Niyyah: Vipi Kutia Niyyah Ya 'Ibaadah Kama Swawm?

 

 

Vipi Kutia Niyyah Ya 'Ibaadah Kama Swawm?

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

 

tunatakiwa tufunge sunna mbali mbali kamav vile sunna za jumatatu na alkhamis hususa kwale mabarubaru ili kupunguza matamanio ya nafsi pamoja na kumcha Allah.vJe katika funga kama hizo za jumatatu na alkhamis tunatakiwa tunuie vipi? Naomba nia yake kwa matmshi ya kwiswahili

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Niyyah ni muhimi katika ‘ibaadah yoyote na hakuna ikhtilaaf baina ya ‘Ulamaa kuhusu hili. Na hii ni rai ya Imaam Maalik, Ahmad ibn Hanbal na Abu Daawuwd kwa kutoa dalili ya Aayah:

 

وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاءَ وَيُقِيمُوا الصَّلَاةَ وَيُؤْتُوا الزَّكَاةَۚ وَذَٰلِكَ دِينُ الْقَيِّمَةِ ﴿٥﴾

Na hawakuamrishwa isipokuwa wamwabudu Allaah wenye kumtakasia Dini, wenye kujiengua na upotofu kuelemea Dini ya haki na wasimamishe Swalaah na watoe Zakaah; na hiyo ndiyo Dini iliyosimama imara.  [Al-Bayyinah: 5]

 

 

 

 

 

Kumaubudu Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Pekee kwa ikhlaasw ni ‘amali ya  moyo, nayo nido niyyah  na amri katika Aayah hiyo inaonyesha kuwa ni fardhi.

 

 

Vile vile katika Sunnah, Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema katika Haidiyth:

 

((إِنَّما الأَعْمَالُ بالنِّيَّاتِ وإنَّما لكُلِّ امْرِىءٍ ما نَوَى))  البخاري  و مسلم

((Matendo  yanategemea (yanalipwa kwa) niyyah na kila mtu atapata kwa mujibu wa kile alichokinuwia)) [Al-Bukhaariy na Muslim].

 

 

Lakini inapasa kutambua kwamba niyyah ya ‘ibaadah yoyote kama ni kujitia twahara, wudhuu, tayammum, Swalaah, Swawm, kutoa Zakaah na kadhalika haitamkwi kwa sauti bali huwekwa moyoni.

 

 

Niyyah inaunganika na elimu. Ikiwa mtu anajua anachotaka kufanya basi tayari niyyah yake imeshaingia moyoni.

 

Kuitamka kwa sauti itakuwa sio kufuata mwendo wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wala si mwendo wa Maswahaba zake, kwa hiyo kuitamka kwa sauti itakuwa ni bid'ah (uzushi).  Na kama ingelikuwa ni jambo lililokuwepo katika Shariy’ah, basi Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) angeliwafundisha Maswahaba zake na mafunzo hayo yangelitufikia sisi pia kwani

 

Niyyah ni jambo ambalo lina uhusiano na kila ‘ibaadah ya Ummah huu; mchana na usiku kwa hiyo ingelikuwa ni muhimu kutaja kwa sauti asingeliacha kutoa mafunzo. 

 

Kutamka niyyah kwa sauti ni jambo lisokuwa na mantiki, kwani  mtu anapotaka kufanya jambo la kawaida huwa hasemi kwa sauti kuwa "mimi nataka kufanya jambo fulani", bali hutia niyyah yake moyoni na kujitayarisha kwa kila njia na wakati maalum hadi atimize jambo lake. Kwa mfano mtu anapotaka kutoka nyumbani kwake na tuseme yuko peke yake, basi hatosema kwa sauti kuwa: “Mimi natoka kwenda kwa Fulani." Au "Natoka kwenda mahali Fulani." Na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ana mifano bora zaidi.

 

Tutatumbue kuwa jambo hili limejulikana sana kutokana na mafunzo yasiyo sahihi tuliyoyapata kutoka kwa wazazi wetu au waalimu kwamba niyyah hutajwa kwa sauti. Kama mfano tunapotaka kuswali mtu hutia niyyah kwa sauti kwa kusema: "Nawaytu fardha Swalaat Adh-Dhwuhr Arba'a Raka’aat…." na kadhalika. Na kwa wengi wetu tunapoambiwa kinyume na hivyo hushangaa na hata kwa wengine huwa ni vigumu kukubali mafunzo sahihi. Kuna baadhi ya watu wanaona wasipokwenda msikitini mwezi wa Ramadhwaan kunuizwa na Imaam “Nawaytu Swawma Ghadin...” basi wanaamini kuwa kesho hawana Swawm kwa kukosa kunuizwa siku hiyo!! Huo ni ujahili wa Dini, na ni jambo ambalo linatakiwa liachwe lisizidi kupoteza wengi maskini wasio na elimu ya Dini yao.

 

Basi inampasa Muislamu aliyezoea kuweka niyyah kwa sauti ajirekebishe na kuweka niyyah moyoni katika ‘ibaadah zake zote, kutokana na mafunzo haya sahihi tunayoyaeleza pamoja na dalili zake.

 

Bonyeza viungo vifuatavyo kwa faida zaidi:

Imaam Ibn 'Uthaymiyn: Kutamka Niyyah Katika ‘Ibaadah Ni Bid’ah Bali Mahali Pake Ni Moyoni

Imaam Ibn Taymiyyah: Kutamka Niyyah Katika ‘Ibaadah Ni Upungufuu Katika Akili Na Dini

17-Imaam Ibn ‘Uthaymiyn: Je, Inafaaa Swiyaam Za Sunnah Bila Ya Kutanguliza Niyyah?

Vipi kutia Niyyah Swalaah za Sunnah?

Vipi Kutia Niyyah Swalaah Za Qiyaamul-Layl?

Imefika Mchana Akaamua Kufunga Sunnah Bila Kuweka Niyyah Kabla, Inasihi?

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share