بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ
الْحَمْدُ لِلَّهِ، وَالصَّلاةُ وَالسَّلامُ عَلَى خَاتَمِ الأَنْبِيَاءِ وَالْمُرْسَلِينَ، الْمَبْعُوثِ رَحْمَةً لِلْعَالَمِينَ، مُحَمَّدٍ وَعَلَى آلِهِ وَأَصْحَابِهِ أَجْمَعِينَ، وَمَنْ تَبِعَهُمْ بِإِحْسَانٍ إِلَى يَوْمِ الدِّينِ
Himdi zote Anastahiki Allaah, na Swalaah na Salaam ziwe juu ya Nabiy na Rasuli wa mwisho, aliyetumwa kuwa Rehma kwa walimwengu, Muhammad, pamoja na ahli zake na Swahaba zake wote, na wanaowafuata kwa ihsaan mpaka Siku ya Malipo.
Al-Asmaa Al-Husnaa (Majina Mazuri kabisa) imetajwa katika Qur-aan mara nne, katika Kauli zifuatazo za Allaah (سبحانه وتعالى):
قُلِ ادْعُوا اللَّـهَ أَوِ ادْعُوا الرَّحْمَـٰنَ ۖ أَيًّا مَّا تَدْعُوا فَلَهُ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ ۚ
Sema: Muiteni Allaah au muiteni Ar-Rahmaan, vyovyote mtakavyomwita basi Yeye Ana Majina Mazuri kabisa. [Al-Israa (17:110)]
Na:
اللَّـهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۖ لَهُ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ ﴿٨﴾
Allaah, hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye. Anayo Majina Mazuri kabisa. [Twaahaa (20:8)]
Na:
وَلِلَّـهِ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ فَادْعُوهُ بِهَا ۖ وَذَرُوا الَّذِينَ يُلْحِدُونَ فِي أَسْمَائِهِ ۚ سَيُجْزَوْنَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿١٨٠﴾
Na Allaah Ana Majina Mazuri kabisa, basi muombeni kwayo. Na waacheni wale wanaopotoa na kuharibu Majina Yake, watalipwa yale waliyokuwa wakiyatenda. [Al-A’raaf (7:180)]
Na:
هُوَ اللَّـهُ الْخَالِقُ الْبَارِئُ الْمُصَوِّرُ ۖ لَهُ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ ۚ يُسَبِّحُ لَهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ﴿٢٤﴾
Yeye Ndiye Allaah, Muumbaji, Mwanzishi wa viumbe bila kasoro, Muundaji sura na umbile, Ana Majina Mazuri kabisa. Kinamsabihi Pekee kila kilichoko katika mbingu na ardhi, Naye Ndiye Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote. [Al-Hashr (59:24)]
Maana Ya Al-Husnaa:
Majina ya Allaah (تعالى) na Sifa Zake yote ni husnaa, yaani yamefikia upeo wa uzuri. Na neno al-husnaa ni la jinsia ya kike la al-ahsan (lililo zuri zaidi), kama vile al-kubraa na asw-sughraa kwa al-akbar na al-asw-ghar. Na yameitwa husnaa kwa sababu kadhaa:
1-Yanaonyesha Sifa za ukamilifu mkubwa.
2-Utukufu wa ilimu yake; ilimu ya Majina Yake ndiyo ilimu tukufu kabisa.
3-Thawabu zilizoahidiwa kwayo: kuingizwa Jannah kwa atakayeyahifadhi (ahswaahaa), thawabu kwa mja anapomdhukuru Allaah kwayo, na kupewa kwa wingi anapomuomba kwayo.
4-Ni mazuri masikioni na nyoyoni.
5-Katika ukamilifu wa uzuri wake ni kwamba Allaah Haombwi isipokuwa kwayo.
Kumpwekesha Allaah Katika Majina Yake Na Kuthibitisha Sifa Zake (سبحانه وتعالى): ‘Aqiydah Ya Ahlus-Sunnah Wal-Jamaa’ah
‘Aqiydah ya Ahlus-Sunnah wal-Jamaa’ah kuhusu Majina Mazuri kabisa ya Allaah (سبحانه وتعالى) na Sifa Zake ni kwamba ni tawqiyfiyyah (yanathibitishwa kwa dalili tu); yanathibitishwa yale Aliyoyathibitisha Mwenyewe Allaah (سبحانه وتعالى) katika Qur-aan na Sunnah, bila ya kuyafanyia ta’twiyl (kuyapinga na kuyakanusha), wala tamthiyl (kuyamithilisha na kuyalinganisha na viumbe), wala takyiyf (kuainisha namna yake na kuuliza ni vipi yalivyo), wala tahriyf (kubadilisha maana yake na kuyapotosha). Na hayo ni katika mambo ya ghaibu yasiyojulikana isipokuwa kwa yale yaliyokuja kutoka kwa Allaah na Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم); kwa hiyo mlango huu si mlango wa ijtihaad (kujitahidi kwa rai).
Hivyo basi, Allaah (سبحانه وتعالى) Anaposema kwamba Ana Qudrah (Uwezo), sisi tunaamini kwamba Anao Uwezo. Anaposema kwamba Yeye Ni Al-Qawiyy (Mwenye Nguvu), sisi tunaamini kwamba Ana Nguvu. Anaposema kwamba Anaona, sisi tunaamini kwamba Anaona, na Anaposema kwamba Anasikia, sisi tunaamini kwamba Anasikia. Lakini Sifa hizo za Uwezo Wake, Nguvu Zake, Kuona Kwake na Kusikia Kwake hazifanani kabisa na za kiumbe chochote! Na Anaposema kwamba Anayo Macho, Mikono na Wajihi, sisi tunaamini kwamba Anayo Macho, Mikono na Wajihi, lakini hakuna kabisa mfano Wake kwa kiumbe chochote. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ ﴿١١﴾
Hakuna chochote kinachofanana Naye, Naye Ni Mwenye Kusikia yote, Mwenye Kuona yote. [Ash-Shuwraa (42:11)]
Kwa hiyo Anapotujulisha kwamba Yeye Ni Al-‘Aliym (Mjuzi wa yote daima), hatuwezi kusema hivyo kwa binaadam. Na kadhaalika hatuwezi kufananisha Sifa Zake nyinginezo na za kiumbe chochote, wala kumfananisha, wala kumlinganisha, wala kumshabihisha Yeye kwa Dhati Yake au Sifa Zake na yeyote. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
فَلَا تَضْرِبُوا لِلَّـهِ الْأَمْثَالَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ ﴿٧٤﴾
Basi msimpigie mifano Allaah. Hakika Allaah Anajua nanyi hamjui. [An-Nahl (16:74)]
Kutozithibitisha Sifa ambazo Allaah (سبحانه وتعالى) Amejithibitishia Mwenyewe ni kuzipotoa na kuzigeuza, na Allaah Ameonya dhidi ya wanaopotoa katika Majina Yake, kama ilivyotangulia katika Al-A’raaf (7:180).
Aina Za Ilhaad (Upotoaji) Katika Majina Ya Allaah:
Ilhaad katika Majina ya Allaah (سبحانه وتعالى) ni kuyageuza Majina hayo, uhakika wake na maana zake mbali na haki iliyothibiti. Na miongoni mwa aina zake ni:
1-Kuyaita masanamu kwayo; kama washirikina walivyoliita sanamu Al-Laat kutokana na Al-Ilaah, Al-‘Uzzaa kutokana na Al-‘Aziyz, na Manaat kutokana na Al-Mannaan, na kuliita sanamu ilaah (mwabudiwa).
2-Kumwita Allaah kwa yasiyolingana na Ujalali Wake; kama Manaswara wanavyomwita “Baba”, wanafalsafa wanavyomwita “Sababu Itendayo”, baadhi ya wapotofu wanavyomwita “Mhandisi wa ulimwengu”, na majina yasiyo Yake yanayotamkwa na baadhi ya watu wa kawaida.
3-Kuyavua Majina maana zake na kukanusha uhakika wake. Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) amesema: “Ilhaad ni kukadhibisha.” Na miongoni mwa hayo ni kauli ya wanaozikanusha Sifa (mu’attwilah) kwamba ni matamshi matupu yasiyoonyesha maana wala kubeba Sifa. Ametukuka Allaah na yale wanayoyasema!
4-Kuzifananisha Sifa kubwa zilizomo ndani ya Majina Mazuri ya Allaah na sifa za viumbe, na hali Allaah Anasema: “Hakuna chochote kinachofanana Naye”, kama ilivyotangulia katika Ash-Shuwraa (42:11).
Hiyo ndiyo ‘Aqiydah sahihi kabisa waliyoiitakidi Salaf wa Ummah, na ndivyo ipasavyo kuzikubali Sifa zote za Allaah (سبحانه وتعالى) bila ya kukisia kwa akili zetu namna yake au mfano wake, wala kuogopa kuzithibitisha zilivyo kwa kukhofia kuzifananisha na za viumbe. Kuzithibitisha vile vile zilivyokuja katika Kitabu Chake, kama Alivyoziita Mwenyewe (عزّ وجلّ) na kama Alivyotaka Yeye, ndio salama kwetu. Tujisalimishe kwa yale Aliyojithibitishia Mwenyewe na aliyoyathibitisha Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم), kwani akili zetu haziwezi kufikia upeo wa kutambua Sifa Zake (عزّ وجلّ). Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَلَا تَقْفُ مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ ۚ إِنَّ السَّمْعَ وَالْبَصَرَ وَالْفُؤَادَ كُلُّ أُولَـٰئِكَ كَانَ عَنْهُ مَسْئُولًا ﴿٣٦﴾
Na wala usifuate usiyo na ilimu nayo. Hakika masikio na macho na moyo; vyote hivyo vitaulizwa. [Al-Israa (17:36)]
Na Anasema pia (سبحانه وتعالى):
يَعْلَمُ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ وَلَا يُحِيطُونَ بِهِ عِلْمًا ﴿١١٠﴾
Anajua yale yaliyoko mbele yao, na yale yaliyoko nyuma yao, na wala hawawezi kufikia kuelewa chochote cha Ujuzi Wake. [Twaahaa (20:110)]
Umuhimu Wa Kuyajua Na Kujifunza Majina Mazuri Kabisa Ya Allaah (سبحانه وتعالى) Na Sifa Zake:
1-Ilimu Ya Majina Ya Allaah Na Sifa Zake Ni Kumtambua Allaah Na Utukufu Wake:
Unapotaka kuamiliana na mtu, hapana shaka utataka kujua jina lake, kun-yah yake na khabari zake ili upate ufahamu bayana kumhusu hadi uridhike kuamiliana naye. Allaah (سبحانه وتعالى) Ametuumba, Naye Ndiye Anayeturuzuku kila kitu, na tunakhofu Ghadhabu Zake na tunataraji Rehma Yake Atughufurie madhambi yetu na Asituadhibu. Kwa hiyo hapana budi kutambua yale yanayomridhisha ili Naye Aturidhie, na kutambua yale yanayomghadhibisha ili tujiepushe nayo. Kama vile ambavyo huwezi kumpenda usiyemjua, vilevile huwezi kumkhofu Allaah (سبحانه وتعالى) na kumpenda kwa haki inavyostahiki isipokuwa kwa kuutambua Utukufu Wake, na njia mojawapo ni kuyatambua Majina Yake Mazuri kabisa na Sifa Zake. Na haiwezekani kumwabudu Allaah kwa baswiyrah (utambuzi), wala kumuomba kwa Majina Yake, kabla ya kuyajua na kuzifahamu maana zake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَلَا تَكُونُوا كَالَّذِينَ نَسُوا اللَّـهَ فَأَنسَاهُمْ أَنفُسَهُمْ ۚ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْفَاسِقُونَ ﴿١٩﴾
Na wala msiwe kama wale waliomsahau Allaah, Naye (Allaah) Akawasahaulisha nafsi zao. Hao ndio mafasiki. [Al-Hashr (59:19)]
Hivyo, kumtambua Allaah kunapelekea kumpenda, kumkhofu, kutawakali Kwake, kumtakasia niyyah (ikhlaasw) katika amali, na kutaraji Rehma Yake.
2-Ilimu Ya Majina Ya Allaah Na Sifa Zake Ni Ilimu Ya Msingi:
Ilimu ya Majina ya Allaah na Sifa Zake ni ilimu ya msingi, kwani ni aina ya tatu ya Tawhiyd. Na Tawhiyd ndilo jambo kuu walilokuja nalo Rusuli wote katika ulinganiaji wao, na ni ilimu bora na tukufu kabisa kuitambua. Nalo ndilo lengo kuu la kuumbwa kwetu: kumpwekesha Allaah (سبحانه وتعالى) katika ‘ibaadah.
3-Ilimu Ya Majina Ya Allaah Na Sifa Zake Inazidisha Imaan:
Ilimu ya Majina ya Allaah na Sifa Zake ni sababu ya kuzidisha imaan, kama alivyosema Imaam As-Sa’diy (رحمه الله): “Hakika kuamini Asmaa Allaah Al-Husnaa na kuyatambua kunajumuisha aina tatu za Tawhiyd: Tawhiyd Ar-Rubuwbiyyah, Tawhiyd Al-Uluwhiyyah (‘Ibaadah) na Tawhiyd Al-Asmaa wasw-Swifaat. Na aina hizi ndizo roho ya imaan, na ndizo furaha halisi na kitulizo cha dhiki za moyo, na ndizo asili yake na lengo lake. Basi kila mja anapozidi kuyatambua Majina ya Allaah na Sifa Zake, ndivyo inavyozidi imaan yake na kuthibiti yakini yake.” [At-Tawdhwiyh Wal-Bayaan Li-Shajaratil-Iymaan Lis-Sa’diy (41)]
4-Ilimu Ya Majina Ya Allaah Na Sifa Zake Ni Sababu Ya Kupata Jannah:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((إِنَّ لِلَّهِ تِسْعَةً وَتِسْعِينَ اسْمًا، مِائَةً إِلاَّ وَاحِدًا، مَنْ أَحْصَاهَا دَخَلَ الْجَنَّةَ))
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika Allaah Ana Majina tisini na tisa, mia kasoro moja; atakayeyahifadhi (ahswaahaa) ataingia Jannah.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]
Ahswaahaa imekusudiwa: Kuyafahamu maana zake, kuyahifadhi, kuyafanyia kazi, na kumuomba Allaah kwayo, kama Anavyosema Allaah (سبحانه وتعالى) katika Al-A’raaf (7:180) iliyotangulia.
Imaam Ibn Al-Qayyim na Al-Khattwaabiy wamezikusanya maana za ahswaahaa katika daraja tatu zinazokaribiana:
i-Kuyahifadhi: kuyahesabu matamshi yake na idadi yake mpaka mtu ayahifadhi yote, kama walivyosema Al-Bukhaariy na An-Nawawiy, wakitoa dalili kwa riwaayah nyingine ya Muslim: “Atakayeyahifadhi ataingia Jannah.”
ii-Kuyafahamu: kufahamu maana zake na yanayoonyeshwa nayo, na kuyachunga vizuri.
iii-Kumuomba kwayo: Du’aa ya kumsifu na kumwabudu, na Du’aa ya kumuomba haja.
Na Al-Qurtwubiy amesema: “Katika Ukarimu wa Allaah (تعالى) ni kwamba atakayefikia kuyahifadhi Majina haya katika daraja mojawapo kati ya hizi, pamoja na niyyah sahihi, Allaah Atamuingiza Jannah. Na daraja hizi tatu ni za waliotangulia (as-saabiquwn), maswiddiyq, na watu wa kuliani (asw-haab al-yamiyn).”
Imaam Ibn ‘Uthaymiyn (رحمه الله) amesema: “Ahswaahaa haimaanishi kuyaandika Majina ya Allaah (سبحانه وتعالى) kwenye karatasi na kuyakariri mpaka mtu ayahifadhi, bali inamaanisha:
i-Kujifunza kuyatamka.
ii-Kufahamu maana zake.
iii-Kumwabudu Allaah kwayo, kwa njia mbili:
Kwanza: Kumuomba Du’aa kwayo, kwa sababu Allaah Anasema: “Na Allaah Ana Majina Mazuri kabisa, basi muombeni kwayo.” Kwa hiyo yafanye kuwa ni wasiylah (njia ya kujikurubisha) ya Du’aa yako, na uchague Jina linalowafikiana na haja yako. Unapotaka kuomba maghfirah, useme:
يَا غَفُورُ اغْفِرْ لِي
Yaa Mwingi wa Kughufuria, Nighufurie.
Na usiseme:
يَا شَدِيدَ الْعِقَابِ اغْفِرْ لِي
Yaa Mkali wa Kuakibu, Nighufurie. Kwani hii inakuwa kama ni istihzaa (kufanyia mzaha). Linalopasa (ukimwita Allaah hivyo) ni kusema: Yaa Mkali wa Kuakibu, Niepushe na Ikabu Yako.
Pili: Katika ‘ibaadah zako, vitendo vyako vionyeshe maana ya Majina Yake. Kwa mfano, Ar-Rahiym (Mwenye Kurehemu) linakusudia Rehma; basi fanya amali njema zitakazosababisha kupata Rehma ya Allaah.
Hiyo ndiyo maana ya ahswaahaa. Basi yatakapotekelezwa hayo, ndipo itakapostahiki kuingizwa Jannah.” [Majmuw’ Fataawa wa Rasaail Ibn ‘Uthaymiyn (1/74)]
Na mwenye kuzitafakari Du’aa zilizokuja katika Qur-aan na Sunnah, ataona kwamba kila Du’aa inayomalizika kwa Jina katika Majina Mazuri ya Allaah, Jina hilo linanasibiana na jambo linaloombwa, kama Du’aa ya Nabiy Ibraahiym na Ismaa’iyl (عليهما السلام):
رَبَّنَا تَقَبَّلْ مِنَّا ۖ إِنَّكَ أَنتَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ ﴿١٢٧﴾
Rabb wetu, Tutakabalie, hakika Wewe Ni Mwenye Kusikia yote, Mjuzi wa yote. [Al-Baqarah (2:127)]
Na katika kumwabudu Allaah kwa Majina Yake ni: kutubia Kwake kwa sababu Yeye Ni At-Tawwaab (Mwingi wa Kupokea Tawbah); kumdhukuru kwa ulimi wako kwa sababu Yeye Ni As-Samiy’ (Mwenye Kusikia yote); kumwabudu kwa viungo vyako kwa sababu Yeye Ni Al-Baswiyr (Mwenye Kuona yote); kumkhofu kwa siri kwa sababu Yeye Ni Al-Latwiyf Al-Khabiyr (Mjuzi wa ya dhahiri na ya siri); na kutawakali Kwake katika wahka wako kwa sababu Yeye Ni Al-Wakiyl Al-Kaafiy (Mtegemewa, Mwenye Kutosheleza); na hivyo hivyo kwa Majina Yake yote.
5-Fadhila Nyinginezo Za Kuyajua Majina Ya Allaah Na Kuyafanyia Kazi:
a-Kupata baraka, kwani baraka hupatikana kwa kulitaja Jina Lake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
تَبَارَكَ اسْمُ رَبِّكَ ذِي الْجَلَالِ وَالْإِكْرَامِ ﴿٧٨﴾
Tabaarak, Limebarikika Jina la Rabb wako Mwenye Ujalali na Ukarimu. [Ar-Rahmaan (55:78)]
b-Kujikurubisha kwa Allaah na kupata Ma’iyyah Yake (Kuwa Pamoja Naye) maalumu.
c-Ni sababu ya kuitikiwa Du’aa, kwa Kauli Yake: “basi muombeni kwayo.”
d-Kuzijua maana zake na kuzifanyia kazi ni chanzo kikuu cha furaha ya kweli; kwani anayeliadhimisha Jambo la Allaah, mambo yote ya dunia huwa madogo kwake.
e-Kila mja anapozidi kuyajua Majina ya Allaah, ndivyo dhana yake njema kwa Allaah inavyozidi kuwa nzuri.
f-Kama alivyosema Abuu ‘Abdillaah Al-Antwaakiy: “Aliye mjuzi zaidi wa Allaah ndiye mwenye kumkhofu zaidi.”
Majina Ya Allaah Si Tisini Na Tisa Pekee:
‘Ulamaa wamekubaliana kwamba Majina ya Allaah si tisini na tisa pekee, wala hayana idadi maalumu, kama walivyonukuu An-Nawawiy, Ibn Taymiyyah na wengineo; kwani haiwezekani Majina Yake yawe na mwisho, kwa kuwa Sifa Zake na Fadhila Zake hazina mwisho. Na dalili yake ni Hadiyth ifuatayo:
عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ مَسْعُودٍ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((مَا أَصَابَ أَحَدًا قَطُّ هَمٌّ وَلاَ حَزَنٌ فَقَالَ: اللَّهُمَّ إِنِّي عَبْدُكَ، وَابْنُ عَبْدِكَ، وَابْنُ أَمَتِكَ، نَاصِيَتِي بِيَدِكَ، مَاضٍ فِيَّ حُكْمُكَ، عَدْلٌ فِيَّ قَضَاؤُكَ، أَسْأَلُكَ بِكُلِّ اسْمٍ هُوَ لَكَ، سَمَّيْتَ بِهِ نَفْسَكَ، أَوْ عَلَّمْتَهُ أَحَدًا مِنْ خَلْقِكَ، أَوْ أَنْزَلْتَهُ فِي كِتَابِكَ، أَوِ اسْتَأْثَرْتَ بِهِ فِي عِلْمِ الْغَيْبِ عِنْدَكَ، أَنْ تَجْعَلَ الْقُرْآنَ رَبِيعَ قَلْبِي، وَنُورَ صَدْرِي، وَجَلاَءَ حُزْنِي، وَذَهَابَ هَمِّي، إِلاَّ أَذْهَبَ اللَّهُ هَمَّهُ وَحُزْنَهُ، وَأَبْدَلَهُ مَكَانَهُ فَرَجًا)). فَقِيلَ: يَا رَسُولَ اللَّهِ، أَلاَ نَتَعَلَّمُهَا؟ فَقَالَ: ((بَلَى، يَنْبَغِي لِمَنْ سَمِعَهَا أَنْ يَتَعَلَّمَهَا))
Amesimulia ‘Abdullaah bin Mas’uwd (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakuna yeyote aliyefikwa na wahka au huzuni kisha akasema:
اللَّهُمَّ إِنِّي عَبْدُكَ، وَابْنُ عَبْدِكَ، وَابْنُ أَمَتِكَ، نَاصِيَتِي بِيَدِكَ، مَاضٍ فِيَّ حُكْمُكَ، عَدْلٌ فِيَّ قَضَاؤُكَ، أَسْأَلُكَ بِكُلِّ اسْمٍ هُوَ لَكَ، سَمَّيْتَ بِهِ نَفْسَكَ، أَوْ عَلَّمْتَهُ أَحَدًا مِنْ خَلْقِكَ، أَوْ أَنْزَلْتَهُ فِي كِتَابِكَ، أَوِ اسْتَأْثَرْتَ بِهِ فِي عِلْمِ الْغَيْبِ عِنْدَكَ، أَنْ تَجْعَلَ الْقُرْآنَ رَبِيعَ قَلْبِي، وَنُورَ صَدْرِي، وَجَلاَءَ حُزْنِي، وَذَهَابَ هَمِّي
Yaa Allaah, hakika mimi ni mja Wako, mwana wa mja Wako, mwana wa kijakazi Chako. Utosi wangu uko Mkononi Mwako, Hukumu Yako inapita juu yangu, Qadhwaa Yako juu yangu ni ya uadilifu. Nakuomba kwa kila Jina ambalo ni Lako, Ulilojiita Mwenyewe, au Ulilomfundisha yeyote katika viumbe Vyako, au Ulioliteremsha katika Kitabu Chako, au Ulilojihusisha nalo katika Ilimu ya ghaibu iliyoko Kwako, Uijaalie Qur-aan kuwa ni rabiy’ (uhuisho na furaha) wa moyo wangu, na nuru ya kifua changu, na kuondoka kwa huzuni yangu, na kutoweka kwa wahka wangu.
(Akisema hivyo) isipokuwa Allaah Atamuondoshea wahka wake na huzuni yake, na Atambadilishia mahali pake faraja.” Pakasemwa: Yaa Rasula-Allaah, je, tusijifunze (maneno hayo)? Akasema: “Ndio, inampasa anayeyasikia kuyajifunza.” [Ahmad (1/391), Al-Haakim (1/509), na ameisahihisha Imaam Al-Albaaniy katika As-Silsilah Asw-Swahiyhah (199) na Al-Kalim Atw-Twayyib (124)]
Shaykh Al-Islaam Ibn Taymiyyah (رحمه الله) amesema: “Hii (Du’aa katika Hadiyth hiyo) ni dalili kwamba Allaah Ana Majina zaidi ya tisini na tisa.” [Majmuw’ Al-Fataawa (6/374)]
Na Imaam Ibn Al-Qayyim (رحمه الله) amesema: “Majina Mazuri (ya Allaah) hayaingii katika hesabu wala hayana idadi maalumu; kwani Allaah (تعالى) Ana Majina na Sifa Alizojihusisha nazo katika Ilimu ya ghaibu iliyoko Kwake, hayajui Malaika aliyekurubishwa wala Nabiy aliyetumwa.”
Na Al-Bayhaqiy amesema kwamba kutajwa kwa Majina tisini na tisa hakukanushi mengineyo, bali yamehusishwa kwa kutajwa kwa sababu ndiyo Majina mashuhuri zaidi na yenye maana zilizo wazi zaidi, na ndiyo yaliyokuja nayo khabari kwamba atakayeyahifadhi ataingia Jannah.
Na Imaam Ibn ‘Uthaymiyn (رحمه الله) alipoulizwa kuhusu idadi ya Majina ya Allaah, alisema: “Majina ya Allaah hayana idadi maalumu, na dalili ni kauli yake (صلى الله عليه وآله وسلم) katika Hadiyth Swahiyh iliyotangulia: “...au Ulilojihusisha nalo katika Ilimu ya ghaibu iliyoko Kwako.” Basi yale Aliyojihusisha nayo Allaah katika Ilimu ya ghaibu hayawezi kujulikana, na yasiyojulikana hayawezi kuhesabika. Ama kauli yake (صلى الله عليه وآله وسلم): “Hakika Allaah Ana Majina tisini na tisa, atakayeyahifadhi ataingia Jannah,” haimaanishi kwamba Hana Majina mengine isipokuwa haya tu, bali inamaanisha kwamba atakayeyahifadhi Majina haya tisini na tisa ataingia Jannah. Kauli yake: “Man ahswaahaa” (atakayeyahifadhi) ni ukamilisho wa sentensi ya mwanzo, wala si sentensi iliyojitenga. Ni kama vile Mwarabu anaposema: “Nina farasi mia niliowaandaa kwa ajili ya jihaad katika Njia ya Allaah”; hii haimaanishi kwamba msemaji ana farasi mia tu, bali hawa mia ndio aliowaandaa kwa jambo hilo.” [Majmuw’ Fataawa Ibn ‘Uthaymiyn (1/122)]
Orodha Ya Majina Tisini Na Tisa Haikuthibiti Kutoka Kwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):
Hakuna Hadiyth iliyothibiti kutoka kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) inayoorodhesha Majina tisini na tisa. Walioyaorodhesha ni wapokezi watatu wa Hadiyth kwa ijtihaad yao, kisha orodha hizo zikaambatanishwa na Hadiyth ya Majina tisini na tisa, na baadhi ya watu wakadhani kwamba ni maneno ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم). Riwaayah hizo zimekuja kwa njia tatu:
1-Kupitia Al-Waliyd bin Muslim, nayo ndiyo mashuhuri zaidi: [At-Tirmidhiy (3849)], [Ibn Hibbaan (2384)], [Al-Haakim (1/16)], [Ibn Mandah: Kitaab At-Tawhiyd (2/205)] na [Al-Bayhaqiy: As-Sunan Al-Kubraa (20312)].
2-Kupitia ‘Abdul-Malik bin Muhammad Asw-Swan’aaniy: [Ibn Maajah (3994)].
3-Kupitia ‘Abdul-‘Aziyz bin Al-Huswayn bin At-Tarjumaan: [Al-Haakim (1/17)] na [Al-Bayhaqiy: Al-Asmaa Wasw-Swifaat].
Orodha hizi ni ijtihaad yao wala si lazima kwa Ummah, na ni kosa kuitegemea hesabu hiyo na kuwawekea watu mpaka kwayo. Kwa mfano, katika Qur-aan na Sunnah kuna Majina yasiyokuwemo katika riwaayah ya Al-Waliyd, kama vile Ar-Rabb, Al-Mannaan, Al-Witr na Ash-Shaafiy, na mengineyo mengi.
Na Shaykh Al-Islaam Ibn Taymiyyah (رحمه الله) amesema kuhusu riwaayah hizo tatu kwamba Wanazuoni wa Hadiyth wamekubaliana kwamba si maneno ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم), bali ni maneno ya baadhi ya Salaf. Kwa sababu hiyo orodha za Majina Mazuri zimetofautiana kwa kutofautiana kwa ‘Ulamaa, kama Al-Khattwaabiy, Al-Qurtwubiy, Ibn Al-Qayyim, As-Sa’diy, Ibn ‘Uthaymiyn na Ibn Baaz (رحمهم الله).
Al-Ism Al-A’dhwam (Jina Tukufu Kabisa La Allaah):
Allaah Ana Jina Tukufu kuliko Majina Yake yote; Akiombwa kwalo Hutoa, na Akiitwa kwalo Huitikia. Na Imaam As-Sa’diy (رحمه الله) ametahadharisha kosa la kudhani kwamba Jina hilo halijui isipokuwa aliyehusishwa na Allaah kwa karama isiyo ya kawaida; kwani Allaah Amehimiza kuyajua Majina Yake, na Amewasifu wanaoyajua, wanaoyafahamu na wanaomuomba kwayo. Na miongoni mwa dalili zake ni:
1-Hadiyth ya Buraydah Al-Aslamiy (رضي الله عنه):
عَنْ بُرَيْدَةَ الأَسْلَمِيِّ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) سَمِعَ رَجُلاً يَقُولُ: اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ أَنِّي أَشْهَدُ أَنَّكَ أَنْتَ اللَّهُ لاَ إِلَهَ إِلاَّ أَنْتَ الأَحَدُ الصَّمَدُ الَّذِي لَمْ يَلِدْ وَلَمْ يُولَدْ وَلَمْ يَكُنْ لَهُ كُفُوًا أَحَدٌ. فَقَالَ: ((لَقَدْ سَأَلْتَ اللَّهَ بِالاِسْمِ الَّذِي إِذَا سُئِلَ بِهِ أَعْطَى وَإِذَا دُعِيَ بِهِ أَجَابَ))
Amesimulia Buraydah Al-Aslamiy (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alimsikia mtu akisema:
اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ أَنِّي أَشْهَدُ أَنَّكَ أَنْتَ اللَّهُ لاَ إِلَهَ إِلاَّ أَنْتَ الأَحَدُ الصَّمَدُ الَّذِي لَمْ يَلِدْ وَلَمْ يُولَدْ وَلَمْ يَكُنْ لَهُ كُفُوًا أَحَدٌ
Yaa Allaah, hakika mimi nakuomba kwa kuwa nashuhudia kwamba Wewe Ndiye Allaah, hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Wewe, Al-Ahad (Mmoja Pekee), Asw-Swamad (Mwenye Kukusudiwa kwa haja zote), Ambaye Hakuzaa wala Hakuzaliwa, wala Hana yeyote anayefanana Naye.
Akasema: “Kwa yakini umemuomba Allaah kwa Jina Ambalo Akiombwa kwalo Hutoa, na Akiitwa kwalo Huitikia.” [Abuu Daawuwd (1493), At-Tirmidhiy (3475), Ibn Maajah (3857); At-Tirmidhiy amesema: Hasan Ghariyb]
2-Hadiyth ya Anas (رضي الله عنه):
عَنْ أَنَسٍ (رضي الله عنه) أَنَّهُ كَانَ مَعَ رَسُولِ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) جَالِسًا وَرَجُلٌ يُصَلِّي ثُمَّ دَعَا: اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ بِأَنَّ لَكَ الْحَمْدَ، لاَ إِلَهَ إِلاَّ أَنْتَ الْمَنَّانُ، بَدِيعُ السَّمَوَاتِ وَالأَرْضِ، يَا ذَا الْجَلاَلِ وَالإِكْرَامِ، يَا حَيُّ يَا قَيُّومُ. فَقَالَ النَّبِيُّ (صلى الله عليه وسلم): ((لَقَدْ دَعَا اللَّهَ بِاسْمِهِ الْعَظِيمِ الَّذِي إِذَا دُعِيَ بِهِ أَجَابَ وَإِذَا سُئِلَ بِهِ أَعْطَى))
Amesimulia Anas (رضي الله عنه) kwamba alikuwa amekaa pamoja na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم), na mtu mmoja akiswali, kisha akaomba:
اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ بِأَنَّ لَكَ الْحَمْدَ، لاَ إِلَهَ إِلاَّ أَنْتَ الْمَنَّانُ، بَدِيعُ السَّمَوَاتِ وَالأَرْضِ، يَا ذَا الْجَلاَلِ وَالإِكْرَامِ، يَا حَيُّ يَا قَيُّومُ
Yaa Allaah, hakika mimi nakuomba kwa kuwa Himdi ni Zako, hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Wewe, Al-Mannaan (Mwingi wa kuneemesha), Mbunifu wa mbingu na ardhi (bila ya mfano uliotangulia), Yaa Mwenye Ujalali na Ukarimu, Yaa Uliye Hai daima, Yaa Msimamizi wa kila kitu.
Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Kwa yakini amemuomba Allaah kwa Jina Lake Tukufu Ambalo Akiitwa kwalo Huitikia, na Akiombwa kwalo Hutoa.” [Abuu Daawuwd (1495), An-Nasaaiy (1300), Ibn Maajah (3858); Imaam Al-Albaaniy amesema isnaad yake ni nzuri (jayyid) katika As-Silsilah Asw-Swahiyhah (3411)]
3-Hadiyth ya Abuu Umaamah (رضي الله عنه):
عَنْ أَبِي أُمَامَةَ (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((اسْمُ اللَّهِ الأَعْظَمُ الَّذِي إِذَا دُعِيَ بِهِ أَجَابَ فِي سُوَرٍ ثَلاَثٍ: الْبَقَرَةِ وَآلِ عِمْرَانَ وَطه))
Amesimulia Abuu Umaamah (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Jina Tukufu kabisa la Allaah, Ambalo Akiombwa kwalo Huitikia, liko katika Suwrah tatu: Al-Baqarah, Aal-‘Imraan na Twaahaa.” [Ibn Maajah (3856), na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh Al-Jaami’ (979)]
Imesemwa kwamba Jina hilo limefichwa kama ilivyofichwa Laylatul-Qadr na saa ya kuitikiwa Du’aa siku ya Ijumaa, ili Muumini ahimike kumuomba Allaah kwa Majina Yake yote. Na ‘Ulamaa wamekhitilafiana kuhusu Jina hilo; baadhi yao wamelitaja na wengine wamekataa kuliainisha. Lakini Jina linalojirudia katika Hadiyth tatu hizo ni “Allaah”. Na katika Hadiyth ya tatu imesemwa kwamba ni Al-Hayyu Al-Qayyuwm, kwa kuwa hayakuja kwa pamoja isipokuwa katika Suwrah hizo tatu, na imesemwa kwamba ni “Allaah”, kwa kuwa katika Suwrah hizo zimekuja: “Allaah, hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye.” Na hiyo ndiyo kauli ya Ibn Al-Qayyim, Al-Khattwaabiy, Al-Qurtwubiy, Atw-Twabariy na wengineo.
Mambo Muhimu Kuhusu Majina Ya Allaah:
1-Mengi katika Majina Mazuri ya Allaah yamekuja kwa sura za kusisitiza wingi (mubaalaghah), kama Rahmaan, Rahiym, Ghafuwr na Ghaffaar, kuonyesha kudumu na wingi wa maana ya Jina.
2-Allaah Ana Sifa inayopatikana kutokana na kuunganishwa Majina mawili, iliyo zaidi ya maana ya kila moja peke yake, kama Al-Hamiyd Al-Majiyd.
3-Baadhi ya Majina yanayokuja kwa jozi hayafai kutajwa moja peke yake, kama Al-Muqaddim na Al-Muakh-khir, na Al-Qaabidhw na Al-Baasitw.
4-Haifai Allaah kusifiwa kwa kinyume cha Sifa Zake; hasifiwi kwa kinyume cha ‘uluww (kuwa juu), wala kwa kinyume cha Al-‘Adhwiym (Adhimu).
5-Baadhi ya Majina hayafai kuitwa kwayo binaadam, kama Allaah, Ar-Rahmaan, Al-Khaaliq, Al-Khallaaq na Al-Baariu.
6-Baadhi ya Majina yanafaa kuitwa kwayo binaadam yakiambatanishwa na kitu, kama rabb ad-daar (mwenye nyumba).
7-Haikuwekwa katika sharia kulitaja Jina la Allaah au Jina lolote Lake peke yake likirudiwarudiwa, kama wanavyofanya baadhi ya wasiojua kwa kulirudia mara elfu na zaidi katika halqah huku wakiyumbayumba; kwani halikuja katika adhkaar sahihi isipokuwa likiambatanishwa na kumtakasa na kumsifu Allaah.
Majina Yanayokuja Kwa Kuunganishwa (Al-Asmaa Al-Mudhwaafah) Na Kwa Nini Hayakuwekwa Kila Moja Katika Makala Yake:
Katika Qur-aan kuna maneno ambayo Allaah (سبحانه وتعالى) Amejisifu nayo yakiwa yameunganishwa na neno jingine (mudhwaaf), kama: فَاطِرُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ (Mwanzilishi wa mbingu na ardhi), عَالِمُ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ (Mjuzi wa ghaibu na dhahiri), ذُو الْمَعَارِجِ (Mwenye njia za kupandia), ذُو الطَّوْلِ (Mwenye fadhila na ukarimu), غَافِرُ الذَّنْبِ (Mwenye kughufuria dhambi), قَابِلُ التَّوْبِ (Mwenye kupokea tawbah), شَدِيدُ الْعِقَابِ (Mkali wa kuadhibu), رَفِيعُ الدَّرَجَاتِ (Mwenye daraja za juu), ذُو الْعَرْشِ (Mwenye ‘Arsh), مَالِكُ الْمُلْكِ (Mfalme wa ufalme wote) na ذُو الْفَضْلِ الْعَظِيمِ (Mwenye fadhila adhimu). Na miongoni mwa dalili zake ni Kauli Zake (سبحانه وتعالى):
تَنزِيلُ الْكِتَابِ مِنَ اللَّـهِ الْعَزِيزِ الْعَلِيمِ﴿٢﴾ غَافِرِ الذَّنبِ وَقَابِلِ التَّوْبِ شَدِيدِ الْعِقَابِ ذِي الطَّوْلِ ۖ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۖ إِلَيْهِ الْمَصِيرُ﴿٣﴾
Ni uteremsho wa Kitabu kutoka kwa Allaah Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mjuzi wa yote. Mwenye Kughufuria dhambi, Anayepokea tawbah, Mkali wa Kuakibu, Mwenye wingi wa Ukarimu, hakuna Muabudiwa wa haki ila Yeye, Kwake ndio mahali pa kuishia. [Ghaafir (40:2-3)]
رَفِيعُ الدَّرَجَاتِ ذُو الْعَرْشِ يُلْقِي الرُّوحَ مِنْ أَمْرِهِ عَلَىٰ مَن يَشَاءُ مِنْ عِبَادِهِ لِيُنذِرَ يَوْمَ التَّلَاقِ﴿١٥﴾
(Allaah) Mwenye ‘Uluwa juu ya vyeo na daraja. Mwenye ‘Arsh, Anapelekea Ar-Ruwh (Wahy) kwa Amri Yake kwa Amtakaye miongoni mwa Waja Wake, ili aonye Siku ya kukutana. [Ghaafir (40:15)]
سَأَلَ سَائِلٌ بِعَذَابٍ وَاقِعٍ﴿١﴾ لِّلْكَافِرِينَ لَيْسَ لَهُ دَافِعٌ﴿٢﴾ مِّنَ اللَّـهِ ذِي الْمَعَارِجِ﴿٣﴾
Muulizaji ameuliza kuhusu adhabu itakayotokea. Kwa makafiri, ambayo hakuna wa kuikinga. Kutoka kwa Allaah Mwenye Uluwa na fadhila tele. [Al-Ma’aarij (70:1-3)]
هُوَ اللَّـهُ الَّذِي لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۖ عَالِمُ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ ۖ هُوَ الرَّحْمَـٰنُ الرَّحِيمُ﴿٢٢﴾
Yeye Ni Allaah, Ambaye hakuna muabudiwa wa haki ila Yeye. Mjuzi wa ya ghaibu na ya dhahiri, Yeye Ndiye Ar-Rahmaan, Mwenye Kurehemu. [Al-Hashr (59:22)]
قُلِ اللَّـهُمَّ مَالِكَ الْمُلْكِ تُؤْتِي الْمُلْكَ مَن تَشَاءُ وَتَنزِعُ الْمُلْكَ مِمَّن تَشَاءُ وَتُعِزُّ مَن تَشَاءُ وَتُذِلُّ مَن تَشَاءُ ۖ بِيَدِكَ الْخَيْرُ ۖ إِنَّكَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴿٢٦﴾
Sema: Ee Allaah Mfalme Uliyemiliki ufalme wote, Unampa ufalme Umtakaye, na Unamuondoshea ufalme Umtakaye, na Unamtukuza Umtakaye, na Unamdhalilisha Umtakaye, kheri imo Mkononi Mwako. Hakika Wewe Ni Muweza wa kila kitu. [Aal-‘Imraan (3:26)]
‘Ulamaa wa Ahlus-Sunnah wamekubaliana kwamba maneno haya yote ni sifa za kweli za Allaah (سبحانه وتعالى), na inafaa kumwomba na kumsifu kwayo kama yalivyokuja katika nususi, kama du’aa ya Nabiy Yuwsuf (عليه السلام): “Mwanzilishi wa mbingu na ardhi! Wewe ni Mlinzi wangu duniani na Aakhirah…” [Yuwsuf (12:101)]. Lakini wamekhitilafiana kama yahesabiwe kuwa ni Majina (Asmaa) yanayosimama peke yake katika orodha ya Majina Mazuri, au ni sifa na khabari za matendo Yake tu.
Baadhi ya ‘Ulamaa wameona kwamba Majina haya yaliyounganishwa ni Majina ya Allaah, na inafaa kumwita kwayo kwa namna yalivyokuja katika nususi, wala hakuna dalili ya kuyaondoa katika Majina Mazuri [Dorar, makala: Asmaa Allaah Al-Husnaa Ath-Thaabitah Fil-Kitaab Was-Sunnah]. Na wengine wameona kwamba ni sifa na khabari za matendo ya Allaah, na kwamba mlango wa sifa na matendo ni mpana kuliko mlango wa Majina; kwani si kila kitendo Alichojisifu nacho Allaah kinazaa Jina. Imaam Ibn Al-Qayyim (رحمه الله) amesema:
أَطْلَقَ اللَّهُ عَلَى نَفْسِهِ أَفْعَالًا لَمْ يَتَسَمَّ مِنْهَا بِأَسْمَاءِ الْفَاعِلِ، كَأَرَادَ، وَشَاءَ، وَأَحْدَثَ، وَلَمْ يُسَمَّ بِالْمُرِيدِ وَالشَّائِي وَالْمُحْدِثِ، كَمَا لَمْ يُسَمِّ نَفْسَهُ بِالصَّانِعِ وَالْفَاعِلِ وَالْمُتْقِنِ وَغَيْرِ ذَلِكَ مِنَ الْأَسْمَاءِ الَّتِي أَطْلَقَ عَلَى نَفْسِهِ؛ فَبَابُ الْأَفْعَالِ أَوْسَعُ مِنْ بَابِ الْأَسْمَاءِ
“Allaah Amejisifu kwa matendo ambayo Hakujiita kutokana nayo kwa majina ya mtendaji, kama: Ametaka, Amependa, na Ameanzisha; wala Hakuitwa Al-Muriyd, Ash-Shaaiy wala Al-Muhdith; kama ambavyo Hakujiita As-Swaani’ (Mtengenezaji), Al-Faa’il (Mtendaji), Al-Mutqin (Mwenye kutengeneza kwa umahiri) na mengineyo katika Aliyojinasibishia. Basi mlango wa matendo ni mpana kuliko mlango wa Majina.” [Badaai’ Al-Fawaaid; imenukuliwa katika Al-Mawsuw’ah Al-‘Aqadiyyah ya Dorar (dorar.net/aqeeda/447)]
Na ‘Ulamaa wamesisitiza kwamba Majina na Sifa za Allaah ni tawqiyfiyyah; yaani kuyathibitisha kunategemea dalili za kisharia, wala akili haina nafasi ya kuyathibitisha [Imaam Ibn ‘Uthaymiyn: Al-Qawaa’id Al-Muthlaa].
Uamuzi Wa Alhidaaya.com:
Kwa sababu hizo, Alhidaaya imeamua kutoyaweka maneno haya yaliyounganishwa kila moja katika makala yake peke yake, kama Jina la Allaah katika mfululizo huu, kwa sababu zifuatazo:
1-Tahadhari katika mas-ala ya ‘Aqiydah: Majina ya Allaah ni tawqiyfiyyah, na ‘Ulamaa wamekhitilafiana juu ya maneno haya; basi tumechagua kutoyaorodhesha kama Majina yanayosimama peke yake, ili tusimnasibishie Allaah Jina kwa jambo lenye khitilafu.
2-Mengi katika hayo ni sifa za matendo (kama kuanzisha, kughufuria na kupokea tawbah), na mlango wa matendo ni mpana kuliko mlango wa Majina, kama alivyosema Imaam Ibn Al-Qayyim (رحمه الله).
3-Maana zake zote zimekwisha kuelezwa ndani ya makala za Majina yanayohusiana nayo; kwa mfano: فَاطِرُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ katika Al-Khaaliq, Al-Baariu na Badiy’ As-Samaawaati Wal-Ardhw; عَالِمُ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ katika Al-‘Aliym na Al-Khabiyr; ذُو الْمَعَارِجِ na رَفِيعُ الدَّرَجَاتِ katika Al-‘Aliyy na Al-A’laa; غَافِرُ الذَّنْبِ katika Al-Ghafuwr na Al-Ghaffaar; قَابِلُ التَّوْبِ katika At-Tawwaab; مَالِكُ الْمُلْكِ katika Al-Maalik na Al-Malik; na ذُو الطَّوْلِ na ذُو الْفَضْلِ الْعَظِيمِ katika Al-Kariym na Al-Wahhaab.
4-Kuepusha utata kwa msomaji kuhusu idadi na orodha ya Majina, na kumwekea wazi kwamba kila Jina lililowekwa katika makala peke yake lina dalili na limeorodheshwa na ‘Ulamaa.
Ama Majina matatu yaliyounganishwa ambayo yameandikiwa makala zake: Badiy’ As-Samaawaati Wal-Ardhw (073), Nuwr As-Samaawaati Wal-Ardhw (074) na Dhul-Jalaali Wal-Ikraam (075), yamewekwa kwa sababu yamo katika orodha tuliyoifuata ya Kalemtayeb, na yamethibiti katika Hadiyth Swahiyh: Badiy’ As-Samaawaati Wal-Ardhw na Dhul-Jalaali Wal-Ikraam yamo katika du’aa ambayo Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alisema kwamba mwenye kuiomba ameomba kwa Jina Tukufu kabisa la Allaah (rejea Hadiyth ya Anas (رضي الله عنه) juu); na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ameamrisha: “أَلِظُّوا بِيَا ذَا الْجَلاَلِ وَالإِكْرَامِ” [At-Tirmidhiy (3524); Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha]; na Nuwr As-Samaawaati Wal-Ardhw limo katika du’aa ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) katika kisimamo cha usiku: “أَنْتَ نُورُ السَّمَوَاتِ وَالأَرْضِ” [Al-Bukhaariy] [Muslim].
Kazi hii ya kutarjum na kuelezea Majina ya Allaah na Sifa Zake tuliyoyakusanya humu hakika ni mukhtasari tu, kwa sababu ilimu yake ni pana mno, haiwezekani kuijumuisha katika makala fupi kama hizi. Lakini tunatumai kwamba mukhtasari huu utampa msomaji maarifa ya kutosha kutambua maana za msingi za Majina ya Allaah na Sifa Zake.
Haya ndiyo Aliyotuwezesha Allaah kwa Tawfiyq Yake, huku tukimuomba Aijaalie kazi hii iwe ya ikhlaasw Kwake, ilete manufaa kwa jamii, na Atutakabalie. Aamiyn.
Na Allaah Mjuzi zaidi