Ugonjwa Wa Ndege Ulioingia, Je, Inajuzu Kuwaua Kuku Na Bata?

 

 

SWALI:

Asalam alaykum warahmatullah wa barakatuh

Na anza kwa kumshuru Mungu ambaye yeye ndiye mueza wa kila kitu pia nikitaka ziada ana amani zimuendeye Mtume na waislam watakao mfata mtume hadi soku ya mwisho. Pia niki kutakieni kila la kheri kwa Mwenyezi Mungu kutokana na juhudi ambayo mnayo jitolea kwa kutuelimisha sisi.

Mimi swala langu ni hili mimi ni mwislam naishi nchi bara ulaya, sasa nimepata kazi kuwakamata  kuku  ama bata wagonjwa ili kuwatia  sehemu penye gaz ili wafe, jee hiyo kazi inajuzu mimi kuifanya ? 

Natumayi majibu inshallah wabillah ataufiki.

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kwanza tunapenda na sisi kutoa shukurani kwa du'aa zenu nzuri mnazotuombea nyote mnaotuma maswali yenu pamoja na wengineo wanaoingia ALHIDAAYA kutafuta faida mbali mbali. Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atutakabalie hizo du'aa na Atuzidishie uwezo wa kuelemishana kwa kadiri Anavyotujaalia. Aamiyn

Shukran kwa swali lako hili ambalo ni nyeti sana. Suala la kazi ni suala ambalo limehimizwa sana na Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) katika Qur’an na kutiliwa mkazo sana na Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadithi zake tukufu. Baada ya kusema hayo hatuna budi sisi kuzingatia kazi tunayofanya kwani zipo kazi ambazo haziendi sambamba na misingi ya Uislamu. Kazi kama hizo inakuwa ni haramu kuzifanya.

 

Tunapokuja katika suala lako inatakiwa tuelewe kuwa tumekatazwa kisheria kutoa roho ya kiumbe chochote pasi na ruhusa ya kisheria na inapobidi kutolewa basi inatakiwa itolewe kwa njia ambayo ni nzuri na ya muruwa. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

Hakika Allah Ameamrisha ihsani (wema) katika kila kitu. Kwa hivyo, mkiua ueni vizuri; na mkichinja chinjeni vizuri. Kila mmoja wenu akitie makali kisu chake, na akipunguzie uchungu kichinjwa chake” (Muslim kutoka kwa Abu Ya‘laa Shaddaad ibn Aws [Radhiya Allahu 'anhu]).

 

Na katika msingi wa Uislamu wapo wanyama ambao wanaweza kuuliwa kwa sababu ya amri ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye amesema:

Aina TANO ya wanyama wanaweza kuuliwa hata katika Haram. Hawa ni kunguru, kipanga, nge, panya na mbwa mwenye kichaa (au mkali)” (al-Bukhaariy, Muslim na Maalik kutoka kwa ‘Aa’ishah [Radhiya Allahu 'anhu], na kwenye riwaya ya Muslim kuna nyongeza ya 'nyoka').

Wasiokuwa hawa hawafai kuuliwa isipokuwa kwa sababu ya kuliwa ikiwa wanaliwa au kuondoa madhara ambayo huenda yakapatikana kwa sababu ya ugonjwa ambao kwa tafiti barabara zilizofanywa zimeonyesha kuwa huenda wakawaambukiza binadamu ugonjwa kama ilivyo sasa katika Bara Ulaya na Asia kwa homa hii ya ndege. Lakini suala la kujiuliza sisi ni je, imehakikishwa kuwa kweli huu ugonjwa huwapata wanaadamu kwa ima kula nyama ya hao kuku au kwa kukaa nao pamoja? Au ni maoni tu ya wanasayansi kuwa jambo hilo hutokea bila ya wao kufanya utafiti? Na je, wale kuku au bata wanaouliwa wanapimwa kabla ya kuuliwa au wanashikwa tu walio wazima na wagonjwa na kuuliwa? Ikiwa wanachanganywa wazima na wagonjwa jambo hilo litakuwa halifai kisheria na hivyo kazi hiyo kuifanya haitafaa.

 

Ikiwa ni kweli kuwa wanaadamu hupatikana na ugonjwa kutoka kwa ndege hao basi kisheria ndege hao wanaweza kuuliwa kwa njia nzuri ili kuwaepusha wanaadamu na madhara kutoka kwao. Kwa sababu Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amemkirimu na Kumtukuza binadamu, na viumbe vyote vimeletwa katika kumtumikia yeye mwanadamu ambaye ana majukumu. Lakini inayofaa kutumiwa inatakiwa iwe ni ya kibinadamu na wala sio ya kinyama na ikiwa watakuwa wanatiwa katika gasi basi watakuwa wanawaadhibiwa sana, na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametuusia tuchinje vizuri.

 

Lakini kwa maslahi ya binadamu ikiwa hiyo ndiyo njia ya pekee kuepusha magonjwa hayo kuenea baada ya utafiti basi itakuwa inakubaliwa na hivyo kazi yako ni halali. Ikiwa ipo njia nyingine iliyo nzuri lakini wakubwa hawataki tu kwa maslahi yao wenyewe, njia hiyo munayotumia itakuwa haifai na itabidi ufanye juhudi kuwaeleza hilo. Na wewe ndio muamuzi wa suala hilo kwani unaishi katika mazingira hayo na unaelewa yale ambayo yanayoweza kufanyika na yasiyoweza.

 

Na Allah Anajua zaidi.

 

 

Share