Skip to main content
Majina Mazuri Ya Allaah Jina 073 kati ya 103
073-Al-Jawaad

Al-Jawaad: Mwingi wa Ukarimu; Mwingi wa kutoa na kuneemesha bila ya kikomo, Ambaye Ukarimu Wake umewaenea viumbe Vyake vyote, Waumini na makafiri, wala Hazina Zake hazipungui kwa kutoa.

Jina hili tukufu limethibiti katika Sunnah ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):

عَنْ طَلْحَةَ بْنِ عُبَيْدِ اللَّهِ وَابْنِ عَبَّاسٍ (رضي الله عنهم) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((إِنَّ اللَّهَ تَعَالَى جَوَادٌ يُحِبُّ الْجُودَ، وَيُحِبُّ مَعَالِيَ الأَخْلاَقِ، وَيَكْرَهُ سَفْسَافَهَا))

Amesimulia Twalhah bin ‘Ubaydillaah na Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهم) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika Allaah (تعالى) Ni Jawaad (Mwingi wa Ukarimu), Anapenda ukarimu, na Anapenda tabia za hadhi ya juu, na Anachukia tabia duni.” [Al-Bayhaqiy katika Shu’ab Al-Iymaan na Abuu Nu’aym katika Al-Hilyah, na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh Al-Jaami’ (1744)]

Jina hili halikuja katika Qur-aan kwa tamko lake, bali limethibiti katika Sunnah. Na ‘Ulamaa wamelithibitisha Jina hili miongoni mwa Majina ya Allaah. Imaam Ibn ‘Uthaymiyn (رحمه الله) amelitaja katika orodha yake ya Majina ya Allaah yaliyothibiti katika Sunnah, akasema:

ومن سنة رسول الله صلى الله عليه وسلم: الجميل، الجواد، الحكم، الحيي

“Na katika Sunnah ya Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم): Al-Jamiyl, Al-Jawaad, Al-Hakam, Al-Hayiyy…” [Al-Qawaa’id Al-Muthlaa]

Na Imaam Ibn Al-Qayyim (رحمه الله) amesema katika An-Nuwniyyah:

وَهُوَ الْجَوَادُ فَجُودُهُ عَمَّ الْوُجُودَ جَمِيعَهُ بِالْفَضْلِ وَالْإِحْسَانِ ... وَهُوَ الْجَوَادُ فَلَا يُخَيِّبُ سَائِلًا وَلَوْ أَنَّهُ مِنْ أُمَّةِ الْكُفْرَانِ

“Naye Ni Al-Jawaad, Ukarimu Wake umevienea viumbe vyote kwa Fadhila na Ihsaan… Naye Ni Al-Jawaad, Hamkatishi tamaa muombaji yeyote, hata kama ni miongoni mwa umma wa makafiri.”

Maana Ya Al-Jawaad:

Al-Juwd katika lugha ni wingi wa kutoa na ukarimu. Na Al-Jawaad Ni Mwenye Kutoa kwa wingi, kwa Ukarimu, bila ya Kuzuia wala Kukoma.

1-Al-Jawaad Ni Ambaye Ukarimu Wake umewaenea viumbe vyote; Anampa mwema na muovu, Muumini na kafiri, katika Neema za dunia, na Anawahusisha Waumini na Ukarimu Wake wa Aakhirah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

كُلًّا نُّمِدُّ هَـٰؤُلَاءِ وَهَـٰؤُلَاءِ مِنْ عَطَاءِ رَبِّكَ ۚ وَمَا كَانَ عَطَاءُ رَبِّكَ مَحْظُورًا ﴿٢٠﴾

Wote hao Tunawakunjulia - hawa na hao - katika Hiba za Rabb wako. Na hazikuwa Hiba za Rabb wako zenye kuzuiliwa. [Al-Israa (17:20)]

2-Hazina za Al-Jawaad hazipungui kwa kutoa; Mkono Wake umejaa, Anatoa usiku na mchana. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((يَدُ اللَّهِ مَلأَى لاَ يَغِيضُهَا نَفَقَةٌ، سَحَّاءُ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ، أَرَأَيْتُمْ مَا أَنْفَقَ مُنْذُ خَلَقَ السَّمَاءَ وَالأَرْضَ فَإِنَّهُ لَمْ يَغِضْ مَا فِي يَدِهِ))

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Mkono wa Allaah umejaa, hakuupunguzi utoaji; unamimina (kheri) usiku na mchana. Je, mnaona Alichokitoa tangu Alipoumba mbingu na ardhi? Hakika hakijapunguza kilichomo Mkononi Mwake.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

3-Al-Jawaad Lau Angewapa viumbe wote kila walichokiomba, wa mwanzo wao na wa mwisho wao, hilo lisingepunguza chochote katika Ufalme Wake. Amesema Allaah (تعالى) katika Hadiyth Al-Qudsiy:

عَنْ أَبِي ذَرٍّ (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) فِيمَا رَوَى عَنِ اللَّهِ تَبَارَكَ وَتَعَالَى أَنَّهُ قَالَ: ((... يَا عِبَادِي لَوْ أَنَّ أَوَّلَكُمْ وَآخِرَكُمْ وَإِنْسَكُمْ وَجِنَّكُمْ قَامُوا فِي صَعِيدٍ وَاحِدٍ فَسَأَلُونِي فَأَعْطَيْتُ كُلَّ إِنْسَانٍ مَسْأَلَتَهُ مَا نَقَصَ ذَلِكَ مِمَّا عِنْدِي إِلاَّ كَمَا يَنْقُصُ الْمِخْيَطُ إِذَا أُدْخِلَ الْبَحْرَ ...))

Amesimulia Abuu Dharr (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema katika aliyoyapokea kutoka kwa Allaah (تبارك وتعالى) kwamba Amesema: “… Enyi Waja Wangu! Lau wa mwanzo wenu na wa mwisho wenu, na watu wenu na majini wenu wangesimama katika uwanja mmoja wakaniomba, Nikampa kila mmoja alichokiomba, hilo lisingepunguza chochote katika Nilivyo navyo isipokuwa kama inavyopunguza sindano inapoingizwa baharini …” [Muslim]

4-Al-Jawaad Anapenda ukarimu na tabia za hadhi ya juu, na Anawapenda wakarimu, na Anachukia ubakhili na tabia duni (rejea Hadiyth juu). Na Amewaahidi wanaotoa katika Njia Yake kwamba Atawazidishia malipo mara nyingi. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

مَّثَلُ الَّذِينَ يُنفِقُونَ أَمْوَالَهُمْ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ كَمَثَلِ حَبَّةٍ أَنبَتَتْ سَبْعَ سَنَابِلَ فِي كُلِّ سُنبُلَةٍ مِّائَةُ حَبَّةٍ ۗ وَاللَّـهُ يُضَاعِفُ لِمَن يَشَاءُ ۗ وَاللَّـهُ وَاسِعٌ عَلِيمٌ ﴿٢٦١﴾

Mfano wa wale wanaotoa mali zao katika Njia ya Allaah ni kama mfano wa punje moja ya mbegu iliyotoa mashuke saba, katika kila shuke kuna punje mia. Na Allaah Humzidishia Amtakaye, na Allaah Ni Mwenye Wasaa, Mjuzi wa yote. [Al-Baqarah (2:261)]

Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Jawaad:

1-Tambua Kwamba Kila Neema Uliyonayo Ni Kutoka Kwa Al-Jawaad:

Tambua, ee Mja wa Al-Jawaad, kwamba kila Neema uliyonayo, ya mwili, mali, familia, ilimu na Dini, ni Ukarimu wa Al-Jawaad juu yako; basi usiinasibishe kwa nafsi yako, bali mhimidi Yeye Peke Yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَمَا بِكُم مِّن نِّعْمَةٍ فَمِنَ اللَّـهِ ۖ ثُمَّ إِذَا مَسَّكُمُ الضُّرُّ فَإِلَيْهِ تَجْأَرُونَ﴿٥٣﴾

Na Neema yoyote mliyo nayo, basi ni kutoka kwa Allaah. Kisha inapokuguseni dhara, mnamlilia Yeye tu kuomba msaada. [An-Nahl (16:53)]

2-Mwombe Al-Jawaad Kila Unachokihitaji Bila Kusita:

Kumbuka kwamba Al-Jawaad Anapenda kuombwa, na Haurudishi mkono wa Mja Wake mtupu anapomnyanyulia mikono yake; basi muombe haja zako zote, kubwa na ndogo, kwa yakini kwamba Atakuitikia. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ سَلْمَانَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((إِنَّ رَبَّكُمْ تَبَارَكَ وَتَعَالَى حَيِيٌّ كَرِيمٌ يَسْتَحْيِي مِنْ عَبْدِهِ إِذَا رَفَعَ يَدَيْهِ إِلَيْهِ أَنْ يَرُدَّهُمَا صِفْرًا))

Amesimulia Salmaan (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika Rabb wenu (تبارك وتعالى) Ni Mwenye Haya, Karimu; Anamwonea haya Mja Wake anapomnyanyulia mikono yake kuirudisha mitupu.” [Abuu Daawuwd (1488), At-Tirmidhiy (3556), na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha]

Na Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَقَالَ رَبُّكُمُ ادْعُونِي أَسْتَجِبْ لَكُمْ ۚ إِنَّ الَّذِينَ يَسْتَكْبِرُونَ عَنْ عِبَادَتِي سَيَدْخُلُونَ جَهَنَّمَ دَاخِرِينَ﴿٦٠﴾

Na Rabb wenu Amesema: Niombeni, Nitakuitikieni. Hakika wale wanaotakabari katika kuniabudu wataingia Jahannam wadhalilike. [Ghaafir (40:60)]

3-Kuwa Mkarimu Kwa Kumfuata Rasuli Wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم):

Kumbuka kwamba Al-Jawaad Anapenda ukarimu; na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa mkarimu kuliko watu wote, na alikuwa mkarimu zaidi katika Ramadhwaan. Basi mfuate katika ukarimu wake:

عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ (رضي الله عنهما) قَالَ: ((كَانَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) أَجْوَدَ النَّاسِ، وَكَانَ أَجْوَدُ مَا يَكُونُ فِي رَمَضَانَ حِينَ يَلْقَاهُ جِبْرِيلُ))

Amesimulia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) kwamba: “Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa mkarimu kuliko watu wote, na alikuwa mkarimu zaidi katika Ramadhwaan pale Jibriyl alipokuwa akikutana naye.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

4-Usiogope Ufakiri Unapotoa Kwa Ajili Ya Al-Jawaad:

Tambua, ee Mja wa Al-Jawaad, kwamba shaytwaan anakutishia ufakiri ili akuzuie kutoa, na Al-Jawaad Anakuahidi Maghfirah na Fadhila, na Ameahidi kukilipa kila unachokitoa. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

الشَّيْطَانُ يَعِدُكُمُ الْفَقْرَ وَيَأْمُرُكُم بِالْفَحْشَاءِ ۖ وَاللَّـهُ يَعِدُكُم مَّغْفِرَةً مِّنْهُ وَفَضْلًا ۗ وَاللَّـهُ وَاسِعٌ عَلِيمٌ ﴿٢٦٨﴾

Shaytwaan anakutishieni ufukara na anakuamrisheni machafu, (ubakhili), na Allaah Anakuahidini Maghfirah kutoka Kwake na Fadhila. Na Allaah Ni Mwenye Wasaa, Mjuzi wa yote. [Al-Baqarah (2:268)]

Na Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

قُلْ إِنَّ رَبِّي يَبْسُطُ الرِّزْقَ لِمَن يَشَاءُ مِنْ عِبَادِهِ وَيَقْدِرُ لَهُ ۚ وَمَا أَنفَقْتُم مِّن شَيْءٍ فَهُوَ يُخْلِفُهُ ۖ وَهُوَ خَيْرُ الرَّازِقِينَ ﴿٣٩﴾

Sema: Hakika Rabb wangu Anamkunjulia rizki Amtakaye kati ya Waja Wake na Humkadiria kwa kipimo (Amtakaye). Na kitu chochote mtoacho, basi Yeye Atakilipa, Naye Ni Mbora wa wenye kuruzuku. [Saba-a (34:39)]

5-Tambua Kwamba Swadaqah Haipunguzi Mali:

Kumbuka kwamba Al-Jawaad Hukibariki na Hukizidisha kile unachokitoa, wala swadaqah haipunguzi mali yako. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) عَنْ رَسُولِ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((مَا نَقَصَتْ صَدَقَةٌ مِنْ مَالٍ، وَمَا زَادَ اللَّهُ عَبْدًا بِعَفْوٍ إِلاَّ عِزًّا، وَمَا تَوَاضَعَ أَحَدٌ لِلَّهِ إِلاَّ رَفَعَهُ اللَّهُ))

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Swadaqah haipunguzi mali; na Allaah Hamzidishii Mja kwa kusamehe kwake isipokuwa utukufu; na hajinyenyekezi yeyote kwa ajili ya Allaah isipokuwa Allaah Humnyanyua.” [Muslim]

6-Toa Katika Vile Unavyovipenda:

Tambua kwamba ukarimu wa kweli ni kutoa katika mali unayoipenda, si kutoa kile usichokihitaji tu; na Al-Jawaad Anakijua kila unachokitoa. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

لَن تَنَالُوا الْبِرَّ حَتَّىٰ تُنفِقُوا مِمَّا تُحِبُّونَ ۚ وَمَا تُنفِقُوا مِن شَيْءٍ فَإِنَّ اللَّـهَ بِهِ عَلِيمٌ ﴿٩٢﴾

Hamtoweza kuufikia wema uliokunjuka mpaka mtoe katika vile mnavyovipenda. Na kitu chochote mnachotoa basi hakika Allaah kwacho Ni Mjuzi. [Aal-‘Imraan (3:92)]

7-Jiepushe Na Ubakhili Na Uchu Wa Nafsi:

Kumbuka, ee Mja wa Al-Jawaad, kwamba Al-Jawaad Anachukia ubakhili, na kwamba mafanikio ni kwa yule anayeepushwa na uchu wa nafsi yake, kama walivyokuwa Answaar waliowapendelea ndugu zao kuliko nafsi zao. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَالَّذِينَ تَبَوَّءُوا الدَّارَ وَالْإِيمَانَ مِن قَبْلِهِمْ يُحِبُّونَ مَنْ هَاجَرَ إِلَيْهِمْ وَلَا يَجِدُونَ فِي صُدُورِهِمْ حَاجَةً مِّمَّا أُوتُوا وَيُؤْثِرُونَ عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ وَلَوْ كَانَ بِهِمْ خَصَاصَةٌ ۚ وَمَن يُوقَ شُحَّ نَفْسِهِ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ﴿٩﴾

Na wale waliokuwa na masikani (Madiynah) na wakawa na iymaan kabla yao, wanawapenda wale waliohajiri kwao, na wala hawahisi choyo yoyote vifuani mwao kwa yale waliyopewa (Muhaajiruna), na wanawapendelea kuliko nafsi zao japokuwa wao wenyewe wanahitaji. Na yeyote anayeepushwa na ubakhili na tamaa ya uchu wa nafsi yake, basi hao ndio wenye kufaulu. [Al-Hashr (59:9)]

8-Toa Kwa Ajili Ya Wajihi Wa Al-Jawaad Bila Kutaka Malipo Kwa Watu:

Tambua kwamba Al-Jawaad Anakubali ukarimu ulio kwa ikhlaasw kwa ajili Yake; basi usitoe kwa ajili ya kusifiwa wala kurudishiwa, bali toa kwa ajili ya Wajihi Wake tu, kama walivyosifiwa Waja Wake wema. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَيُطْعِمُونَ الطَّعَامَ عَلَىٰ حُبِّهِ مِسْكِينًا وَيَتِيمًا وَأَسِيرًا﴿٨﴾ إِنَّمَا نُطْعِمُكُمْ لِوَجْهِ اللَّـهِ لَا نُرِيدُ مِنكُمْ جَزَاءً وَلَا شُكُورًا﴿٩﴾

Na wanalisha chakula, juu ya kuwa wao wanakipenda, masikini na mayatima na mateka. Hakika sisi tunakulisheni kwa ajili ya Wajihi wa Allaah, hatukusudii kutoka kwenu jazaa wala shukurani. [Al-Insaan (76:8-9)]

9-Mshukuru Al-Jawaad Ili Akuzidishie:

Kumbuka kwamba kushukuru Neema za Al-Jawaad kwa moyo, kwa ulimi na kwa vitendo ndiko kunakozidisha Neema hizo; na kuzikufuru ndiko kunakoziondosha. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَإِذْ تَأَذَّنَ رَبُّكُمْ لَئِن شَكَرْتُمْ لَأَزِيدَنَّكُمْ ۖ وَلَئِن كَفَرْتُمْ إِنَّ عَذَابِي لَشَدِيدٌ﴿٧﴾

Na pindi Alipotangaza Rabb wenu: Ikiwa mtashukuru, bila shaka Nitakuzidishieni (Neema Zangu), na mkikufuru, basi hakika Adhabu Yangu ni kali. [Ibraahiym (14:7)]

10-Usikate Tamaa Na Ukarimu Wa Al-Jawaad Hata Ukiwa Umekosea:

Tambua, ee Mja wa Al-Jawaad, kwamba Ukarimu Wake hauishii katika Neema za dunia tu, bali unawaenea hata waliokosea wanaporudi Kwake kwa tawbah; basi usikate tamaa kamwe na Rehma Yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

قُلْ يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ أَسْرَفُوا عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ لَا تَقْنَطُوا مِن رَّحْمَةِ اللَّـهِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ جَمِيعًا ۚ إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ﴿٥٣﴾

Sema: Enyi Waja Wangu ambao wamepindukia mipaka juu ya nafsi zao: Msikate tamaa na Rehma ya Allaah, hakika Allaah Anaghufuria dhambi zote. Hakika Yeye Ndiye Mwenye Kughufuria, Mwenye Kurehemu. [Az-Zumar (39:53)]

11-Shikamana Na Tabia Za Hadhi Ya Juu Na Jiepushe Na Tabia Duni:

Kumbuka kwamba Al-Jawaad Anapenda tabia za hadhi ya juu na Anachukia tabia duni (rejea Hadiyth juu); basi jipambe kwa ukarimu, upole, kusamehe, ukweli na kutimiza ahadi, na jiepushe na ubakhili, uongo, husda na kila tabia duni, ili uwe miongoni mwa Anaowapenda Al-Jawaad.

12-Mwombe Al-Jawaad Fadhila Zake Kila Unapotoka Msikitini:

Omba du’aa, ee Mja wa Al-Jawaad, kwa du’aa aliyotufundisha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) wakati wa kuingia na kutoka msikitini, kwani Fadhila zote ziko Mikononi Mwake:

عَنْ أَبِي حُمَيْدٍ أَوْ عَنْ أَبِي أُسَيْدٍ (رضي الله عنهما) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((إِذَا دَخَلَ أَحَدُكُمُ الْمَسْجِدَ فَلْيَقُلِ: اللَّهُمَّ افْتَحْ لِي أَبْوَابَ رَحْمَتِكَ، وَإِذَا خَرَجَ فَلْيَقُلِ: اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ مِنْ فَضْلِكَ))

Amesimulia Abuu Humayd au Abuu Usayd (رضي الله عنهما) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Mmoja wenu anapoingia msikitini aseme: Allaahumma-ftah liy abwaaba rahmatika (Ee Allaah! Nifungulie milango ya Rehma Yako). Na anapotoka aseme: Allaahumma inniy as-aluka min fadhwlika (Ee Allaah! Hakika mimi nakuomba katika Fadhila Zako).” [Muslim]

Na Allaah Mjuzi zaidi