Waislam Tuache Kumzulia Uongo Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)

 

Abu Faatwimah

 

Assalamu 'alaykum,

Ndugu Waislam,

E mail yoyote ile yenye kusema kama hivi ‘Read if you are muslim’ na namna hii ni vyema usiisome wala usiitume kwa mtu kwani yaliyomo ndani mara nyingi huwa ni mambo yenye kwenda kinyume na mafundisho ya Mtume Muhammad (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam), au ni uzushi au uwongo unaotungwa na waongo kutaka kuwaharibia Waislamu Dini yao na kuwapoteza na mafundisho sahihi ya Dini yao, hivyo ni vyema ui-delete na umnasihi mwenye kawaida ya kukutumia e mail kama hizo kuwa ndoto ni jambo linalomuhusu mwenye kuota na sio mwengine katika sisi, na kama ndoto ni njema/nzuri basi anachotakiwa ni kumuomba Allaah Amuwafikishe akipate hicho alichokiota kama ni kizuri na kama kinyume chake basi amuombe Allaah Amuepushe na shari hiyo na amkinge.

Sasa na tuingie ndani ya habari inayotakiwa isomwe kama sisi ni Waislamu na itumwe kwa wengine ili mambo yetu yawe mazuri yatengenekee.

 

DONT DELETE! IF YO ARE A MUSLIM! PLEASE READ THIS!

 

Wapi tunatakiwa au tunapendekezewa kutumia matamshi (tishio) kama,

 IF YOU ARE A MUSLIM!

 

Ukiwa na urafiki/ushoga na Qur-aan itakushika mkono na kuudhibiti mdomo wako na kukupelekea kwa tawfiki yake Mola kutumia  matamshi kwa munasaba wake sio kuyatupa kama mtoto anayejifundisha kusema, matamshi kama haya IF YO ARE A MUSLIM! pahala pake ni kama hapa:

 

KAMA WEWE MUISLAMU BASI MBONA HUSWALI!

KAMA WEWE MUISLAMU BASI MBONA HUSOMI QUR-AAN!

KAMA WEWE MUISLAMU BASI MBONA HUVAI HIJABU AU MKEO MBONA HAVAI!

 

Angalia kwa utulivu wapi Qur-aan imetumia tamshi IF YO ARE A MUSLIM!

 

Qur-aan inasema:"Na wasipokuitikieni, basi jueni ya kwamba (hii Qur-aan) imeteremshwa kwa ujuzi wa Allaah, na kwamba hapana mungu ila Yeye. Basi je! Nyinyi ni Waislamu?" Suurat Huud aya ya 14,

Pia Qur-aan inasema:

"Na Muusa alisema: Enyi watu wangu! Ikiwa nyinyi mmemuamini Allaah, basi mtegemeeni Yeye, ikiwa nyinyi ni Waislamu." Yuunus, aya ya 84. 

 

From Madina Sheikh Ahmed fell asleep reading the Quraan.

 

Tunatakiwa tuisome Qur-aan tukiwa na uchangamfu na ukihisi machofu au kama umechoka basi usiisome kwani hutokuwa unaisoma, na kama mpaka ikapelekea kufikia kusinzia wachilia mbali kulala mpaka ukaota basi ulikuwa huisomi Qur-aan, ulikuwa unapoteza wakati au unapitisha wakati au unatafuta usingizi kwa matatizo yako ya kutopata usingizi, kwani Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam), hakupata kusoma Qur-aan mpaka akashikwa na usingizi au akaota, kwa hiyo sheikh huyu alikuwa hasomi Qur-aan alikuwa akitafuta usingizi. 

 

Then he dreamt the Prophet Muhammed (saw) standing in front of him

 

Tunataikiwa tuelewe kuwa al-Habiyb Muhammad (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) anaonekanwa katika ndoto, lakini si kwa kila mtu hasa watu kama hawa wenye kutafuta usingizi kwa kuisoma Qur-aan, hawawezi kumuota al-Habiyb Muhammad (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam), wenye kujaaliwa kumuona al-Habiyb Muhammad (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) ni wale wenye kushikamana na mafundisho yake na sio kusambaza na kueneza uwongo au uzushi au mambo kama haya yasiyo kuwa na asili katika Uislam.  Hivyo ndoto ya jisheikh letu ni ndoto ya ndaria na simulizi za watu wa kale na wenye kupenda kuonekanwa wanasikilizwa katika jamii. 

 

Ndoto huwa amri kwa Mitume (‘Alayhimus Salaam) kama ilivyothibiti na kuja katika Qur-aan: 

"Basi alipofika makamo ya kwenda na kurudi pamoja naye, alimwambia: Ewe mwanangu! Hakika mimi nimeona usingizini kuwa ninakuchinja. Basi angalia wewe, waonaje? Akasema: Ewe baba yangu! Tenda unavyoamrishwa, utanikuta mimi, InshaAllaah, katika wanao subiri. Basi wote wawili walipojisalimisha, na akamlaza juu ya kipaji. Tulimwita: Ewe Ibraahiym! Umekwishaitimiliza ndoto. Hakika hivi ndivyo tunavyowalipa wanaotenda mema. Hakika haya ni majaribio yaliyo dhaahiri. Basi tukamtolea fidia kwa dhabihu mtukufu. Na tukamwachia (sifa njema) kwa watu waliokuja baadaye. Iwe salama kwa Ibraahiym! Hivi ndivyo tunavyowalipa wanaofanya mema. Hakika yeye ni katika waja wetu walioamini" Asw-Swaaffaat, aya ya 102-111,

Pia Qur-aan inasema:

"Hakika Allaah Amemtimizia Mtume wake ndoto ya haki. Bila ya shaka nyinyi mtauingia Msikiti Mtakatifu, InshaAllaah, kwa amani, na hali mmenyoa vichwa vyenu na mmepunguza nywele. Hamtakuwa na khofu. Yeye Anajua msiyoyajua. Basi Atakupeni kabla ya haya Ushindi karibuni." Al-Fat-h, aya ya 27.  

 

Na si kila mwenye kuota ana uwezo wa kuaguwa ndoto yake na pia si kila mtu ana ujuzi huo, ndio Qur-aan ikatupa habari za ndoto na waaguzi wake huwa watu wa namna gani? Qur-aan inasema:

 

"Wakaingia gerezani pamoja naye vijana wawili. Mmoja wao akasema: Hakika mimi nimeota nakamua mvinyo. Na mwingine akasema: Mimi nimeota nimebeba mikate juu ya kichwa changu, na ndege wanaila. Hebu tuambie tafsiri yake, kwani sisi tunakuona wewe ni katika watu wema. Akasema: Hakitakufikilieni chakula mtakachopewa ila nitakwambieni hakika yake kabla hakijakufikieni. Haya ni katika yale Aliyonifundisha Mola wangu Mlezi. Hakika mimi nimeacha mila ya watu wasiomuamini Allaah, na wakawa hawaiamini Akhera." Yuusuf, aya ya 36-37.  

 

Kila mtu huota lakini muaguzi wa ndoto ni lazima awe mtu mwenye sifa maalumu, awe mtu mwenye kushikamana na mafundisho aliyokuja nayo al-Habiyb Muhammad (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) ili aweze kufikishwa kwa tawfiki yake Mola kuweza kuaguwa ndoto za waotaji, na sio biashara ya kujipatia fedha au umaarufu, ama aliye mbali na mafundisho kama mwenye kutafuta usingizi na njia aliyoiona ni kusoma akaamua kuisoma Qur-aan ili apate kulala huyo ndoto yake haina athari wala umuhimu wo wote ule katika Uislam na waislamu pia. 

 

The Prophet said whoever reads this news to someone else, 'I WILL ON THE DAY OF JUDGEMENT MAKE HIM A PLACE IN PARADISE, AND IF SOMEONE DOES NOT BELIEVE THIS NEWS TO BE TRUE THEY WILL BE BANISHED FROM Paradise!'If a poor person gives out this news to other people his/her good wish Will come true.  

 

Huku hasa ndiko kumzulia uongo al-Habiyb Muhammad (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) kwa makusudi, na mwenye kumzulia uongo kama huyu anajipalilia na kujitengezea pahala pake Motoni sio kwengineko.  Wapi kumepokea habari hii katika vita vyote vya Hadiyth, wapi kumepatikanwa simulizi hii katika vitabu vyema kushikamana na mafundisho ya al-Habiyb Muhammad (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam). 

 

'I WILL ON THE DAY OF JUDGEMENT MAKE HIM A PLACE IN PARADISE........

The Prophet said 'KEEP FAST, DO PRAYERS, GIVE ZAKAAT AND GIVE KINDNESS TO THE POOR'  

 

Al-Habiyb Muhammad (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) haelewi nini atafanywa yeye! vipi atakuwa na uwezo wa kumpa mtu Jannah, yeye al-Habiyb Muhammad (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) ameletwa awe Muonyaji na Mtoa habari njema na sio kuwatengea watu sehemu katika Pepo, Pepo ni ya Allaah na Humtunuku Amtakae na wa mwanzo katika hao ni yule aliyeshikamana na mafundisho aliyokuja nayo al-Habiyb Muhammad (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) na sio anayemzulia uongo na kutaka uongo huo utanganzwe na usambazwe kwa wenye kumpenda na kumfuata al-Habiyb Muhammad (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam). 

 

AND

IF SOMEONE DOES NOT BELIEVE THIS NEWS TO BE TRUE THEY WILL BE BANISHED FROM Paradise!

 

Habari hii ni uongo tena anayezuliwa uongo huu ni yule aliyeletwa watu wamfuate na sio vyengine, msambazaji anataka watu waamini, habari ambayo ni uongo na mwenye kukataa kuiamini basi hatopata Pepo.  Uhakika na ukweli ni kuwa huu ni uongo, na baada ya kuelewa kuwa ni uzushi na uongo anaozuliwa al-Habiyb Muhammad (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) basi mwenye kuueneza huenda akawa anajitengenezea pahala Motoni na mwenye kushikamana nao huenda akakosa hiyo Pepo yenyewe, hivyo kuamini yasiyothibiti katika Uislamu na unayoelewa kuwa ni uongo ni kujikosesha Pepo.

 

'If a poor person gives out this news to other people his/her good wish Will come true.  

 

Maskini amekosa nini hata awe ndiye msambazaji wa habari za uongo, masikini wengi ndio wakaazi wa Peponi na ndio wengi wasiokuwa hata na internet na e mail zenye kupelekea mtu kueneza uongo na uzushi kama huu. Tajiri hana haja ya kueneza uongo kwani yeye kwa mtazamo wa jisheikh letu ni kuwa anachokisema huwa ni kweli ndio akawa hana haja ya wish zake kuwa kweli kwani yeye anacho kila akitakacho, na maskini anahitaji awe na kitu na ni mwenye kuota na kutamani, hivyo akitaka apate anayoyatamani asamabze uongo na uzushi kwa lengo la kuwaharibia na kujiharibia yeye mwenyewe fursa yake ya kuingia Peponi.  Ukitaka wish zako ziwe true basi kuwa mcha Mungu, Qur aaan inasema:

 

"...Na anayemcha Allaah Humtengezea njia ya kutokea.  Na Humruzuku kwa jiha asiotazamia. Na anayemtegemea Allaah Yeye Humtosha" At-Twalaaq, aya ya 2-3 pia inasema:

"…Hiyo ni amri ya Mwenyezi Mungu Amekuteremshieni. Na Anayemcha Mwenyezi Mungu Atamfutia maovu yake, na Atampa ujira mkubwa". At-Twalaaq, aya ya 5

Na mwisho inasema kuwa kama wewe kweli unataka wish zako ziwe true na ufanikiwe katika mambo yako yote, na kuwa wish kubwa anayotamani aipate Muislam ni Pepo, basi huna haja ya kuzua uongo wala kumzulia al-Habiyb Muhammad (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam), bali kuwa hivi:

"Mtume anayekusomeeni Aya za Allaah zinazobainisha, ili kuwatoa walioamini na wakatenda mema kutoka gizani kuwapeleka kwenye nuru. Na mwenye kumuamini Allaah, na akatenda mema, Atamwingiza katika Bustani zipitazo mito kati yake, wadumu humo milele. Allaah Amekwisha mpa riziki nzuri."
 At-Twalaaq aya ya 11.

 

Kupata Pepo ambayo inatafutwa na wenye hamu nayo katika mwezi huu wa Ramadhaan na hasa hasa katika siku kumi hizi za mwisho ndio wish kubwa kwa wenye akili, iman na kumtarajia Allaah na Siku ya Qiyaamah na wengi wao ni maskini Basi je! Nyinyi ni Waislamu?"  

 

Sheikh Ahmed said if this is not true then my death will Be off a Non-Muslim.  

 

Bila ya shaka wala wasi wasi wo wote ule hii habari sio kweli, haijathibiti kutoka kwa al-Habiyb Muhammad (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) hata kama kuna mambo ndani yake yenye kusisitizwa na Uislam, lakini habari hii ni uongo unaozuliwa al-Habiyb Muhammad (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam). Na kwanini tutumie uongo na tuzuwe katika kuwapendelezea watu mambo ambayo yamethibiti katika Hadiyth tena kwa matamshi mazuri yenye nuru na mwangaza.

 

my death will Be off a Non-Muslim Person

 

Muislam hatakiwi aombe, ajiombe wala awaombee wenzake kuwa wafe hali ya kuwa sio Muislam, ukiwa rafiki/shoga wa Qur-aan utaona nini ushauri wake katika kutafuta ukiwa uwe nani, Qur-aan inasema:

"Enyi mlio amini! Mcheni Allaah kama ipasavyo kumcha; wala msife ila nanyi ni Waislamu" Al-'Imraan aya ya 102

 

Pia unatutaka katika mambo ya kuusia watoto wetu tuige watu wema na waja wema, sio tuusie mali tu na mambo ya kimaajabu bali tuwausie kuwa wafanye wafanyavyo lakini wahakikishe kuwa wanakufa hali ya kuwa ni Waislamu, na huu ndio wasii wa Mitume kwa dhurriya wao, Qur-aan inasema:

"Na Ibraahiym akawausia wanawe, na pia Yaaqub: Enyi wanangu! Hakika Allaah amekuteulieni Dini hii; basi msife ila nanyi mmekuwa Waislamu, wanyenyekevu.   Je! Mlikuwapo yalipomfikia Yaaqub mauti, akawaambia wanawe: Mtamuabudu nani baada yangu? Wakasema: Tutamuabudu Mungu wako na Mungu wa baba zako, Ibraahiym na Ismaa’iyl na Is- haaq, Mungu Mmoja tu, na sisi tunasilimu kwake." Al-Baqarah, aya ya 132 -133.

 

Vipi utajiombea ufe kinyume na ushauri wa Qur-aan, na hata kama ikiwa habari ni ya kweli kama inavyodaiwa kuwa jisheikh letu la vitabuni alivyodai, basi hakuna haja ya kujiombea kufa hivyo, cha kufanya ni kumuomba Allaah Akuwafikishe kufuata yaliyothibiti na kuachana na uongo na uzushi tena uongo na uzushi unaozuliwa al-Habiyb Muhammad (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam).

 

Forward it to 40 people he had 8,000 thousand, take prophet in his Business.

 

Mwenye kutaka faida na kumea biashara yake basi ushauri wa Qur-aan ni huu:

"Mfano wa wanaotumia mali zao katika Njia ya Allaah ni kama mfano wa punje moja iliyochipuza mashuke saba. Katika kila shuke zimo punje mia. Na Allaah Humzidishia Amtakaye, na Allaah ni Mwenye wasaa na Mwenye kujua." Al-Baqarah, aya ya 26

Pia Qur-aan inasema:

"Enyi mlioamini! Nikuonyesheni biashara itakayokuokoeni na adhabu iliyo chungu? Muaminini Allaah na Mtume Wake, na piganeni Jihadi katika Njia ya Allaah kwa mali yenu na nafsi zenu. Haya ni bora kwenu, ikiwa nyinyi mnajua. Atakusameheni dhambi zenu, na Atakutieni katika Mabustani yapitiwayo na mito kati yake, na maskani nzuri nzuri katika Bustani za milele. Huko ndio kufuzu kukubwa.  Na kinginecho mkipendacho, nacho ni nusura itokayo kwa Allaah, na ushindi ulio karibu! Na wabashirieni Waumini!" as-Swaff, aya ya 10-13.

 

Whoever Forwards this will get his/her reward in three days.

 

Kuna Hadiyth nyingi kupita wingi wa habari wanazozisambaza wanomzulia al-Habiyb Muhammad (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) zenye kuonyesha kuwa ukitenda jambo utalipwa hivi na hivi au utapata hivi na hivi au utakuwa hivi na hivi na sio utapata malipo yako katika kipndi cha siku tatu!  Waislamu wanapotekeleza jambo huwa na Iymaan na matarajio ya kutunukiwa Alichonacho Mola na hicho sio baada ya siku tatu Allaahumma iwe shahada katika Jihaad amabyo yawezekana ikawa hata baada ya dakika tatu wachilia mbali siku tatu ama mengineyo ambayo Waislamu hujipendekeza kwa Mola ni kwa ajili yake Mola na ad-Daarul Aakhirah na sio vyengine. Hivyo malipo ya hapa dunia sio lengo kwa amali yoyote ile ya Muislam.

 

One Person did not believe this news and his son died. One kept Saying he will forward it today, tomorrow but never forward this News he died as well.  

 

Haya matamshi pekee yanathibisha na kubainisha kuwa muandishi au msambazaji hana 'Aqiydah /itikadi ya Kiislamu, sasa vipi mwenye 'Aqiydah sahihi asambaze jambo lenye kwenda kinyume na Dini yake na mafundisho ya al-Habiyb Muhammad (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam)! Mwenye kuamini au kuitakidi kuwa kifo chake au cha mtoto wake kimetokea kwa sababu fulani na sio kuwa Allaah Ndiye Mwenye kufisha na kuhuisha basi Uislamu wake una matatizo, na mwenye kuamini kuwa kama akifanya au kutofanya jambo fulani (kutosambaza uzushi na uongo kama huu) atapatwa na madhara ikiwemo kifo huyo si katika wenye kushikama na kufuata mafunzo na itikadi sahihi aliyokuja nayo al-Habiyb Muhammad (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam). Kitachokupata kimeshaandikwa kuwa kikupate na kisichokusibu hakiwezi kukusibu hata kama Majini na watu wote watashirikiana. Wino ushakauka na kalamu ishanyayuliwa. Hivyo ukifa ndio siku yako ishafika na sio jengine na akifa wako hali kadhalika.

 

Ndugu katika Iymaan, tuwe na tahadhari sana na kuanzia leo tuwekeni dhamira ya kupigana vita na e mails za namna hiyo zenye kumzulia Mtume wetu mpenzi na zenye kuwapotezea Waislam wakati wao mkubwa. Tuhakikishe tunaacha kueneza mambo yasiyo na dalili wala ushahidi katika Dini, na pindi tunapopata e mails kama hizo, tujibu haraka na kuwakanya wanaozituma na kuwanasihi inshaAllaah.

 

Tunamuomba Allaah Awahifadhi katika ‘Aqiydah sahihi na kuwatakabalia ‘amali zenu. Aamiyn

 

Share