Al-Matiyn: Mwenye Nguvu Madhubuti, Shadidi
Al-Matiyn ni Mwenye nguvu shadidi, Ambaye nguvu Zake hazidhoofiki, na wala Hapatwi na mashaka wala taklifa wala uchovu katika matendo Yake. Nguvu Zake (سبحانه وتعالى) ni timilifu, kamilifu, hazipungui wala hazidhoofiki; na hii inaonyesha kwamba Allaah (تعالى) Amefikia upeo wa mwisho katika nguvu. Na Imaam Al-Ghazaaliy (رحمه الله) amesema: Al-Mataanah inaonyesha ushadidi wa nguvu kwa Allaah (تعالى).1
Jina Hili la Allaah, Al-Matiyn, limetajwa katika Qur-aan mara moja tu, katika Suwrah Adh-Dhaariyaat, pale Aliposema:
إِنَّ اللَّـهَ هُوَ الرَّزَّاقُ ذُو الْقُوَّةِ الْمَتِينُ ﴿٥٨﴾
Hakika Allaah Ndiye Mwingi wa Kuruzuku, Mwenye Nguvu Madhubuti. [Adh-Dhaariyaat (51:58)]
Na Al-Matiyn kilugha ni kitu kilicho thabiti katika nguvu zake, kilichoshikamana barabara, kigumu. Na asili ya neno hili katika lugha inaonyesha ugumu wa kitu pamoja na urefu na upanuzi wake; na Al-Matn ni sehemu ngumu na iliyoinuka ya ardhi. Na mzizi wake م ت ن una maana nne: kuwa na nguvu na ugumu; kuwa imara; kuwa thabiti na mwenye azma; na kuwa na sifa yoyote kwa kiwango cha juu. Basi Al-Matiyn ni kitu chenye nguvu kubwa na uthabiti, ambacho msingi wake hautikisiki.
Na Allaah (تبارك وتعالى) Ana maana nyingi katika Jina Hili na ukamilifu wake:
1-Yeye Ni Mwenye nguvu, Mkali mno kwa kila kinachohitajia hikmah.2
2-Naye Mtukufu Ni Mkali Ambaye nguvu Zake haziishi, wala matendo Yake hayafuatiwi na mashaka wala taabu wala taklifa,3 kwa ukamilifu wa Utukufu Wake, Nguvu Zake na ukamilifu wa Uwezo Wake.
3-Naye Mtukufu Ndiye Al-Matiyn: Mwenye kuenea, Aliyefikia upeo wa mwisho wa ukamilifu katika Dhati Yake, katika Sifa Zake na katika Matendo Yake.4
Tofauti Kati Ya Al-Qawiyy Na Al-Matiyn:
Al-Qawiyy ni Mwenye Sifa ya nguvu zisizokwisha. Ama Al-Matiyn, ni Yule Ambaye pamoja na Nguvu Zake zisizoshindika, Yeye Ni Thabiti na Madhubuti kwa Dhati Yake. Na mchanganyiko huu wa kuwa na nguvu kamilifu pamoja na uthabiti kamili, una maana kwamba hakuna yeyote awezaye kupinga Matendo Yake wala kuzuia Amri Zake zisitekelezwe! Na kwa kuwa maana ya Al-Matiyn ni Mwenye nguvu shadidi, basi Taathira ya imaan kwa Jina Hili inakaribiana na ile ya Jina la Allaah Al-Qawiyy.
Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Matiyn:
1-Kuwa Thabiti Katika Dini Yako:
Sifa ya uthabiti ya Al-Matiyn ikupe ilhamu ya kushikamana na Dini yako wakati wote. Na njia za kuthibitika katika Uislamu ni: kushikamana na Qur-aan na kujitahidi kuifahamu ili utekeleze amri zake na makatazo yake; kuzidisha amali njema; kusoma maisha ya Manabii (عليهم السلام) na kuwaiga; na kutafakari neema za Jannah, adhabu ya moto na machungu ya mauti. Vilevile walinganie wengine katika Dini ya Allaah, kwani kushughulika na kheri kunakukinga na vishawishi vya shaytwaan; na jiweke karibu na watu walio thabiti katika Uislamu, na uwe mwenye kuwapa wengine ilhamu ya kuthibitika. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
يُثَبِّتُ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا بِالْقَوْلِ الثَّابِتِ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الْآخِرَةِ ۖ وَيُضِلُّ اللَّـهُ الظَّالِمِينَ ۚ وَيَفْعَلُ اللَّـهُ مَا يَشَاءُ ﴿٢٧﴾
Allaah Huwathibitisha wale walioamini kwa kauli thabiti katika uhai wa dunia na Aakhira. Na Allaah Huwaacha kupotoka madhalimu. Na Allaah Anafanya Atakavyo. [Ibraahiym (14:27)]
2-Mtegemee Al-Matiyn Hata Ukiwa Dhaifu:
Tambua, ee Mja wa Al-Matiyn: Muumini wa kweli anajua kwamba Allaah Ni Qawiyy, Matiyn, Muweza wa kila kitu; Anatimiza matarajio, na Anakifanya kilicho mbali kiwe karibu. Basi ukiwa dhaifu na Rabb wako Ni Matiyn, usikhofu! Kwani anayemtegemea Allaah humtosheleza, na anayejitosheleza kwa Allaah humkwasisha. Na Allaah (تبارك وتعالى) Hapendi moyo wa Muumini ushikamane na mwingine asiyekuwa Yeye, wala amtegemee mwingine, wala amlalamikie mwingine. Tazama Nabiy Ibraahiym (عليه السلام) alipowaacha ahli zake; mwanamke dhaifu na mtoto mdogo, katika bonde lisilokuwa na mmea wowote, akimtegemea Allaah kwa kuamini Nguvu Zake:
رَّبَّنَا إِنِّي أَسْكَنتُ مِن ذُرِّيَّتِي بِوَادٍ غَيْرِ ذِي زَرْعٍ عِندَ بَيْتِكَ الْمُحَرَّمِ رَبَّنَا لِيُقِيمُوا الصَّلَاةَ فَاجْعَلْ أَفْئِدَةً مِّنَ النَّاسِ تَهْوِي إِلَيْهِمْ وَارْزُقْهُم مِّنَ الثَّمَرَاتِ لَعَلَّهُمْ يَشْكُرُونَ ﴿٣٧﴾
Rabb wetu! Hakika mimi nimewaweka baadhi ya dhuria wangu katika bonde lisilokuwa na mmea wowote, kwenye Nyumba Yako Tukufu (Al-Ka’bah), ee Rabb wetu ili wasimamishe Swalaah. Basi Zijaalie nyoyo za watu zielekee kwao na Uwaruzuku mazao ili wapate kushukuru. [Ibraahiym (14:37)]
3-Kuwa Muumini Mwenye Nguvu Na Mtake Msaada Al-Matiyn:
Muumini anayemjua Al-Matiyn hujitahidi kuwa na nguvu katika imaan yake, ibaada zake na katika kila jambo lenye kumnufaisha, huku akimtaka msaada Al-Matiyn na wala hakati tamaa. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((الْمُؤْمِنُ الْقَوِيُّ خَيْرٌ وَأَحَبُّ إِلَى اللَّهِ مِنَ الْمُؤْمِنِ الضَّعِيفِ، وَفِي كُلٍّ خَيْرٌ، احْرِصْ عَلَى مَا يَنْفَعُكَ، وَاسْتَعِنْ بِاللَّهِ وَلاَ تَعْجِزْ ...))
Amesimulia Abu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Muumini mwenye nguvu ni bora na anapendeza zaidi kwa Allaah kuliko Muumini dhaifu, na katika kila mmoja wao kuna kheri. Pupia yale yanayokunufaisha, na mtake msaada Allaah, wala usishindwe ...” [Muslim]
4-Tahadhari Na Kujiona Una Nguvu Ukaasi Amri Ya Al-Matiyn:
Allaah Al-Matiyn Ametusimulia kuhusu nyumati zilizoasi Amri Yake na Rusuli Wake, na zikajigamba kwa nguvu zao, basi Akazihesabu hesabu kali. Miongoni mwao ni kina ‘Aad waliosema: “Nani mwenye nguvu zaidi kuliko sisi?” Na nguvu ya kweli ni kushikamana na Allaah Pekee, kwa watu binafsi na kwa nyumati. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَفِي عَادٍ إِذْ أَرْسَلْنَا عَلَيْهِمُ الرِّيحَ الْعَقِيمَ ﴿٤١﴾ مَا تَذَرُ مِن شَيْءٍ أَتَتْ عَلَيْهِ إِلَّا جَعَلَتْهُ كَالرَّمِيمِ ﴿٤٢﴾
Na kwa kina ‘Aad, Tulipowapelekea upepo wa adhabu, mkame. Haukuacha chochote ulichokifikia ila ulikifanya kama kilichobungulika na kuoza. [Adh-Dhaariyaat (51:41-42)]
5-Mpango Wa Al-Matiyn Juu Ya Madhalimu Ni Madhubuti:
Tambua kwamba Al-Matiyn Huwapa muhula madhalimu, lakini mpango Wake ni madhubuti usioshindwa. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَأُمْلِي لَهُمْ ۚ إِنَّ كَيْدِي مَتِينٌ ﴿١٨٣﴾
Nami Ninawapa muhula. Hakika Mpango Wangu (wa adhabu) ni wenye nguvu. [Al-A’raaf (7:183)]
6-Kuwa Na Yakini Na Mpango Thabiti Wa Al-Matiyn:
Mpango wa Allaah ni thabiti; hakuna chochote wala yeyote awezaye kuushinda. Allaah Huwaacha watu kwa muda mrefu kwa Hikmah Yake; wapo wanaopinga Uislamu kwa miaka kisha wakaongoka, na wapo wanaoendelea katika maovu wakazidishiwa adhabu. Na Waumini hupata fursa ya kuzidisha thawabu na daraja za juu katika Jannah kwa juhudi zao katika muda huo. Hata kama watu watakupangia njama, Al-Matiyn Atawanusuru Waumini maadamu wana ikhlaasw, na ushindi wa mwisho utakuwa wao. Basi mtegemee Al-Matiyn na jitahidi kuwa na ikhlaasw katika kila amali. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
فَذَرْنِي وَمَن يُكَذِّبُ بِهَـٰذَا الْحَدِيثِ ۖ سَنَسْتَدْرِجُهُم مِّنْ حَيْثُ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٤٤﴾ وَأُمْلِي لَهُمْ ۚ إِنَّ كَيْدِي مَتِينٌ ﴿٤٥﴾
Basi Niache na anayekadhibisha Qur-aan hii. Tutawavuta pole pole adhabuni kwa namna wasiyoijua. Nami Ninawapa muhula. Hakika mpango Wangu ni thabiti. [Al-Qalam (68:44-45)]
7-Usikate Tamaa, Faraja Ya Al-Matiyn Iko Karibu:
Huu ni ujumbe kwa aliyefikwa na huzuni, hali yake ikadhoofika, akachoshwa na maisha yake, akabanwa na dhiki za siku na akaonja uchungu wa mateso: Pokea bishara njema kwamba kuna ufunguzi ulio karibu, nusura iliyo bayana, faraja baada ya shida, wepesi baada ya uzito, na nguvu baada ya udhaifu; kwani Rabb wako Ni Al-Matiyn, Hashindwi na kitu. Tazama kisa hiki:
Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
لِيُنفِقْ ذُو سَعَةٍ مِّن سَعَتِهِ ۖ وَمَن قُدِرَ عَلَيْهِ رِزْقُهُ فَلْيُنفِقْ مِمَّا آتَاهُ اللَّـهُ ۚ لَا يُكَلِّفُ اللَّـهُ نَفْسًا إِلَّا مَا آتَاهَا ۚ سَيَجْعَلُ اللَّـهُ بَعْدَ عُسْرٍ يُسْرًا﴿٧﴾
Ili mwenye wasaa agharimu kwa wasaa wake, na aliyebaniwa rizki yake, basi agharimie katika kile Alichompa Allaah. Allaah Haikalifishi nafsi yoyote ile isipokuwa kwa kile Alichoipa. Allaah Atajaalia baada ya ugumu kuwa wepesi. [Atw-Twalaaq (65:7)]
Na Anasema pia:
فَإِنَّ مَعَ الْعُسْرِ يُسْرًا ﴿٥﴾ إِنَّ مَعَ الْعُسْرِ يُسْرًا ﴿٦﴾
Basi hakika pamoja na kila ugumu kuna wepesi. Hakika pamoja na kila ugumu kuna wepesi. [Ash-Sharh (94:5-6)]
8-Jifunze Siyrah Upate Nguvu Katika Imaan:
Tambua, ee Mja wa Al-Matiyn: Ili kuimarisha utambulisho wako wa Kiislamu, jifunze Siyrah ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) na visa vya waliotangulia ambao walikuwa thabiti katika Dini yao juu ya mitihani mikubwa. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ خَبَّابِ بْنِ الأَرَتِّ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((كَانَ الرَّجُلُ فِيمَنْ قَبْلَكُمْ يُحْفَرُ لَهُ فِي الأَرْضِ فَيُجْعَلُ فِيهِ، فَيُجَاءُ بِالْمِنْشَارِ فَيُوضَعُ عَلَى رَأْسِهِ فَيُشَقُّ بِاثْنَتَيْنِ، وَمَا يَصُدُّهُ ذَلِكَ عَنْ دِينِهِ، وَيُمْشَطُ بِأَمْشَاطِ الْحَدِيدِ مَا دُونَ لَحْمِهِ مِنْ عَظْمٍ أَوْ عَصَبٍ، وَمَا يَصُدُّهُ ذَلِكَ عَنْ دِينِهِ ...))
Amesimulia Khabbaab bin Al-Aratt (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Alikuwa mtu miongoni mwa waliokuwa kabla yenu akichimbiwa shimo ardhini na kutiwa ndani yake, kisha huletwa msumeno ukawekwa juu ya kichwa chake akapasuliwa vipande viwili, na hilo halikumzuia na Dini yake. Na alikuwa akichanwa kwa vitana vya chuma kwenye nyama yake hadi mifupa na mishipa, na hilo halikumzuia na Dini yake ...” [Al-Bukhaariy]
9-Al-Matiyn Huwathibitisha Waumini Kwa Kauli Thabiti:
Uthabiti wa kweli katika dunia na kaburini ni kutoka kwa Al-Matiyn. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
يُثَبِّتُ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا بِالْقَوْلِ الثَّابِتِ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الْآخِرَةِ ۖ وَيُضِلُّ اللَّـهُ الظَّالِمِينَ ۚ وَيَفْعَلُ اللَّـهُ مَا يَشَاءُ﴿٢٧﴾
Allaah Huwathibitisha wale walioamini kwa kauli thabiti katika uhai wa dunia na Aakhira. Na Allaah Huwaacha kupotoka madhalimu. Na Allaah Anafanya Atakavyo. [Ibraahiym (14:27)]
10-Muombe Al-Matiyn Akuthibitishe Katika Dini Yake:
Kuwa thabiti katika nyakati za raha na shida iwe ni katika Du’aa zako za kila siku, kwani moyo hubadilika badilika. Hifadhi Du’aa hii aliyokuwa akiikithirisha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) na umuombe Al-Matiyn kwa dhati ya moyo wako:
عَنْ أَنَسٍ (رضي الله عنه) قَالَ: كَانَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) يُكْثِرُ أَنْ يَقُولَ: ((يَا مُقَلِّبَ الْقُلُوبِ ثَبِّتْ قَلْبِي عَلَى دِينِكَ))
Amesimulia Anas (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akikithirisha kusema:
يَا مُقَلِّبَ الْقُلُوبِ ثَبِّتْ قَلْبِي عَلَى دِينِكَ
Ee Mwenye Kupindua nyoyo, Uthibitishe moyo wangu juu ya Dini Yako. [At-Tirmidhiy (2140), na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh At-Tirmidhiy]
Na Allaah Mjuzi zaidi