Ramadhwaan: Uzushi Wa Swalaah Makhsusi Za Siku Kumi La Mwisho Wa Ramadhwaan

 

 

Uzushi Wa Swalaah Makhsusi Za Siku Kumi La Mwisho Wa Ramadhaan

www.alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Assalam allaykum warahmatullahi
Kwanza napenda kuwapongeza wote wanaoshiriki katika kazi hii ya kuelimisha umma wa kiislam hasa kwa sisi ambao tuko kwenye nchi hizi za kimagharibi . Ahsanteni sana na allah atawajaza majazo mema leo duniani na kesho akhera. Suali langu ni hili tokea kukaribia kumi la mwisho la mwezi huu mtukufu wa ramadhan nimekuwa napokea email kutoka watu mbali mbali zinazoelezea kuhusu sala ya laylatul Qadri ambayo husaliwa  kwa rakaa zaidi ya kumi na moja pamoja sura zake maalum  kwa kila siku (yaani kila siku na sura zake maalum) kwa mfano kuna siku usome sura zinazoanza na haa mim na nyenginezo pia ikiwemo salatul tasbihi. hivyo naomba nasaha zenu watu wa alhidaaya kwani tumo ndani utata mkubwa waislam. Assalam alaykum warahmatullhi

Barua yenyewe ni hii:

ASSALAM ALAYKUM,
NDUGU ZANGU WAISLAM NAWAOMBA TUFANYE BIDII NA JITIHADA NA KUHAKIKISHA
KILA MMOJA WETU ANATEKELEZA SALA HII PINDI HALI IKIMRUHUSU, INSHAALLAH.

TAREHE 21 USIKU - MWEZI WA RAMADHANI
a) USIKU WA TAREHE 21 SALI RAKAA 4, TOA SALAM KILA BAADA YA RAKAA 2. KILA RAKAA SOMA SURAT FAT-HA x 1, AL-QADIR x 1 NA IKHLAS x 1 UKIMALIZA MSALIE MTUME (S.A.W) x 70.
b) USIKU HUO HUO - SALI RAKAA 2, KILA RAKAA SOMA SURAT FAT-HA x 1,
AL-QADIR x 1 NA IKHLAS x 3. BAADA YA SALAM VUTA URADI
UFUATAO:
"ASTAGHGIRULLAHI LLADHI LAILAHA ILLA HUWA
WAATUBU ILAYHI" x 70.
c) VILE VILE USIKU HUO HUO WA TAREHE 21 SOMA SURAT QADR x 21.

 USIKU WA TAREHE 23 - MWEZI WA RAMADHANI

a) SALI RAKAA 4(MBILI MBILI), KILA RAKAA SOMA SURAT FAT-HA x 1,
AL-QADIR x 1 NA IKHLAS x 1. BAADA YA SALAM MSALIE MTUME (S.A.W) x 70.
b) USIKU HUO HUO - SALI RAKAA 8 (MBILI MBILI), KILA RAKAA SOMA SURAT FAT-HA x 1, AL- QADIR x 1 NA IKHLAS x 1. UKIMALIZA VUTA URADI UFUATAO:
"SUB-HANA LLAHA WALHAMDULLILLAHI WALAILAHA ILLALLAHU WALLAHU AKBARU" x 70.
c) VILE VILE USIKU HUO HUO WA TAREHE 21 SOMA SURAT YASEEN x 1 NA ARRAHMAN x 1.
 
USIKU WA TAREHE 25 - MWEZI WA RAMADHANI
a) SALI RAKAA 4 (MBILI MBILI), KILA RAKAA SOMA SURAT FAT-HA x 1,
AL-QADIR x 3 NA IKHLAS x 3. BAADA YA SALAM LETE ISTIGHFARA
"ASTAGHFIRULLAHI LLADHI LAILAHA ILLA HUWA WAATUBU ILAYHI" x 70.
(Sala hii ni nzuri kwa kusamehewa dhambi zako).
b) USIKU HUO HUO - SALI RAKAA 2, KILA RAKAA SOMA SURAT FAT-HA x 1,
AL- QADIR x 1 NA IKHLAS x 15. UKIMALIZA SOMA "LAILAHA ILLALLAH MUHAMMAD RASULULLAH" 
c) VILE VILE USIKU HUO HUO WA TAREHE 25 SOMA SURAT DUKHAN x 7
UNAEPUSHWA NA ADHABU YA KABURINI. VILE VILE SOMA SURAT FAT-HA x 7.

 USIKU WA TAREHE 27 - MWEZI WA RAMADHANI

 a) SALI RAKAA 4 (MBILI MBILI), KILA RAKAA SOMA SURAT FAT-HA x 1,
AL-QADIR x 3 NA IKHLAS x 50. BAADA YA KUTOA SALAM SUJUDU NA USOME:
 SUB-HANA LLAHA WALHAMDULLILLAHI WALAILAHA ILLALLAHU WALLAHU AKBARU.
Kisha omba haja zako kwa Mola wako (yeye ndie mtoaji).
 b) USIKU HUO HUO SOMA SURA SABA (7) ZENYE KUANZA NA "HAAMMIIM". PIA
SOMA SURAT "MULK"x 7.

SALAT TAS-BIHI.
VIZURI KUSALIWA MWEZI WA RAMADHAN NA HASA TAREHE 26.

KUMI LA MWISHO LA RAMADHAN:

a) KILA SIKU SOMA "LAILAHA ILLA-LLAH SADIQAN LAILATUL QADR".
b) VILE VILE KATIKA KUMI HILI KILA SIKU BAADA YA SALA YA ISHAA SOMA
SURAT
QADR x 7.
 
IJUMAA LA MWISHO WA MWEZI WA RAMADHANI KABLA YA SALA YA ADHUHURI SOMA
SURAT QADR x 3.

 1. BAADA YA SALA YA ADHUHURI/IJUMAA SALI RAKAA 2:
RAKAA YA KWANZA SOMA SURAT FAT-HA x 1, IKHLAS x 10,
ZULZILAT x 1.
RAKAA YA PILI SOMA SURAT FAT-HA x 1, ALKAFIRUN x 3. BAADA YA SALAM
MSALIE MTUME (SAW) x 10, BAADAE
 2. SALI RAKAA 2 NYENGINE:
RAKAA YA KWANZA SOMA SURAT FAT-HA x 1, TAKATHUR x 1, IKHLAS x 10.
RAKAA YA PILI SOMA SURAT FAT-HA x 1, AYATUL KURSIYYU x 3, IKHLAS x 25
(Thawabu za sala hii zinaendelea
mpaka siku ya kiama).
 
NDUGU MUISLAM, TUPATE NINI TENA KUTOKA KWA MOLA WETU, KILA YA NJIA YA KUJJIPATIA MEMA AMETUWEKEA.
 
MTUMIE NA MUISLAM MWENZIO IKIWA NI MWENYE KUAMINI NA MWENYE IMANI YA
KWELI.WAALAYKUM SSALAAM.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Hakika ndugu Waislamu, kutokana mitandao ya jamii siku hizi uzushi mwingi umekuwa unarushwa na kuwafikia Waislamu wengi ambao nao bila ya kujua wanapata mafunzo yasiyo sahihi, nao wanawatumia wenzao, hivyo hivyo inaendelea hadi kuwafikia maelfu wa Waislamu.

 

Yafutayo ni maelezo tunayowatahadhirsha ndugu zetu wote kuhusu ujumbe huu:

 

 

1-Si Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) bali ni maneno yaliyopangwa na baadhi ya watu.  

 

2-Ibada yoyote ile kwa mpangilio wa idadi na namba, inahitaji ushahidi na dalili. Zikikosekana basi inatupasa kuziacha na kutozifanyia kazi.

 

3-Ujumbe kama huo unaorushwa hakika unwashughulisha sana Waislam na wengi wakihadaika wakidhani ni mambo ya Dini na hali ni mambo yasiyokuwepo na yaliyotungwa tu na watu.

 

4-Inawasababisha pia Waislam kukosa kheri na fadhila za kufanya ibada zilizothibiti zenye dalili ambazo zingewaongezea ujira mkubwa haswa katika masiku haya matukufu ambayo tumesisitizwa sana kuongeza juhudi katika ibada.

 

Tunatoa nasaha kwa ndugu zetu katika Iymaan musiwe na haraka ya kueneza mambo ambayo yanadhaniwa ni Hadiyth au mafunzo ya Dini na hali ni utungo tu kutoka kwa wasio na kazi ila kuwashughulisha watu na kuwapotezea muda wao kwa mambo ambayo hayawezi kuwapatia ujira bali watarudishiwa wao na kutopata kitu zaidi ya kupoteza muda. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kapinga hilo sana na kalikemea vikali pale aliposema:

(Mwenye Kuzusha jambo katika DINI yetu hii, basi litarejeshwa kwake) [Al-Bukhaariy na Muslim]. Yaani hatopata kitu zaidi ya kuua muda wake na kujichosha bure!

 

Tujihadhari na ujumbe tupatazo kwenye mitandao ya kijamii kwani nyingi huwa ni za kutungwa jambo ambalo ametukaza nalo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

((من كذب علي متعمدا فليتبوأ مقعده من النار)) متفق عليه

((Atakayeniongopea makusudi basi ajitayarishie makazi yake motoni))  [Al-Bukhaariy Na Muslim]

 

Tunawaomba ndugu zetu msome makala muhimu zifuatazo ambazo zina maelezo mengi kuhusu hatari ya kusambaza uzushi, ili kila mmoja wetu ajiepushe na uovu huo:

Bonyeza hapa:

 

Waislam Tuache Kumzulia Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa ‘Aalihi Wa Sallam) Uongo

 

Hatari Ya Kueneza Hadiyth Dhaifu Na Visa Vya Uongo

 

Mwenye Kufanya Na Kuelimisha Sunnah Nzuri Katika Uislam Na Mwenye Kuelimisha Uzushi

 

Uzushi Wa Swalah Za Usiku

 

Tambueni kuwa ujumbe wowote unaoonekana wa kidini kama huo ni kujiepusha nao kwa sababu  hauna dalili, wala ushahidi kuliposemwa maneno hayo, nani kasema? Wapi kasema? Nani kapokea, Vitabu gani n.k!

 

Madhara makubwa huwafikia Waislamu kuupokea ujumbe kama huo kwani utakuwa wangapi wameshaanza kuuhifadhi na kuusoma na kuufanyia kazi kwa kuswali Swalah hizo na kuacha kuswali Swalah zilizothibiti, au kusoma Qur-aan na mengine yenye ushahidi.

 

Makala zifuatazo ni ambazo zinapasa kufanyiwa kazi masikku kumi haya matukufu.

 

Laylatul-Qadr- Vipi Uweze Kuupata Usiku Huu?

 

Siku Kumi Za Mwisho Za Ramadhwaan

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share