Kumuoa Aliyezini Baada Ya Kutubia

SWALI

JE NINARUHUSIWA KUMUOA MSICHANA AMBAYE ALIKWISHA ZINI AKATUBIA?

 


JIBU

AlhamduliLLaah - Himdi Na Sifa Zote Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukran kwa maswali yako kadhaa kuhusu mas-ala tofauti lakini yote yakiwa takriban kwa njia moja au nyengine ambayo ni kuhusu ndoa na unyumba. Yafuatayo chini ni majibu ya maswali yako hayo:

 

Ni wazi kuwa Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Husamehe madhambi yote ikiwemo dhambi la uzinzi kama alivyosema: “Sema: Enyi waja Wangu mliojidhulumu nafsi zenu! Msikate tamaa na rehema ya Allaah; bila shaka Allah Husamehe dhambi zote; hakika Yeye ni Mwingi wa kusamehe na Mwingi wa kurehemu” (39: 53).

Na hasa kuhusu kusamehewa dhambi la zinaa, Anasema Aliyetukuka: “Na wale wasiomwomba mungu mwengine pamoja na Allaah, wala hawaui nafsi aliyoiharimisha Allah isipokuwa kwa haki, wala hawazini - na atakaye fanya hayo atapata madhara. Atazidishiwa adhabu Siku ya Qiyaama, na atadumu humo kwa kufedheheka. Isipokuwa atakayetubu, na akaamini, na akatenda vitendo vyema. Basi hao Allah Atayabadilisha maovu yao yawe mema. Na Allah ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. Na aliyetubu na akafanya mema, basi hakika huyo ametubu kweli kweli kwa Allah” (25: 68 – 71). Tafadhali tazama sehemu zilizopigwa msitari kwa kuweza kuelewa zaidi ayah zilizo juu.

 

Na kuhusu mas-ala ya kusamehewa kwa dhambi hilo, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mche Allah popote ulipo. Na ufuatilize jambo baya kwa jema, litalifuta (hilo baya)” (at-Tirmidhiy, ambaye amesema ni Hadith Hasan, na katika baadhi ya nuskha ni Hasan Swahiyh, pia na Ahmad, ad-Daarimiy, nayo ni Hadiyth Swahiyh).

 

Kuhusu mas-ala haya Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema: “Mwanamume mzinifu hatamwoa ila mwanamke mzinifu au mwanamke mushrik, na hamna atakayemwoa mwanamke mzinifu isipokuwa mwanamume mzinifu au mushrik; na ndoa kama hizo zimeharamishwa kwa Waumini wa kweli. …Isipokuwa wale wenye kutubu baada ya hayo na kujirekebisha; bila shaka Allah ni Msamehevu na Mrehemevu” (24: 3, 5).

 

Kuhusu ayah hizi anasema Ibn Kathiyr: “Amesema Imaam Ahmad kuwa haifai ndoa baina ya wazinifu mpaka watubu, akitubu inasihi nikaah. Na hivyo ndivyo alivyosema Imaam Abu Muhammad ibn Abi Haatim ambaye amemnukuu Ibn ‘Abbaas (Radhiya Llaahu ‘anhuma) kuwa alikuja mtu ambaye amezini akamuuliza kama anaweza kumuoa yule mwanamke baada ya kuwa ametubia, lakini watu wamemwambia haifai kwa kumsomea ayah ya 3 (hapo juu). Ibn ‘Abbaas (Radhiya Llaahu ‘anhuma) alimwambia hiyo si mahali pake, unaweza kumuoa. Na wanazuoni wengine wanasema kuwa ayah hii imetenguliwa hukumu yake na ile ayah, ‘Na waozeni wajane miongoni mwenu’ (24: 32), yaani Waislamu” (Tafsiyrul Qur-aanl ‘Adhiym, Mj. 3, uk. 270 – 272).

 

Naye Shaykh Muhammad ‘Aliy asw-Swaabuuniy anauliza, je inasihi ndoa na mwanamke mzinifu? Naye akajibu kwa kusema: “Wametofautiana wanazuoni wa zamani katika jambo hili katika makundi mawili:

 

(a) Kuharamishwa ndoa, nayo ni rai ya ‘Aliy, al-Baraa’, ‘Aaishah na Ibn Mas‘uud (Radhiya Llaahu ‘anhum).

 

(b) Kujuzu ndoa na aliyezini, nayo ni rai ya Abu Bakr, ‘Umar, Ibn ‘Abbaas (Radhiya Llaahu ‘anhum) na ni madhehebu ya Jamhuur na kwayo wamesema Mafakihi wanne na Maimamu waliojitahidi.

 

Dalili za Rai ya Kwanza ya wanaosema kuwa haifai

 

Wametoa dalili wanaoharamisha kwa dhahiri ya ayah nayo ni kauli ya Aliyetukuka: “Mwanamume mzinifu hatamwoa ila mwanamke mzinifu au mwanamke mushrik” (24: 3). Wakasema: Dhahiri ya ayah hii ni habari na uhakika wake ni kukataza na kuharamisha kwa dalili nyengine katika ayah hiyo: “Na ndoa kama hizo zimeharamishwa kwa Waumini wa kweli”. Na amesema ‘Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu): Anapozini mtu yeyote anatenganishwa baina yake na mkewe, na hivyo hivyo akizini mke.

 

Na wametoa dalili kwa yaliyotokea kwa Marthad ibn Abi Marthad (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliyekuwa Swahaba, naye alizini na ‘Inaaq, mwanamke malaya Makkah wakati wa ujahiliya. Alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumuomba ruhusa amuoe. Alimuomba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mara mbili bila kujibiwa. Alipomuomba mara ya tatu, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimsomea ayah hii na akamwambia asimuoe (Abu Daawuud na at-Tirmidhiy). Na zipo Hadiyth nyengine kutoka kwa Ibn ‘Umar na ‘Ammaar (Radhiya Llaahu ‘anhum) zinazoelezea jambo hilo.

 

 

Dalili za Rai ya Pili ya wanaosema inafaa (Rai ya Jamhuur)

 

Wametoa dalili zao kwa kuruhusiwa ndoa kama ifuatavyo:

 

(i)    Hadiyth ya ‘Aaishah (Radhiya Llaahu ‘anha) kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa kuhusu mtu aliyezini na mwanamke na akataka kumuoa, akasema: “Mwanzo ni uchafu na mwisho ndoa, na haramu haifanyi halali kuwa haramu” (Atw-Twabaraaniy na ad-Daaraqutwniy).

 

(ii)   Iliyopokewa kutoka kwa Ibn ‘Umar (Radhiya Llaahu ‘anhuma) kuwa: “Alipokuwa Abu Bakr yuko Msikitini mara akaja mtu ambaye alikuwa anataka kumwambia kitu lakini hakuweza kueleza kwa ufasaha. Abu Bakr alimwomba ‘Umar amchukue yule mtu kando ili amdadisi kuwa anataka kusema nini. Alipomwuliza, alimwambia kuwa kuna mgeni aliyemtembea naye amezini na binti yake. Hapo ‘Umar alimpiga kwenye kifua chake na kumwambia: ‘Ole wako, kwa nini usingesitiri aibu ya binti yako?’ Abu Bakr aliamuru wote wawili wapatiwe adhabu, kisha akawaoza na kuhamishwa mbali na mji kwa mwaka mmoja” (Qaadhi Abu Bakr Ibn al-‘Arabiy, Ahkaamul Qur-aan, Mj. 3, uk. 1319).

(iii)   Imepokewa kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhiya Llaahu ‘anhuma) aliulizwa kuhusu mas-ala hayo, akasema: “Mwanzo ni uchafu, na mwisho ni ndoa. Mfano wa hilo ni kama mfano wa mtu aliyeiba tunda katika bustani, baada ya hapo alikuja kwa mwenye bustani na kununua kutoka kwake matunda yake. Aliyoiba ni haramu, na aliyonunua ni halali” (Tafsiyrul Qurtwubiy, Mj. 12, uk. 170).

(iv)   Wameawili ayah hii tukufu: “Mwanamume mzinifu hatamwoa ila mwanamke mzinifu au mwanamke mushrik” (24: 3). Hii imechukuliwa kwa ujumla na wingi wake, na maana yake ni kuwa fasiki (asi) mwovu ambaye ni mzinifu hatamani kuoa Muumini mwanamke mwema, hakika ni kuwa yeye ana hamu ya kuoa aliye asi mwovu mfano wake au mshirikina. Na mwanamke asi mbaya hana hamu ya kuolewa na Muumini mwema miongoni mwa wanaume, kwani hakika yake ni kuwa yeye ataka jinsi ya mfano wake wa asi na mushirikina.

(v)   Na wamesema baadhi ye wengine: Ayah hii hukumu yake imetenguliwa na ayah nyengine ya Suratun Nuur: 32 (Tafsiyr Aayaatul Ahkaam minal Qur-aan, Mj. 2, uk. 36 – 37).

Na Dkt. ‘Aliy ‘Abdul-Haliym Mahmuud katika kitabu chake at-Tarbiyyatul Islaamiyyah Fiy Suratin Nuur, uk. 36 – 41 amesema yafuatayo: “Muislamu hafai kuoa au kuolewa na mzinifu ambaye bado yupo katika kazi hiyo na wala hajatubia.. Wanazuoni wengine wanaona kuwa makusudio ya ayah hii tukufu ina maana ya jimai kwa neno Yankihu Katazo hapa ni ikiwa wazinifu wamepatiwa adhabu haitofaa kuolewa au kuoa mwengine na hiyo ni kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ‘Haoi mzinifu aliyepigwa mijeledi isipokuwa mfano wake’ (Abu Daawuud). Na wanazuoni wengine wanasema ayah hii ilikuwa ni hasa kwa Marthad (Radhiya Llaahu ‘anhuma) na kahaba aliyeitwa ‘Inaaq. Na wengine wanasema yeyote mwenye kuzini na mwanamke anafaa amuoe na asiolewe na mwengine yeyote, nayo ni kauli ya Ibn ‘Umar, Saalim, Jaabir ibn Zayd, ‘Atwaa’, Twaawuus, Maalik ibn Anas na Abu Haniyfah”.

Kwa muhtasari ni kuwa wazinifu wakitubia na kujirekebisha basi wanaweza kuoana.

Kwa kupata maelezo zaidi soma Maswali na Majibu katika viungo vifuatavyo katika Alhidaaya:

Ndoa Ya Wazinifu

 Ndoa Baada Ya Kutubu Zinaa

 Ndoa Waliofanya Zinaa

 Wazinifu Waliotubu Wanawea Kufanya Ndoa Na Waliotakasika?

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share