Skip to main content

Majina Mazuri Ya Allaah048 - Al-Waduwd

Majina Mazuri Ya Allaah Jina 048 kati ya 103
Al-Waduwd — Majina Mazuri ya Allaah

Al-Waduwd: Mwenye Mapenzi Tele Halisi

Mawaddah ni mapenzi. Na Al-Waduwd (تعالى) Ni Mwenye kuwapenda viumbe Vyake, Mwenye kuwasifu, Mwenye kuwafanyia ihsaan, Mwenye huruma kwa Waja Wake, Mwenye kumpenda anayerejea Kwake na kutubia. Anawapenda Awliyaa Wake na Anajipendekeza kwao kwa maghfirah na Neema; Huwaridhia, Hukubali amali zao, na Huwajaalia kukubalika ardhini.

Neno Al-Waduwd linatokana na mzizi و د د wenye maana ya kupenda, kuwa na huba, na kutamani. Na katika lugha ya Kiarabu, al-hubb ni hisia ya mapenzi iliyomo moyoni, ama al-wudd ni mapenzi makubwa ya kudumu yanayodhihirika katika vitendo. Na Al-Waduwd liko katika wazani wa fa’uwl unaoonyesha wingi na kudumu; kwa hiyo Mapenzi ya Allaah ni makubwa, ya kudumu, na yanadhihirika katika Neema, Fadhila, Rehma, Mwongozo na Maghfirah Anazowapa Waja Wake.

Jina Hili Al-Waduwd limetajwa katika Qur-aan mara mbili, na mara zote mbili limekuja pamoja na maghfirah na tawbah, kuonyesha kwamba Allaah Anawapenda Waja Wake wanaotubia, na kwamba istighfaar humpatia mja Mapenzi ya Allaah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَاسْتَغْفِرُوا رَبَّكُمْ ثُمَّ تُوبُوا إِلَيْهِ ۚ إِنَّ رَبِّي رَحِيمٌ وَدُودٌ ﴿٩٠﴾

Na ombeni maghfirah kwa Rabb wenu, kisha tubieni Kwake. Hakika Rabb wangu ni Mwenye kurehemu, Mwenye upendo khalisi. [Huwd (11:90)]

Na Anasema pia (سبحانه وتعالى):

وَهُوَ الْغَفُورُ الْوَدُودُ ﴿١٤﴾

Naye Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Upendo halisi. [Al-Buruwj (85:14)]

Na Allaah (تبارك وتعالى) Ni Al-Waduwd kwa namna tatu:1

1-Mwenye Mapenzi Kwa Awliyaa Wake:

Haya ni Mapenzi makubwa ya hali ya juu kabisa ya Allaah (تعالى), nayo ni maalumu kwa Awliyaa Wake na wacha Allaah. Yeye Ndiye Aliyeweka kila sababu ya mapenzi kati Yake na wao, Akazivuta nyoyo zao Kwake, na Akawajaalia kupenda kulitaja Jina Lake kwa nyoyo zilizosalimika na vifua vilivyokunjuka, kwa kumjua Yeye na Sifa Zake tukufu.2

2-Mwenye Mapenzi Kwa Wenye Maasi Kwa Maghfirah Yake:

Hayo ni Mapenzi Yake kwa wanaotubia miongoni mwa Waja Wake wenye maasi, kwa kuwawekea sababu za kupata Maghfirah Yake na njia za kusamehewa, na dalili zinazothibitisha upana wa Rehma Yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

قُلْ يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ أَسْرَفُوا عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ لَا تَقْنَطُوا مِن رَّحْمَةِ اللَّـهِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ جَمِيعًا ۚ إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ ﴿٥٣﴾

Sema: Enyi Waja Wangu ambao wamepindukia mipaka juu ya nafsi zao: Msikate tamaa na Rehma ya Allaah, hakika Allaah Anaghufuria dhambi zote. Hakika Yeye Ndiye Mwenye Kughufuria, Mwenye Kurehemu. [Az-Zumar (39:53)]

Na Anasema pia (سبحانه وتعالى):

وَلَا يَأْتَلِ أُولُو الْفَضْلِ مِنكُمْ وَالسَّعَةِ أَن يُؤْتُوا أُولِي الْقُرْبَىٰ وَالْمَسَاكِينَ وَالْمُهَاجِرِينَ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ ۖ وَلْيَعْفُوا وَلْيَصْفَحُوا ۗ أَلَا تُحِبُّونَ أَن يَغْفِرَ اللَّـهُ لَكُمْ ۗ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٢٢﴾

Na wala wasiape wale wenye fadhila miongoni mwenu na wenye wasaa wa mali kuwa hawatowapa (swadaqah) jamaa wa karibu, na masikini, na Muhaajiriyn katika Njia ya Allaah. Na wasamehe na waachilie mbali. Je, hampendi Allaah Akughufurieni? Na Allaah Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu. [An-Nuwr (24:22)]

Na Anasema tena (سبحانه وتعالى):

وَاكْتُبْ لَنَا فِي هَـٰذِهِ الدُّنْيَا حَسَنَةً وَفِي الْآخِرَةِ إِنَّا هُدْنَا إِلَيْكَ ۚ قَالَ عَذَابِي أُصِيبُ بِهِ مَنْ أَشَاءُ ۖ وَرَحْمَتِي وَسِعَتْ كُلَّ شَيْءٍ ۚ فَسَأَكْتُبُهَا لِلَّذِينَ يَتَّقُونَ وَيُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَالَّذِينَ هُم بِآيَاتِنَا يُؤْمِنُونَ ﴿١٥٦﴾ الَّذِينَ يَتَّبِعُونَ الرَّسُولَ النَّبِيَّ الْأُمِّيَّ الَّذِي يَجِدُونَهُ مَكْتُوبًا عِندَهُمْ فِي التَّوْرَاةِ وَالْإِنجِيلِ يَأْمُرُهُم بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَاهُمْ عَنِ الْمُنكَرِ وَيُحِلُّ لَهُمُ الطَّيِّبَاتِ وَيُحَرِّمُ عَلَيْهِمُ الْخَبَائِثَ وَيَضَعُ عَنْهُمْ إِصْرَهُمْ وَالْأَغْلَالَ الَّتِي كَانَتْ عَلَيْهِمْ ۚ فَالَّذِينَ آمَنُوا بِهِ وَعَزَّرُوهُ وَنَصَرُوهُ وَاتَّبَعُوا النُّورَ الَّذِي أُنزِلَ مَعَهُ ۙ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ ﴿١٥٧﴾

Na Tuandikie katika dunia hii mazuri na katika Aakhirah. Hakika sisi tumerudi kutubu Kwako. (Allaah) Akasema: Adhabu Yangu Nitamsibu nayo Nimtakaye. Na Rehma Yangu imeenea kila kitu. Basi Nitawaandikia wale wenye taqwa na wanaotoa Zakaah na ambao wao wanaziamini Aayaat (na Ishara, Hoja, Dalili) Zetu. Wale wanaomfuata Rasuli; Nabiy asiyejua kusoma wala kuandika ambaye wanamkuta ameandikwa kwao katika Tawraat na Injiyl, anawaamrisha mema na anawakataza munkari, na anawahalalishia vilivyo vizuri na anawaharamishia vilivyo vibaya na anawaondoshea mizigo yao na minyororo iliyokuwa juu yao. Basi wale waliomwamini na wakamtukuza, na wakamnusuru na wakafuata Nuru (Qur-aan) ambayo imeteremshwa pamoja naye, hao ndio wenye kufaulu. [Al-A’raaf (7:156-157)]

Na katika ukamilifu wa Mapenzi Yake kwa wanaotubia ni kwamba Hufurahi sana kwa tawbah yao, na Yeye Ni Mwenye huruma zaidi kwao kuliko mama kwa mwanawe:

عَنْ عُمَرَ بْنِ الْخَطَّابِ (رضي الله عنه) قَالَ: قَدِمَ عَلَى النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) سَبْيٌ، فَإِذَا امْرَأَةٌ مِنَ السَّبْيِ قَدْ تَحْلُبُ ثَدْيَهَا تَسْقِي، إِذَا وَجَدَتْ صَبِيًّا فِي السَّبْيِ أَخَذَتْهُ فَأَلْصَقَتْهُ بِبَطْنِهَا وَأَرْضَعَتْهُ، فَقَالَ لَنَا النَّبِيُّ (صلى الله عليه وسلم): ((أَتُرَوْنَ هَذِهِ طَارِحَةً وَلَدَهَا فِي النَّارِ؟)) قُلْنَا: لاَ، وَهِيَ تَقْدِرُ عَلَى أَنْ لاَ تَطْرَحَهُ. فَقَالَ: ((لَلَّهُ أَرْحَمُ بِعِبَادِهِ مِنْ هَذِهِ بِوَلَدِهَا))

Amesimulia ‘Umar bin Al-Khattwaab (رضي الله عنه): Waliletwa mateka kwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم), na mwanamke mmoja miongoni mwa mateka alikuwa akikamua maziwa ya matiti yake (kumtafuta mwanawe). Alipomuona mtoto miongoni mwa mateka, alimchukua, akamkumbatia tumboni mwake na akamnyonyesha. Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akatuambia: “Je, mnamuona mwanamke huyu atamtupa mwanawe motoni?” Tukasema: Hapana, naye akiweza kutomtupa. Akasema: “Allaah Ni Mwenye huruma zaidi kwa Waja Wake kuliko huyu kwa mwanawe.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

3-Mwenye Mapenzi Kwa Waja Wake Wote Kwa Neema Zake:

Hayo ni Mapenzi Yake kwa Waja Wake wote kwa Neema kubwa za dhahiri na za siri; kwa Neema hizo wanabakia na kuishi, na Amewatimizia kwa Mapenzi Yake mahitaji yao ya msingi na haja zao. Na kwa Mapenzi hayo, Amewaongoza katika imaan na Uislamu, ambao ndio Neema kubwa kabisa.3

Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Waduwd:

1-Mpende Al-Waduwd Na Rasuli Wake Kuliko Vyote:

Tambua, ee Mja wa Al-Waduwd: Yeye Pekee (سبحانه وتعالى) Ndiye Anayestahiki kupendwa kwa Dhati Yake, na Yeye Ndiye lengo la kila mapenzi. Na tofautisha baina ya kupenda kwa ajili ya Allaah, ambako ni imaan, na kupenda pamoja na Allaah (kumpenda yeyote kama unavyompenda Allaah), ambako ni shirki. Na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَنَسٍ (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((ثَلاَثٌ مَنْ كُنَّ فِيهِ وَجَدَ حَلاَوَةَ الإِيمَانِ: أَنْ يَكُونَ اللَّهُ وَرَسُولُهُ أَحَبَّ إِلَيْهِ مِمَّا سِوَاهُمَا، وَأَنْ يُحِبَّ الْمَرْءَ لاَ يُحِبُّهُ إِلاَّ لِلَّهِ، وَأَنْ يَكْرَهَ أَنْ يَعُودَ فِي الْكُفْرِ كَمَا يَكْرَهُ أَنْ يُقْذَفَ فِي النَّارِ))

Amesimulia Anas (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Mambo matatu atakayekuwa nayo atapata utamu wa imaan: Allaah na Rasuli Wake wawe ni wapenzi zaidi kwake kuliko wengineo, ampende mtu hampendi isipokuwa kwa ajili ya Allaah, na achukie kurudi katika ukafiri kama anavyochukia kutupwa motoni.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

2-Mfuate Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Upate Mapenzi Ya Al-Waduwd:

Jipendekeze kwa Rabb wako kwa kutekeleza Amri Zake na kujiepusha na Makatazo Yake, kwani Allaah Anampenda anayemtii na Anamchukia anayemuasi. Na kujiepusha na maasi ni dalili kubwa zaidi ya mapenzi kuliko kutenda mema tu, kwani mema huyatenda mwema na muovu, lakini kuacha maasi hakuwi isipokuwa kwa Muumini mwenye ukamilifu wa ‘ubuwdiyyah. Na katika mapenzi ya mja kwa Rabb wake ni kuridhika na Qadhwaa na Qadar Yake, kuipenda Qur-aan na kuitekeleza, na kumpenda Rasuli (صلى الله عليه وآله وسلم) na Sunnah zake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

قُلْ إِن كُنتُمْ تُحِبُّونَ اللَّـهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللَّـهُ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ ۗ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٣١﴾

Sema: Mkiwa mnampenda Allaah, basi nifuateni mimi, Allaah Atakupendeni na Atakughufurieni dhambi zenu. Na Allaah Ni Mwingi wa Kughufiria, Mwenye Kurehemu. [Aal-‘Imraan (3:31)]

3-Jikurubishe Kwa Al-Waduwd Kwa Faradhi Kisha Kwa Nawaafil:

Tambua kwamba anayependwa na Allaah, Humuingiza katika Ma’iyyah (Kuwa Pamoja Naye) Yake maalumu. Na njia ya kupata Mapenzi ya Al-Waduwd ni kutekeleza kwanza yale Aliyokufaradhishia, kisha kuzidisha ibaada za Sunnah mpaka Akupende:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((إِنَّ اللَّهَ قَالَ: مَنْ عَادَى لِي وَلِيًّا فَقَدْ آذَنْتُهُ بِالْحَرْبِ، وَمَا تَقَرَّبَ إِلَيَّ عَبْدِي بِشَيْءٍ أَحَبَّ إِلَيَّ مِمَّا افْتَرَضْتُ عَلَيْهِ، وَمَا يَزَالُ عَبْدِي يَتَقَرَّبُ إِلَيَّ بِالنَّوَافِلِ حَتَّى أُحِبَّهُ، فَإِذَا أَحْبَبْتُهُ كُنْتُ سَمْعَهُ الَّذِي يَسْمَعُ بِهِ، وَبَصَرَهُ الَّذِي يُبْصِرُ بِهِ، وَيَدَهُ الَّتِي يَبْطِشُ بِهَا، وَرِجْلَهُ الَّتِي يَمْشِي بِهَا، وَإِنْ سَأَلَنِي لأُعْطِيَنَّهُ، وَلَئِنِ اسْتَعَاذَنِي لأُعِيذَنَّهُ))

Amesimulia Abu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika Allaah Amesema: Atakayemfanyia uadui walii Wangu, basi Nimemtangazia vita. Na mja Wangu hajikurubishi Kwangu kwa kitu Ninachokipenda zaidi kuliko yale Niliyomfaradhishia. Na mja Wangu ataendelea kujikurubisha Kwangu kwa (ibaada za) nawaafil mpaka Nimpende. Nikishampenda, Huwa usikizi wake anaosikilizia, na uoni wake anaoonea, na mkono wake anaoshikia, na mguu wake anaotembelea. Na akiniomba, bila shaka Nitampa, na akiniomba kinga, bila shaka Nitamkinga.” [Al-Bukhaariy]

4-Tambua Kwamba Anayependwa Na Al-Waduwd Hupendwa Na Viumbe:

Tambua kwamba Al-Waduwd Akimpenda mja, Huwafanya viumbe Vyake wampende, na jina lake hutajwa mbinguni kwa sauti ya Jibriyl (عليه السلام):

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((إِذَا أَحَبَّ اللَّهُ الْعَبْدَ نَادَى جِبْرِيلَ: إِنَّ اللَّهَ يُحِبُّ فُلاَنًا فَأَحْبِبْهُ، فَيُحِبُّهُ جِبْرِيلُ، فَيُنَادِي جِبْرِيلُ فِي أَهْلِ السَّمَاءِ: إِنَّ اللَّهَ يُحِبُّ فُلاَنًا فَأَحِبُّوهُ، فَيُحِبُّهُ أَهْلُ السَّمَاءِ، ثُمَّ يُوضَعُ لَهُ الْقَبُولُ فِي الأَرْضِ))

Amesimulia Abu Hurayrah (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Allaah Akimpenda mja, Humwita Jibriyl: Hakika Allaah Anampenda fulani, basi mpende. Jibriyl humpenda, kisha Jibriyl huwanadia watu wa mbinguni: Hakika Allaah Anampenda fulani, basi mpendeni. Watu wa mbinguni humpenda, kisha huwekewa kukubalika ardhini.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

5-Penda Na Chukia Kwa Ajili Ya Al-Waduwd:

Tambua kwamba kila mapenzi yako yawe kwa ajili ya Al-Waduwd; ukimpenda mtu au kitu, kipende kwa ajili ya Allaah, na vivyo hivyo chuki yako. Jiulize: kwa nini unawapenda watu? Wapende wanaomcha Allaah na wanaoamrisha mema na kukataza maovu, na utapata fadhila hii:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((إِنَّ اللَّهَ يَقُولُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ: أَيْنَ الْمُتَحَابُّونَ بِجَلاَلِي؟ الْيَوْمَ أُظِلُّهُمْ فِي ظِلِّي يَوْمَ لاَ ظِلَّ إِلاَّ ظِلِّي))

Amesimulia Abu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika Allaah Atasema Siku ya Qiyaamah: Wako wapi wanaopendana kwa ajili ya Ujalali Wangu? Leo Nitawafunika kivuli katika Kivuli Changu, siku ambayo hakuna kivuli isipokuwa Kivuli Changu.” [Muslim]

6-Harakisha Kutubia Na Kuomba Maghfirah Kwa Al-Waduwd:

Kwa kuwa Jina Hili limeambatana na maghfirah na tawbah, basi harakisha kutubia kwa Al-Waduwd, kwani Anafurahi sana kwa tawbah ya Mja Wake:

عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((لَلَّهُ أَشَدُّ فَرَحًا بِتَوْبَةِ عَبْدِهِ حِينَ يَتُوبُ إِلَيْهِ مِنْ أَحَدِكُمْ كَانَ عَلَى رَاحِلَتِهِ بِأَرْضِ فَلاَةٍ فَانْفَلَتَتْ مِنْهُ وَعَلَيْهَا طَعَامُهُ وَشَرَابُهُ فَأَيِسَ مِنْهَا، فَأَتَى شَجَرَةً فَاضْطَجَعَ فِي ظِلِّهَا قَدْ أَيِسَ مِنْ رَاحِلَتِهِ، فَبَيْنَا هُوَ كَذَلِكَ إِذَا هُوَ بِهَا قَائِمَةً عِنْدَهُ، فَأَخَذَ بِخِطَامِهَا ثُمَّ قَالَ مِنْ شِدَّةِ الْفَرَحِ: اللَّهُمَّ أَنْتَ عَبْدِي وَأَنَا رَبُّكَ، أَخْطَأَ مِنْ شِدَّةِ الْفَرَحِ))

Amesimulia Anas bin Maalik (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Allaah Anafurahi zaidi kwa tawbah ya mja Wake anapotubia Kwake kuliko mmoja wenu aliyekuwa juu ya kipando chake katika jangwa, kikamponyoka na juu yake kuna chakula chake na kinywaji chake, akakata tamaa nacho. Akauendea mti, akajilaza kivulini mwake akiwa amekata tamaa na kipando chake. Mara akiwa katika hali hiyo, akakiona kimesimama mbele yake. Akaishika hatamu yake, kisha kwa ukubwa wa furaha akasema: Yaa Allaah! Wewe ni mja wangu nami ni rabb wako! Akakosea kwa sababu ya ukubwa wa furaha.” [Muslim]

7-Zidisha Ilimu Ya Dini Yako:

Tambua kwamba Mapenzi ya Al-Waduwd yamo katika fitwrah (maumbile) ya mja, lakini yanapata nguvu kwa ilimu na usalama wa fitwrah, na yanadhoofika kwa ujinga, matamanio na shubha (utata). Kila Muislamu anapozidi kuijua Dini ya Allaah, ndivyo mapenzi yake kwa Allaah yanavyokuwa na nguvu zaidi. Na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ مُعَاوِيَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: سَمِعْتُ النَّبِيَّ (صلى الله عليه وسلم) يَقُولُ: ((مَنْ يُرِدِ اللَّهُ بِهِ خَيْرًا يُفَقِّهْهُ فِي الدِّينِ))

Amesimulia Mu’aawiyah (رضي الله عنه): Nimemsikia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: “Ambaye Allaah Anamtakia kheri, Humfahamisha Dini.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

8-Penda Kusoma Suwrah Al-Ikhlaasw:

Tambua, ee Mja wa Al-Waduwd: Ukitaka Allaah Akupende, penda kumtaja Yeye na Sifa Zake. Na Suwrah Al-Ikhlaasw ni miongoni mwa Suwrah zilizojumuisha Sifa za Allaah, basi zidisha kuisoma kwa mapenzi:

عَنْ عَائِشَةَ (رضي الله عنها) أَنَّ النَّبِيَّ (صلى الله عليه وسلم) بَعَثَ رَجُلاً عَلَى سَرِيَّةٍ، وَكَانَ يَقْرَأُ لأَصْحَابِهِ فِي صَلاَتِهِمْ فَيَخْتِمُ بِـ قُلْ هُوَ اللَّهُ أَحَدٌ، فَلَمَّا رَجَعُوا ذَكَرُوا ذَلِكَ لِلنَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) فَقَالَ: ((سَلُوهُ لأَيِّ شَيْءٍ يَصْنَعُ ذَلِكَ؟)) فَسَأَلُوهُ فَقَالَ: لأَنَّهَا صِفَةُ الرَّحْمَنِ، وَأَنَا أُحِبُّ أَنْ أَقْرَأَ بِهَا. فَقَالَ النَّبِيُّ (صلى الله عليه وسلم): ((أَخْبِرُوهُ أَنَّ اللَّهَ يُحِبُّهُ))

Amesimulia ‘Aaishah (رضي الله عنها): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alimtuma mtu kuongoza kikosi cha jeshi, naye alikuwa akiwaswalisha wenzake na kumalizia kisomo chake kwa: ﴿قُلْ هُوَ اللَّهُ أَحَدٌ﴾. Waliporudi walimweleza Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) jambo hilo, akasema: “Muulizeni kwa nini anafanya hivyo?” Wakamuuliza, akasema: Kwa sababu ni Sifa ya Ar-Rahmaan, nami napenda kuisoma. Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Mwambieni kwamba Allaah Anampenda.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

9-Wapendee Wenzako Unayoyapenda Nafsi Yako:

Tambua kwamba mwenzako akipata ndoa, kazi au neema uliyoikosa, furahi kwa ajili yake hata ikiwa ni vigumu, na idhibiti nafsi yako, ukitambua kwamba Al-Waduwd Ndiye Anayetoa na Kuzuia. Utaona utulivu moyoni mwako badala ya hasadi na wasiwasi kwa furaha ya wengine. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَنَسٍ (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((لاَ يُؤْمِنُ أَحَدُكُمْ حَتَّى يُحِبَّ لأَخِيهِ مَا يُحِبُّ لِنَفْسِهِ))

Amesimulia Anas (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hatoamini mmoja wenu mpaka ampendee nduguye yale anayoyapenda nafsi yake.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

10-Mueleze Al-Waduwd Haja Zako:

Kumweleza Al-Waduwd wasiwasi na haja zako ni ibaada yenyewe. Anapenda umrudie na umweleze shida zako, huku ukikumbuka jinsi Alivyo karibu nawe na jinsi unavyompenda. Mfano mzuri ni mama yake Maryam (عليها السلام), ambaye alikuwa na uhusiano wa karibu na Allaah, na Allaah Akamkubalia Du’aa yake:

إِذْ قَالَتِ امْرَأَتُ عِمْرَانَ رَبِّ إِنِّي نَذَرْتُ لَكَ مَا فِي بَطْنِي مُحَرَّرًا فَتَقَبَّلْ مِنِّي ۖ إِنَّكَ أَنتَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ ﴿٣٥﴾

Pale aliposema mke wa ‘Imraan: Rabb wangu! Hakika mimi nimeweka nadhiri Kwako kilichomo katika tumbo langu kuwa ni wakfu kukutumikia, basi Nitakabalie. Hakika Wewe Ni Mwenye Kusikia yote, Mjuzi wa yote. [Aal-‘Imraan (3:35)]

11-Omba Du’aa Ya Kupata Mapenzi Ya Al-Waduwd:

Omba du’aa, ee Mja wa Al-Waduwd, Akujaalie Mapenzi Yake, mapenzi ya wanaompenda, na mapenzi ya amali zitakazokukurubisha katika Mapenzi Yake, kwa du’aa aliyoifundisha Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم), naye akasema: “Hakika ni haki, basi isomeni na mjifunze.”

عَنْ مُعَاذِ بْنِ جَبَلٍ (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) فِي حَدِيثٍ طَوِيلٍ، قَالَ: ((... اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ فِعْلَ الْخَيْرَاتِ، وَتَرْكَ الْمُنْكَرَاتِ، وَحُبَّ الْمَسَاكِينِ، وَأَنْ تَغْفِرَ لِي وَتَرْحَمَنِي، وَإِذَا أَرَدْتَ فِتْنَةً فِي قَوْمٍ فَتَوَفَّنِي غَيْرَ مَفْتُونٍ، وَأَسْأَلُكَ حُبَّكَ، وَحُبَّ مَنْ يُحِبُّكَ، وَحُبَّ عَمَلٍ يُقَرِّبُ إِلَى حُبِّكَ)) قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((إِنَّهَا حَقٌّ فَادْرُسُوهَا ثُمَّ تَعَلَّمُوهَا))

Amesimulia Mu’aadh bin Jabal (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم), katika Hadiyth ndefu, amesema: “…

اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ فِعْلَ الْخَيْرَاتِ، وَتَرْكَ الْمُنْكَرَاتِ، وَحُبَّ الْمَسَاكِينِ، وَأَنْ تَغْفِرَ لِي وَتَرْحَمَنِي، وَإِذَا أَرَدْتَ فِتْنَةً فِي قَوْمٍ فَتَوَفَّنِي غَيْرَ مَفْتُونٍ، وَأَسْأَلُكَ حُبَّكَ، وَحُبَّ مَنْ يُحِبُّكَ، وَحُبَّ عَمَلٍ يُقَرِّبُ إِلَى حُبِّكَ

Yaa Allaah! Hakika mimi nakuomba kutenda mambo ya kheri, na kuacha maovu, na kuwapenda masikini, na Unighufurie na Unirehemu; na Utakapotaka kuwatia watu katika fitna, Unifishe bila ya kufitinika. Nakuomba Mapenzi Yako, na mapenzi ya anayekupenda, na mapenzi ya amali itakayonikurubisha katika Mapenzi Yako.” Kisha Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Hakika hayo ni haki, basi yasomeni kisha mjifunze.” [At-Tirmidhiy (3235), na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh At-Tirmidhiy (3235)]

Na Allaah Mjuzi zaidi

  • 1Tafsiyr As-Sa’diy (5/498), Al-Haqq Al-Waadhwih Al-Mubiyn (69).
  • 2Asmaa Allaah Al-Husnaa, Ar-Raaziy (288), Fat-hu Ar-Rahiym Al-Malik Al-‘Allaam, As-Sa’diy (40).
  • 3Fat-hu Ar-Rahiym Al-Malik Al-‘Allaam, As-Sa’diy (41), Tawdhwiyh Al-Kaafiyah Ash-Shaafiyah (125).