Kuchinja - Fadhila, Hikmah Na Hukmu Zake

Kuchinja - Fadhila, Hikmah Na Hukmu Zake

 

www.alhidaaya.com

 

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'alaa):

 

فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ ﴿٢﴾

Basi swali kwa ajili ya Rabb wako na chinja kwa ajili Yake. [Al-Kawthar: 2]

 

Kuchinja ni moja ya ‘ibaadah za Kiislam ambayo inatukumbusha Tawhiyd ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'alaa) na Baraka Zake kwetu, pamoja na kutupa mafunzo ya utiifu wa baba yetu Ibraahiym kwa Rabb wake na kumpwekesha Allaah. Hivyo ‘ibaadah hii ya kuchinja ni muhimu sana kwa Muislamu, na inatupasa tuizingatie kwa makini na kuitekeleza.

 

 

Ubainifu Wake:

 

Ni kuchinja kondoo, ngamia au ng'ombe au mbuzi siku ya 'Iydul-Adhwhaa na siku za Tashriyq (siku ya 11, 12, 13 Dhul-Hijjah) ili kujikurubisha kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'alaa).

 

 

Hukmu Yake:

 

Wanavyuoni wamekhitilafiana kuhusu hukmu yake, hivyo kuna kauli mbili:

 

Ya Kwanza:  Kuchinja ni  Sunnah Muakkadah (Sunnah iliyosisitizwa) na hii ndio rai iliyotiliwa nguvu kabisa na Ma-Imaam Maalik, Shaafi'iyy, Ahmad bin Hanbal na wengineo. 

 

 

Ya Pili: Kuchinja ni waajib kwa kila mwenye uwezo. Rai hii ni ya Abuu Haniyfah na wengineo. Inawajibika katika familia ya kila nyumba ya Muislamu, ambayo watu wake wanao uwezo wa kuchinja. Wakanukuu  kauli za Allaah (Subhaanahu wa Ta'alaa):

 

فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ ﴿٢﴾

2. Basi swali kwa ajili ya Rabb wako na chinja kwa ajili Yake. [Al-Kawthar: 2]

 

 وَالْبُدْنَ جَعَلْنَاهَا لَكُم مِّن شَعَائِرِ اللَّـهِ لَكُمْ فِيهَا خَيْرٌ ۖ  

36. Na ngamia na ng’ombe Tumekufanyieni kuwa ni miongoni mwa Ishara za Allaah; kwa hao mnapata khayr nyingi. [Al-Hajj: 36]

 

Pia wakanukuu Hadiyth kadhaa za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Athaar. 

 

Aliulizwa Imaam Muhammad bin 'Uthaymiyn kama masikini inampasa achinje. Akajibu "Ikiwa anao uwezo wa kuchinja basi achinje ili apate khayr hizi na kama hana uwezo basi haimpasi".

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam),

 

 (( ضحى بكبشين أملحين أقرنين ذبحهما بيده وسمى وكبر)) رواه البخاري ومسلم 

alichinja kondoo wawili walionona, walio na pembe, aliwachinja kwa mikono yake akataja jina la Allaah, Akamtukuza kwa kusema BimiLLaahi Allaahu Akbar [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Maoni ya Wanachuoni wengi kuhusu fadhila, hukmu na hekima ni kama yafuatayo:

 

 

Fadhila Zake:

 

Kuna ushahidi kwamba ‘ibaadah ya kuchinja ina fadhila kubwa kwa sababu ya kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

 عن عائشة رضي الله عنها أن النبي صلى الله عليه وسلم قال: ((ما عمل ابن آدم يوم النحر عملاً أحبُّ إلى الله من إراقة الدم، وإنه ليؤتى يوم القيامة بقرونها، وأظلافها، وأشعارها، وإن الدم ليقع من الله عز وجل بمكان قبل أن يقع على الأرض، فطيبوا بها نفساً))

Kutoka kwa mama wa Waumini 'Aaishah (Radhwiya Allaahu anhaa) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakuna kitendo cha mwana Aadam kilichokuwa ni kipenzi kabisa kwa Allaah siku ya kuchinja kama kumwaga  damu (kuchinja). Atakuja (huyo mnyama) siku ya Qiyaamah na pembe zake, kucha zake na nywele zake. Damu yake itamwagika mahali fulani Allaah Anapajua kabla ya kumwagika katika ardhi. Hivyo zipendezesheni nafsi kwayo)) [At-Tirmidhiy]

 

 

Hikmah Yake:

 

1. Kujikurubisha Kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'alaa) kama Anavyosema katika kauli Yake: 

 

فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ ﴿٢﴾

2. Basi swali kwa ajili ya Rabb wako na chinja kwa ajili Yake. [Al-Kawthar: 2]

 

Anasema pia:

 

قُلْ إِنَّ صَلَاتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿١٦٢﴾

162. Sema: “Hakika Swalaah yangu, na kuchinja kafara na ‘ibaadah zangu na uhai wangu na kufa kwangu ni kwa ajili ya Allaah Pekee Rabb wa walimwengu.”

 

لَا شَرِيكَ لَهُ ۖ وَبِذَٰلِكَ أُمِرْتُ وَأَنَا أَوَّلُ الْمُسْلِمِينَ ﴿١٦٣﴾

163. Hana mshirika, na kwa hayo ndio nimeamrishwa, nami ni Muislamu wa kwanza. [Al-An'aam: 162-163]. 

 

  لَن يَنَالَ اللَّـهَ لُحُومُهَا وَلَا دِمَاؤُهَا وَلَـٰكِن يَنَالُهُ التَّقْوَىٰ مِنكُمْ ۚ كَذَٰلِكَ سَخَّرَهَا لَكُمْ لِتُكَبِّرُوا اللَّـهَ عَلَىٰ مَا هَدَاكُمْ ۗ وَبَشِّرِ الْمُحْسِنِينَ ﴿٣٧﴾

37. Haimfikii Allaah nyama zake wala damu yake, lakini inamfikia taqwa kutoka kwenu. Hivyo ndivyo Tulivyowatiisha kwenu ili mpate kumtukuza Allaah; Allaahu Akbar, kwa yale Aliyokuongozeni; na wabashirie wafanyao ihsaan. [Al-Hajj: 37]

 

Na kafara ni kuchinja kwa kujikurubisha kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'alaa)

 

 

2. Kuihuisha Sunnah Mojawapo Ya Tawhiyd, wakati Allaah Alipompa wahyi Ibraahiym (alayhis-salaam) amchinje mwanawe Ismaa'iyl. Kisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'alaa) Akampa fidia ya kondoo, akamchinja badala yake. Allaah (Subhaanahu wa Ta'alaa) Anasema:

 

وَفَدَيْنَاهُ بِذِبْحٍ عَظِيمٍ ﴿١٠٧﴾

107. Na Tukamfidia kwa dhabihu adhimu. [Aswaaffaat: 107]          

 

 

3.  Muislam kuweza kuwalisha nyama familia yake pamoja na jamaa zake siku ya 'Iyd na kueneza Rahmah miongoni mwa masikini na mafakiri.

 

 

4. Kutoa shukurani kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'alaa)  kutujaalia kuwa na wanyama wafugwao kama Anavyosema:

 

وَالْبُدْنَ جَعَلْنَاهَا لَكُم مِّن شَعَائِرِ اللَّـهِ لَكُمْ فِيهَا خَيْرٌ ۖ فَاذْكُرُوا اسْمَ اللَّـهِ عَلَيْهَا صَوَافَّ ۖ فَإِذَا وَجَبَتْ جُنُوبُهَا فَكُلُوا مِنْهَا وَأَطْعِمُوا الْقَانِعَ وَالْمُعْتَرَّ ۚ كَذَٰلِكَ سَخَّرْنَاهَا لَكُمْ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ ﴿٣٦﴾

36. Na ngamia na ng’ombe Tumekufanyieni kuwa ni miongoni mwa Ishara za Allaah; kwa hao mnapata khayr nyingi. Basi tajeni Jina la Allaah juu yao wanapopangwa safu (kuchinjwa). Na waangukapo ubavu, basi kuleni kutoka humo, na lisheni waliokinai na wanaolazimika kuomba. Hivyo ndivyo Tulivyowatiisha kwa ajili yenu ili mpate kushukuru.

 

لَن يَنَالَ اللَّـهَ لُحُومُهَا وَلَا دِمَاؤُهَا وَلَـٰكِن يَنَالُهُ التَّقْوَىٰ مِنكُمْ ۚ كَذَٰلِكَ سَخَّرَهَا لَكُمْ لِتُكَبِّرُوا اللَّـهَ عَلَىٰ مَا هَدَاكُمْ ۗ وَبَشِّرِ الْمُحْسِنِينَ ﴿٣٧﴾

37. Haimfikii Allaah nyama zake wala damu yake, lakini inamfikia taqwa kutoka kwenu. Hivyo ndivyo Tulivyowatiisha kwenu ili mpate kumtukuza Allaah; Allaahu Akbar, kwa yale Aliyokuongozeni; na wabashirie wafanyao ihsaan.

  [Al-Hajj: 36-37]

 

 

Hukmu Za Hali Ya Mnyama 

 

Umri Wake:                            

 

Kondoo wawe ni kondoo ambao wamekamilisha umri wa mwaka mmoja takriban. Mbuzi wawe wamekamilisha umri wa mwaka mmoja na kuingia mwaka wa pili. Ngamia wawe wamekamilisha umri wa miaka minne na kuingia wa tano. Ng'ombe wawe wamekamilisha miaka miwili na kuingia mwaka wa tatu, kama alivyosema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

((لا تذبحوا إلا مسنة إلا أن تعسر عليكم فتذبحوا جذعة من الضأن)) رواه مسلم

((Msichinjie ila mnyama mwenye makamo isipokuwa ikiwa ni shida kwenu, hivyo mchinje kondoo (japo wa chini ya umri wa mwaka lakini awe zaidi ya umri wa miezi sita)) [Muslim] 

 

Usalama Wake:

 

Asiwe na kasoro yoyote kwani Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi   wa aalihi wa sallam) amesema:

 

((أربع لا تجوز في الأضاحي: العوراء البيّن عورها، والمريضة البيّن مرضها،  والعرجاء  البيّن ظلعها،  والعجفاء  التي لا تنقي))  

((Mambo manne (kasoro nne) hayapasi katika kuchinja; mwenye jicho chongo lenye kudhihirika, mnyama mgonjwa mwenye kudhihirika ugonjwa wake, kilema mwenye kudhihirika kuchechemea kwake na aliyedhoofika ambaye hana nyama katika mifupa yake)) [Swahiyh Al-Jaami']  

 

 

Wakati Wa Kuchinja:

 

Kuchinja asubuhi ya siku ya 'Iyd baada ya Swalaah. Hairuhusiwi kuchinja kabla ya Swalaah kama alivyosema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

حديث أنس  رضي الله عنه- قال: قال رسول الله -صلى الله عليه وسلم: ((من ذبح قبل الصلاة فإنما ذبح لنفسه، ومن ذبح بعد الصلاة فقد تم نسكه وأصاب سنة المسلمين)) البخاري ومسلم

Kutoka kwa Anas (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayechinja kabla ya Swalaah atakuwa amejichinjia kwa ajili yake mwenyewe. Na Atakayechinja baada ya Swalaah atakamilisha kafara (kichinjo) yake na atapata   (atatekeleza) Sunnah ya Waislam)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Anaweza kuchinja siku ya pili ya 'Iyd au kuchelewesha hadi siku ya mwisho ya Ayyaamut-Tashriyq (siku za Tashriyq) ambayo ni siku ya kumi na tatu Dhul-Hijjah.     

      

  (... وفي كل أيام التشريق ذبح))  

((...siku zote za Tashriyq ni siku za kuchinja)) [Ahmad]

 

 

Yanayopendekezeka  Katika Kuchinja:

 

Kumpwekesha Allaah:

 

Inapendekezeka kumuelekeza mnyama Qiblah wakati wa kumchinja na kusema:

  

((بسم الله والله اكبر، اللهم هذا منك ولك))

((BismiLLaah, wa Allaahu Akbar, Ee Allaah hii ni kutoka Kwako na kwa ajili Yako))

 

 

Kuchinja mwenyewe ni bora zaidi:

 

Inapendekezeka Muislamu achinje mwenyewe na akimuwakilisha mtu kumchinjia pia inaruhusiwa hakuna ikhtilaaf katika jambo hili baina ya 'Ulamaa.   

 

 

Kugawa Nyama:

 

Inapendekeza kuigawa nyama kwanza kwa familia yake, na pia kuwagawia swadaqah masikini,   majirani, marafiki, n.k. kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'alaa):

 

لِّيَشْهَدُوا مَنَافِعَ لَهُمْ وَيَذْكُرُوا اسْمَ اللَّـهِ فِي أَيَّامٍ مَّعْلُومَاتٍ عَلَىٰ مَا رَزَقَهُم مِّن بَهِيمَةِ الْأَنْعَامِ ۖ فَكُلُوا مِنْهَا وَأَطْعِمُوا الْبَائِسَ الْفَقِيرَ ﴿٢٨﴾

28. Ili washuhudie manufaa yao; na walitaje Jina la Allaah katika siku maalumu kwa yale Aliyowaruzuku kati ya wanyama wenye miguu minne wa mifugo. Basi kuleni humo, na lisheni mwenye shida fakiri.  [Al-Hajj: 28]

 

وَالْبُدْنَ جَعَلْنَاهَا لَكُم مِّن شَعَائِرِ اللَّـهِ لَكُمْ فِيهَا خَيْرٌ ۖ فَاذْكُرُوا اسْمَ اللَّـهِ عَلَيْهَا صَوَافَّ ۖ فَإِذَا وَجَبَتْ جُنُوبُهَا فَكُلُوا مِنْهَا وَأَطْعِمُوا الْقَانِعَ وَالْمُعْتَرَّ ۚ

36. Na ngamia na ng’ombe Tumekufanyieni kuwa ni miongoni mwa Ishara za Allaah; kwa hao mnapata khayr nyingi. Basi tajeni Jina la Allaah juu yao wanapopangwa safu (kuchinjwa). Na waangukapo ubavu, basi kuleni kutoka humo, na lisheni waliokinai na wanaolazimika kuomba. [Al-Hajj: 36]

 

Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)

((كلوا وأطعموا وادخروا)). رواه البخاري

((Kuleni, lisheni na mbakishe [akiba])) [Al-Bukhaariy]

 

Na usemi mwengine kutoka kwa Muslim kutoka kwa mama wa Waumini 'Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa):

 

عن عائشة رضي الله عنها أن النبي صلى الله عليه وسلّم قال: ((كلوا وادخروا وتصدقوا)) رواه مسلم.

 ((Kuleni, bakisheni na mtoe swadaqah)) [Muslim]

 

Inaruhusiwa pia kuigawa nyama yote swadaqah na Inaruhusiwa kubakisha sehemu.  

 

 

Haifai Kumpa Chochote Katika Nyama Mchinjaji Kama Ni Ujira:

 

Hairuhusiwi kumlipa mchinjaji aliyewakilishwa kuchinja baadhi ya nyama kama ujira wake kutokana na Hadiyth ifuatayo: 

 

عن علي قال‏:‏ أمرني رسول الله صلى الله عليه وسلم أن أقوم على بدنه وأن  أتصدق بلحومها وجلدها وأجلتها ‏(‏وأجلتها‏:‏ أي لباسها الذي يقيها البرد‏)  وأن لا أعطي الجزار منها شيئا، وقال‏:‏ نعطيه من عندنا‏.

Kutoka kwa 'Aliy (Radhwiya Allaahu 'anhu): "Rasuli wa Alllaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliniamrisha kuchinja? Na kutoa nyama, ngozi na kile kinachomfunika kumhifadhi na baridi kuvitolea swadaqah na nisimpe chochote katika nyama hiyo. ((Tutampa kitu tulichonacho)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Ufafanuzi Zaidi:

 

Ukichinja AL-HADYI, mchinjaji hapewi katika nyama alioichinja lakini anapewa ujira wake. AL-HADYI ni kuchinja na wewe upo katika Hajj.

 

Ukichinja UDHWHIYAH, mchinjaji anaweza akapewa katika nyama hiyo aliyoichinja kama swadaqah ikiwa ni masikini. UDHWHIYAH ni kichinjo kwa wale wasiokuwa katika Hajj. Walio katika Hajj kichinjo kinaitwa AL-HADYI. 

 

 

Mnyama Mmoja Anatosheleza Familia Nzima:

 

Kuchinja mnyama mmoja anatosheleza katika kila familia japo kama kuna watu wengi katika familia kutokana na kauli ya:

  أبي أيوب -رضي الله عنه- لما سئل: كيف كانت الضحايا على عهد رسول الله؟  فقال: "كان الرجل يضحي بالشاة عنه وعن أهل بيته"  (الترمذي)

Abuu Ayyuwb (Radhwiya Allaahu 'anhu) alipoulizwa: "Uchinjaji ulikuwa vipi zama za Rasuli wa Allaah?" Akajibu: "Mtu alikuwa anachinja kondoo mmoja kwa ajili yake na familia yake" [At-Trimidhiy]

 

Yanayompasa Kufanya  Mwenye Kutaka Kuchinja:

 

Baada ya kutia Niyyah ya kuchinja, asikate mtu nywele wala kucha mpaka amalize kuchinja kama tulivyoamrishwa katika

Hadiyth ifuatayo:

 

عن أم سلمة رضي الله عنها، أن النبي صلى الله عليه وسلم قال:  ((إذا رأيتم هلال ذي الحجة وأراد أحدكـم أن يضحّي فليمسك عــن شعره وأظفاره))  ، وفي راوية (( فلا يأخذ من شعره ولا من أظفـاره حتى يضحّي  )) مسلم

Imetoka kwa Ummu Salamah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:  ((Ukiandama mwezi wa Dhul-Hijjah na ikiwa  yuko anayetaka kuchinja basi azuie (asikate) nywele zake na kucha zake)).

 

Na katika riwaya nyingine ((Asikate nywele wala kucha mpaka atakapomaliza kuchinja)) [Muslim na wengineo]

 

 

Mwenye Uwezo Wa Kuchinja Zaidi Ya Mmoja:

 

Mwenye uwezo wa kuchinja zaidi ya mmoja na akipenda achinje kama alivyochinja Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa ajili ya Ummah wa Kiislam wote. Hivyo Muislam asiye na uwezo wa kuchinja naye atapata fadhila hizi za kuchinja, naye mchinjaji atachuma thawabu za Waislam wote wasio na uwezo. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alifanya hivyo:

وعن أبي رافع رضي الله عنه «أن النبي صلى لله عليه وسلّم كان يضحي  بكبشين أحدهما عنه وعن آله، والاخر عن أمته جميعاً»، رواه أحمد

Kutoka ka Abuu Raafi' (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba: Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akichinja kondoo wawili; mmoja kwa ajili yake na familia yake na wa mwengine kwa ajili ya Ummah wake wote)) [Ahmad]

 

Kutoka kwa Jaabir kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa akichinja kwa ajili ya Ummah akisema:

 (( بسم الله والله أكبر. اللهم هذا عني وعمن لم يضح من أمتي)) رواه أحمد وأبو داود والترمذي.

((BismiLLaah, wa Allaahu Akbar, Ee Allaah hii kwa ajili yangu na kwa ajili ya wasio na uwezo katika Ummah wangu)) [Ahmad, Abu Daawuud na At-Tirmidhiy]

 

Wa BiLLaahi at-Tawfiyq

 

  

Share