As-Sittiyr: Mwingi wa kusitiri; Anayesitiri aibu na madhambi ya Waja Wake, wala Hawaumbui, na Anayependa sitara.
Jina hili tukufu limethibiti katika Sunnah, pamoja na Jina Al-Hayiyy:
عَنْ يَعْلَى بْنِ أُمَيَّةَ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) رَأَى رَجُلاً يَغْتَسِلُ بِالْبَرَازِ، فَصَعِدَ الْمِنْبَرَ فَحَمِدَ اللَّهَ وَأَثْنَى عَلَيْهِ ثُمَّ قَالَ: ((إِنَّ اللَّهَ عَزَّ وَجَلَّ حَلِيمٌ حَيِيٌّ سِتِّيرٌ، يُحِبُّ الْحَيَاءَ وَالسَّتْرَ، فَإِذَا اغْتَسَلَ أَحَدُكُمْ فَلْيَسْتَتِرْ))
Amesimulia Ya’laa bin Umayyah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alimwona mtu akioga uwanjani (bila sitara), akapanda minbari, akamhimidi Allaah na kumsifu, kisha akasema: “Hakika Allaah (عزّ وجلّ) Ni Mpole, Mwenye haya, Mwingi wa kusitiri; Anapenda haya na sitara. Basi mmoja wenu akioga, ajisitiri.” [Abuu Daawuwd (4012), An-Nasaaiy (406), na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha]
Maana Ya As-Sittiyr:
1-Allaah (سبحانه وتعالى) Anawasitiri Waja Wake duniani, na Anamsitiri Muumini hata Siku ya Qiyaamah. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنِ ابْنِ عُمَرَ (رضي الله عنهما) قَالَ: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) يَقُولُ: ((إِنَّ اللَّهَ يُدْنِي الْمُؤْمِنَ فَيَضَعُ عَلَيْهِ كَنَفَهُ وَيَسْتُرُهُ فَيَقُولُ: أَتَعْرِفُ ذَنْبَ كَذَا؟ أَتَعْرِفُ ذَنْبَ كَذَا؟ فَيَقُولُ: نَعَمْ أَيْ رَبِّ، حَتَّى إِذَا قَرَّرَهُ بِذُنُوبِهِ وَرَأَى فِي نَفْسِهِ أَنَّهُ هَلَكَ قَالَ: سَتَرْتُهَا عَلَيْكَ فِي الدُّنْيَا، وَأَنَا أَغْفِرُهَا لَكَ الْيَوْمَ))
Amesimulia Ibn ‘Umar (رضي الله عنهما): Nimemsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: “Hakika Allaah Atamkurubisha Muumini, Atamwekea Hifadhi Yake na Atamsitiri, kisha Atasema: Je, unaijua dhambi kadhaa? Je, unaijua dhambi kadhaa? Atasema: Ndiyo, yaa Rabbi. Mpaka Atakapomkirisha madhambi yake, na akaona katika nafsi yake kwamba ameangamia, Atasema: Nilikusitiria duniani, na leo Ninakughufuria.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]
2-Na Anapenda sitara kwa Waja Wake, katika miili yao na katika aibu zao (rejea Hadiyth ya Ya’laa (رضي الله عنه) juu).
Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, As-Sittiyr:
1-Tambua Kwamba As-Sittiyr Anakusitiri Kila Siku:
Tambua kwamba lau si sitara ya As-Sittiyr, watu wangejua madhambi yako yote; basi mshukuru na utubie.
2-Wasitiri Ndugu Zako Waislamu:
Kumbuka, ee Mja wa As-Sittiyr, kwamba anayemsitiri Muislamu, Allaah Humsitiri Siku ya Qiyaamah. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ عُمَرَ (رضي الله عنهما) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((الْمُسْلِمُ أَخُو الْمُسْلِمِ، لاَ يَظْلِمُهُ وَلاَ يُسْلِمُهُ ... وَمَنْ سَتَرَ مُسْلِمًا سَتَرَهُ اللَّهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ))
Amesimulia ‘Abdullaah bin ‘Umar (رضي الله عنهما) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Muislamu ni nduguye Muislamu; hamdhulumu wala hamwachi (kwa adui) … Na atakayemsitiri Muislamu, Allaah Atamsitiri Siku ya Qiyaamah.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]
3-Usiifichue Sitara Aliyokuwekea As-Sittiyr:
Tahadhari na kutangaza madhambi yako ambayo As-Sittiyr Ameyasitiri. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) يَقُولُ: ((كُلُّ أُمَّتِي مُعَافًى إِلاَّ الْمُجَاهِرِينَ، وَإِنَّ مِنَ الْمَجَانَةِ أَنْ يَعْمَلَ الرَّجُلُ بِاللَّيْلِ عَمَلاً، ثُمَّ يُصْبِحَ وَقَدْ سَتَرَهُ اللَّهُ عَلَيْهِ فَيَقُولَ: يَا فُلاَنُ، عَمِلْتُ الْبَارِحَةَ كَذَا وَكَذَا، وَقَدْ بَاتَ يَسْتُرُهُ رَبُّهُ، وَيُصْبِحُ يَكْشِفُ سِتْرَ اللَّهِ عَنْهُ))
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Nimemsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: “Ummah wangu wote watasamehewa isipokuwa wanaotangaza (maasi yao). Na katika kutangaza ni mtu kufanya kitendo usiku, kisha anaamka asubuhi na Allaah Amemsitiri, akasema: Yaa fulani! Jana usiku nilifanya kadhaa na kadhaa. Amelala usiku Rabb wake Akimsitiri, na anaamka asubuhi anaifichua sitara ya Allaah juu yake.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]
4-Usizifuatilie Aibu Za Watu:
Kumbuka kwamba As-Sittiyr Amekataza kupeleleza na kusengenya. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اجْتَنِبُوا كَثِيرًا مِّنَ الظَّنِّ إِنَّ بَعْضَ الظَّنِّ إِثْمٌ ۖ وَلَا تَجَسَّسُوا وَلَا يَغْتَب بَّعْضُكُم بَعْضًا ۚ أَيُحِبُّ أَحَدُكُمْ أَن يَأْكُلَ لَحْمَ أَخِيهِ مَيْتًا فَكَرِهْتُمُوهُ ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ تَوَّابٌ رَّحِيمٌ﴿١٢﴾
Enyi walioamini! Jiepusheni sana na dhana, kwani hakika baadhi ya dhana ni dhambi. Na wala msichunguzane, na wala msisengenyane nyinyi kwa nyinyi. Je, anapenda mmoja wenu kwamba ale nyama ya nduguye aliyekufa? Basi mmelichukia hilo! Na mcheni Allaah! Hakika Allaah Ni Mwingi wa Kupokea Tawbah, Mwenye Kurehemu. [Al-Hujuraat (49:12)]
5-Jisitiri Kimwili Kama Anavyopenda As-Sittiyr:
Tambua, ee Mja wa As-Sittiyr, kwamba sitara ya mwili ni sehemu ya haya na imaan (rejea Hadiyth ya Ya’laa (رضي الله عنه) juu), na vazi la taqwa ndilo bora. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
يَا بَنِي آدَمَ قَدْ أَنزَلْنَا عَلَيْكُمْ لِبَاسًا يُوَارِي سَوْآتِكُمْ وَرِيشًا ۖ وَلِبَاسُ التَّقْوَىٰ ذَٰلِكَ خَيْرٌ ۚ ذَٰلِكَ مِنْ آيَاتِ اللَّـهِ لَعَلَّهُمْ يَذَّكَّرُونَ ﴿٢٦﴾
Enyi wana wa Aadam! Kwa yakini Tumekuteremshieni libasi (nguo) inayositiri tupu zenu na libasi ya mapambo. Na libasi ya taqwa ndiyo bora zaidi. Hizo ni katika Aayaat (Ishara, Dalili, Hoja) za Allaah ili wapate kukumbuka. [Al-A’raaf (7:26)]
6-Tubia Kwa Siri Unapokosea:
Kumbuka kwamba As-Sittiyr Amekusitiri; basi tubia Kwake kwa siri, na usiwaeleze watu dhambi zako.
7-Usipende Maovu Yaenee Katika Jamii:
Tahadhari, ee Mja wa As-Sittiyr, na kupenda kueneza habari za maovu na aibu za Waumini. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
إِنَّ الَّذِينَ يُحِبُّونَ أَن تَشِيعَ الْفَاحِشَةُ فِي الَّذِينَ آمَنُوا لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ ۚ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ ﴿١٩﴾
Hakika wale wanaopenda uenee uchafu wa kashfa kwa wale walioamini, watapata adhabu iumizayo duniani na Aakhirah. Na Allaah Anajua nanyi hamjui. [An-Nuwr (24:19)]
8-Tumaini Sitara Ya As-Sittiyr Siku Ya Qiyaamah:
Tambua kwamba As-Sittiyr Atamsitiri Muumini Siku ya Qiyaamah na Kumghufuria (rejea Hadiyth ya Ibn ‘Umar (رضي الله عنهما) juu); basi zidisha mema na istighfaar.
9-Wasitiri Walio Chini Ya Usimamizi Wako:
Kumbuka, ee Mja wa As-Sittiyr, kwamba wazazi, walimu na viongozi wanapaswa kuwasitiri walio chini yao na kuwarekebisha kwa siri badala ya kuwaumbua.
10-Mwombe As-Sittiyr Akusitiri Aibu Zako:
Omba du’aa, ee Mja wa As-Sittiyr, kila asubuhi na jioni: “اللَّهُمَّ اسْتُرْ عَوْرَاتِي، وَآمِنْ رَوْعَاتِي” (Yaa Allaah! Nisitiri aibu zangu, na Unitulize khofu zangu). Rejea du’aa kamili katika 019-As-Salaam.
Na Allaah Mjuzi zaidi