Skip to main content

Majina Ya Allaah Mazuri Na Sifa Zake: أسماء الله الحسنى وصفاته038-Majina Ya Allaah Mazuri Na Sifa Zake أسماء الله الحسنى وصفاته: AR-RAAZIQ, AR-RAZAAQ

أسماء الله الحسنى وصفاته

Majina Ya Allaah Mazuri Na Swifa Zake

Alhidaaya.com

الرَّازِق - الرَّزَّاق

038-Ar-Raaziq, Ar-Razzaaq

Ar-Raaziq: Mtoaji Rizqi: Yeye Ndiye Anayewapa rizqi viumbe wote na Amezipanga rizqi zao kabla ya kuwaumba na Amedhamini kuzikamilisha hata kama ni baada ya muda.

Jina Hili limetajwa katika Qur-aan mara kadhaa kwa ujumla. Miongoni mwa Aayah ni Kauli Yake Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

وَالَّذِينَ هَاجَرُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ ثُمَّ قُتِلُوا أَوْ مَاتُوا لَيَرْزُقَنَّهُمُ اللَّـهُ رِزْقًا حَسَنًا ۚ وَإِنَّ اللَّـهَ لَهُوَ خَيْرُ الرَّازِقِينَ ﴿٥٨﴾

Na wale waliohajiri katika Njia ya Allaah, kisha wakauawa, au wakafa, bila shaka Allaah Atawaruzuku riziki nzuri. Na hakika Allaah bila shaka Yeye Ndiye Mbora wa wenye kuruzuku. [Al-Hajj (22:58)]

Ar-Razzaaq: Mwingi Wa Kuruzuku: Ni jina linaloelezea wingi wa Rizqi Zake kwa viumbe Wake. Yeye Allaah (‘Azza wa Jalla) Anawaruzuku viumbe kabla ya wao kumuomba. Pia Anawaruzuku hata pale wanapomuasi.

Ar-Razzaaq limetajwa katika Qur-aan mara moja, lakini neno la rizq limetajwa zaidi ya mara mia. [1]

إِنَّ اللَّـهَ هُوَ الرَّزَّاقُ ذُو الْقُوَّةِ الْمَتِينُ ﴿٥٨﴾

Hakika Allaah Ndiye Mwingi wa Kuruzuku, Mwenye Nguvu Madhubuti. [Adh-Dhaariyaat (51:58)]

Allaah Ndiye Ar-Raaziq, Ar-Razzaaq kwa Waja Wake wote. Mwenye kudhamini rizqi ya kila aliyemo ulimwenguni, kila nafsi, kila wakati, Hajawapa Waumini pekee na kuwanyima makafiri, wala anayemuunga na kumnusuru na Yule aliyekuwa ni adui Yake, bali Rizqi Zake zinaenea kwa dhaifu asiye na uwezo na kwa tajiri mwenye nguvu, Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

وَمَا مِن دَابَّةٍ فِي الْأَرْضِ إِلَّا عَلَى اللَّـهِ رِزْقُهَا وَيَعْلَمُ مُسْتَقَرَّهَا وَمُسْتَوْدَعَهَا ۚ كُلٌّ فِي كِتَابٍ مُّبِينٍ﴿٦﴾

Na hakuna kiumbe chochote kitembeacho katika ardhi isipokuwa riziki yake iko kwa Allaah, na (Allaah) Anajua mahali pake pa kustakiri na pa kuhifadhiwa kwake. Yote yamo katika Kitabu kinachobainisha. [Huwd (11:6)]

Hakuna mwenye kuruzukiwa popote awaye, juu au chini ila atapata Rizqi Yake Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na ataenezwa na Ukarimu Wake, Yeye Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Hutoa rizqi kwa Anayemtaka na Hukadiria, na Anawapa Waja Wake wote ardhini Rizqi Zake, Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema: 

فَلْيَنظُرِ الْإِنسَانُ إِلَىٰ طَعَامِهِ ﴿٢٤﴾ أَنَّا صَبَبْنَا الْمَاءَ صَبًّا ﴿٢٥﴾ ثُمَّ شَقَقْنَا الْأَرْضَ شَقًّا ﴿٢٦﴾ فَأَنبَتْنَا فِيهَا حَبًّا ﴿٢٧﴾ وَعِنَبًا وَقَضْبًا ﴿٢٨﴾ وَزَيْتُونًا وَنَخْلًا ﴿٢٩﴾ وَحَدَائِقَ غُلْبًا ﴿٣٠﴾ وَفَاكِهَةً وَأَبًّا ﴿٣١﴾ مَّتَاعًا لَّكُمْ وَلِأَنْعَامِكُمْ ﴿٣٢﴾

Basi atazame binaadam chakula chake. Kwamba Sisi Tumemimina maji kwa uneemefu. Kisha Tukaipasua ardhi ikafunguka (kwa mimea). Tukaotesha humo nafaka. Na mizabibu na mimea ya mboga (ikatwayo ikamea tena). Na mizaituni na mitende. Na mabustani yaliyositawi na kusongamana. Na matunda na majani ya malisho ya wanyama. Yakiwa ni manufaa kwenu na kwa wanyama wenu wa mifugo. [‘Abasa (80:24-32)]

Na rizqi kwa Waja Wake ni aina mbili: 

i-Aina ambayo ina sababu: Kama vile Allaah Alivyofanya kuhusu kilimo, biashara na viwanda na mfano wake katika njia nyingi za kupata rizqi watu wote. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

وَجَعَلْنَا لَكُمْ فِيهَا مَعَايِشَ وَمَن لَّسْتُمْ لَهُ بِرَازِقِينَ﴿٢٠﴾

Na Tukakuwekeeni humo njia na mbinu za maisha, na ya hao ambao nyinyi si wenye kuwaruzuku. [Al-Hijr (15:20)]

Yaani ni sababu ambazo nyinyi mnapata rizqi.

ii-Aina nyingine ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Humpa mja rizqi bila kuwa na sababu kutoka kwake (yaani bila ya jitihada ya mja), ni Kumpa rizqi kutoka mbinguni moja kwa moja, au katika mikono ya mtu mwingine bila ya yule aliyepewa rizqi ile kuitafuta. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ الْأَرْضَ فِرَاشًا وَالسَّمَاءَ بِنَاءً وَأَنزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَخْرَجَ بِهِ مِنَ الثَّمَرَاتِ رِزْقًا لَّكُمْ ۖ فَلَا تَجْعَلُوا لِلَّـهِ أَندَادًا وَأَنتُمْ تَعْلَمُونَ ﴿٢٢﴾

Ambaye Amewafanyieni ardhi kuwa ni tandiko na mbingu kuwa ni paa, na Akateremsha kutoka mbinguni maji, Akawatolea kwayo matunda kuwa ni riziki zenu. Basi msimfanyie Allaah waliolingana naye na hali ya kuwa nyinyi mnajua. [Al-Baqarah (2:22)]

Na katika ukamilifu wa Rizqi Yake (Subhaanahu wa Ta’aalaa), Hutoa kwa sababu na bila ya kuwa na sababu, kuombwa au bila ya kuombwa.  Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa): 

وَاللَّـهُ يَرْزُقُ مَن يَشَاءُ بِغَيْرِ حِسَابٍ ﴿٢١٢﴾

Na Allaah Humruzuku Amtakaye bila ya hesabu. [Al-Baqarah (2:212)]

Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Ar-Raaziq, Ar-Razzaaq:

1-Mpwekeshe Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa kutambua kwamba Neema zote zinatoka Kwake na kwamba Yeye Pekee Ndiye Mwenye Kuruzuku. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اذْكُرُوا نِعْمَتَ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ ۚ هَلْ مِنْ خَالِقٍ غَيْرُ اللَّـهِ يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ ۚ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۖ فَأَنَّىٰ تُؤْفَكُونَ ﴿٣﴾

Enyi watu! Kumbukeni Neema za Allaah kwenu. Je, kuna muumbaji yeyote badala ya Allaah Anayekuruzukuni kutoka mbinguni na ardhini? Hapana Muabudiwa wa haki ila Yeye. Basi vipi mnaghilibiwa? [Faatwir (35:3)]

2-Kumbuka Neema nyingi mno za Allaah (‘Azza wa Jalla) zisizohesabika na Rizqi Zake nyingi duniani, bali kumbuka kwamba, hata katika Jannah Atakuruzuku kwa mazuri:

وَبَشِّرِ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ أَنَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ ۖ كُلَّمَا رُزِقُوا مِنْهَا مِن ثَمَرَةٍ رِّزْقًا ۙ قَالُوا هَـٰذَا الَّذِي رُزِقْنَا مِن قَبْلُ ۖ وَأُتُوا بِهِ مُتَشَابِهًا ۖ وَلَهُمْ فِيهَا أَزْوَاجٌ مُّطَهَّرَةٌ ۖ وَهُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴿٢٥﴾

Na wabashirie wale walioamini na wakatenda mema, kwamba watapata Jannaat (bustani) zipitazo chini yake mito, kila watakaporuzukiwa humo katika matunda kuwa ni riziki husema: Haya ndiyo yale tuliyoruzukiwa kabla. Na wataletewa hali ya kuwa yanashabihiana, na watapata humo wake waliotakaswa, nao humo watadumu. [Al-Baqarah (2:25)]

3-Usitafute rizqi kwa njia ya haraam, bali tafuta njia ya halaal, kwani baadhi ya watu wanamuasi Allaah katika hilo! Na omba du’aa ifuatayo:

 اللَّهُمَّ اكْفِنِي بِحَلالِكَ عن حَرَامِكَ وَأغْنِنِي بِفَضْلِكَ عَمَّنْ سِوَاكَ 

Ee Allaah nitosheleze na Vyako vya halaal dhidi ya Vyako ambavyo ni haraam, na nitajirishe kwa Fadhila Zako kutokana na asiyekuwa Wewe.[At-Tirmidhiy, taz. Swahiyh Sunan At-Tirmidhiy (2822)]

4-Usitumie rizqi yako katika yaliyoharamishwa kama vile ulevi, kamari na mengineyo. Au yaliyokemewa, kama vile kutumia kwa israaf na tabdhiyr (ubadhirifu).

5-Ridhika na rizqi Aliyokuruzuku Allaah, na kumbuka kwamba hakuna atakayeweza kukuzuilia au kukuzidishia isipokuwa Allaah. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 مَّا يَفْتَحِ اللَّـهُ لِلنَّاسِ مِن رَّحْمَةٍ فَلَا مُمْسِكَ لَهَا ۖ وَمَا يُمْسِكْ فَلَا مُرْسِلَ لَهُ مِن بَعْدِهِ ۚ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ﴿٢﴾

Rehma yoyote Anayoifungua Allaah kwa watu, basi hakuna wa kuizuia, na Anayoizuia, basi hakuna wa kuipeleka baada Yake, Naye Ni Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote. [Faatwir (35:2)]

Na katika Sunnah ni Hadiyth zifuatazo:

عن ابنِ عباسٍ رضي الله عنهما، قَالَ: كنت خلف النَّبيّ صلى الله عليه وسلم يومًا، فَقَالَ: ((يَا غُلامُ، إنِّي أعلّمُكَ كَلِمَاتٍ: احْفَظِ اللهَ يَحْفَظْكَ، احْفَظِ اللهَ تَجِدْهُ تُجَاهَكَ، إِذَا سَألْتَ فَاسأَلِ الله، وإِذَا اسْتَعَنْتَ فَاسْتَعِنْ باللهِ. وَاعْلَمْ: أنَّ الأُمَّةَ لَوْ اجْتَمَعَتْ عَلَى أنْ يَنْفَعُوكَ بِشَيءٍ لَمْ يَنْفَعُوكَ إلا بِشَيءٍ قَدْ كَتَبهُ اللهُ لَكَ، وَإِن اجتَمَعُوا عَلَى أنْ يَضُرُّوكَ بِشَيءٍ لَمْ يَضُرُّوكَ إلا بِشَيءٍ قَدْ كَتَبَهُ اللهُ عَلَيْكَ، رُفِعَتِ الأَقْلاَمُ وَجَفَّتِ الصُّحفُ)) رواه الترمذي، وَقالَ: حديث حسن صحيح

‘Abdullaah bin ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) amesema: Siku moja nilikuwa nyuma ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) (juu ya mnyama). Akaniambia: “Ee kijana, mimi nitakufundisha maneno: Mhifadhi Allaah Naye Atakuhifadhi. Mhifadhi Allaah utamkuta yupo mbele yako. Unapoomba, muombe Allaah. Unapotaka msaada, mtake Allaah. Fahamu kuwa, lau ummah (wote) utajikusanya ili wakunufaishe kwa jambo, basi hawataweza kukunufaisha ila kwa jambo Alilokuandikia Allaah; na wakijumuika ili wakudhuru kwa jambo, hawataweza kukudhuru ila kwa jambo Alilokuandikia Allaah. Kalamu zimeshasimama na karatasi zimeshakauka.” [At-Tirmidhiy, na amesema: Hadiyth Hasan Swahiyh]

عن جابر بن عبدالله  رضي الله عنه: قال رسول الله صلى الله عليه وآله وسلم: لا تَستبطِئُوا الرِّزقَ، فإنَّهُ لمْ يكنْ عبدٌ لِيموتَ حتى يَبلُغَهُ آخِرُ رِزقٍ هوَ لهُ، فاتَّقُوا اللهَ، وأجْملُوا في الطَّلَبِ، أخذُ الحلالِ، وتركُ الحرامِ

Amesimulia Jaabir bin ‘Abdillaah (Radhwiya Allaahu ‘anhu): Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Usiwe na papara kwa ajili ya rizqi, kwani hakuna mja atakayekufa hadi apate rizqi yake ya mwisho. Basi mcheni Allaah, na muwe na kiasi katika kutafuta, mkichukua yaliyo halaal na mkiacha yaliyo haraam.” [Ibn Maajah, Ibn Hibbaan, Atw-Twabaraaniy na ameisahihisha Al-Albaaniy: Swahiyh Al-Jaami’ (7323)]

Na Du’aa ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambayo tunaisoma kila siku katika nyiradi za baada ya Swalaah, imethibitisha hilo kwamba hakuna atakayeweza kukuzuilia rizqi ya Allaah:

لا إلهَ إلاّ اللّهُ وحدَهُ لا شريكَ لهُ، لهُ المُـلْكُ ولهُ الحَمْد، وهوَ على كلّ شَيءٍ قَدير، اللّهُـمَّ لا مانِعَ لِما أَعْطَـيْت، وَلا مُعْطِـيَ لِما مَنَـعْت، وَلا يَنْفَـعُ ذا الجَـدِّ مِنْـكَ الجَـد

Hapana mwabudiwa wa haki ila Allaah hali ya kuwa Peke Yake Hana mshirika, ni Wake Ufalme, na ni Zake Himdi, na Yeye ni Muweza wa kila kitu.  Ee Allaah, hakuna mwenye kukizuia Ulichokitoa, wala mwenye kutoa Ulichokizuia, na wala utajiri wa mtu haumnufaishi mwenye utajiri mbele Yako. [Hadiyth ya Al-Mughiyrah bin Shu’bah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) - Al-Bukhaariy (1/255)]

6-Usikimbilie kutafuta rizqi ukaacha Swalaah kwani Allaah Ni Mbora wa kuruzuku kama Anavyosema: 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا نُودِيَ لِلصَّلَاةِ مِن يَوْمِ الْجُمُعَةِ فَاسْعَوْا إِلَىٰ ذِكْرِ اللَّـهِ وَذَرُوا الْبَيْعَ ۚ ذَٰلِكُمْ خَيْرٌ لَّكُمْ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ﴿٩﴾ فَإِذَا قُضِيَتِ الصَّلَاةُ فَانتَشِرُوا فِي الْأَرْضِ وَابْتَغُوا مِن فَضْلِ اللَّـهِ وَاذْكُرُوا اللَّـهَ كَثِيرًا لَّعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ﴿١٠﴾ وَإِذَا رَأَوْا تِجَارَةً أَوْ لَهْوًا انفَضُّوا إِلَيْهَا وَتَرَكُوكَ قَائِمًا ۚ قُلْ مَا عِندَ اللَّـهِ خَيْرٌ مِّنَ اللَّـهْوِ وَمِنَ التِّجَارَةِ ۚ وَاللَّـهُ خَيْرُ الرَّازِقِينَ﴿١١﴾

Enyi walioamini! Inaponadiwa kwa ajili ya Swalaah siku ya Ijumaa, basi kimbilieni kwenda kumdhukuru Allaah na acheni kuuza na kununua. Hivyo ni kheri kwenu zaidi mkiwa mnajua. Na inapomalizika Swalaah, basi tawanyikeni katika ardhi, na tafuteni Fadhila za Allaah, na mdhukuruni Allaah kwa wingi ili mpate kufaulu. Na wanapoona tijara au pumbao wanaikimbilia na wanakuacha umesimama. Sema: Yaliyoko kwa Allaah ni bora zaidi kuliko pumbao na tijara, na Allaah Ni Mbora wa wenye kuruzuku. [Al-Jumu’ah (62:9-11)]

7-Omba Du’aa nyenginezo za kujaaliwa rizqi na kubarikiwa nayo:

Du’aa ifuatayo ni katika nyiradi za asubuhi:

اللّهُـمَّ إِنِّـي أَسْأَلُـكَ عِلْمـاً نافِعـاً وَرِزْقـاً طَيِّـباً، وَعَمَـلاً مُتَقَـبَّلاً

Ee Allaah, hakika nakuomba ilimu yenye kunufaisha na rizqi njema na amali zenye kutakabaliwa. [Hadiyth ya Ummu Salamah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) - Ibn Maajah (925), taz. Swahiyh Ibn Maajah (1/152)]  

Na Du’aa nyenginezo:

اللّهُـمَّ اغْفِـرْ لي، وَارْحَمْـني، وَاهْدِنـي، وَاجْبُرْنـي، وَعافِنـي وَارْزُقْنـي وَارْفَعْـني

Ee Allaah, nighufurie, na nirehemu, na nihidi na niunge kunitengenezea niliyoharamika nayo, na nipe afya, na niruzuku, na nipandishe [daraja]. 

[Asw-haabus-Sunan isipokuwa An-Nasaaiy. Nyiradi katika kikao baina ya Sajdah mbili]

اللَّهُمَّ اغْفِرْ لِي ذَنْبِي، وَوَسِّعْ لِي فِي دَارِي، وَبَارِكْ لِي فِيمَا رَزَقْتَنِي

Ee Allaah nighufurie dhambi zangu, na nipanulie katika nyumba yangu, na nibarikie katika Uliyoniruzuku. [At-Tirmidhiy, Ahmad - Swahiyh Al-Jaami’ (1265) - Zaad Al-Ma’aad (2/354)]

اللَّهُمَّ اجْعَلْ أَوْسَعَ رِزْقِكَ عَلَيَّ عِنْدَ كِبَرِ سِنِّي وَانْقِطَاعِ عُمُرِي 

Ee Allaah, Jaalia ukunjufu wa Rizqi Yako kwangu wakati wa uzee wangu, na kukatika umri wangu. 

[Al-Haakim, Swahiyh Al-Jaami’ (1/396), As-Silsilah Asw-Swahiyhah (1539)]

اللَّهُمَّ لَكَ الْحَمْدُ كُلُّهُ، اللَّهُمَّ لاَ قَابِضَ لِمَا بَسَطْتَ، وَلاَ بَاسِطَ لِمَا قَبَضْتَ، وَلاَ هَادِيَ لِمَا أَضْلَلْتَ، وَلاَ مُضِلَّ لِمَنْ هَدَيْتَ، وَلاَ مُعْطِيَ لِمَا مَنَعْتَ، وَلاَ مَانِعَ لِمَا أَعْطَيْتَ، وَلاَ مُقَرِّبَ لِمَا بَاعَدْتَ، وَلاَ مُبَاعِدَ لِمَا قَرَّبْتَ، اللَّهُمَّ ابْسُطْ عَلَيْنَا مِنْ بَرَكَاتِكَ، وَرَحْمَتِكَ، وَفَضْلِكَ، وَرِزْقِكَ. 

Ee Allaah, Himdi ni Zako zote. Ee Allaah, hakuna mwenye kuzuia Ulivyovikunjua, wala mwenye kukunjua Ulivyozuia, wala mwenye kumhidi Uliyempotoa, wala kumpotoa Uliyemhidi, wala mwenye kutoa Ulichokizuia, wala mwenye kuzuia Ulichokitoa, wala mwenye kukurubisha Ulichoweka mbali, wala mwenye kuweka mbali Ulichokiweka karibu. Ee Allaah tukunjulie katika Baraka Zako, na Rahmah Zako, na Fadhila Zako, na Rizqi Yako. [Ahmad, na Al-Bukhaariy ameitoa katika Al-Adabul-Mufrad (699), na Al-Albaaniy ameipa daraja ya Swahiyh katika Takhriyj Fiqhus-Siyrah (348), Swahiyh Al-Adabil-Mufrad lil-Bukhaariy (538/259), na Majma’u Az-Zawaaid (6/124)]

  1. [1]

     Sha-nu Ad-Du’aa (uk. 54).

  2. ^

     Israaf: Kutumia kwa zaidi ya mahitaji. Tabdhiyr ni kutumia kwa israaf iliyopinduka mipaka kwa kujionyesha kwa watu  na kushindana na kujifakharisha.