Skip to main content

Majina Mazuri Ya Allaah075-Al-Waarith

Majina Mazuri Ya Allaah Jina 075 kati ya 103
075-Al-Waarith

Al-Waarith: Mrithi; Atakayebaki daima baada ya kutoweka viumbe vyote, Ambaye kila kitu kitarejea Kwake, Atairithi ardhi na waliomo humo, na urithi wa mbingu na ardhi ni Wake Pekee.

Jina hili tukufu limethibiti katika Qur-aan. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَإِنَّا لَنَحْنُ نُحْيِي وَنُمِيتُ وَنَحْنُ الْوَارِثُونَ﴿٢٣﴾

Na hakika Sisi Tunahuisha na Tunafisha, na Sisi Ndio Warithi. [Al-Hijr (15:23)]

Na Anasema Allaah (سبحانه وتعالى) kuhusu du’aa ya Nabiy Zakariyyaa (عليه السلام):

وَزَكَرِيَّا إِذْ نَادَىٰ رَبَّهُ رَبِّ لَا تَذَرْنِي فَرْدًا وَأَنتَ خَيْرُ الْوَارِثِينَ ﴿٨٩﴾

Na Zakariyyaa, alipomwita Rabb wake: Rabb wangu! Usiniache pekee, Nawe Ndiye Mbora wa wenye kubaki. [Al-Anbiyaa (21:89)]

Na Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَكَمْ أَهْلَكْنَا مِن قَرْيَةٍ بَطِرَتْ مَعِيشَتَهَا ۖ فَتِلْكَ مَسَاكِنُهُمْ لَمْ تُسْكَن مِّن بَعْدِهِمْ إِلَّا قَلِيلًا ۖ وَكُنَّا نَحْنُ الْوَارِثِينَ ﴿٥٨﴾

Na miji mingapi Tumeiangamiza! Ilipinduka mno mipaka ya kukanusha haki na neema za maisha yake. Basi hayo ni masikani yao yasiyokaliwa baada yao isipokuwa kidogo tu. Na Tukawa Sisi Warithi. [Al-Qaswasw (28:58)]

Jina hili limekuja katika Qur-aan likimhusu Allaah (سبحانه وتعالى) mara tatu, kwa tamko la wingi: (الْوَارِثُونَ) mara moja na (الْوَارِثِينَ) mara mbili, katika Aayaat hizi. Na ‘Ulamaa wamelithibitisha Jina hili miongoni mwa Majina ya Allaah; Imaam Ibn ‘Uthaymiyn (رحمه الله) amelitaja katika orodha yake ya Majina ya Allaah yaliyothibiti katika Qur-aan [Al-Qawaa’id Al-Muthlaa].

Maana Ya Al-Waarith:

Al-Waarith katika lugha ni mwenye kubakia baada ya kuondoka mwingine, na kupata alichokuwa nacho aliyeondoka. Na Allaah (سبحانه وتعالى) Ni Al-Waarith kwa maana Atabakia baada ya kutoweka kwa viumbe vyote, na kila walichokuwa nacho kitarejea Kwake. Amesema Imaam Al-Baghawiy (رحمه الله) katika kuifasiri kauli ya Zakariyyaa (عليه السلام): “Nawe Ndiye Mbora wa wenye kubaki”:

ثناء على الله بأنه الباقي بعد فناء الخلق وأنه أفضل من بقي حيا

“Ni kumsifu Allaah kwamba Yeye Ndiye Mwenye kubakia baada ya kutoweka viumbe, na kwamba Yeye Ni Mbora wa aliyebaki hai.” [Tafsiyr Al-Baghawiy]

Na amesema Imaam As-Sa’diy (رحمه الله):

أي: خير الباقين، وخير من خلفني بخير

“Yaani: Mbora wa wenye kubakia, na Mbora wa atakayeshika nafasi yangu (kwa watakaobaki baada yangu) kwa kheri.” [Tafsiyr As-Sa’diy]

1-Al-Waarith Ni Atakayebakia daima baada ya kutoweka kila kiumbe; kila kilichoko juu ya ardhi kitatoweka, na Wajihi Wake Utabakia. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

كُلُّ مَنْ عَلَيْهَا فَانٍ ﴿٢٦﴾ وَيَبْقَىٰ وَجْهُ رَبِّكَ ذُو الْجَلَالِ وَالْإِكْرَامِ ﴿٢٧﴾

Kila aliyekuwa juu yake (ardhi) ni mwenye kutoweka. Na utabakia Wajihi wa Rabb wako Mwenye Ujalali na Ukarimu. [Ar-Rahmaan (55:26-27)]

Na Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَلَا تَدْعُ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ ۘ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۚ كُلُّ شَيْءٍ هَالِكٌ إِلَّا وَجْهَهُ ۚ لَهُ الْحُكْمُ وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ ﴿٨٨﴾

Na wala usiombe pamoja na Allaah mwabudiwa mwingine. Hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye. Kila kitu ni chenye kuhiliki isipokuwa Wajihi Wake. Hukumu ni Yake Pekee na Kwake Pekee mtarejeshwa. [Al-Qaswasw (28:88)]

2-Al-Waarith Atairithi ardhi na waliomo humo, na viumbe vyote vitarejeshwa Kwake; na urithi wa mbingu na ardhi ni Wake Peke Yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

إِنَّا نَحْنُ نَرِثُ الْأَرْضَ وَمَنْ عَلَيْهَا وَإِلَيْنَا يُرْجَعُونَ ﴿٤٠﴾

Hakika Sisi Tutairithi ardhi na waliokuwemo humo, na Kwetu watarejeshwa. [Maryam (19:40)]

3-Al-Waarith Ndiye Anayemrithisha Amtakaye miongoni mwa Waja Wake ardhi duniani, na Huwarithisha Waumini wenye taqwa Jannah Aakhirah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

قَالَ مُوسَىٰ لِقَوْمِهِ اسْتَعِينُوا بِاللَّـهِ وَاصْبِرُوا ۖ إِنَّ الْأَرْضَ لِلَّـهِ يُورِثُهَا مَن يَشَاءُ مِنْ عِبَادِهِ ۖ وَالْعَاقِبَةُ لِلْمُتَّقِينَ ﴿١٢٨﴾

Muwsaa akawaambia kaumu yake: Ombeni msaada kwa Allaah na vuteni subira. Hakika ardhi ni ya Allaah, Humrithisha Amtakaye katika Waja Wake. Na mwisho (mzuri) ni kwa wenye taqwa. [Al-A’raaf (7:128)]

Na Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

تِلْكَ الْجَنَّةُ الَّتِي نُورِثُ مِنْ عِبَادِنَا مَن كَانَ تَقِيًّا ﴿٦٣﴾

Hiyo ni Jannah ambayo Tutawarithisha miongoni mwa Waja Wetu waliokuwa na taqwa. [Maryam (19:63)]

Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Waarith:

1-Tambua Kwamba Mali Yako Ni Amana Ya Al-Waarith:

Tambua, ee Mja wa Al-Waarith, kwamba mali uliyonayo si yako kwa hakika, bali ni ya Allaah; Amekufanya kuwa mwenye kushika nafasi ndani yake kwa muda tu, kisha itarudi Kwake au kwa warithi wako. Basi itumie katika kumtii. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

آمِنُوا بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ وَأَنفِقُوا مِمَّا جَعَلَكُم مُّسْتَخْلَفِينَ فِيهِ ۖ فَالَّذِينَ آمَنُوا مِنكُمْ وَأَنفَقُوا لَهُمْ أَجْرٌ كَبِيرٌ ﴿٧﴾

Muaminini Allaah na Rasuli Wake, na toeni kutokana na yale Aliyokufanyieni kuwa warithi kwayo. Basi wale walioamini miongoni mwenu, na wakatoa, watapata ujira mkubwa. [Al-Hadiyd (57:7)]

2-Mali Yako Ya Kweli Ni Ile Uliyoitanguliza:

Kumbuka kwamba mali unayoikusanya na kuiacha itarithiwa na wengine, na mali yako ya kweli ni ile uliyoitoa kwa ajili ya Allaah na ukaitanguliza kwa Aakhirah yako. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ مَسْعُودٍ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ النَّبِيُّ (صلى الله عليه وسلم): ((أَيُّكُمْ مَالُ وَارِثِهِ أَحَبُّ إِلَيْهِ مِنْ مَالِهِ؟)) قَالُوا: يَا رَسُولَ اللَّهِ، مَا مِنَّا أَحَدٌ إِلاَّ مَالُهُ أَحَبُّ إِلَيْهِ. قَالَ: ((فَإِنَّ مَالَهُ مَا قَدَّمَ، وَمَالُ وَارِثِهِ مَا أَخَّرَ))

Amesimulia ‘Abdullaah bin Mas’uwd (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Ni nani miongoni mwenu ambaye mali ya mrithi wake inapendeza zaidi kwake kuliko mali yake mwenyewe?” Wakasema: Ee Rasuli wa Allaah! Hakuna yeyote miongoni mwetu isipokuwa mali yake inapendeza zaidi kwake. Akasema: “Basi hakika mali yake ni ile aliyoitanguliza, na mali ya mrithi wake ni ile aliyoiacha nyuma.” [Al-Bukhaariy]

3-Usiipende Dunia Kupita Kiasi, Kwani Hutabaki Nayo:

Tambua, ee Mja wa Al-Waarith, kwamba hakuna kitakachobaki kwako katika mali yako isipokuwa ulichokila ukakimaliza, au ulichokivaa ukakichakaza, au ulichokitoa swadaqah ukakitanguliza. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ الشِّخِّيرِ (رضي الله عنه) قَالَ: أَتَيْتُ النَّبِيَّ (صلى الله عليه وسلم) وَهُوَ يَقْرَأُ: أَلْهَاكُمُ التَّكَاثُرُ، قَالَ: ((يَقُولُ ابْنُ آدَمَ: مَالِي مَالِي، وَهَلْ لَكَ يَا ابْنَ آدَمَ مِنْ مَالِكَ إِلاَّ مَا أَكَلْتَ فَأَفْنَيْتَ، أَوْ لَبِسْتَ فَأَبْلَيْتَ، أَوْ تَصَدَّقْتَ فَأَمْضَيْتَ))

Amesimulia ‘Abdullaah bin Ash-Shikh-khiyr (رضي الله عنه) kwamba: Nilimjia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) naye akisoma: “Alhaakumut-takaathur” (Kumekushughulisheni kushindana kwa wingi), akasema: “Binaadam anasema: Mali yangu! Mali yangu! Na je, una nini ee binaadam katika mali yako isipokuwa ulichokila ukakimaliza, au ulichokivaa ukakichakaza, au ulichokitoa swadaqah ukakitanguliza?” [Muslim]

Na Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

الْمَالُ وَالْبَنُونَ زِينَةُ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۖ وَالْبَاقِيَاتُ الصَّالِحَاتُ خَيْرٌ عِندَ رَبِّكَ ثَوَابًا وَخَيْرٌ أَمَلًا ﴿٤٦﴾

Mali na watoto ni pambo la uhai wa dunia. Na mema yanayobakia ni bora mbele ya Rabb wako kwa thawabu na matumaini mema zaidi. [Al-Kahf (18:46)]

4-Toa Katika Njia Ya Al-Waarith Kabla Hayajakufikia Mauti:

Kumbuka kwamba urithi wa mbingu na ardhi ni wa Allaah Pekee, na kwamba utaiacha mali yako; basi itoe katika Njia Yake kabla hayajakufikia mauti ukajuta. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَمَا لَكُمْ أَلَّا تُنفِقُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَلِلَّـهِ مِيرَاثُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ لَا يَسْتَوِي مِنكُم مَّنْ أَنفَقَ مِن قَبْلِ الْفَتْحِ وَقَاتَلَ ۚ أُولَـٰئِكَ أَعْظَمُ دَرَجَةً مِّنَ الَّذِينَ أَنفَقُوا مِن بَعْدُ وَقَاتَلُوا ۚ وَكُلًّا وَعَدَ اللَّـهُ الْحُسْنَىٰ ۚ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ ﴿١٠﴾

Na mna nini hata hamtoi katika Njia ya Allaah, na hali urithi wa mbingu na ardhi ni wa Allaah Pekee! Hawi sawa miongoni mwenu aliyetoa kabla ya Ushindi (wa Makkah) na akapigana. Hao watapata daraja kuu kabisa kuliko wale waliotoa baadae na wakapigana. Na wote Allaah Amewaahidi malipo mazuri kabisa. Na Allaah kwa yale myatendayo Ni Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri. [Al-Hadiyd (57:10)]

Na Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَأَنفِقُوا مِن مَّا رَزَقْنَاكُم مِّن قَبْلِ أَن يَأْتِيَ أَحَدَكُمُ الْمَوْتُ فَيَقُولَ رَبِّ لَوْلَا أَخَّرْتَنِي إِلَىٰ أَجَلٍ قَرِيبٍ فَأَصَّدَّقَ وَأَكُن مِّنَ الصَّالِحِينَ﴿١٠﴾

Na toeni katika yale Tuliyokuruzukuni kabla hayajamfikia mmoja wenu mauti akasema: Rabb wangu! Lau Ungeliniakhirisha mpaka muda wa karibu hivi, nikatoa swadaqah na nikawa miongoni mwa Swalihina. [Al-Munaafiquwn (63:10)]

5-Jiepushe Na Ubakhili, Kwani Uliyoyafanyia Ubakhili Yatarithiwa:

Tambua, ee Mja wa Al-Waarith, kwamba mali unayoifanyia ubakhili haitakufaa, bali itarithiwa baada yako na itakuwa shari kwako Siku ya Qiyaamah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَلَا يَحْسَبَنَّ الَّذِينَ يَبْخَلُونَ بِمَا آتَاهُمُ اللَّـهُ مِن فَضْلِهِ هُوَ خَيْرًا لَّهُم ۖ بَلْ هُوَ شَرٌّ لَّهُمْ ۖ سَيُطَوَّقُونَ مَا بَخِلُوا بِهِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۗ وَلِلَّـهِ مِيرَاثُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۗ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ ﴿١٨٠﴾

Wala wasidhani kabisa wale wanaofanya ubakhili kwa yale Aliyowapa Allaah katika Fadhila Zake kwamba hayo ni kheri kwao, bali ni shari kwao. Watafungwa kongwa yale waliyoyafanyia ubakhili Siku ya Qiyaamah. Na Ni Wake Allaah Pekee urithi wa mbingu na ardhi. Na Allaah kwa yale myatendayo Ni Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri. [Aal-‘Imraan (3:180)]

6-Usidanganyike Na Wingi Wa Mali Na Watoto:

Kumbuka kwamba aliyekufuru akajifakharisha kwa mali yake na watoto wake, Al-Waarith Atamrithi yote hayo, naye atamjia peke yake bila chochote. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَنَرِثُهُ مَا يَقُولُ وَيَأْتِينَا فَرْدًا ﴿٨٠﴾

Na Tutamrithi yale anayoyasema (mali na watoto), na atatujia peke yake! [Maryam (19:80)]

7-Jitahidi Uwe Miongoni Mwa Warithi Wa Jannah Ya Al-Firdaws:

Tambua kwamba Al-Waarith Huwarithisha Jannah wenye taqwa (rejea juu: Maryam (19:63)); basi jipambe kwa sifa za Waumini walizozitaja mwanzoni mwa Suwrah Al-Muuminuwn: khushuu’ katika Swalaah, kujiepusha na upuuzi, kutoa Zakaah, kuhifadhi tupu, kuchunga amana na ahadi, na kuzihifadhi Swalaah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

أُولَـٰئِكَ هُمُ الْوَارِثُونَ ﴿١٠﴾ الَّذِينَ يَرِثُونَ الْفِرْدَوْسَ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴿١١﴾

Hao ndio warithi. Ambao watarithi (Jannah ya) Al-Firdaws, wao humo ni wenye kudumu. [Al-Muuminuwn (23:10-11)]

8-Subiri Kwani Al-Waarith Huwarithisha Ardhi Wenye Taqwa:

Kumbuka, ee Mja wa Al-Waarith, kwamba madhalimu hawatabaki na ufalme wao, kwani ardhi ni ya Allaah, Humrithisha Amtakaye (rejea juu: Al-A’raaf (7:128)); basi subiri na mtegemee Allaah, kwani mwisho mwema ni kwa wenye taqwa. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَنُرِيدُ أَن نَّمُنَّ عَلَى الَّذِينَ اسْتُضْعِفُوا فِي الْأَرْضِ وَنَجْعَلَهُمْ أَئِمَّةً وَنَجْعَلَهُمُ الْوَارِثِينَ ﴿٥﴾

Na Tukataka Tuwafanyie fadhila wale waliokandamizwa katika ardhi, na Tuwafanye viongozi na Tuwafanye wenye kurithi. [Al-Qaswasw (28:5)]

9-Rithi Ilimu Ya Manabii, Kwani Hiyo Ndiyo Urithi Unaobaki:

Tambua kwamba Manabii hawakurithisha dinari wala dirhamu, bali walirithisha ilimu; basi jitahidi kuchukua fungu lako katika urithi huo kwa kujifunza Qur-aan na Sunnah. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي الدَّرْدَاءِ (رضي الله عنه) قَالَ: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) يَقُولُ: ((... وَإِنَّ الْعُلَمَاءَ وَرَثَةُ الأَنْبِيَاءِ، وَإِنَّ الأَنْبِيَاءَ لَمْ يُوَرِّثُوا دِينَارًا وَلاَ دِرْهَمًا، وَرَّثُوا الْعِلْمَ، فَمَنْ أَخَذَهُ أَخَذَ بِحَظٍّ وَافِرٍ))

Amesimulia Abud-Dardaa (رضي الله عنه) kwamba amemsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: “… Na hakika ‘Ulamaa ni warithi wa Manabii; na hakika Manabii hawakurithisha dinari wala dirhamu, bali wamerithisha ilimu; basi atakayeichukua, amechukua fungu kubwa kamili.” [Abuu Daawuwd (3641), At-Tirmidhiy (2682), na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha]

10-Kumbuka Mauti Na Kurejea Kwako Kwa Al-Waarith:

Kumbuka, ee Mja wa Al-Waarith, kwamba wewe na kila ulichonacho ni vya Allaah, na kwamba utarejea Kwake; basi unapofikwa na msiba useme kama walivyosifiwa wenye kusubiri. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

الَّذِينَ إِذَا أَصَابَتْهُم مُّصِيبَةٌ قَالُوا إِنَّا لِلَّـهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ﴿١٥٦﴾

Wale ambao unapowafika msiba husema: Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea. [Al-Baqarah (2:156)]

11-Mwombe Al-Waarith Kama Alivyomwomba Zakariyyaa (عليه السلام):

Omba du’aa kwa Al-Waarith Akutunukie dhuria wema watakaokurithi katika Dini na kheri, kama alivyoomba Zakariyyaa (عليه السلام) akisema: “Nawe Ndiye Mbora wa wenye kubaki” (rejea juu: Al-Anbiyaa (21:89)); Naye Allaah Akamwitikia. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

قَالَ رَبِّ إِنِّي وَهَنَ الْعَظْمُ مِنِّي وَاشْتَعَلَ الرَّأْسُ شَيْبًا وَلَمْ أَكُن بِدُعَائِكَ رَبِّ شَقِيًّا ﴿٤﴾ وَإِنِّي خِفْتُ الْمَوَالِيَ مِن وَرَائِي وَكَانَتِ امْرَأَتِي عَاقِرًا فَهَبْ لِي مِن لَّدُنكَ وَلِيًّا ﴿٥﴾ يَرِثُنِي وَيَرِثُ مِنْ آلِ يَعْقُوبَ ۖ وَاجْعَلْهُ رَبِّ رَضِيًّا ﴿٦﴾

Akasema: Rabb wangu! Hakika mimi mifupa imeninyong’onyea na kichwa kimeng’aa mvi, na wala sikuwa mwenye kunyimwa katika kukuomba Duaa, ee Rabb wangu. Nami nakhofia jamaa zangu nyuma yangu, na mke wangu ni tasa. Basi Nitunukie kutoka kwako (mwana) mrithi. Anirithi na arithi kizazi cha Ya’quwb, na Mjaalie Rabb wangu awe mwenye kuridhisha. [Maryam (19:4-6)]

Na Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

فَاسْتَجَبْنَا لَهُ وَوَهَبْنَا لَهُ يَحْيَىٰ وَأَصْلَحْنَا لَهُ زَوْجَهُ ۚ إِنَّهُمْ كَانُوا يُسَارِعُونَ فِي الْخَيْرَاتِ وَيَدْعُونَنَا رَغَبًا وَرَهَبًا ۖ وَكَانُوا لَنَا خَاشِعِينَ ﴿٩٠﴾

Basi Tukamuitikia na Tukamtunukia Yahyaa, na Tukamtengenezea mke wake. Hakika wao walikuwa wakikimbilia katika mambo ya kheri na wakituomba kwa raghba na khofu, na walikuwa wenye kutunyenyekea. [Al-Anbiyaa (21:90)]

Na Allaah Mjuzi zaidi