Skip to main content
Majina Mazuri Ya Allaah Jina 074 kati ya 103
074-Al-Hafiyy

Al-Hafiyy: Mwenye Kuwahurumia sana na Kuwajali Waja Wake; Mwenye Upole na Wema mwingi kwao, Anayeyashughulikia mambo yao, Anayewakirimu na Kuwaitikia wanapomwomba, na khaswa Awliyaa Wake Waumini.

Jina hili tukufu limethibiti katika Qur-aan, katika kauli ya Nabiy Ibraahiym (عليه السلام) kwa baba yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

قَالَ سَلَامٌ عَلَيْكَ ۖ سَأَسْتَغْفِرُ لَكَ رَبِّي ۖ إِنَّهُ كَانَ بِي حَفِيًّا ﴿٤٧﴾

(Ibraahiym) akasema: Salaamun ‘Alayka. (Amani iwe juu yako). Nitakuombea maghfirah kwa Rabb wangu. Hakika Yeye daima Ni Mwenye Kunihurumia sana. [Maryam (19:47)]

Jina hili limekuja mara moja katika Qur-aan, katika Aayah hii. Na ‘Ulamaa wamelithibitisha miongoni mwa Majina ya Allaah; Imaam Ibn ‘Uthaymiyn (رحمه الله) amelitaja katika orodha yake ya Majina ya Allaah yaliyothibiti katika Qur-aan [Al-Qawaa’id Al-Muthlaa].

Maana Ya Al-Hafiyy:

Al-Hafiyy katika lugha ni mwenye kumfanyia mwingine wema na upole kwa wingi, na mwenye kulijali na kulishughulikia jambo lake kwa undani. Na kutokana na maana ya undani, Allaah (سبحانه وتعالى) Amesema kuhusu wanaouliza juu ya Saa (Qiyaamah):

يَسْأَلُونَكَ عَنِ السَّاعَةِ أَيَّانَ مُرْسَاهَا ۖ قُلْ إِنَّمَا عِلْمُهَا عِندَ رَبِّي ۖ لَا يُجَلِّيهَا لِوَقْتِهَا إِلَّا هُوَ ۚ ثَقُلَتْ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ لَا تَأْتِيكُمْ إِلَّا بَغْتَةً ۗ يَسْأَلُونَكَ كَأَنَّكَ حَفِيٌّ عَنْهَا ۖ قُلْ إِنَّمَا عِلْمُهَا عِندَ اللَّـهِ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ ﴿١٨٧﴾

Wanakuuliza kuhusu Saa (Qiyaamah), lini kutokea kwake? Sema: Hakika ujuzi wake uko kwa Rabb wangu. Hakuna wa kuidhihirisha wakati wake isipokuwa Yeye. Ni nzito katika mbingu na ardhi. Haitokufikieni isipokuwa kwa ghafla. Wanakuuliza kama kwamba wewe unaijua vyema. Sema: Hakika ujuzi wake uko kwa Allaah (Pekee), lakini watu wengi hawajui. [Al-A’raaf (7:187)]

1-Al-Hafiyy Ni Mwenye Rehma na Huruma kubwa kwa Waja Wake, Anayewajali na kuyashughulikia mambo yao. Amesema Imaam As-Sa’diy (رحمه الله) katika kuifasiri kauli ya Ibraahiym (عليه السلام):

أي: رحيما رءوفا بحالي، معتنيا بي

“Yaani: Mwenye Kunirehemu, Mwenye Huruma kwa hali yangu, Mwenye Kunijali.” [Tafsiyr As-Sa’diy]

2-Al-Hafiyy Ni Mwenye Upole kwa Waja Wake, na katika Upole Wake ni kuwaongoza kwenye kumwabudu Yeye Peke Yake. Amesema Imaam Ibn Kathiyr (رحمه الله):

قال ابن عباس وغيره: لطيفا، أي: في أن هداني لعبادته والإخلاص له

“Amesema Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) na wengineo: (Maana yake ni) Mwenye Upole; yaani katika kuniongoza kwenye kumwabudu Yeye na kumtakasia ‘ibaadah.” [Tafsiyr Ibn Kathiyr]

Na amesema As-Suddiy (رحمه الله): “Al-Hafiyy Ni Yule Anayelishughulikia jambo lake (kwa kulijali).” [Tafsiyr Ibn Kathiyr]

3-Al-Hafiyy Huziitikia du’aa za Awliyaa Wake na Huwakirimu. Ibraahiym (عليه السلام) alipojitenga na kaumu yake na wanavyoviabudu, akamwomba Rabb wake kwa matumaini, Al-Hafiyy Alimtunukia watoto wema waliokuwa Manabii. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَأَعْتَزِلُكُمْ وَمَا تَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ وَأَدْعُو رَبِّي عَسَىٰ أَلَّا أَكُونَ بِدُعَاءِ رَبِّي شَقِيًّا ﴿٤٨﴾ فَلَمَّا اعْتَزَلَهُمْ وَمَا يَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ وَهَبْنَا لَهُ إِسْحَاقَ وَيَعْقُوبَ ۖ وَكُلًّا جَعَلْنَا نَبِيًّا ﴿٤٩﴾

Na natengana nanyi na mnavyoviomba badala ya Allaah. Na namuomba Rabb wangu, asaa nisijekuwa mwenye kunyimwa duaa yangu kwa kumwomba Rabb wangu. Basi alipotengana nao na wanayoyaabudu badala ya Allaah, Tulimtunukia Is-haaq, na (mjukuu) Ya’quwb. Na kila mmoja wao Tulimjaalia kuwa Nabiy. [Maryam (19:48-49)]

4-Na katika Kuwajali kwa Al-Hafiyy Awliyaa Wake ni kuwaokoa na shida na kuwahifadhi na maadui zao, kama Alivyomwokoa Ibraahiym (عليه السلام) alipotupwa motoni. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

قُلْنَا يَا نَارُ كُونِي بَرْدًا وَسَلَامًا عَلَىٰ إِبْرَاهِيمَ ﴿٦٩﴾

Tukasema: Ee moto! Kuwa baridi, na salama juu ya Ibraahiym. [Al-Anbiyaa (21:69)]

Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Hafiyy:

1-Tambua Kwamba Al-Hafiyy Ni Mwenye Huruma Kwako Kuliko Mama Kwa Mwanawe:

Tambua, ee Mja wa Al-Hafiyy, kwamba Rabb wako Anakujali na Anakuhurumia kuliko mama anavyomhurumia mtoto wake. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alipomuona mwanamke miongoni mwa mateka akimkumbatia mtoto wake na kumnyonyesha, alisema:

عَنْ عُمَرَ بْنِ الْخَطَّابِ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ لَنَا رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((أَتَرَوْنَ هَذِهِ طَارِحَةً وَلَدَهَا فِي النَّارِ؟)) قُلْنَا: لاَ، وَهِيَ تَقْدِرُ عَلَى أَنْ لاَ تَطْرَحَهُ. فَقَالَ: ((لَلَّهُ أَرْحَمُ بِعِبَادِهِ مِنْ هَذِهِ بِوَلَدِهَا))

Amesimulia ‘Umar bin Al-Khattwaab (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alituambia: “Je, mnamuona huyu atamtupa mtoto wake motoni?” Tukasema: Hapana, naye anaweza kutomtupa. Akasema: “Hakika Allaah Ni Mwenye Rehma zaidi kwa Waja Wake kuliko huyu kwa mtoto wake.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

2-Mwombe Al-Hafiyy Kwa Yakini Kwamba Hatakunyima:

Kumbuka kwamba Ibraahiym na Zakariyyaa (عليهما السلام) walimwomba Rabb wao kwa yakini kwamba Hawatanyimwa du’aa zao, kwa kuwa walijua Ujali Wake kwao; basi nawe muombe Al-Hafiyy kwa yakini na matumaini (rejea juu: Maryam (19:48)). Anasema Allaah (سبحانه وتعالى) kuhusu du’aa ya Zakariyyaa (عليه السلام):

قَالَ رَبِّ إِنِّي وَهَنَ الْعَظْمُ مِنِّي وَاشْتَعَلَ الرَّأْسُ شَيْبًا وَلَمْ أَكُن بِدُعَائِكَ رَبِّ شَقِيًّا ﴿٤﴾

Akasema: Rabb wangu! Hakika mimi mifupa imeninyong’onyea na kichwa kimeng’aa mvi, na wala sikuwa mwenye kunyimwa katika kukuomba Duaa, ee Rabb wangu. [Maryam (19:4)]

Na Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ ۖ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ ۖ فَلْيَسْتَجِيبُوا لِي وَلْيُؤْمِنُوا بِي لَعَلَّهُمْ يَرْشُدُونَ ﴿١٨٦﴾

Na watakapokuuliza Waja Wangu kuhusu Mimi, basi (waambie) hakika Mimi Niko Karibu (kwa ujuzi). Naitikia duaa ya muombaji anaponiomba. Hivyo basi waniitikie Mimi na waniamini Mimi, wapate kuongoka. [Al-Baqarah (2:186)]

3-Mtegemee Al-Hafiyy Katika Mambo Yako Yote:

Tambua kwamba anayemtegemea Al-Hafiyy, Yeye Humtosheleza, na Humjali katika kila hali yake. Ibraahiym (عليه السلام) alipotupwa motoni alimtegemea Rabb wake, Naye Akamwokoa:

عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ (رضي الله عنهما) قَالَ: ((حَسْبُنَا اللَّهُ وَنِعْمَ الْوَكِيلُ، قَالَهَا إِبْرَاهِيمُ (عليه السلام) حِينَ أُلْقِيَ فِي النَّارِ، وَقَالَهَا مُحَمَّدٌ (صلى الله عليه وسلم) حِينَ قَالُوا: إِنَّ النَّاسَ قَدْ جَمَعُوا لَكُمْ فَاخْشَوْهُمْ فَزَادَهُمْ إِيمَانًا وَقَالُوا: حَسْبُنَا اللَّهُ وَنِعْمَ الْوَكِيلُ))

Amesimulia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) kwamba: “Hasbuna-Allaahu wa ni’mal-Wakiyl (Allaah Anatutosheleza, Naye Ni Mzuri Alioje Mtegemewa); aliyasema Ibraahiym (عليه السلام) alipotupwa motoni, na aliyasema Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) walipoambiwa: Hakika watu wamejumuika dhidi yenu, basi waogopeni; lakini hilo liliwazidishia imaan, wakasema: Hasbuna-Allaahu wa ni’mal-Wakiyl.” [Al-Bukhaariy]

Na Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَيَرْزُقْهُ مِنْ حَيْثُ لَا يَحْتَسِبُ ۚ وَمَن يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ فَهُوَ حَسْبُهُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ بَالِغُ أَمْرِهِ ۚ قَدْ جَعَلَ اللَّـهُ لِكُلِّ شَيْءٍ قَدْرًا﴿٣﴾

Na Atamruzuku kutoka njia ambayo hatazamii. Na yeyote anayetawakali kwa Allaah, basi Yeye Humtosheleza. Hakika Allaah Anatimiza Kusudio Lake. Allaah Amejaalia makadirio kwa kila kitu. [Atw-Twalaaq (65:3)]

4-Mshitakie Al-Hafiyy Huzuni Zako Na Shida Zako:

Kumbuka, ee Mja wa Al-Hafiyy, kwamba Yeye Ndiye Anayeijali hali yako kuliko yeyote; basi mshitakie Yeye Peke Yake majonzi yako na huzuni zako, kama alivyofanya Nabiy Ya’quwb (عليه السلام). Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

قَالَ إِنَّمَا أَشْكُو بَثِّي وَحُزْنِي إِلَى اللَّـهِ وَأَعْلَمُ مِنَ اللَّـهِ مَا لَا تَعْلَمُونَ ﴿٨٦﴾

Akasema: Hakika mimi nashitakia dhiki ya majonzi yangu na huzuni zangu kwa Allaah. Na najua kutoka kwa Allaah yale msiyoyajua. [Yuwsuf (12:86)]

5-Mdhanie Al-Hafiyy Dhana Njema:

Tambua kwamba Al-Hafiyy Yuko pamoja na dhana ya Mja Wake juu Yake; basi mdhanie dhana njema katika du’aa zako, tawbah yako na shida zako. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ النَّبِيُّ (صلى الله عليه وسلم): ((يَقُولُ اللَّهُ تَعَالَى: أَنَا عِنْدَ ظَنِّ عَبْدِي بِي، وَأَنَا مَعَهُ إِذَا ذَكَرَنِي))

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Allaah (تعالى) Anasema: Mimi Niko kwenye dhana ya Mja Wangu juu Yangu, na Niko pamoja naye anaponidhukuru.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

6-Jikurubishe Kwa Al-Hafiyy Kwa ‘Ibaadah Ili Akujali Zaidi:

Kumbuka kwamba Ujali maalumu wa Al-Hafiyy ni kwa Awliyaa Wake; na kadiri unavyojikurubisha Kwake kwa faradhi na naafilah, ndivyo Anavyokupenda, Akakuitikia na Akakulinda. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema katika Hadiyth Al-Qudsiy:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((إِنَّ اللَّهَ قَالَ: ... وَمَا يَزَالُ عَبْدِي يَتَقَرَّبُ إِلَيَّ بِالنَّوَافِلِ حَتَّى أُحِبَّهُ ... وَإِنْ سَأَلَنِي لأُعْطِيَنَّهُ، وَلَئِنِ اسْتَعَاذَنِي لأُعِيذَنَّهُ))

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika Allaah Amesema: … Na Mja Wangu ataendelea kujikurubisha Kwangu kwa (‘ibaadah za) naafilah mpaka Nimpende … Na akiniomba, bila shaka Nitampa; na akiniomba kinga, bila shaka Nitamkinga.” [Al-Bukhaariy]

7-Mshukuru Al-Hafiyy Kwa Kukuongoza Na Kukuneemesha:

Tambua kwamba katika Ujali mkubwa wa Al-Hafiyy kwako ni kukuongoza kwenye Tawhiyd na kumwabudu Yeye (rejea juu: kauli ya Ibn ‘Abbaas). Basi mshukuru kama alivyomtaja Ibraahiym (عليه السلام) Rabb wake kwa Neema Zake juu yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

الَّذِي خَلَقَنِي فَهُوَ يَهْدِينِ ﴿٧٨﴾ وَالَّذِي هُوَ يُطْعِمُنِي وَيَسْقِينِ ﴿٧٩﴾ وَإِذَا مَرِضْتُ فَهُوَ يَشْفِينِ ﴿٨٠﴾ وَالَّذِي يُمِيتُنِي ثُمَّ يُحْيِينِ ﴿٨١﴾ وَالَّذِي أَطْمَعُ أَن يَغْفِرَ لِي خَطِيئَتِي يَوْمَ الدِّينِ ﴿٨٢﴾

Ambaye Ameniumba, Naye Ananiongoza. Na Ambaye Ndiye Anayenilisha na Ananinywesha. Na ninapokuwa mgonjwa, basi Yeye Ananiponyesha. Na Ambaye Atanifisha kisha Atanihuisha. Na Ambaye natumai Atanighufuria makosa yangu Siku ya Malipo. [Ash-Shu’araa (26:78-82)]

8-Wajali Watu Na Uwafanyie Upole Hata Wanaokukosea:

Kumbuka, ee Mja wa Al-Hafiyy, kwamba Ibraahiym (عليه السلام) alimjibu baba yake aliyemtisha kwa upole na kwa maneno mazuri: “Salaamun ‘Alayka” (rejea juu: Maryam (19:47)). Basi wajali watu, uwahurumie na uwafanyie upole, kama alivyokuwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) mwenye kuwajali Waumini. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

لَقَدْ جَاءَكُمْ رَسُولٌ مِّنْ أَنفُسِكُمْ عَزِيزٌ عَلَيْهِ مَا عَنِتُّمْ حَرِيصٌ عَلَيْكُم بِالْمُؤْمِنِينَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ﴿١٢٨﴾

Kwa yakini amekujieni Rasuli anayetokana na nyinyi wenyewe, yanamtia mashaka (na huzuni) yanayokutaabisheni, anakujalini, kwa Waumini ni mwenye huruma mno, mwenye rehma. [At-Tawbah (9:128)]

9-Tambua Kwamba Ujali Wa Al-Hafiyy Kwa Waumini Ni Ahadi Yake:

Kumbuka, ee Mja wa Al-Hafiyy, kwamba Ujali Wake hauwahusu Manabii peke yao; Alipomwokoa Yuwnus (عليه السلام) kutoka katika giza la tumbo la samaki baada ya kumwomba, Aliahidi kwamba hivyo ndivyo Anavyowaokoa Waumini. Basi muombe katika kila dhiki, ukiwa na yakini ya Ahadi Yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَذَا النُّونِ إِذ ذَّهَبَ مُغَاضِبًا فَظَنَّ أَن لَّن نَّقْدِرَ عَلَيْهِ فَنَادَىٰ فِي الظُّلُمَاتِ أَن لَّا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنتَ سُبْحَانَكَ إِنِّي كُنتُ مِنَ الظَّالِمِينَ ﴿٨٧﴾ فَاسْتَجَبْنَا لَهُ وَنَجَّيْنَاهُ مِنَ الْغَمِّ ۚ وَكَذَٰلِكَ نُنجِي الْمُؤْمِنِينَ ﴿٨٨﴾

Na Dhan-Nuwn (Yuwnus), alipoondoka akiwa ameghadhibika, akadhani kwamba Hatutamdhikisha. Akaita vizani kwamba: Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Wewe, Utakasifu ni Wako, hakika mimi nilikuwa miongoni mwa madhalimu. Basi Tukamuitikia, na Tukamuokoa kutokana na ghamu. Na hivyo ndivyo Tuwaokoavyo Waumini. [Al-Anbiyaa (21:87-88)]

10-Mwombe Al-Hafiyy Kwa Du’aa Ya Ibraahiym (عليه السلام):

Omba du’aa kwa Al-Hafiyy kwa du’aa ya Ibraahiym (عليه السلام) Akujaalie wewe na dhuria wako kuwa wenye kusimamisha Swalaah, na Akughufurie wewe, wazazi wako na Waumini. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

رَبِّ اجْعَلْنِي مُقِيمَ الصَّلَاةِ وَمِن ذُرِّيَّتِي ۚ رَبَّنَا وَتَقَبَّلْ دُعَاءِ﴿٤٠﴾ رَبَّنَا اغْفِرْ لِي وَلِوَالِدَيَّ وَلِلْمُؤْمِنِينَ يَوْمَ يَقُومُ الْحِسَابُ ﴿٤١﴾

Rabb wangu! Nijaalie niwe mwenye kusimamisha Swalaah pamoja na dhuria wangu. Rabb wetu! Nitakabalie duaa yangu. Rabb wetu! Nighufurie mimi na wazazi wangu wawili na Waumini Siku itakayosimama hesabu. [Ibraahiym (14:40-41)]

Na Allaah Mjuzi zaidi