Kuandikiwa Kombe Na Kufukizwa Vikaratasi Vinavyoandikwa Inafaa?

 

SWALI:

 

Assalam Alaykum kwanza napeleka shukran zng za dhati kwake subhanahu wataala, thumma nyie mlojitolea fiysabilillah kutuokoa sisi ktk shirki na kuyarekebisha matendo yetu, suali langu je mtoto mdogo kuandikiwa ktk vikaratas hati zisojulikana na kuambiwa uviroweke kisha umnyweshe (kombe) inafaa? Sina mushkila ikiwa itandikwa qur-an au dua bali mushkila ktk hati zisojulikana au kuchanganya aya na hati nyengine za kiarab au kuvichoma nakumfukiza mtoto

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kuhusu kombe, japo inaandikwa kwa maandishi yanayofahamika ya Aayah za Qur-aan ingawa kuna baadhi ya Maulamaa wamesema inafaa kwa kudai kuwa Swahaba Ibn ‘Abbaas alitumia, lakini Qauli yenye nguvu na Maulamaa wengi wanapingana nayo kwa kutokuwa na ushahidi sahihi wa hili na pia kutofundishwa njia hiyo na Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye alifundisha njia zote za kutibu au kujikinga na uchawi, husda, kijicho, na hayo ya marohani n.k. kwa kutufundisha du’aa mbalimbali na Aayah za Qur-aan ambazo baadhi yake tunakutajia chini. Hivyo, ni bora uachane na hayo mambo ya kombe ambayo yana utata na ufuate zile njia sahihi zilizothibiti.

Baadhi ya wanaojiita Mashaykh na waalimu wanatumia njia hizo kula pesa za Waislam.

 

Njia nyengine ni kuwa na muda wa wewe mwenyewe kusoma zile Aayah na Surah ambazo ni kinga kwa Muislamu kama alivyotufundisha Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kama Suratul Ikhlaasw, al-Falaq na an-Naas asubuhi na jioni. Na Suratul Baqarah Aayah za 1-5, 255–257 na 284–286. Na pia kusoma Qur-aan  sana.  Pia kusoma Adhkaara za asubuhi na jioni ambazo pindi ukizidumisha basi zitakutosheleza kabisa kujikinga wewe na familia yako kutokana na kila balaa na shari . Nazo zinapatikana katika kiungo kifuatacho:

 

28 Nyiradi Za Asubuhi Na Jioni

 

Na nyiradi na du’aa zote nyinginezo utakazozihitaji katika maisha yako ya kila siku utazipata katika kitabu kifuatacho. Na humu pia zimo du’aa za kuwakinga watoto:

 

Hiswnul Muslim

 49 Dua'a Inayo Kingwa Nayo Watoto.

Tunamuomba Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Akupatie shifaa kwa njia iliyo sahihi.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share