika Mukhtaswar Swahiyh Al-Al-Bukhaariy na. 951. Imerikodiwa na Imaam Al-Al-Bukhaariy].

 

Ikiwa mwanamke asiyo Twahara atafunga basi swawm yake haikubaliki kwani katika masharti ya kukubalika swawm ya mwanamke ni awe katika Twahara. Mwanamke pia itamlazimu alipe siku alizokosa kufunga. ´Aaishah (Radhwiya Allaahu ´anhu) amesema:

 

“Tulipokuwa tukipatwa na siku zetu za ada wakati wa Nabiy (Swalla Allaahu ´alayhi wa Sallam) tuliamrishwa kulipa Swawm za siku tuliokosa kufunga na hatukuamrishwa kulipa Swalah tulizokosa.’’ [Imesahihishwa na Shaykh Al-Albaaniy katika Swahiyh Sunan At-Tirmidhiy na.630. Imerikodiwa na Imaam Muslim, Abu Dawuud, At-Tirmidhiy na An-An-Nasaaiy].

 

Yanayomlazimu Mtu Mzima Na Mwenye Ugonjwa Wa Kuendelea

 

Asioweza kufunga, kwa ajili ya utu uzima au kwa ajili sababu nyenginezo, hatofunga badili yake atalisha maskini mmoja kwa kila siku aliokosa kufunga. Allaah (Subhanahu wa Ta’aalaa) Amesema:

 وَعَلَى الَّذِينَ يُطِيقُونَهُ فِدْيَةٌ طَعَامُ مِسْكِينٍ

“Na wale wasioweza, watoe fidiya kwa kumlisha masikini. (kwa kila siku).” [Al-Baqarah: 184)

 

‘Atwaa’ amesema alimsikiya Ibn ´Abbaas akisoma Aayah hii kisha akasema ‘’Haikuondolewa. Inawahusu watu wazima waume kwa wake ambao hawawezi kufunga. Ndio watalisha masikini mmoja kwa kila siku ambayo hawakufunga.” [Imesahihishwa na Shaykh Al-Albaaniy katika I’rwa al-Ghaliyl na.912 na Imerikodiwa na Imaam Al-Bukhaariy].

  

Mwanamke Mja Mzito (Mwenye Mimba) Au Mwenye Kunyonyesha

 

Mwanamke mwenye mimba au mwenye kunyonyesha ambaye hana uwezo wa kufunga ama ambaye anahofia afya ya mtoto wake anaweza asifunge, atalisha maskini mmoja na hawajibiki kuilipa siku aliyokula. Ibn ´Abbaas amesema:

 

“Ruhusa amepewa mtu mzima mume au mke ambapo wataoneleya tabu kufunga, hawatofunga ambapo hawatopendeleya kufunga na watalisha maskini mmoja kwa kila siku ya kufunga. Kisha hawatalipa siku walizokosa kufunga hii iliondolewa baada ya Aayah hii:

 

 وَعَلَى الَّذِينَ يُطِيقُونَهُ فِدْيَةٌ طَعَامُ مِسْكِينٍ

Na kwa wale wanaoiweza lakini kwa mashaka na kutaabika watoe fidia; kulisha masikini. [Al-Baqarah: 184]

  

Baada ya hapo ikahakikishwa kuwa mtu mzima mume au mke ambao hawawezi kufunga na mwanamke mwenye mimba au mwenye kunyonyesha, ikiwa watahofia, hawatafunga na watalisha maskini kwa kila siku ambayo hawakufunga. [Msururu wa Riwaayah hii ni madhubuti imeripotiwa na Al-Bayhaqiy]. Pia imerikodiwa kuwa alisema, ikiwa wakati wa Ramadhwaan mwanamke mwenye mimba anahofia afya yake, au mwenye kunyonyesha anahofia afya ya mtoto wake, hawatafunga na watalisha maskini mmoja kwa kila siku ambayo hawakufunga na hawatalipa siku hizo kwa kufunga. [Imesahihishwa na Shaykh Al-Albaaniy katika I’rwa al-Ghaliyl mjallad 4 uk.19].

 

Nafi’iy alisema ’Mmoja katika mabanati wa Ibn ´Umar aliolewa na mwanamume wa ki-Quraysh. Akapata mimba na wakati wa Ramadhwaan anashikwa na kiu sana. Ibn ´Umar akamwambiya funguwa swawm yako na ulishe masikini kwa kila siku.’’ [Msururu wa Riwaayah ni Swahiyh na Imesahihishwa na Shaykh Al-Albaaniy katika I’rwa al-Ghaliyl mjallad 4 uk.20. Imerikodiwa na ad-Daraqutniy].

 

Kiwango gani cha chakula anawajibika kulisha?

 

Imeelezwa kwamba Anas Ibn Malik alidhoofika sana na hakuweza kufunga mwaka mzima akatayarisha sufuriya Thariyd (Mkate na nyama uliolowana katika supu) kisha akaalika masikini thelathini akawalisha mpaka wakaridhika’’. [Msururu wa Riwaayah hii ni Swahiyh pia imesahihishwa na Shaykh Al-Albaaniy katika I’rwa al-Ghaliyl, mjallad 4 uk.21 imerikodiwa na ad-Daraqutniy].

 

Yaliyo Muhimu Kwa Ujumla Wa Kutekeleza ´Ibaadah Ya Swawm (Kufunga)

 

1).     Niyyah.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amesema:

 

 وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاء وَيُقِيمُوا الصَّلَاةَ وَيُؤْتُوا الزَّكَاةَ وَذَلِكَ دِينُ الْقَيِّمَةِ

Na hawakuamrishwa isipokuwa wamwabudu Allaah wenye kumtakasia Dini, wenye kujiengua na upotofu kuelemea Dini ya haki na wasimamishe Swalaah na watoe Zakaah; na hiyo ndiyo Dini iliyosimama imara. [Al- Bayyinah: 05]

 

Nabiy (Swalla Allaahu ´alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

’’Kila kitendo hulipwa (kutokana na) niyyah na kila mtu ni lili alilonuwiya.’’

 

Na niyyah mahala pake ni moyoni. Niyyah ya kufunga ni lazima iwe moyoni kila usiku kabla ya wakati wa Fajr kuingiya.

 

Hafsah (Radhwiya Allaahu ´anha) amesema Nabiy (Swalla Allaahu ´alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

‘’Hana swawm asiyenuwia kufunga kabla ya fajr.’’ [Imesahihishwa na Shaykh Al-Albaaniy katika Swahiyh al-Jamiy´ as-Saghiyr, na.6238. Pia imerikodiwa na Abu Dawuud, At-Tirmidhiy na An-Nasaaiy].

 

2).     Kujiepusha katika masiku ya kuamka na swawm na chochote chenye kubatilisha swawm yako (tangu wakati wa adhaana ya pili) na usiku mpaka kutakapopambauka (Jua kuchomoza).

 

Amesema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

  وَكُلُواْ وَاشْرَبُواْ حَتَّى يَتَبَيَّنَ لَكُمُ الْخَيْطُ الأَبْيَضُ مِنَ الْخَيْطِ الأَسْوَدِ مِنَ الْفَجْرِ ثُمَّ أَتِمُّواْ الصِّيَامَ إِلَى الَّليْلِ

Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu uzi mweupe (mapambazuko) wa Alfajiri kutokana na uzi mweusi (wa kiza cha usiku). Kisha timizeni Swiyaam mpaka usiku. [Al-Baqarah: 187].

  

Mambo Sita Yanayobatilisha Swawm

                                                                                          

a).   na b).   Kula au kunywa kwa kukusudia.

 

c).   Kujitapisha kusudi.

 

d).   na f).   Mwanamke atakapopata ada yake mwezi akiwa katika swawm.

 

g).   Kitendo cha Jimai.

 

Mambo Yaliyopendekezwa Kwa Mwenye Swawm

 

Imependekezwa kwa mwenye kufunga afuate Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu ´alayhi wa aalihi wa sallam) katika kujitayarisha na swawm yake nayo ni haya yafuatayo;

 

i.     Kula daku

 

Amehadithia Anas (Radhwiya Allaahu ´anhu) Nabiy (Swalla Allaahu ´alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

‘’Kuleni daku, kwani kula huko daku kuna baraka.” [Imeripotiwa na Imaam Al-Bukhaariy, Muslim, At-Tirmidhiy na Nasaa’y na Ibn Maajah].

 

Na ‘’kuleni daku’’ hata kama kwa kunywa maji inatosheleza. ´Abdullaah Ibn ´Amr amehadithia Nabiy (Swalla Allaahu ´alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

’’Kuleni daku japo kwa kunwa tama la maji.’’ [Imesahihishwa na Shaykh Al-Albaaniy katika Swahiyh al-Jamiy´ as-Swaghiyr na.2945 imeripotiwa na Ibn Hibbaan].

 

Pia Imependekezwa kuchelewesha kula daku. Amehadithiya Anas kutoka kwa Zayd ibn Thabit ambaye amesema:

 

‘’Nabiy (Swalla Allaahu ´alayhi wa aalihi wa sallam) alikula daku kisha akatoka kwenda kuswali. Anas akamuuliza “Kulikuwa na muda gani baina chakula cha daku na adhaana?” Akajibu: “Ilikuwa kiasi cha kusoma Aayah khamsini za Qur-aan". [Imeripotiwa na Imam Al-Bukhaariy na Muslim].

 

Pia ameruhusiwa amalize chakula chake anaposikia Adhaana ya Fajr. Abu Hurayrah amehadithia Nabiy (Swalla Allaahu ´alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Endapo mmoja wenu atasikiya adhaana na mkononi mwake ana kinywaji, asirudishe kinywaji hicho mpaka aridhike nacho.’’(yaani anywe mpaka amalize haja yake). [Imesahihishwa na Shaykh al-Albaaniy katika al-Jami' as-Swaghiyr na.607].

 

ii.     Kujiepusha na maneno ya Upuuzi na mambo yasofaidisha Swawm yako.

 

Amehadithia Abu Hurayrah Nabiy (Swalla Allaahu ´alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

’’Ikiwa mmoja wenu yuko ndani ya swawm ajiepushe na kitendo cha jimai na mabishano. Na kukitoka mmoja anataka kupigana nawe basi mwambiye ‘’Mimi Nimefunga’’. [Imeripotiwa na Imaam Al-Bukhaariy na Muslim na An-Nasaaiy]. Tena amehadithiya Nabiy (Swalla Allaahu ´alayhi wa Sallam) amesema:

 

’’Yeyote ambaye hatowacha kusema uongo na kutenda kwa uongo basi Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) hana haja yake kwa kuwacha chakula chake na kinywaji chake’’. [Imesahihishwa na Shaykh Al-Albaaniy katika mukhtasar Swahiyh Al-Al-Bukhaariy na.921].

 

iii.     Kuwa na moyo kutoa na kujifunza Kusoma Qur-aan

 

Ibn ´Abbaas amesema:’’Nabiy (Swalla Allaahu ´alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa mwenye moyo wa kutoa mali katika watu wote na akifanya vizuri kabisa. Alikuwa akitoa zaidi katika mwezi wa Ramadhwaan anapoonana na Malaika wa Allaah Jibriyl (´alayhis-salaam). Jibriyl anaonana naye kila usiku wa Ramadhwaan mpaka mwezi umalizike. Nabiy (Swalla Allaahu ´alayhi wa Sallam) atasoma naye Qur-aan. Anapoonana na Jibriyl, alikuwa na moyo zaidi wa kufanya mema kuliko kuifadisha swawm yake’’. [Imeripotiwa na Imaam Al-Bukhaariy na Muslim].

 

iv.     Kukimbilia (kuharakisha) kufungua swawm

 

Sahl Ibn Sa'd amehadithiya Nabiy (Swalla Allaahu ´alayhi wa Sallam) amesema:

 

’’Watu watakuwa katika kheri endapo watakimbilia kufungua swawm zao’’.

 

v.      Kufungua Swawm na yale yaliotajwa katika Hadiyth ikiwa ni rahisi kufanya hivo.

 

Anas amehadithia Nabiy (Swalla Allaahu ´alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akifunguwa swawm yake na Tende zilioiva kabla kusali. Kama si zilioiva alikuwa akifungua na Tende kavu. Kama hiyo pia haikupatikana basi alikuwa akifunguwa na kinywaji cha maji. [Ni Hadiyth Hasan Swahiyh katika al-Jamiy´ as-Swaghiyr na.2065]

 

Mambo Yanayofaa Kufanywa Na Mwenye Kufunga
 

·       Anaruhusiwa kujisuuza kichwa na maji ya baridi.

 

·       Kusukutua na maji bila kuyamiza na kutiya maji puani bila kuingiya ndani ya mwili.

 

·       Kuumikwa ama kutoa damu kwa ajili ya matibabu.

 

·       Kumbusu au kumgusa mke wako bila matamanio kwa mwenye kuweza kujizuwiya.

 

·       Mwenye kuamka asubuhi na akiwa katika janaba.

 

·       Kuchelewesha kufungua swawm mpaka saa ya kula daku.

 

·     Kutumia mswaki, manukato, wanja, dawa ya macho na kudungwa sindano kwa ajili ya matibabu.

 

 

Wa Swalla Allaahu wa Sallam ´alaa RasuuliLLaah.

 

Share