Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
النُّشُوْزُ وَعِلَاجُهُ
Uasi Wa Mke Kwa Mume Na Njia Za Kuutibu
03: Hatua Za Kutibu Uasi Wa Mke: (B) Hatua Ya Pili: Atamsusa Kitanda:
Hii ni kwa Kauli Yake Ta'aalaa:
"وَاهْجُرُوهُنَّ فِي الْمَضَاجِعِ"
"Na wahameni katika malazi". [An-Nisaa: 34]
Kumsusa hapa kuna maana ya kutolala naye kitanda kimoja ili kumshinikiza apate kurudi kwenye utiifu. Kwanza, atamtisha kwamba hatolala naye kitanda kimoja, na hatomuingilia, kwani huenda akawa ni katika wanawake wasioliweza hilo. Na kama atarudi kwenye utiifu itakuwa basi, lakini akiendelea na uasi wake, basi atamhama kikweli.
'Ulamaa wamezungumza mengi kuhusiana na namna ya kumsusa mke kitanda. Kuna waliosema kuwa ni kuacha kumjimai. Wengine wanasema kuwa atamjimai, lakini wakati wa kufanyika tendo hatozungumza naye, kwa kuwa tendo la jimai ni haki ya pamoja kati yao, na mume akimtia adabu kwa kutomuingilia, basi yeye pia ataumia kwa kuikosa jimai. Lakini wengine wamesema kuwa atamgomea kumuingilia wakati anapokuwa mkewe ameshikwa na hamu sana.ya jimai, na si wakati yeye (mume) anaposhikwa na hamu, kwa kuwa kususa ni kwa ajili ya kumtia adabu mke na si mume.
Lililo sawa ni kumsusa kwa namna yoyote anayoona inafaa kumrejesha katika utiifu kwa mujibu wa mazingira yalivyo. Pamoja na hayo, mume anatakiwa asimsuse mkewe isipokuwa ndani ya nyumba yao kama alivyosema Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam):
"وَلاَ تَهْجُرْ إِلا فِي البَيْتِ"
"Wala usimsuse isipokuwa ndani ya nyumba". [Hadiyth Hasan. Abu Daawuwd (2142) na Ibn Maajah (1850). Imetajwa nyuma]
Na hii ni ili watu wa nje wasipate kujua, kwani wakijua, itakuwa ni udhalilisho kwake, na hili linaweza kukoleza zaidi tatizo akazidi ukorofi. Kuchunga hili na mfano wake, kutasaidia kurudisha tena mtangamano na utulivu kati ya mke na mume.
Lakini, endapo ataona kumsusa nje ya nyumba kutakuwa na maslahi ya kisharia, basi atafanya hivyo. Ni kama alivyofanya Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa wakeze nje ya nyumba zao kwa muda wa mwezi mzima.
Kadhalika, anatakiwa asionyeshe ususiaji huo kwa watoto, kwani hilo litajenga kwenye roho zao shari na uharibifu.
Muda Wa Kumsusa:
'Ulamaa wana kauli mbili kuhusiana na ukomo wa muda wa kumsusa mke jimai:
Ya kwanza: Ni mwezi mmoja, na anaweza kuongeza hadi kufikia miezi minne. Ni madhehebu ya 'Ulamaa wa Kimaalik, na dalili yao ni kwamba Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliwafanyia wakeze "الإيْلاءُ" kwa muda wa mwezi mmoja, na kwamba muda wa "الإيْلاءُ" ni miezi minne tu.
["الإيْلاءُ" ni mume kumwapia mkewe kwamba hatomuingilia kwa muda wa miezi minne]
Kufanya "الإيْلاءُ" hapa kama ni kipimo hakuendani, kwa kuwa kumhama mke kutokana na uasi wake, ni kwa ajili ya kumtia adabu ili aache ukorofi wake, lakini kwa upande wa "الإيْلاءُ" , hiyo mume anaweza kuifanya hata bila mke kuwa mkorofi. Na kwa ajili hiyo, "الإيْلاءُ" hairuhusiwi kwa zaidi ya miezi minne kwa sababu ni dhulma kwa mwanamke. Isitoshe, "الإيْلاءُ" ni kiapo.
Ya pili: Atamsusa muda atakao mpaka aache tabia yake. Ni madhehebu ya Jumhuwr ya 'Ulamaa. Dalili yao wanasema kwamba aayah inayozungumzia kumsusa mwanamke haijaweka ukomo wa muda, na asili ni kuachwa wazi mpaka ije dalili ya kuainisha muda.
Faida:
Inaruhusiwa kumsusa kwa kuacha kumsemesha na kuzungumza naye. Lakini 'Ulamaa wamekhitilafiana kuhusu muda wake. Jumhuwr ya 'Ulamaa wamesema kwamba haijuzu kutozungumza naye kwa zaidi ya siku tatu hata kama ataendelea na uasi wake kutokana na neno lake Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema:
"لا يَحِلُّ لِمُسْلِم أَنْ يَهْجُرَ أَخَاهُ فَوْقَ ثَلَاثَةِ أَيَّام"
"Si halali kwa Muislamu kumsusa nduguye kwa zaidi ya siku tatu". [Hadiyth Swahiyh. Al-Bukhaariy na Muslim]
Inaweza kusemwa: Ikiwa kumsusa kwa mazungumzo katika siku tatu hakujaleta tija, basi zaidi ya hapo haitasaidia, kwa kuwa taathira yake ni ndogo zaidi kwa mwanamke kuliko ya kumsusa jimai.
Baadhi ya 'Ulamaa wa Kishaafi'iy wanaona kwamba inafaa kwa mume kutozungumza na mkewe mwasi kwa zaidi ya siku tatu ikiwa ni kwa lengo la kumtia adabu na kumrejesha kwenye utiifu. Dalili yao wanasema kwamba Rasuli (Swalla Allaah 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliwasusa Maswahaba watatu ambao hawakwenda naye vitani kwa zaidi ya siku tatu.
Basi ikiwa mwanamke ni katika ambao haisaidii kuwasusa kwa maneno au kwa jimai kutokana na ususuavu wa tabia, hapo itabidi mume atumie njia ya tatu.