Skip to main content

Majina Mazuri Ya Allaah049 - Al-Waliyy

Majina Mazuri Ya Allaah Jina 049 kati ya 103
Al-Waliyy — Majina Mazuri ya Allaah

Al-Waliyy: Rafiki Mlinzi, Msaidizi, Msimamizi

Yeye Ndiye Mwenye kuyatawalia mambo na kuyasimamia, Mmiliki wa uendeshaji wa kila kitu, Mwenye kutoa Neema, Mwenye kunusuru. Na neno waliyy linatokana na muwaalaah, yaani ukaribu, na waliyy ni kinyume cha adui. Mzizi wake و ل ي una maana ya kuwa karibu, kuwa rafiki na msaidizi, kulinda na kutetea kwa mapenzi, kuelekea kitu, na kuwa bwana na mmiliki. Na Al-Waliyy (سبحانه وتعالى) Amejumuisha ukaribu, mapenzi, ulinzi na hifadhi, pamoja na kuwa Yeye Ndiye Rabb na Mmiliki wa ulimwengu.

Jina Hili limekuja katika Aayah nyingi kwa sura mbalimbali, kama “Naye Ni Mlinzi wao” na “Wewe Ni Mlinzi wangu”, na kwa sura ya وَلِيّ bila ya nyongeza limekuja mara kumi na sita. Na mara nyingi limekuja mahali pa kuwatia nguvu, kuwasaidia na kuwanusuru Waumini. Miongoni mwa Aayah hizo ni Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى):

أَمِ اتَّخَذُوا مِن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ ۖ فَاللَّـهُ هُوَ الْوَلِيُّ وَهُوَ يُحْيِي الْمَوْتَىٰ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴿٩﴾

Je, wamejichukulia badala Yake marafiki wandani na walinzi? Basi Allaah Yeye Ndiye Mlinzi, Naye Ndiye Anayehuisha wafu, Naye juu ya kila kitu Ni Muweza. [Ash-Shuwraa (42:9)]

Na Anasema pia (سبحانه وتعالى):

وَهُوَ الَّذِي يُنَزِّلُ الْغَيْثَ مِن بَعْدِ مَا قَنَطُوا وَيَنشُرُ رَحْمَتَهُ ۚ وَهُوَ الْوَلِيُّ الْحَمِيدُ ﴿٢٨﴾

Naye Ndiye Anayeteremsha mvua baada ya kuwa wamekata tamaa, na Anaeneza Rehma Yake. Naye Ndiye Mlinzi, Mwenye Kustahiki Kuhimidiwa kwa yote. [Ash-Shuwraa (42:28)]

Maana Ya Jina Hili La Allaah, Al-Waliyy:

Jina hili la Allaah, Al-Waliyy, lina maana ya Yule Anayekutawalia mambo yako, na kusimamia hali yako na hali za viumbe Wake wengine. Na maandiko yanaonyesha kwamba Uwalii Wake uko wa aina mbili: uwalii wa jumla kwa viumbe wote, na uwalii maalumu kwa Waumini, kama ifuatavyo:1

1-Uwalii Wa Jumla:

Allaah (تعالى) Ni Al-Waliyy kwa Waja Wake wote; Anayeendesha mambo ya ardhi na mbingu saba kila wakati. Hatuna mlinzi isipokuwa Yeye; Anatuletea manufaa na kutuondolea madhara. Na huu ni uwalii wa ujumla kwa Waja Wake wote; wema na waovu, Waumini na makafiri. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَمَن يُضْلِلِ اللَّـهُ فَمَا لَهُ مِن وَلِيٍّ مِّن بَعْدِهِ

Na aliyepotolewa na Allaah basi hatopata rafiki mlinzi (na msaidizi) baada Yake. [Ash-Shuwraa (42:44)]

2-Uwalii Maalumu:

Huu ni kwa Awliyaa Wake na wacha Allaah. Huwatoa katika viza vya ujinga, ukafiri na maasi, na kuwapeleka katika nuru ya ilimu, imaan na utiifu; Huwanusuru dhidi ya maadui zao, na Huwatengenezea mambo yao ya dunia na ya Dini. Ni uwalii unaohitajia huruma, islaah, hifadhi na mapenzi. Na uwalii huu ni maalumu kwa Waumini; ama makafiri, haisemwi kwamba Allaah Ni Mlinzi wao, kwa kuzikanusha Neema Zake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

ذَٰلِكَ بِأَنَّ اللَّـهَ مَوْلَى الَّذِينَ آمَنُوا وَأَنَّ الْكَافِرِينَ لَا مَوْلَىٰ لَهُمْ ﴿١١﴾

Hivyo ni kwa kuwa Allaah Ni Mlinzi wa wale walioamini na kwamba makafiri hawana mlinzi. [Muhammad (47:11)]

Allaah Huwalinda Waja Wake Waumini kulingana na mapenzi yao Kwake. Na ndio maana Allaah Amemkemea anayejichukulia walii badala Yake, kinyume na Awliyaa Wake ambao hawakujichukulia walii yeyote asiyekuwa Yeye; na huo ndio ukamilifu wa muwaalaah.2

Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Waliyy:

1-Allaah Pekee Ndiye Al-Waliyy Wa Kweli:

Kila mlinzi asiyekuwa Allaah ni dhaifu; Al-Waliyy wa kweli ni Yeye Anayehuisha wafu na Muweza wa kila kitu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

أَمِ اتَّخَذُوا مِن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ ۖ فَاللَّـهُ هُوَ الْوَلِيُّ وَهُوَ يُحْيِي الْمَوْتَىٰ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ﴿٩﴾

Je, wamejichukulia badala Yake marafiki wandani na walinzi? Basi Allaah Yeye Ndiye Mlinzi, Naye Ndiye Anayehuisha wafu, Naye juu ya kila kitu Ni Muweza. [Ash-Shuwraa (42:9)]

2-Kuwa Na Imaan Na Taqwa Upate Amani Na Furaha:

Uwalii wa Allaah kwa Waumini unawapatia amani na furaha; hawahuzuniki kwa yaliyopita wala hawakhofu yajayo. Na njia ya kuupata ni imaan na taqwa. Basi jenga uhusiano na Qur-aan, muombe Al-Waliyy Akujaalie kuifahamu na kuitekeleza, kumbuka Jannah kila siku, na jifunze Majina na Sifa za Allaah ili yazidi mapenzi yako na khofu yako Kwake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

أَلَا إِنَّ أَوْلِيَاءَ اللَّـهِ لَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ ﴿٦٢﴾ الَّذِينَ آمَنُوا وَكَانُوا يَتَّقُونَ ﴿٦٣﴾

Tanabahi! Hakika Vipenzi wa Allaah hawana khofu na wala hawatohuzunika. Ambao wameamini na wakawa wana taqwa. [Yuwnus (10:62-63)]

3-Wafanye Allaah, Rasuli Wake Na Waumini Kuwa Marafiki Wako Wandani:

Tambua, ee Mja wa Al-Waliyy: Uwalii wa Muumini ni kwa Allaah, Rasuli Wake na Waumini wenzake, si kwa maadui wa Dini. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

إِنَّمَا وَلِيُّكُمُ اللَّـهُ وَرَسُولُهُ وَالَّذِينَ آمَنُوا الَّذِينَ يُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَيُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَهُمْ رَاكِعُونَ ﴿٥٥﴾

Hakika Rafiki wenu Mlinzi ni Allaah na Rasuli Wake na wale walioamini, ambao wanasimamisha Swalaah na wanatoa Zakaah hali ya kuwa wananyenyekea. [Al-Maaidah (5:55)]

4-Tahadhari! Uwalii Hupatikana Kwa Amali, Si Kwa Madai:

Taqwa ni daraja ya juu kabisa ya kujikurubisha kwa Allaah na kupata Uwalii Wake. Kwa hiyo uwalii wa Allaah hupatikana kwa amali; mja huupata kwa imaan ya kweli, ilimu thabiti, amali njema za kuendelea, na kufuata Mwongozo wa Allaah. Si kipawa kisicho na sababu kama wanavyodhani baadhi ya wajinga na waliopindukia mipaka, waliowanasibishia uwalii wendawazimu, mafasiki, madhalimu na wazushi kwa sababu tu ya mambo ya ajabu na viinimacho vya kishaytwaan kama kuingia motoni na kubeba nyoka. Ametukuka Allaah na wanayoyasema! Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

إِنَّهُمْ لَن يُغْنُوا عَنكَ مِنَ اللَّـهِ شَيْئًا ۚ وَإِنَّ الظَّالِمِينَ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ ۖ وَاللَّـهُ وَلِيُّ الْمُتَّقِينَ ﴿١٩﴾

Hakika wao hawatokufaa chochote mbele ya Allaah. Na hakika madhalimu ni marafiki wanaoshirikiana wao kwa wao. Na Allaah Ni Rafiki Mlinzi wa wenye taqwa. [Al-Jaathiyah (45:19)]

5-Al-Waliyy Anawatetea Vipenzi Vyake:

Tambua, ee Mja wa Al-Waliyy: Katika Hadiyth Al-Qudsiy, Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((إِنَّ اللَّهَ قَالَ: مَنْ عَادَى لِي وَلِيًّا فَقَدْ آذَنْتُهُ بِالْحَرْبِ، وَمَا تَقَرَّبَ إِلَيَّ عَبْدِي بِشَيْءٍ أَحَبَّ إِلَيَّ مِمَّا افْتَرَضْتُ عَلَيْهِ، وَمَا يَزَالُ عَبْدِي يَتَقَرَّبُ إِلَيَّ بِالنَّوَافِلِ حَتَّى أُحِبَّهُ))

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika Allaah Amesema: Atakayemfanyia uadui walii Wangu, basi Nimemtangazia vita. Na Mja Wangu hajikurubishi Kwangu kwa kitu Ninachokipenda zaidi kuliko yale Niliyomfaradhishia. Na Mja Wangu huendelea kujikurubisha Kwangu kwa Sunnah mpaka Nimpende…” [Al-Bukhaariy]

6-Mtegemee Al-Waliyy Pekee:

Jikumbushe kwamba Al-Waliyy Ndiye Mlinzi bora wa kumkimbilia kila wakati, na mtegemee Yeye Pekee. Yeye Anawajua maadui zako, na Yeye Ndiye Anayetosheleza kuwa Mlinzi na Msaidizi; hakuna mwingine atakayekulinda wala kukunusuru badala Yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَمَا أَنتُم بِمُعْجِزِينَ فِي الْأَرْضِ ۖ وَمَا لَكُم مِّن دُونِ اللَّـهِ مِن وَلِيٍّ وَلَا نَصِيرٍ ﴿٣١﴾

Nanyi si wenye kuweza kukwepa ardhini, na wala hamna badala Yake mlinzi yeyote wala mwenye kunusuru. [Ash-Shuwraa (42:31)]

7-Jitahidi Kuwa Walii Wa Al-Waliyy:

Tambua, ee Mja wa Al-Waliyy: Usidhani kwamba ‘Ulamaa peke yao ndio wanaoweza kuwa Awliyaa; nawe unaweza kuwa walii wa Allaah (عزّ وجلّ). Anza kwa kuzitilia umuhimu ibaada za faradhi, kama kuswali Swalaah kwa wakati wake na kwa unyenyekevu, kisha zikamilishe kwa ibaada nyingi za Sunnah, na jifunze Sunnah za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) uzitekeleze katika maisha yako:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((إِنَّ اللَّهَ قَالَ: مَنْ عَادَى لِي وَلِيًّا فَقَدْ آذَنْتُهُ بِالْحَرْبِ، وَمَا تَقَرَّبَ إِلَيَّ عَبْدِي بِشَيْءٍ أَحَبَّ إِلَيَّ مِمَّا افْتَرَضْتُ عَلَيْهِ، وَمَا يَزَالُ عَبْدِي يَتَقَرَّبُ إِلَيَّ بِالنَّوَافِلِ حَتَّى أُحِبَّهُ))

Amesimulia Abu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika Allaah Amesema: Atakayemfanyia uadui walii Wangu, basi Nimemtangazia vita. Na mja Wangu hajikurubishi Kwangu kwa kitu Ninachokipenda zaidi kuliko yale Niliyomfaradhishia. Na mja Wangu ataendelea kujikurubisha Kwangu kwa (ibaada za) nawaafil mpaka Nimpende.” [Al-Bukhaariy]

8-Al-Waliyy Huwasimamia Watu Wema:

Tambua kwamba Al-Waliyy Anawatawalia na kuwasimamia watu wema katika mambo yao yote. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

إِنَّ وَلِيِّيَ اللَّـهُ الَّذِي نَزَّلَ الْكِتَابَ ۖ وَهُوَ يَتَوَلَّى الصَّالِحِينَ ﴿١٩٦﴾

Hakika Mlinzi wangu Ni Allaah Ambaye Ameteremsha Kitabu, Naye Ndiye Anayewalinda na kuwasaidia Swalihina. [Al-A’raaf (7:196)]

9-Kuwa Rafiki Mwema Kwa Nduguzo:

Tambua, ee Mja wa Al-Waliyy: Kuwa rafiki mwenye mapenzi kwa wengine, ukilinda haki zao, na litekeleze kwa uzito jukumu lolote ulilopewa la kumwakilisha mtu au kumsaidia katika mambo yake. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((... وَاللَّهُ فِي عَوْنِ الْعَبْدِ مَا كَانَ الْعَبْدُ فِي عَوْنِ أَخِيهِ))

Amesimulia Abu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “... Na Allaah Yuko katika kumsaidia mja maadamu mja yuko katika kumsaidia nduguye.” [Muslim]

10-Muombe Al-Waliyy Akutawalie Mambo Yako:

Daima utahitaji msaada na Ulinzi wa Al-Waliyy, basi muombe Akulinde na Akusaidie katika maisha haya, wakati wa kufa, kaburini, na Siku ya Hesabu. Na miongoni mwa Du’aa alizotufunza Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ni Du’aa ya Qunuwt:

اللَّهُمَّ اهْدِنِي فِيمَنْ هَدَيْتَ، وَعَافِنِي فِيمَنْ عَافَيْتَ، وَتَوَلَّنِي فِيمَنْ تَوَلَّيْتَ، وَبَارِكْ لِي فِيمَا أَعْطَيْتَ، وَقِنِي شَرَّ مَا قَضَيْتَ، فَإِنَّكَ تَقْضِي وَلاَ يُقْضَى عَلَيْكَ، وَإِنَّهُ لاَ يَذِلُّ مَنْ وَالَيْتَ، تَبَارَكْتَ رَبَّنَا وَتَعَالَيْتَ

Yaa Allaah, Niongoze pamoja na Uliowaongoza, na Nipe afya pamoja na Uliowapa afya, na Nitawalie (mambo yangu) pamoja na Uliowatawalia, na Nibarikie katika Ulichonipa, na Nikinge na shari ya Ulichokihukumu; kwani hakika Wewe Unahukumu wala Huhukumiwi, na hakika hadhaliliki Uliyemfanya walii Wako. Umebarikika Rabb wetu na Umetukuka. [Abuu Daawuwd, At-Tirmidhiy (464), An-Nasaaiy, Ibn Maajah, na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh At-Tirmidhiy]

Na Allaah Mjuzi zaidi

  • 1Lisaan Al-‘Arab (5/411), Asmaa Allaah Al-Husnaa, Dkt. Mahmuwd Ar-Radhwaaniy (498).
  • 2Al-Haqq Al-Waadhwih Al-Mubiyn (12), Fat-hu Ar-Rahiym Al-Malik Al-‘Allaam (51), Tafsiyr Suwrah Al-Baqarah, Ibn ‘Uthaymiyn (3/461), Al-Jawaab Al-Kaafiy (332).