Kisa Cha Aswhaabul-Kahf (Watu Wa Pangoni) Sehemu Ya 4

 

Imekusanywa Na: www.alhidaaya.com

 

Baada ya kumalizika kisa cha Asw-haabul-Kahf, Allaah (سبحانه وتعالى) Anaendelea kutupa mwanga na mfunzo kuhusu sababu ya kuteremshwa kisa hicho, pamoja na funzo muhimu kwa Muislamu kuhusu kusema ‘In Shaa Allaah pale anapotaka kutenda jambo la mustaqbal.

 

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى)

 

 

 وَلاَ تَقُولَنَّ لِشَيْءٍ إِنِّي فَاعِلٌ ذَلِكَ غَدًا .  إِلاَّ أَن يَشَاء اللَّهُ وَاذْكُر رَّبَّكَ إِذَا نَسِيتَ وَقُلْ عَسَى أَن يَهْدِيَنِ رَبِّي لأَقْرَبَ مِنْ هَذَا رَشَدًا .  وَلَبِثُوا فِي كَهْفِهِمْ ثَلَاثَ مِائَةٍ سِنِينَ وَازْدَادُوا تِسْعًا. قُلِ اللَّهُ أَعْلَمُ بِمَا لَبِثُوا لَهُ غَيْبُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ أَبْصِرْ بِهِ وَأَسْمِعْ مَا لَهُم مِّن دُونِهِ مِن وَلِيٍّ وَلَا يُشْرِكُ فِي حُكْمِهِ أَحَدًا

Wala usiseme kamwe kwa jambo lolote lile: Hakika nitalifanya hilo kesho. Isipokuwa (kusema) In Shaa Allaah! (Allaah Akipenda) Na mkumbuke Mola wako pale unaposahau, na sema: 'Asaa Mola wangu Ataniongoa kwenye uongozi ulio karibu zaidi kuliko huu. Na walikaa katika pango lao miaka mia tatu, na wakazidisha tisa. Sema: Allaah Anajua zaidi muda waliokaa. Ni Zake tu siri za mbingu na ardhi. Kuona kulioje na kusikia Kwake! Hawana mlinzi isipokuwa Yeye, wala Hamshirikishi yeyote katika hukumu Yake. [Al-Kahf: 23-29].

 

Umuhimu wa kusema In Shaa Allaah:

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 وَلاَ تَقُولَنَّ لِشَيْءٍ إِنِّي فَاعِلٌ ذَلِكَ غَدًا .  إِلاَّ أَن يَشَاء اللَّهُ

Wala usiseme kamwe kwa jambo lolote lile: Hakika nitalifanya hilo kesho. Isipokuwa (kusema) In Shaa Allaah! (Allaah Akipenda) 

 

Allaah (سبحانه وتعالى) Anamfundisha Mtume (صلى الله عليه  وآله وسلم)  kwamba anapoazimia kufanya kitendo, lazima asema 'In Shaa Allaah' (Allaah Akipenda) kwani Yeye Allaah (سبحانه وتعالى) Ndiye Mwenye Qudra (uwezo) wa kila kitu, Ndiye Mwenye Kudabiri mambo yote, na Ndiye Mjuzi wa mambo ya 'ghayb' (yasiyoonekana). Hakuna jambo linalowezea kutendeka ila kwa matakwa Yake.

Imepokelewa toka kwa  Abu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Mtume (صلى الله عليه  وآله وسلم) amesema:

 

((قَالَ سُلَيْمَان بْن دَاوُد لَأَطُوفَنَّ اللَّيْلَة عَلَى سَبْعِينَ اِمْرَأَة))   وَفِي رِوَايَة ((تِسْعِينَ اِمْرَأَة)) وَفِي رِوَايَة ((مِائَة اِمْرَأَة.  تَلِد كُلّ اِمْرَأَة مِنْهُنَّ غُلَامًا يُقَاتِل فِي سَبِيل اللَّه فَقِيلَ لَهُ))  وَفِي رِوَايَة ((قَالَ لَهُ الْمَلَك.  قُلْ إِنْ شَاءَ اللَّه. فَلَمْ يَقُلْ فَطَافَ بِهِنَّ فَلَمْ يَلِد مِنْهُنَّ إِلَّا اِمْرَأَة وَاحِدَة نِصْف إِنْسَان)) فَقَالَ رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((وَاَلَّذِي نَفْسِي بِيَدِهِ لَوْ قَالَ إِنْ شَاءَ اللَّه لَمْ يَحْنَث وَكَانَ دَرَكًا لِحَاجَتِهِ))   وَفِي رِوَايَة ((وَلَقَاتَلُوا فِي سَبِيل اللَّه فُرْسَانًا أَجْمَعِينَ)) "

((Nabii Sulaymaan bin Daawuwd عليهما السلام alisema: "Usiku wa leo nitawatembelea [nitafanya kitendo cha ndoa] wanawake sabini)) Katika riwaaya nyingine: ((wake tisini)) Katika riwaaya nyingine ((wake mia. Kila mmoja wao azae mtoto wa kiume ambao watapigana Fiy SabiyliLlaah [Katika njia ya Allaah] Akaaambiwa)). Katika riwaaya nyingine:  ((Malaika akamwambia: sema In Shaa Allaah, lakini hakusema. Akawatembelea wanawake hao lakini hakuna aliyezaa isipokuwa mmoja tu ambaye alizaa mtoto aliyeumbika nusu tu)) Mtume (صلى الله عليه  وآله وسلم) akasema: ((Naapa kwa Yule Ambaye nafsi yangu iko mikononi Mwake, angelisema In Shaa Allaah, asingeliharibu kiapo chake na hivyo ingelimsaidia kupata alichotaka)) Katika riwaaya nyingine: ((Wangelipigana kama wapanda farasi kwa ajili ya Allaah)) [Fat-h Al-Baariy 6: 41, Muslim 3: 1275].

 

Sababu ya kuteremka Aayah hizi:

 

Ibn 'Abbaas amesema: “Quraysh (Makafiri wa Makkah) walimtuma An-Nadr bin Al-Haarith na 'Uqbah bin Abi Mu'iytw kwa Mapadri Wayahudi walioko Madiynah na wakawaambia "Nendeni na waulizeni kuhusu Muhammad na wasimulieni kuhusu yeye Muhammad anayoyasema, kwani wao ni watu wa kwanza wa kupewa vitabu na wanayo elimu ya mitume kuliko sisi".

Wakaenda Maquraysh hao wawili na walipofika Madiynah waliwauliza mapadri ya Kiyahudi kuhusu Mtume (صلى الله عليه  وآله وسلم). Wakawaelezea Mayahudi sifa zote za Mtume (صلى الله عليه  وآله وسلم). Kisha wakasema: "Nyinyi ni watu wa Tawraat na sisi tumekuja kwenu ili mtujulishe kuhusu sahibu yetu".

 

Marabai wa kiyahudi wakawaambia, "Muulizeni mas-alah matatu tutakayokupeni mkamuulize. Pindi akijibu haya mas-ala matatu, basi yeye ni Mtume aliyetumwa na Allaah. Lakini akishindwa kujibu basi atakuwa anajisemea mambo yasiyokuwa ya kweli, na hapo mfanye mnavyotaka.

Muulizeni:

  1. Kuhusu vijana wa wakati wa kale ni kisa chao. Kwani kisa chao ni cha kustaajabisha. (Asw-haabul-Kahf – vijana Wa pangoni)

  2. Nini kisa cha mtu aliyesafiri sana hadi akafika Mashariki na Magharibi ya dunia, yaani Dhul-Qarnayn.

  3. Muulizeni kuhusu roho (nafsi) ni kitu gani hicho?

 

An-Nadr na 'Uqbah wakarudi Makkah kwa Maquraysh na kuwaambia, "Enyi Quraysh! Sisi tumekuja na uamuzi wa suluhisho ambalo litatatua na kumaliza mashaakil baina yetu na Muhammad. Mapadri Wayahudi wametuambia tumuulize Muhammad mas-ala matatu". Wakawaelezea mas-alah yenyewe, kisha wakamuendea Mtume (صلى الله عليه  وآله وسلم)   umuuliza hayo mas-ala. Mtume (صلى الله عليه  وآله وسلم) akawaambia:

((أُخْبِرُكُم غَدَا عَمَّ سَأَلْتُم عَنْهُ))

((Nitakujulisheni kesho mambo mliyoyauliza))

 

Lakini hakusema In Shaa Allaah. Wakaondoka zao kisha Mtume (صلى الله عليه  وآله وسلم)  akakaa siku kumi na tano bila ya Jibriyl (عليه السلام)  kumjia kama ilivyo kawaida yake kumpa Wahyi (ufunuzi) kutoka kwa Allaah (سبحانه وتعالى). Watu wa Makkah wakaanza kumtilia shaka na kupita kusema, "Muhammad katuahidi kutujibu mas-ala tuliyomuuliza siku ya pili na hadi leo siku ya kumi na tano zimepita hakutujibu lolote katika hayo".

Mtume (صلى الله عليه  وآله وسلم) akafikwa na huzuni sana kwa kuchelewa kupata Wahyi kutoka kwa Allaah (سبحانه وتعالى). Akasikitika kuhusu  maneno ya watu wa Makkah waliyokuwa wakisema. Kisha Jibriyl (عليه السلام)  akaja kumteremshia Suwrah ya 'Al-Kahf' ambayo  ilimliwaza Mtume (صلى الله عليه  وآله وسلم) baada ya kuwa na huzuni kutokana na maneno ya watu wa Makkah. Allaah (سبحانه وتعالى) Akanza kumfunulia wahyi kwa kumwambia: 

 فَلَعَلَّكَ بَاخِعٌ نَّفْسَكَ عَلَى آثَارِهِمْ إِن لَّمْ يُؤْمِنُوا بِهَذَا الْحَدِيثِ أَسَفًا

Huenda ukajihiliki nafsi yako kwa ajili yao, kuwasikitikia kwa kuwa hawayaamini mazungumzo haya!  [Al-Kahf: 6].

Maana:  Usijiangamize nafsi yako kwa majuto". Qataadah kasema, "Kujiua kwa hasira na huzuni kwa ajili yao" [Atw-Twabariy 17:597-598].

Mujaahid kasema, "kwa hamu." [Atw-Twabariy 17:598].

Pia ina maana kwamba: "Usisikitike nao, wewe fikisha kwao ujumbe tu na yeyote atakayekwenda njia ya haki basi ni kwa ajili ya manufaa yake, na atakayekwenda njia ya upotofu basi ni khasara yake mwenyewe, kwa hiyo wewe usijiangamize nafsi yako kwa huzuni juu yao."

Aayah zinaendelea:  

 

 إِنَّا جَعَلْنَا مَا عَلَى الْأَرْضِ زِينَةً لَّهَا لِنَبْلُوَهُمْ أَيُّهُمْ أَحْسَنُ عَمَلًا. وَإِنَّا لَجَاعِلُونَ مَا عَلَيْهَا صَعِيدًا جُرُزًا .

Kwa hakika Tumevifanya vilivyoko juu ya ardhi kuwa ni pambo lakeili Tuwafanyie mtihani, ni nani kati yao wenye vitendo vizuri zaidi. Na hakika Sisi Tutavifanya vyote vilio juu ya ardhi kuwa kama nchi iliyopigwa na ukame. [Al-Kahf: 7-8].

Kisha Allaah (سبحانه وتعالى) Akampa fundisho Mtume Wake   (صلى الله عليه  وآله وسلم) kuhusu kusema In Shaa Allaah anapokusudia jambo lolote: 

 وَلاَ تَقُولَنَّ لِشَيْءٍ إِنِّي فَاعِلٌ ذَلِكَ غَدًا .  إِلاَّ أَن يَشَاء اللَّهُ وَاذْكُر رَّبَّكَ إِذَا نَسِيتَ وَقُلْ عَسَى أَن يَهْدِيَنِ رَبِّي لأَقْرَبَ مِنْ هَذَا رَشَدًا

Wala usiseme kamwe kwa jambo lolote lile: Hakika nitalifanya hilo kesho. Isipokuwa In Shaa Allaah (Akipenda Allaah) Na mkumbuke Mola wako pale unaposahau, na sema: 'Asaa Mola wangu Ataniongoa kwenye uongozi ulio karibu zaidi kuliko huu.

 وَاذْكُر رَّبَّكَ إِذَا نَسِيتَ

Na mkumbuke Mola wako pale unaposahau.

 

Maana: Ukisahau kusema In Shaa Allaah basi sema pale unapokumbuka. Hii ni rai ya Abu 'Aaliyah na Al-Hasan Al-Baswriy [Atw-Twabariy 17:645.

Ibn 'Abbaas aliifasiri Aayah hii kuwa mtu anaweza kusema In Shaa Allaah hata baada ya mwaka ikiwa amesahau kusema baada ya kuweka kiapo au kusema atafanya jambo fulani. Hivi atakuwa amefanya Sunnah ya kusema In Shaa Allaah hata kama baada ya kuvunja kiapo. Hii vile vile ni rai ya Ibn Jariyr [At-Twabariy 17:646]. Lakini kasema hii haina maana kwamba inafidia kuvunja kiapo cha mtu, bali mtu anapovunja kiapo lazima afanye kafara yake (malipo ya kiapo). Na Allaah Anajua zaidi

 

 وَقُلْ عَسَى أَن يَهْدِيَنِ رَبِّي لأَقْرَبَ مِنْ هَذَا رَشَدًا

 na sema: 'Asaa Mola wangu Ataniongoa kwenye uongozi ulio karibu zaidi kuliko huu.

 

Maana: “Ee Mtume:  ikiwa umeulizwa jambo lolote ambalo hulijui, basi muombe Allaah (سبحانه وتعالى) kwa kurudi Kwake ili Akuongoze kujibu lililo haki". Na Allaah Anajua zaidi

 

Kusema In Shaa Allaah ni fundisho kwetu sote:

 

Inampasa kila Muislamu anapokusudia jambo au anapotoa ahadi fulani aseme In Shaa Allaah, kwani uwezekano wa kutendeka jambo au kutokutendeka kunategema na kupenda Kwake Allaah (سبحانه وتعالى). Hii ni kwa sababu hatuna ujuzi wa mambo ya ghaibu. Mfano wanapoagana watu kukutana siku au mahali au saa kadhaa huenda isiwezekani kwa sababu:

  1. Huenda mmoja wao akaaga dunia kabla ya siku hiyo ya kukutana.

  2. Sehemu walioagana inaweza kuwa imefikwa na maafa ikawa haiko tena.

  3. Inawezekana kutokea dharura ikashindikana kukutana wakati uliopangwa.    

Kwa hiyo ni muhimu sana kumtegemea Allaah (سبحانه وتعالى) Aliwezeshe  jambo kutendeka kwa uwezo na matakwa Yake.

Allaah (سبحانه وتعالى) Ametaja kuhusu maswali matatu aliyoulizwa Mtume (صلى الله عليه  وآله وسلم)  na Maquraysh wa Makkah katika Aayah zifuatazo: 

1- Kuhusu Aswhaabul-Kahf:     

 أَمْ حَسِبْتَ أَنَّ أَصْحَابَ الْكَهْفِ وَالرَّقِيمِ كَانُوا مِنْ آيَاتِنَا عَجَبًا

Bali unadhani ya kwamba wale Watu wa Pangoni na Maandishi walikuwa ni ajabu miongoni mwa ishara Zetu? [Al-Kahf: 9]

Zikaendelea Aayah kutaja kuhusu vijana hao wa pangoni kama ilivyoelezwa katika kisa chao.

2-Kuhusu Dhul-Qarnayn:

 وَيَسْأَلُونَكَ عَن ذِي الْقَرْنَيْنِ قُلْ سَأَتْلُو عَلَيْكُم مِّنْهُ ذِكْرًا   

Na wanakuuliza khabari za Dhul-Qarnayn. Sema: Nitakusimulieni baadhi ya hadithi yake. [Al-Kahf: 83].

 

3-Kuhusu Roho:

 وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الرُّوحِ قُلِ الرُّوحُ مِنْ أَمْرِ رَبِّي وَمَا أُوتِيتُم مِّن الْعِلْمِ إِلاَّ قَلِيلاً  

Na wanakuuliza kuhusu Roho. Sema: Roho ni katika mambo ya Mola wangu. Nanyi hamkupewa katika ilimu ila kidogo tu. [Al-israa: 85].

 

Muda walioishi Aswhaabul-Kahf  pangoni:

 

Kisa chao kimemalizikia katika Qur-aan kwa kutajwa muda walioishi vijana hao pangoni:

 وَلَبِثُوا فِي كَهْفِهِمْ ثَلَاثَ مِائَةٍ سِنِينَ وَازْدَادُوا تِسْعًا . قُلِ اللَّهُ أَعْلَمُ بِمَا لَبِثُوا لَهُ غَيْبُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ أَبْصِرْ بِهِ وَأَسْمِعْ مَا لَهُم مِّن دُونِهِ مِن وَلِيٍّ وَلَا يُشْرِكُ فِي حُكْمِهِ أَحَدًا  

Na walikaa katika pango lao miaka mia tatu, na wakazidisha tisa. Sema: Allaah Anajua zaidi muda waliokaa. Ni Zake tu siri za mbingu na ardhi. Kuona kulioje na kusikia Kwake! Hawana mlinzi isipokuwa Yeye, wala Hamshirikishi yeyote katika hukumu Yake.

Allaah (سبحانه وتعالى) Anamtajia Mtume (صلى الله عليه  وآله وسلم) muda waliokaa pangoni nao ni kuanzia wakati Alipowapa usingizi wa kufa hadi wakati Alipowafufua, kisha walipojulikana na watu wakati ule. Muda wenyewe ulikuwa ni miaka mia tatu na tisa kwa hesabu ya mwandamo wa mwezi. Tofauti ya miaka mia ya mwandamo na mia ya Sola (Solar) ni miaka mitatu. Ndio maana baada ya Allaah (سبحانه وتعالى) kutaja miaka mia tatu Ameongeza miaka tisa. Yaani miaka 3 x 3 = 9.

قُلِ اللَّهُ أَعْلَمُ بِمَا لَبِثُوا

Sema: Allaah Anajua zaidi muda waliokaa.

Maana: “Utakapoulizwa kuhusu muda waliokaa na wewe huna ujuzi kutoka kwa Allaah (سبحانه وتعالى) basi usijibu kitu ila:

 اللَّهُ أَعْلَمُ بِمَا لَبِثُوا لَهُ غَيْبُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ {{

Allaah Anajua zaidi muda waliokaa. Ni Zake tu siri za mbingu na ardhi.

Maana: Hakuna yeyote anayejua jambo hilo isipokuwa Mwenyewe Allaah (سبحانه وتعالى) pamoja na viumbe Aliowachagua  kuwajulisha. (Hii ni rai ya ma'ulamaa zaidi ya mmoja kama Mujaahid na wengineo waliokuja katika kizazi cha mbele).

 وَلَبِثُوا فِي كَهْفِهِمْ ثَلَاثَ مِائَةٍ سِنِينَ وَازْدَادُوا تِسْعًا   

Na walikaa katika pango lao miaka mia tatu, na wakazidisha tisa.

Qataadah amesema: “Hii ni rai ya Ahlul-Kitaab (Watu Waliopewa kitabu) lakini Allaah (سبحانه وتعالى)  Ameikanusha kwa Kusema:

  قُلِ اللَّهُ أَعْلَمُ بِمَا لَبِثُوا

Sema: Allaah Anajua zaidi muda waliokaa.

Maana: Allaah (سبحانه وتعالى) Anajua zaidi kuliko wanayosema watu [Atw-Twabariy 17: 647]. Hii pia ilikuwa ni rai ya Mutwarraf bin 'Abdillaah [Atw-Twabariy 17:648]. Lakini rai hii iko wazi kujadiliwa kwa sababu Ahlul-Kitaab walivyosema wameishi katika pango kwa muda wa miaka mia tatu bila ya kutaja miaka tisa, walikuwa wakikusudia miaka ya sola (Solar) na si miaka ya mwandamo wa mwezi (kama ambavyo Waislam tunavyotumia kwa kalenda zetu) na Allaah (سبحانه وتعالى)  Amesimulia yale waliyotaja kwani Asingelisema:

 وَازْدَادُوا تِسْعًا

na wakazidisha tisa

Maana iliyo dhahiri ya Aayah ni kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) kutaja uhakika wenyewe na Hakusimulia yale waliyosema Ahlul-Kitaab. (Hii ni rai ya Ibn Jariyr رحمه الله). Na Allaah Anajua zaidi.

 أَبْصِرْ بِهِ وَأَسْمِعْ

Kuona kulioje na kusikia Kwake!

Maana: Allaah (سبحانه وتعالى) Anawaona na Kuwasikia. Ibn Jariyr amesema: "Lugha imetumika hapa ya ufasaha kudhihirisha Himdi ya Allaah (سبحانه وتعالى)" [Atw-Twabariy 17:650].

 

Kifungu cha maneno haya kinaweza kufahamika kwa kumaanisha jinsi Allaah (سبحانه وتعالى) Alivyokuwa na uwezo wa Kuona kila kilichokuweko na jinsi gani Alivyokuwa na uwezo wa Kusikia kila kinachosikilizwa kwani hakuna kinachofichika Kwake.

Inasemekana kuwa Qataadah amesimulia kuhusu kauli hii: 

 أَبْصِرْ بِهِ وَأَسْمِعْ

Kuona kulioje na kusikia Kwake!

"Hakuna anayesikia au kuona zaidi ya Allaah (سبحانه وتعالى)" [Atw-Twabariy 17: 650]

Maana: Allaah (سبحانه وتعالى) Ndiye Mwenye uwezo wa Kuumba na Kuamrisha. Hakun.a wa kupindua Ufalme Wake. Hana mshauri,  msaidizi wala mshirika, Ametakasika na Ametukuka. 

 

Mafunzo Na Hidaaya:

  1. Mja kumfanyia Adabu Allaah (سبحانه وتعالى) kwa kutokusema 'nitafanya jambo fulani' ila baada ya kusema In Shaa Allaah.

  2. Adabu ya mja anaposahau kumtukuza Allaah (سبحانه وتعالى)  amtaje japokuwa anapokumbuka baada ya muda kupita. Na akiapa basi hakimfai kiapo mpaka amtukuze isipokuwa ikiwa imeambatana na maneno yake pale pale.

  3. Utajo sahihi wa muda waliokaa vijana katika pango kwa muda wa miaka mia tatu na tisa kwa hesabu ya miaka mwandamo wa mwezi.  

 


Mwisho

 

 

Marejeo:

Tafsiyr Ibn Kathiyr.

 

 

 

Share