Skip to main content

Yepi Madhambi Makubwa na Yepi Madogo?

Yepi Madhambi Makubwa na Yepi Madogo?

 www.alhidaaya.com

SWALI LA KWANZA:

Kuna siku niliwahi kuiskia Hadiyth inayosema kuwa "mtu akishamaliza kuswali akaleta tasbih mara 33, na tahmid 33 na takbir 33 na akamswalia mtume, Allah subhanahu wataala humfutia madhambi yake hata kama yana wingi kama mfano wa bahari, muhimu tu iwe ni makosa madogo", je makosa makubwa niyapi?

SWALI LA PILI:

Assalam aleikum  

katika sheria kuna madhambi makubwa namadogo! makubwa nayajua jee waweza kunisaidia kunipa mfano wamadhanbi madogo?

JIBU:

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

Kuhusu Adhkaar baada ya kuswali SwalAah ya faradhi, zipo riwaayah kadhaa kuonyesha aina mbalimbali za Adhkaar baada ya Swalaah lakini kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) haijathibiti mahali hapo.

Adhkaar hizo zote utazipata hapa chini kwenye kiungo kifuatacho:

025-Hiswnul-Muslim: Nyiradi Baada Ya Kutoa Salaam Ya Kumaliza Swalaah

Ama kuhusiana na swali lako la madhambi makubwa na madogo, ni haya yafuatayo:

Madhambi Makubwa:

Madhambi makubwa ni yale ambayo yametajwa hivyo katika Qur-aan na Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) nayo ni yale ambayo mja anapoyafanya huwa na hukmu zifuatazo:

1-Allaah Anaalaani kitendo chake.

2-Yamewekewa adhabu kali kama mfano mwenye kuzini na hali ameoa au ameolewa kupigwa mawe hadi kufa au kupigwa bakora 100 kwa asiyeoa au asiyeolewa.

3-Anayoghadhibika nayo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aala).

4-Allaah Anamnyima Rahmah Yake mwenye kutenda.

Hadiyth ifuatayo imeyaelezea baadhi ya madhambi hayo makubwa ambayo yanajulikana kwa Sab'ul-Muwbiqaat (saba yenye kuangamiza).

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه(  عن النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((اجْتَنِبُوا السَّبْعَ الْمُوبِقَاتِ)) قَالُوا: يَا رَسُولَ اللَّهِ وَمَا هُنَّ؟  قَالَ: ((الشِّرْكُ بِاللَّهِ وَالسِّحْرُ وَقَتْلُ النَّفْسِ الَّتِي حَرَّمَ اللَّهُ إِلاَّ بِالْحَقِّ وَأَكْلُ الرِّبَا وَأَكْلُ مَالِ الْيَتِيمِ وَالتَّوَلِّي يَوْمَ الزَّحْفِ وَقَذْفُ الْمُحْصَنَاتِ الْمُؤْمِنَاتِ الْغَافلاَتِ)) متفق عليه

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه)  kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:((Jiepusheni na mambo saba yanayoangamiza!)) Wakauliza: Ni yepi hayo ee Rasuli wa Allaah? Akasema: ((Ni kumshirikisha Allaah, sihri [uchawi], kuua nafsi Aliyoiharamisha Allaah isipokuwa kwa haki, kula ribaa, kula mali ya yatima, kukimbia wakati wa kupambana na adui na kuwatuhumu uzinifu wanawake Waumini waliohifadhika walioghafilika)).  [Al-Bukhaariy, Muslim, An-Nasaaiy, Abu Daawuud]

Tunayaorodhesha hayo yaliyomo kwenye Hadiyth hapo juu na mengine mengi ambayo baadhi ya ‘Ulamaa wamejaribu kuyaorodhesha kwa kuyanyambua katika Qur-aan na Sunnah kulingana na makatazo, makemeo, laana, na adhabu zake.

Na yafuatayo hapa chini madhambi 70 makubwa ni ambayo ameyaorodhesha mwanachuoni mkubwa Imaam Muhammad bin ‘Uthmaan Adh-Dhahabiy kwenye kitabu chake ‘Al-Kabaair’:

1-Kumshikirika Allaah

2-Kuua

3-Uchawi

4-Kuacha Swalaah

6-Kuacha kufunga Swawm ya Ramadhwaan bila udhuru

7-Kutokuhiji kwa mwenye uwezo

8-Kutokuwatii wazazi

9-Kuwahama na kuwakata jamaa na ndugu; kutengana nao

10-Uzinzi (kufanya zinaa)

11-Liwati (matendo ya kaumu Luwt; watu kuingiliana nyuma) mwenye kufanya na kufanywa wote wanaingia.

12-Kula ribaa

13-Kula mali ya yatima na kumdhulumu

14-Kumsingizia Allaah na Rasuli Wake uongo

15-Kukimbia vitani

16-Kiongozi kuwa mdanganyifu kwa raia wake na kutokuwa muadilifu

17-Kiburi, majivuno na kujitukuza

18-Kutoa ushuhuda wa uongo 

19-Kunywa pombe

20-Kamari

21-Kumsingizia mwanamke mtwaharifu kwa uzinifu

22-Kuiba ngawira za vita

23-Wizi

24-Ujambazi

25-Kutoa kiapo cha uongo

26-Dhulma (Kudhulumu)

27-Chumo la haraam.

28-Kupata utajiri kwa njia za haraam.

29-Kujiua

30-Kusema uongo (kila mara)

31-Kutohukumu kwa uadilifu

32-Kutoa na kupokea rushwa

33- Mwanamke kujifananisha na mwanamme na mwanamme kujifananisha na mwanamke kimavazi, kutembea, kuzungumza na mengineyo

34-Udayuthi, ukuwadi, na kutokuwa mwaminifu katika ndoa

35-Kumuoa mwanamke aliyeachika kwa talaka tatu  ili awe halali kwa mume aliyemuacha kumrudia

36-Kutojilinda kurukiwa na mikojo

37-Riyaa (kujionyesha matendo mema)

38-Kutafuta elimu kwa maslahi ya dunia, na kuificha elimu uliyonayo

39-Kufanya khiyana

40-Kutangazia na kuhesabu mema uliyoyatenda

41-Kupinga Qadar

42-Kusikiliza siri za watu

43-Kuhamisha maneno (umbea)

44-Kulaani wengine

45-Kuvunja ahadi

46-Kuwaamini makuhani, watabiri, wapiga ramli (watazamiaji)

47-Mke kutomtii mumewe

48-Kutengeneza masanamu, vinyago, na picha

49-Kupiga mayowe, kuchana nguo, kujipiga na kujikatakata wakati wa msiba

50-Kutokuwa muadilifu kwa watu

51-Kutokuwa na huruma na kuwafanyia ujeuri mke, wafanyakazi, madhaifu na wanyama

52-Kumuudhi jirani

53-Kuwaudhi na kuwatukuna Waislamu

54-Kuwaudhi na kuwafanyia ujeuri watu

55-Isbaal (mwanamme kuvaa nguo ndefu inayovuka viwiko vya miguu kwa kiburi au ufakhari)

56-Mwanaume kuvaa hariri

57-Mtumwa kumkimbia bwana wake

58-Kutokuchinja mnyama kwa ajili ya Allaah

59-Kumwita mtu kwa ubini wa baba asiyekuwa wake huku unajua (kwa makusudi)

60-Kugombana na kupigana

61-Kuzuilia (watu) maji

62-Kupunja kipimo

63-Kujilinda na Aliyoyapanga Allaah

64-Kuwaudhi waja wema vipenzi vya Allaah

65-Mwanaume kuacha kuswali Swalaah ya jama’ah (Msikitini) na kuswali pekee bila udhuru

66-Kuacha kuswali Ijumaa kwa makusudi au kutotilia umuhimu na kupuuzia

68-Kupanga njama na kufanya hila

69-Kuwapeleleza Waislamu kwa ajili ya makafiri na maadui

70-Kuwatukana Maswahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum)

Hayo ni madhambi 70 aliyojaaliwa Imaam Adh-Dhahabiy (Rahimahu Allaah) kuyakusanya kutoka katika Qur-aan na Sunnah.

Madhambi makubwa mengineyo:

71-Kusherehekea sikukuu za makafiri

72-Kunyoa nyusi

73-Kuunga nywele za bandia

74-Kujichora tattoo

75-Kuvunja mkataba (bila sababu ya ki-shariy’ah)

 

76-Kula nguruwe, nyamafu na damu

77-Kutoa kiapo cha uongo kwenye biashara

78-Kudharau na kuzikebehi Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama ndevu, mswaki wa mti, kupunguza nguo isiburuze kwa wanaume n.k.

79-Kuwakebehi na wakuwapa majina mabaya wale wanaozifuata Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)

80-An-Namiymah (Kufitinisha watu)

81-Ghiybah (kusengenya)

Madhambi Madogo:

Madhambi madogo ni yale ambayo hayamo katika fungu hilo hapo juu nayo ni yale ambayo yamekusudiwa katika kauli ya Allaah (Subhanaahu wa Ta'aalaa): 

 الَّذِينَ يَجْتَنِبُونَ كَبَائِرَ الْإِثْمِ وَالْفَوَاحِشَ إِلَّا اللَّمَمَ ۚ  

Wale wanaojiepusha na madhambi makubwa na machafu isipokuwa makosa madogo-madogo.    [An-Najm: 32]

Madhambi hayo ambayo Allaah Humghfuruia mja maadam mja hatoendelea kuyatenda kila mara kwani kuyaendeleza husababisha kugeuka kuwa ni madhambi makubwa. Mfano kuchanganyika wanawake na wanaume, mtu kuzungumza na asiye Mahram wake bila ya sababu ya ki-shariy’ah, husababisha kukaribia zinaa na huenda yakampeleka mja kutumbukia katika maasi hayo makubwa.

Madhambi madogo kama ilivyo dalili katika Qur-aan na Sunnah kwamba kila jema alifanyalo mja hufuta ovu lake, mfano kufanya wudhuu vizuri, madhambi madogo hupuputika.

Madhambi hayo pia yanaweza kuwa ni kama, kutazama picha na sinema chafu zisizofaa, kusikiliza maovu, kusikiliza na kuimba muziki, riyaa (kujionyesha mtu kwa watu asifiwe), kutamka maneno maovu kama kutukana, kuwa na ghadhabu, mwanamme kuburuza nguo yake ikiwa si kwa makusudi, ama kwa makusudi na kiburi basi inaingia kwenye madhambi makubwa, na mengi mengineyo ambayo hayakuwekewa adhabu kali au laana, au ghadhabu ya Allaah.

Na Allaah Anajua zaidi