Skip to main content

Majina Mazuri Ya Allaah052 - Al-Ghaniyy

Majina Mazuri Ya Allaah Jina 052 kati ya 103
Al-Ghaniyy — Majina Mazuri ya Allaah

Al-Ghaniyy: Mkwasi, Mwenye Kujitosheleza

Al-Ghaniyy Ni Yule Ambaye Hamhitajii kiumbe Wake yeyote kwa sababu ya ukamilifu Wake mpana na ukamilifu wa Sifa Zake, na viumbe vyote vinamhitajia Yeye, Neema Zake na Msaada Wake. Amejitosheleza kwa Uwezo Wake na Utukufu wa Mamlaka Yake, na viumbe ni mafakiri Kwake. Yeye Ni Mkwasi kwa Dhati Yake; Ana ukwasi kamili usio na mipaka, si kwa sababu fulani iliyomwajibishia ukwasi huo. Na mja ni fakiri kwa dhati yake, si kwa sababu fulani iliyomwajibishia ufakiri huo; kwa hiyo haiwezekani mja awe isipokuwa ni mja, wala Rabb Awe isipokuwa Ni Rabb.

Jina Hili la Allaah, Al-Ghaniyy, limetajwa katika Qur-aan mara kumi na nane, na mara kumi kati ya hizo limekuja pamoja na Jina Lake Al-Hamiyd (Mwenye Kustahiki Kuhimidiwa). Miongoni mwa Aayah hizo ni Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى):

يَا أَيُّهَا النَّاسُ أَنتُمُ الْفُقَرَاءُ إِلَى اللَّـهِ ۖ وَاللَّـهُ هُوَ الْغَنِيُّ الْحَمِيدُ ﴿١٥﴾

Enyi watu! Nyinyi ni mafakiri kwa Allaah! Na Allaah Ndiye Mkwasi, Mwenye Kustahiki Kuhimidiwa kwa yote. [Faatwir (35:15)]

Na Al-Ghaniyy kilugha ni kinachotosheleza; yaani Yule mwenye kujitosheleza Asiyemhitajia mwingine.1 Na mzizi wake غ ن ي una maana nne: kujitosheleza na kutotegemea wengine; kutokuwa na haja wala uhitaji wowote; kuridhika na kukinai; na kuwa tajiri mwenye mali. Na kinyume cha ghinaa (ukwasi) ni faqr (ufakiri), yaani uhitaji. Kwa hakika hakuna yeyote asiyemhitajia Allaah (عزّ وجلّ), na kila mmoja anamtegemea Yeye Pekee. Basi Al-Ghaniyy Ndiye Pekee Aliyevuka mipaka ya kila haja, Ambaye viumbe wote wanategemea Ukwasi Wake, utajiri Wake na Neema Zake.

Na Allaah (تبارك وتعالى) Ana maana nyingi katika Jina Hili na ukamilifu wake:

1-Allaah Ndiye Al-Ghaniyy, yaani Ndiye Mwenye kujitosheleza kwa ujumla, na kila mmoja ni fakiri Kwake na mwenye kumhitajia katika hali zote; kwa Neema Zake, kwa ihsaan Yake, kwa kumkidhia mahitaji yake, kwa msaada katika mambo ya Dini yake na dunia yake, katika kupata maslahi na kuzuia madhara na mambo mabaya,2 katika kila wakati, hatua, fikra na harakati, kama ilivyotangulia katika Kauli Yake: “Enyi watu! Nyinyi ni mafakiri kwa Allaah!”

2-Miongoni mwa ukamilifu wa kujitosheleza Kwake ni kwamba haumnufaishi utiifu wa wenye kutii, wala hayamdhuru maasi ya wenye kuasi, hata kama viumbe wote watakufuru. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

فِيهِ آيَاتٌ بَيِّنَاتٌ مَّقَامُ إِبْرَاهِيمَ ۖ وَمَن دَخَلَهُ كَانَ آمِنًا ۗ وَلِلَّـهِ عَلَى النَّاسِ حِجُّ الْبَيْتِ مَنِ اسْتَطَاعَ إِلَيْهِ سَبِيلًا ۚ وَمَن كَفَرَ فَإِنَّ اللَّـهَ غَنِيٌّ عَنِ الْعَالَمِينَ ﴿٩٧﴾

Ndani yake kuna Aayaat (Ishara na Dalili) zilizo wazi mahali aliposimama Ibraahiym (kujenga). Na mwenye kuingia humo anakuwa katika amani. Na kwa ajili ya Allaah imewajibika watu watekeleze Hajj katika nyumba (Al-Ka’bah) hiyo kwa mwenye uwezo. Na atakayekufuru, basi hakika Allaah Ni Mkwasi kwa walimwengu. [Aal-‘Imraan (3:97)]

Na Anasema kuhusu Nabiy Muwsaa (عليه السلام) aliyewaambia watu wake: “Mkikufuru nyinyi na wote walioko ardhini, basi hakika Allaah Ni Mkwasi, Mwenye Kustahiki Kuhimidiwa kwa yote.” (Rejea chini: Faida namba 3, Ibraahiym (14:7-8)).

Na Allaah (تعالى) Amesema katika Hadiyth Al-Qudsiy:

عَنْ أَبِي ذَرٍّ (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) فِيمَا رَوَى عَنِ اللَّهِ تَبَارَكَ وَتَعَالَى أَنَّهُ قَالَ: ((... يَا عِبَادِي إِنَّكُمْ لَنْ تَبْلُغُوا ضَرِّي فَتَضُرُّونِي، وَلَنْ تَبْلُغُوا نَفْعِي فَتَنْفَعُونِي ...))

Amesimulia Abu Dharr (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema katika aliyoyapokea kutoka kwa Allaah (تبارك وتعالى) kwamba Amesema: “... Enyi Waja Wangu! Hakika nyinyi hamtoweza kufikia kunidhuru mkanidhuru, na wala hamtoweza kufikia kuninufaisha mkaninufaisha ...” [Muslim]

3-Naye Mtukufu Ndiye Al-Ghaniyy Anayewafanyia wema Waja Wake pamoja na kujitosheleza nao; Anawatakia kheri na Anawaondolea madhara, si kwa kutaka kupata manufaa yoyote kutoka kwa mja wala kujikinga na madhara, bali ni kwa kumhurumia na kumfanyia ihsaan.3 Na ndio maana Ghinaa Yake imekuja pamoja na Rehma Yake; kwani mtu anaweza kuwa na huruma lakini ni fakiri asiweze kufanya lolote, ama Allaah Ni Mkwasi, Mwenye Rehma, basi Ukwasi Wake na Rehma Yake vinampa mja kila kitu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَرَبُّكَ الْغَنِيُّ ذُو الرَّحْمَةِ ۚ إِن يَشَأْ يُذْهِبْكُمْ وَيَسْتَخْلِفْ مِن بَعْدِكُم مَّا يَشَاءُ كَمَا أَنشَأَكُم مِّن ذُرِّيَّةِ قَوْمٍ آخَرِينَ ﴿١٣٣﴾

Na Rabb wako Ni Mkwasi Mwenye Rehma. Akitaka Atakuondosheni na Aweke wengine Awatakao badala yenu kama Alivyokuzalisheni nyinyi kutokana na vizazi vya watu wengine. [Al-An’aam (6:133)]

4-Katika ukamilifu wa kujitosheleza Kwake ni kutakasika na kila sifa ya upungufu na aibu, na kila chenye kukanusha kujitosheleza Kwake; miongoni mwayo ni: Hana mwana, Hana mshirika katika Ufalme Wake, wala Hana msaidizi kwa sababu ya udhaifu, na wala Hafanani na yeyote. Yeye Ni Al-Ghaniyy Aliyekamilika kwa Sifa Zake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَقُلِ الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي لَمْ يَتَّخِذْ وَلَدًا وَلَمْ يَكُن لَّهُ شَرِيكٌ فِي الْمُلْكِ وَلَمْ يَكُن لَّهُ وَلِيٌّ مِّنَ الذُّلِّ ۖ وَكَبِّرْهُ تَكْبِيرًا ﴿١١١﴾

Na sema: AlhamduliLLaah (Himdi Anastahiki Allaah) Ambaye Hakujifanyia mwana na wala Hakuwa na mshirika katika ufalme, na wala Hakuwa dhalili hata Awe (Anahitaji) mlinzi (na msaidizi), na mtukuze matukuzo makubwa kabisa. [Al-Israa (17:111)]

Na Anasema pia (سبحانه وتعالى):

قُلْ هُوَ اللَّـهُ أَحَدٌ ﴿١﴾ اللَّـهُ الصَّمَدُ ﴿٢﴾ لَمْ يَلِدْ وَلَمْ يُولَدْ ﴿٣﴾ وَلَمْ يَكُن لَّهُ كُفُوًا أَحَدٌ ﴿٤﴾

Sema: Yeye Allaah Ni Mmoja Pekee. Allaah Aliyekamilika Sifa za Utukufu Wake, Mkusudiwa haja zote. Hakuzaa wala Hakuzaliwa. Na wala haiwi Awe na yeyote anayefanana na kulingana Naye. [Al-Ikhlaasw (112:1-4)]

5-Yeye Mtukufu Ni Mwenye kujitosheleza na kila mshirika katika Uungu Wake. Allaah (تعالى) Amesema katika Hadiyth Al-Qudsiy:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((قَالَ اللَّهُ تَبَارَكَ وَتَعَالَى: أَنَا أَغْنَى الشُّرَكَاءِ عَنِ الشِّرْكِ، مَنْ عَمِلَ عَمَلاً أَشْرَكَ فِيهِ مَعِي غَيْرِي تَرَكْتُهُ وَشِرْكَهُ))

Amesimulia Abu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Allaah (تبارك وتعالى) Amesema: Mimi Ni Mkwasi kabisa wa washirika kutokana na kushirikishwa. Atakayefanya amali akanishirikisha humo na mwingine, Nitamwacha yeye na shirki yake.” [Muslim]

6-Naye Mtukufu Ni Al-Ghaniyy Mwenye kuwatosheleza viumbe Vyake vyote kwa ukwasi wa jumla; Amethibitisha ufakiri wa viumbe Wake, na Akawapa rizqi na yanayofuatia katika Neema nyingi zisizohesabika, na Akawasahilishia sababu zenye kupelekea kwenye ukwasi. Na lililo muhimu zaidi ni kwamba Allaah (تعالى) Ametajirisha nyoyo za Waja Wake kwa Aliyowapa katika ilimu mbalimbali kuhusu Yeye Muumbaji na hakika za imaan; hivyo Akawatosheleza kwa dunia yao na Aakhirah yao kiasi kwamba nyoyo zao zimeshikamana Naye, zikajitosheleza Kwake, wala hazikumgeukia mwingine asiyekuwa Yeye.4

7-Katika ukamilifu wa kujitosheleza Kwake (تعالى) ni kwamba Anaweza kutekeleza Matakwa Yake katika Muradi Wake wakati wowote Autakao.5

Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Ghaniyy:

1-Tambua Ufakiri Wako Kwa Al-Ghaniyy Na Usijione Umejitosheleza:

Njia ya kupata ukwasi kwa Allaah ni kuwa fakiri Kwake. Na ufakiri huu ni wa aina mbili: ufakiri wa lazima, ambao ni wa jumla, hakuna mwema wala muovu atakayeutoka, kwa sababu kila kiumbe jambo lake liko Mkononi mwa Muumbaji Wake, Anayemruzuku chakula chake na kinywaji chake. Na ufakiri wa khiari, ambao ni matunda ya ilimu mbili tukufu: mja kumjua Rabb wake kwa ukwasi usio na mipaka, na kujijua nafsi yake kwa ufakiri usio na mipaka kwa Allaah. Basi ilimu hizo mbili zikipatikana, huzaa ufakiri ambao ndio ukwasi wake hasa na alama ya kufaulu kwake na furaha yake. Na ufakiri wa ukweli ni kudumu kumhitajia Allaah katika kila hali. Ama mja akisahau ufakiri wake kwa Rabb wake, akajiona amejitosheleza na utiifu Kwake, huvuka mipaka, na kuvuka mipaka ndio daraja ya juu kabisa ya kuidhulumu nafsi. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

كَلَّا إِنَّ الْإِنسَانَ لَيَطْغَىٰ ﴿٦﴾ أَن رَّآهُ اسْتَغْنَىٰ ﴿٧﴾

Laa hasha! Hakika binaadam bila shaka hupindukia mipaka kuasi. Anapojiona kuwa amejitosheleza. [Al-‘Alaq (96:6-7)]

2-Al-Ghaniyy Hahitaji Waja Wake, Na Akigeuka Mtu Atamleta Mwingine:

Tambua, ee Mja wa Al-Ghaniyy: Utiifu wako haumzidishii Allaah kitu, na kukengeuka kwako hakumpunguzii kitu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

هَا أَنتُمْ هَـٰؤُلَاءِ تُدْعَوْنَ لِتُنفِقُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ فَمِنكُم مَّن يَبْخَلُ ۖ وَمَن يَبْخَلْ فَإِنَّمَا يَبْخَلُ عَن نَّفْسِهِ ۚ وَاللَّـهُ الْغَنِيُّ وَأَنتُمُ الْفُقَرَاءُ ۚ وَإِن تَتَوَلَّوْا يَسْتَبْدِلْ قَوْمًا غَيْرَكُمْ ثُمَّ لَا يَكُونُوا أَمْثَالَكُم﴿٣٨﴾

Ha! Nyinyi ndio hawa mnaoitwa ili mtoe katika Njia ya Allaah. Basi yuko miongoni mwenu ambaye anafanya ubakhili, na afanyaye ubakhili, basi hakika hapana ila anafanya ubakhili dhidi ya nafsi yake. Na Allaah Ni Mkwasi, nanyi ni mafakiri. Na mkikengeuka Atabadilisha watu ghairi yenu kisha hawatokuwa mfano wenu. [Muhammad (47:38)]

3-Tahadhari! Usijitosheleze Na Allaah Ukafanya Ubakhili:

Na mwenye kujiona amejitosheleza na Allaah, akafanya ubakhili na akakadhibisha, basi ameandikiwa mashaka. Hata kama wewe ni tajiri, mwenye sura nzuri au kazi nzuri, jikumbushe Nani Mmiliki halisi wa kila kitu, na tumia mali yako, nguvu zako na cheo chako kwa ajili ya kumridhisha Yeye Pekee. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَأَمَّا مَن بَخِلَ وَاسْتَغْنَىٰ ﴿٨﴾ وَكَذَّبَ بِالْحُسْنَىٰ ﴿٩﴾ فَسَنُيَسِّرُهُ لِلْعُسْرَىٰ ﴿١٠﴾

Ama yule afanyaye ubakhili na akajiona amejitosheleza. Na akakadhibisha Al-Husnaa (Jazaa na Kalimah ya laa ilaaha illa Allaah). Basi Tutamuwepesishia kwa yaliyo magumu. [Al-Layl (92:8-10)]

4-Mshukuru Al-Ghaniyy Kwa Kila Neema:

Kila unapopata kheri yoyote, kama kupandishwa cheo kazini, faida ya mali au jambo lolote lenye manufaa kwako, hakikisha jambo la kwanza unalofanya ni kumshukuru Al-Ghaniyy, na umuombe Akusaidie kulitumia kwa hikmah na Alijaalie kuwa ni chanzo cha Baraka kwako. Na tambua kwamba shukurani yako haimzidishii Allaah chochote, bali ni wewe unayenufaika nayo. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَإِذْ تَأَذَّنَ رَبُّكُمْ لَئِن شَكَرْتُمْ لَأَزِيدَنَّكُمْ ۖ وَلَئِن كَفَرْتُمْ إِنَّ عَذَابِي لَشَدِيدٌ ﴿٧﴾ وَقَالَ مُوسَىٰ إِن تَكْفُرُوا أَنتُمْ وَمَن فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا فَإِنَّ اللَّـهَ لَغَنِيٌّ حَمِيدٌ ﴿٨﴾

Na pindi Alipotangaza Rabb wenu: Ikiwa mtashukuru, bila shaka Nitakuzidishieni (Neema Zangu), na mkikufuru, basi hakika Adhabu Yangu ni kali. Na Muwsaa alisema: Mkikufuru nyinyi na wote walioko ardhini, basi hakika Allaah Ni Mkwasi, Mwenye Kustahiki Kuhimidiwa kwa yote. [Ibraahiym (14:7-8)]

5-Ridhika, Kwani Ukwasi Wa Kweli Ni Ukwasi Wa Nafsi:

Tambua, ee Mja wa Al-Ghaniyy, kwamba ukwasi wa kweli si wingi wa mali, bali ni kuridhika kwa nafsi.

Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) ameubainisha ukweli wa ukwasi wa mwana-Aadam; kwamba yule ambaye Allaah Ameweka ukwasi katika nafsi yake basi Amemtajirisha. Basi mwenye kuridhika na aliyogawiwa na Allaah, atakuwa ni tajiri kwa hilo. Na daraja ya juu kabisa ya ukwasi ni kuridhika na Qadar ya Allaah; kwa hiyo jitahidi kuwa na ridhaa kwa kila Anachokupa Al-Ghaniyy au Anachokuzuilia, kwani huo ndio ufunguo wa utulivu wa nafsi yako. Na Imaam Ibn Al-Qayyim (رحمه الله) ametaja daraja tatu za ukwasi: ukwasi wa moyo, nao ni kushikamana kwake na Allaah Pekee; ukwasi wa nafsi, nao ni kunyooka kwake juu ya haki na kusalimika kwake na riyaa; na ukwasi kwa Al-Haqq, nao ni kutafakari Uawali Wake (تعالى), kwamba Yeye Ametangulia vitu vyote, vilikuwa havipo na Yeye Ndiye Aliyevipa uwepo.

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((لَيْسَ الْغِنَى عَنْ كَثْرَةِ الْعَرَضِ، وَلَكِنَّ الْغِنَى غِنَى النَّفْسِ))

Amesimulia Abu Hurayrah (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Ukwasi si kwa wingi wa mali, lakini ukwasi (hasa) ni ukwasi wa nafsi.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

6-Tambua Kwamba Ukwasi Wa Mali Haupingani Na Ufakiri Kwa Allaah:

Ufakiri huu kwa Allaah haupingani na kuwa na mali wala milki. Manabii (عليهم السلام) walikuwa katika kilele chake pamoja na mali zao na ufalme wao; kama Nabiy Ibraahiym (عليه السلام) aliyekuwa mkarimu wa wageni na mwenye mali na mifugo, na vilevile Nabiy Sulaymaan na Nabiy Daawuwd (عليهما السلام), na vilevile Nabiy wetu (صلى الله عليه وآله وسلم). Basi Manabii walikuwa matajiri katika ufakiri wao, na mafakiri katika utajiri wao. Na ufakiri wa kweli ni kutojitosheleza kwa chochote kisichokuwa Allaah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَوَجَدَكَ عَائِلًا فَأَغْنَىٰ ﴿٨﴾

Na Akakukuta mhitaji, Akakutosheleza? [Adhw-Dhwuhaa (93:8)]

7-Jiepushe Na Kuwaomba Watu Bila Ya Haja:

Tambua, ee Mja wa Al-Ghaniyy: Ukwasi ni wa aina mbili: kujitosheleza kwa Allaah, na kujitosheleza na wasiokuwa Allaah. Basi jitahidi usiwe mzigo kwa Waislamu wengine wala usiwe mvivu. Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema kwamba ni bora mmoja wenu kuchukua kamba akaleta mzigo wa kuni mgongoni mwake akauza, na Allaah Akamhifadhi uso wake kwa hilo, kuliko kuwaomba watu ambao huenda wakampa au wasimpe. Na usiwaombe watu kwa ajili ya kuongeza mali yako tu, kwani ameonya kwamba mwenye kuwaomba watu ili kujilimbikizia mali, basi hakika anaomba kaa la moto. Na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amebainisha thawabu za mwenye kujitosheleza kwa Allaah na wasiokuwa Yeye:

عَنْ أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيِّ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((... وَمَنْ يَسْتَعْفِفْ يُعِفَّهُ اللَّهُ، وَمَنْ يَسْتَغْنِ يُغْنِهِ اللَّهُ، وَمَنْ يَتَصَبَّرْ يُصَبِّرْهُ اللَّهُ ...))

Amesimulia Abu Sa‘iyd Al-Khudriyy (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “... Na atakayejizuia (kuomba), Allaah Atamhifadhi, na atakayejitosheleza, Allaah Atamtosheleza, na atakayejikaza kusubiri, Allaah Atampa subira ...” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

8-Toa Katika Njia Ya Al-Ghaniyy Kutokana Na Unachokipenda:

Unapotoa swadaqah, kumbuka kwamba Allaah Ni Mkwasi kabisa, Hahitajii mali yako; bali lengo ni kupunguza tofauti baina ya tajiri na masikini, na ni taqwa yako ndiyo inayomfikia Allaah. Toa kutoka katika mali ya halaal, na usitoe kile ambacho wewe mwenyewe usingekipenda. Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) amesema kwamba Allaah Amewaamrisha watoe kutoka katika mali yao iliyo safi zaidi na bora zaidi, na Amewakataza kutoa kutoka katika mali mbaya, kwa sababu Allaah Ni Twayyib (Mzuri) na Hakubali isipokuwa kilicho kizuri. Basi toa kitu unachokipenda nawe utaona athari yake moyoni mwako! Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

هَا أَنتُمْ هَـٰؤُلَاءِ تُدْعَوْنَ لِتُنفِقُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ فَمِنكُم مَّن يَبْخَلُ ۖ وَمَن يَبْخَلْ فَإِنَّمَا يَبْخَلُ عَن نَّفْسِهِ ۚ وَاللَّـهُ الْغَنِيُّ وَأَنتُمُ الْفُقَرَاءُ ۚ وَإِن تَتَوَلَّوْا يَسْتَبْدِلْ قَوْمًا غَيْرَكُمْ ثُمَّ لَا يَكُونُوا أَمْثَالَكُم ﴿٣٨﴾

Ha! Nyinyi ndio hawa mnaoitwa ili mtoe katika Njia ya Allaah. Basi yuko miongoni mwenu ambaye anafanya ubakhili, na afanyaye ubakhili, basi hakika hapana ila anafanya ubakhili dhidi ya nafsi yake. Na Allaah Ni Mkwasi, nanyi ni mafakiri. Na mkikengeuka Atabadilisha watu ghairi yenu kisha hawatokuwa mfano wenu. [Muhammad (47:38)]

9-Muombe Al-Ghaniyy Kila Wakati:

Tambua, ee Mja wa Al-Ghaniyy: Miongoni mwa ukamilifu wa Ukwasi Wake na Ukarimu Wake ni kwamba Anawaamrisha Waja Wake wamuombe Du’aa kila wakati, na Anawaahidi kuwajibu du’aa zao, kuwakidhia haja zao, na kuwapa katika Fadhila Zake yale waliyoomba na wasiyoyaomba.6

وَقَالَ رَبُّكُمُ ادْعُونِي أَسْتَجِبْ لَكُمْ ۚ إِنَّ الَّذِينَ يَسْتَكْبِرُونَ عَنْ عِبَادَتِي سَيَدْخُلُونَ جَهَنَّمَ دَاخِرِينَ ﴿٦٠﴾

Na Rabb wenu Amesema: Niombeni, Nitakuitikieni. Hakika wale wanaotakabari katika kuniabudu wataingia Jahannam wadhalilike. [Ghaafir (40:60)]

Basi usiogope kamwe kumuomba, kwani ni nani mwingine utakayemuomba? Na njia bora ya kujikurubisha kwa Allaah ni kudumu kumhitajia katika hali zote, kushikamana na Sunnah katika kila kitendo, na kutafuta rizqi ya halaal. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((لَيْسَ شَيْءٌ أَكْرَمَ عَلَى اللَّهِ تَعَالَى مِنَ الدُّعَاءِ))

Amesimulia Abu Hurayrah (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakuna kitu kitukufu zaidi kwa Allaah (تعالى) kuliko Du’aa.” [At-Tirmidhiy (3370), Ibn Maajah, na Imaam Al-Albaaniy ameipa daraja ya Hasan katika Swahiyh At-Tirmidhiy]

10-Omba Du’aa Ya Nabiy Muwsaa Kwa Al-Ghaniyy:

Tumia Du’aa hii nzuri na pana ya Nabiy Muwsaa (عليه السلام) huku ukitambua uhitaji wako kwa Al-Ghaniyy:

رَبِّ إِنِّي لِمَا أَنزَلْتَ إِلَيَّ مِنْ خَيْرٍ فَقِيرٌ

Rabb wangu! Hakika mimi ni mhitajia wa kheri yoyote Utakayoniteremshia. [Al-Qaswasw (28:24)]

Na Allaah Mjuzi zaidi

  • 1Lisaan Al-‘Arab (5/3308), Mu‘jam Maqaayiys Al-Lughah (3/397).
  • 2Tawdhwiyh Al-Kaafiyah Ash-Shaafiyah (119).
  • 3Ighaathat Al-Lahfaan (1/41).
  • 4Tafsiyr As-Sa‘diy (5/629), na Fat-hu Ar-Rahiym Al-Malik Al-‘Allaam (38).
  • 5Al-I‘tiqaad, Al-Bayhaqiy (38).
  • 6Ighaathat Al-Lahfaan (1/47), na Fat-hu Ar-Rahiym Al-Malik Al-‘Allaam (38).