Skip to main content
Majina Mazuri Ya Allaah Jina 100 kati ya 103
Al-Muhsin — Majina Mazuri ya Allaah

Al-Muhsin: Mwenye Kufanya Ihsaan; Mwenye kuwafanyia wema na kuwaneemesha viumbe Vyake kwa fadhila zinazozidi uadilifu, na Aliyefanya uzuri na kutengeneza kwa umahiri kila kitu Alichokiumba.

Jina hili tukufu limethibiti katika Sunnah ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):

عَنْ شَدَّادِ بْنِ أَوْسٍ (رضي الله عنه) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((إِنَّ اللَّهَ مُحْسِنٌ يُحِبُّ الإِحْسَانَ، فَإِذَا قَتَلْتُمْ فَأَحْسِنُوا الْقِتْلَةَ، وَإِذَا ذَبَحْتُمْ فَأَحْسِنُوا الذَّبْحَ، وَلْيُحِدَّ أَحَدُكُمْ شَفْرَتَهُ، ثُمَّ لِيُرِحْ ذَبِيحَتَهُ))

Amesimulia Shaddaad bin Aws (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika Allaah Ni Muhsin (Mwenye Kufanya Ihsaan), Anapenda ihsaan. Basi mtakapoua (kwa haki), fanyeni uzuri katika kuua; na mtakapochinja, fanyeni uzuri katika kuchinja; na mmoja wenu anoe kisu chake, kisha amrahisishie (amstareheshe) mnyama wake anayemchinja.” [‘Abdur-Razzaaq (8603), na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh Al-Jaami’ (1824); na asili yake iko katika Swahiyh Muslim (1955)]

Na katika riwaayah ya Muslim:

عَنْ شَدَّادِ بْنِ أَوْسٍ (رضي الله عنه) قَالَ: ثِنْتَانِ حَفِظْتُهُمَا عَنْ رَسُولِ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) قَالَ: ((إِنَّ اللَّهَ كَتَبَ الإِحْسَانَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ، فَإِذَا قَتَلْتُمْ فَأَحْسِنُوا الْقِتْلَةَ، وَإِذَا ذَبَحْتُمْ فَأَحْسِنُوا الذَّبْحَ، وَلْيُحِدَّ أَحَدُكُمْ شَفْرَتَهُ، فَلْيُرِحْ ذَبِيحَتَهُ))

Amesimulia Shaddaad bin Aws (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema (katika mambo mawili aliyoyahifadhi kutoka kwake): “Hakika Allaah Ameandika (Amefaradhisha) ihsaan juu ya kila kitu. Basi mtakapoua, fanyeni uzuri katika kuua; na mtakapochinja, fanyeni uzuri katika kuchinja; na mmoja wenu anoe kisu chake, na amrahisishie mnyama wake anayemchinja.” [Muslim]

Na ‘Ulamaa wamelithibitisha Jina hili miongoni mwa Majina ya Allaah. Amesema Imaam Ibn ‘Uthaymiyn (رحمه الله):

المحسن: أيضاً من أسماء الله تبارك وتعالى

“Al-Muhsin pia ni miongoni mwa Majina ya Allaah (تبارك وتعالى).”1

Na ingawa Jina hili halikutajwa katika Qur-aan kwa tamko lake, Qur-aan imejaa kutaja Ihsaan Yake kwa viumbe Vyake, Uzuri wa Uumbaji Wake na Mapenzi Yake kwa wafanyao ihsaan. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

الَّذِي أَحْسَنَ كُلَّ شَيْءٍ خَلَقَهُ ۖ وَبَدَأَ خَلْقَ الْإِنسَانِ مِن طِينٍ ﴿٧﴾

Ambaye Amefanya uzuri kila kitu Alichokiumba, na Akaanzisha uumbaji wa binaadam kutokana na udongo. [As-Sajdah (32:7)]

Na Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَأَنفِقُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَلَا تُلْقُوا بِأَيْدِيكُمْ إِلَى التَّهْلُكَةِ ۛ وَأَحْسِنُوا ۛ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُحْسِنِينَ ﴿١٩٥﴾

Na toeni katika Njia ya Allaah wala msijitupe katika maangamizi kwa (kuzuia) mikono yenu (isitoe). Na fanyeni ihsaan, hakika Allaah Anapenda wafanyao ihsaan. [Al-Baqarah (2:195)]

Maana Ya Al-Muhsin:

Ihsaan katika lugha ina maana mbili: kumfanyia mwingine wema na neema kwa kiasi kinachozidi uadilifu, na kulifanya jambo kwa uzuri, umahiri na ukamilifu.2

والإحسان يأتي بمعنيين: 1- الإنعامُ على الغيرِ، وهو زائدٌ على العَدْلِ. 2- الإتقانُ والإحكامُ

1-Al-Muhsin Ni Mwenye kuwafanyia viumbe Vyake wema, fadhila, ukarimu na neema; Huwapa zaidi ya wanavyostahiki, na Hawalipi kwa uadilifu peke yake bali kwa Fadhila Yake. Amesema Imaam Al-Qurtubiy (رحمه الله) kuhusu Jina hili:

معناه راجعٌ إلى معنى المُفْضِل وذي الفَضل والمنَّان والوهَّاب

“Maana yake inarejea kwenye maana ya Al-Mufdhwil (Mwenye kufadhilisha), Dhul-Fadhwl (Mwenye Fadhila), Al-Mannaan (Mwenye kuneemesha) na Al-Wahhaab (Mwingi wa Kutunuku).”3 Na Nabiy Yuwsuf (عليه السلام) alikiri Ihsaan ya Rabb wake juu yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَرَفَعَ أَبَوَيْهِ عَلَى الْعَرْشِ وَخَرُّوا لَهُ سُجَّدًا ۖ وَقَالَ يَا أَبَتِ هَـٰذَا تَأْوِيلُ رُؤْيَايَ مِن قَبْلُ قَدْ جَعَلَهَا رَبِّي حَقًّا ۖ وَقَدْ أَحْسَنَ بِي إِذْ أَخْرَجَنِي مِنَ السِّجْنِ وَجَاءَ بِكُم مِّنَ الْبَدْوِ مِن بَعْدِ أَن نَّزَغَ الشَّيْطَانُ بَيْنِي وَبَيْنَ إِخْوَتِي ۚ إِنَّ رَبِّي لَطِيفٌ لِّمَا يَشَاءُ ۚ إِنَّهُ هُوَ الْعَلِيمُ الْحَكِيمُ ﴿١٠٠﴾

Akawapandisha wazazi wake wawili juu ya kiti cha ufalme, wakaporomoka wote kumsujudia. Na akasema: Ee baba yangu kipenzi! Hii ni tafsiri ya njozi yangu hapo kabla, Rabb wangu Ameijaalia kweli. Na hakika Amenifanyia ihsaan Aliponitoa kutoka jela, na Akakuleteni kutoka jangwani baada ya shaytwaan kuchochea baina yangu na baina ya kaka zangu. Hakika Rabb wangu Ni Latifu kwa Atakayo. Hakika Yeye Ndiye Mjuzi wa yote, Mwenye Hikmah wa yote. [Yuwsuf (12:100)]

2-Al-Muhsin Ni Ambaye Amefanya uzuri na kutengeneza kwa umahiri kila kitu Alichokiumba (rejea juu: As-Sajdah (32:7)), Akampa kila kiumbe umbo linalolingana nacho na Akakamilisha uumbaji wake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ بِالْحَقِّ وَصَوَّرَكُمْ فَأَحْسَنَ صُوَرَكُمْ ۖ وَإِلَيْهِ الْمَصِيرُ﴿٣﴾

Ameumba mbingu na ardhi kwa haki, na Akakutengenezeni sura, kisha Akafanya nzuri zaidi sura zenu, na Kwake ndio mahali pa kuishia. [At-Taghaabun (64:3)]

3-Ihsaan Yake ni Sifa Yake ya daima; hakuna kiumbe kinachokosa Ihsaan Yake hata kwa kufumba na kufumbua. Amesema Imaam Al-Munaawiy (رحمه الله) katika kuisherehesha Hadiyth ya Jina hili:

الإحسان له وصفٌ لازمٌ، لا يخلو موجودٌ عن إحسانه طَرْفةَ عين، فلابدَّ لكل مُكوَّن من إحسانه إليه بنعمة الإيجاد ونعمة الإمداد

“Ihsaan ni Sifa Yake ya kudumu; hakuna kilichopo kinachokosa Ihsaan Yake hata kwa kupepesa jicho; basi kila kiumbe ni lazima kiwe kimefanyiwa Ihsaan Yake kwa neema ya kuumbwa na neema ya kuruzukiwa na kudumishwa.”4 Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَمَا بِكُم مِّن نِّعْمَةٍ فَمِنَ اللَّـهِ ۖ ثُمَّ إِذَا مَسَّكُمُ الضُّرُّ فَإِلَيْهِ تَجْأَرُونَ﴿٥٣﴾

Na Neema yoyote mliyo nayo, basi ni kutoka kwa Allaah. Kisha inapokuguseni dhara, mnamlilia Yeye tu kuomba msaada. [An-Nahl (16:53)]

4-Al-Muhsin Anapenda ihsaan, na Anawapenda wafanyao ihsaan, na Ameandika ihsaan juu ya kila kitu (rejea Hadiyth ya Muslim juu). Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

الَّذِينَ يُنفِقُونَ فِي السَّرَّاءِ وَالضَّرَّاءِ وَالْكَاظِمِينَ الْغَيْظَ وَالْعَافِينَ عَنِ النَّاسِ ۗ وَاللَّـهُ يُحِبُّ الْمُحْسِنِينَ ﴿١٣٤﴾

Ambao wanatoa (kwa ajili ya Allaah) katika hali ya wasaa na katika hali ya shida, na wanazuia ghadhabu, na wenye kusamehe watu. Na Allaah Anapenda wafanyao ihsaan. [Aal-‘Imraan (3:134)]

5-Al-Muhsin Huwalipa wafanyao ihsaan kwa ihsaan iliyo bora zaidi, na Huwazidishia; na jazaa nzuri kabisa ni Jannah, na ziada ni kumuona Allaah (سبحانه وتعالى). Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

لِّلَّذِينَ أَحْسَنُوا الْحُسْنَىٰ وَزِيَادَةٌ ۖ وَلَا يَرْهَقُ وُجُوهَهُمْ قَتَرٌ وَلَا ذِلَّةٌ ۚ أُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ الْجَنَّةِ ۖ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ﴿٢٦﴾

Kwa wale waliofanya ihsaan watapata (huko Jannah) jazaa nzuri kabisa na ziada (kumuona Allaah). Na vumbi halitowafunika nyuso zao wala madhila. Hao ni watu wa Jannah, humo wao watadumu. [Yuwnus (10:26)]

Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Muhsin:

1-Tambua Kwamba Kila Neema Uliyonayo Ni Ihsaan Ya Al-Muhsin:

Tambua kwamba Al-Muhsin Ndiye Aliyekuumba, Akakuruzuku, Akakuongoza na Akakuhifadhi; na kila neema uliyonayo, ndogo au kubwa, ni Ihsaan Yake juu yako (rejea juu: An-Nahl (16:53)). Basi usiinasibishe neema kwa nafsi yako wala kwa mwingine, na tambua kwamba Neema Zake haziwezi kuhesabika. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَآتَاكُم مِّن كُلِّ مَا سَأَلْتُمُوهُ ۚ وَإِن تَعُدُّوا نِعْمَتَ اللَّـهِ لَا تُحْصُوهَا ۗ إِنَّ الْإِنسَانَ لَظَلُومٌ كَفَّارٌ ﴿٣٤﴾

Na Akakupeni kila mlichomuomba. Na mkihesabu Neema za Allaah hamtoweza kuziorodhesha hesabuni. Hakika binaadam ni mwingi wa dhulma, mwingi wa kukufuru. [Ibraahiym (14:34)]

2-Mpwekeshe Al-Muhsin Katika ‘Ibaadah Yako:

Kumbuka, ee Mja wa Al-Muhsin, kwamba Yeye Peke Yake Ndiye Aliyekufanyia ihsaan ya kuumbwa, kutiwa sura nzuri na kuruzukiwa vizuri; basi Yeye Peke Yake Ndiye Anayestahiki kuabudiwa, bila kumshirikisha na chochote. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

اللَّـهُ الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ الْأَرْضَ قَرَارًا وَالسَّمَاءَ بِنَاءً وَصَوَّرَكُمْ فَأَحْسَنَ صُوَرَكُمْ وَرَزَقَكُم مِّنَ الطَّيِّبَاتِ ۚ ذَٰلِكُمُ اللَّـهُ رَبُّكُمْ ۖ فَتَبَارَكَ اللَّـهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ﴿٦٤﴾

Allaah Ambaye Amekufanyieni ardhi kuwa mahali pa makazi, na mbingu kama ni paa, na Akakutieni sura Akazifanya nzuri zaidi sura zenu, na Akakuruzukuni katika vizuri. Huyo Ndiye Allaah Rabb wenu. Basi Tabaaraka-Allaah! (Amebarikika Allaah) Rabb wa walimwengu. [Ghaafir (40:64)]

3-Tafakari Ihsaan Ya Al-Muhsin Katika Kuumbwa Kwako:

Tafakari, ee Mja wa Al-Muhsin, jinsi Alivyokuumba katika umbile bora kabisa, Akakupa akili, kusikia na kuona; na tafakari umahiri wa Uumbaji Wake katika kila kitu (rejea juu: At-Taghaabun (64:3)). Tafakari hiyo ikuzidishie mapenzi Kwake na kumshukuru. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

لَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ فِي أَحْسَنِ تَقْوِيمٍ ﴿٤﴾

Kwa yakini Tumemuumba binaadam katika umbile bora kabisa. [At-Tiyn (95:4)]

4-Tambua Kwamba Al-Muhsin Huzidisha Malipo Ya Wema Na Hapunguzi:

Tambua kwamba katika Ihsaan ya Al-Muhsin ni kwamba Anakuandikia wema hata kwa kuukusudia tu, na Anauzidisha mara kumi hadi mara mia saba na zaidi; na ovu Halikuandikii ila mfano wake tu. Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema katika Hadiyth Al-Qudsiy:

عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ (رضي الله عنهما) عَنِ النَّبِيِّ (صلى الله عليه وسلم) فِيمَا يَرْوِي عَنْ رَبِّهِ عَزَّ وَجَلَّ قَالَ: ((إِنَّ اللَّهَ كَتَبَ الْحَسَنَاتِ وَالسَّيِّئَاتِ ثُمَّ بَيَّنَ ذَلِكَ، فَمَنْ هَمَّ بِحَسَنَةٍ فَلَمْ يَعْمَلْهَا كَتَبَهَا اللَّهُ لَهُ عِنْدَهُ حَسَنَةً كَامِلَةً، فَإِنْ هُوَ هَمَّ بِهَا فَعَمِلَهَا كَتَبَهَا اللَّهُ لَهُ عِنْدَهُ عَشْرَ حَسَنَاتٍ إِلَى سَبْعِمِائَةِ ضِعْفٍ إِلَى أَضْعَافٍ كَثِيرَةٍ، وَمَنْ هَمَّ بِسَيِّئَةٍ فَلَمْ يَعْمَلْهَا كَتَبَهَا اللَّهُ لَهُ عِنْدَهُ حَسَنَةً كَامِلَةً، فَإِنْ هُوَ هَمَّ بِهَا فَعَمِلَهَا كَتَبَهَا اللَّهُ لَهُ سَيِّئَةً وَاحِدَةً))

Amesimulia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema katika aliyoyapokea kutoka kwa Rabb wake (عزّ وجلّ): “Hakika Allaah Ameandika mema na maovu, kisha Akabainisha hilo. Basi atakayekusudia jambo jema asilitende, Allaah Humwandikia Kwake jema moja kamili; na akilikusudia akalitenda, Allaah Humwandikia Kwake mema kumi hadi mara mia saba hadi mara nyingi zaidi. Na atakayekusudia ovu asilitende, Allaah Humwandikia Kwake jema moja kamili; na akilikusudia akalitenda, Allaah Humwandikia ovu moja tu.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

5-Mwabudu Al-Muhsin Kama Kwamba Unamuona:

Kumbuka, ee Mja wa Al-Muhsin, kwamba daraja ya juu kabisa ya Dini ni ihsaan, nayo ni kumwabudu Allaah kwa hali ya kumuona au kuyakinisha kwamba Yeye Anakuona; hali hii ikuzidishie khushuu’ katika Swalaah yako na ikuzuilie maasi. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alipoulizwa na Jibriyl (عليه السلام) kuhusu ihsaan alisema:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) فِي حَدِيثِ جِبْرِيلَ قَالَ: مَا الإِحْسَانُ؟ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((أَنْ تَعْبُدَ اللَّهَ كَأَنَّكَ تَرَاهُ، فَإِنْ لَمْ تَكُنْ تَرَاهُ فَإِنَّهُ يَرَاكَ))

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) katika Hadiyth ya Jibriyl kwamba aliuliza: Ihsaan ni nini? Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Ni kumwabudu Allaah kama kwamba unamuona; na ikiwa wewe humuoni, basi hakika Yeye Anakuona.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

6-Boresha Uislamu Wako Ili Al-Muhsin Akuzidishie Malipo:

Tambua, ee Mja wa Al-Muhsin, kwamba unapoufanya Uislamu wako kuwa mzuri kwa kutekeleza Amri Zake kwa ikhlaasw na kufuata Sunnah, na kujiepusha na Makatazo Yake, Al-Muhsin Anakuzidishia malipo ya kila jema unalolitenda. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((إِذَا أَحْسَنَ أَحَدُكُمْ إِسْلاَمَهُ فَكُلُّ حَسَنَةٍ يَعْمَلُهَا تُكْتَبُ لَهُ بِعَشْرِ أَمْثَالِهَا إِلَى سَبْعِمِائَةِ ضِعْفٍ، وَكُلُّ سَيِّئَةٍ يَعْمَلُهَا تُكْتَبُ لَهُ بِمِثْلِهَا))

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Mmoja wenu anapoufanya Uislamu wake kuwa mzuri, basi kila jema analolitenda huandikiwa mfano wake mara kumi hadi mara mia saba; na kila ovu analolitenda huandikiwa mfano wake (mmoja tu).” [Al-Bukhaariy]

7-Fanya Ihsaan Kama Al-Muhsin Alivyokufanyia Ihsaan:

Kumbuka kwamba Al-Muhsin Amekuamrisha uwafanyie wengine ihsaan kama Alivyokufanyia ihsaan; basi tumia mali, ilimu, cheo na nguvu Alizokupa katika kuwanufaisha Waja Wake, bila kuwasimbulia wala kutaka malipo kutoka kwao. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَابْتَغِ فِيمَا آتَاكَ اللَّـهُ الدَّارَ الْآخِرَةَ ۖ وَلَا تَنسَ نَصِيبَكَ مِنَ الدُّنْيَا ۖ وَأَحْسِن كَمَا أَحْسَنَ اللَّـهُ إِلَيْكَ ۖ وَلَا تَبْغِ الْفَسَادَ فِي الْأَرْضِ ۖ إِنَّ اللَّـهَ لَا يُحِبُّ الْمُفْسِدِينَ ﴿٧٧﴾

Na tafuta katika yale Aliyokupa Allaah makazi ya Aakhirah. Na wala usisahau fungu lako katika dunia. Na fanya ihsaan kama Alivyokufanyia Allaah ihsaan, na wala usitake ufisadi ardhini. Hakika Allaah Hapendi mafisadi. [Al-Qaswasw (28:77)]

8-Wafanyie Ihsaan Wazazi Wako, Jamaa Na Wanaohitaji:

Tambua kwamba Al-Muhsin Ameunganisha haki ya kumwabudu Yeye Peke Yake pamoja na kuwafanyia ihsaan wazazi wawili, jamaa wa karibu, mayatima na masikini, na kuzungumza na watu kwa uzuri; basi wape haki zao kwa wema na upole. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَإِذْ أَخَذْنَا مِيثَاقَ بَنِي إِسْرَائِيلَ لَا تَعْبُدُونَ إِلَّا اللَّـهَ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا وَذِي الْقُرْبَىٰ وَالْيَتَامَىٰ وَالْمَسَاكِينِ وَقُولُوا لِلنَّاسِ حُسْنًا وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَآتُوا الزَّكَاةَ ثُمَّ تَوَلَّيْتُمْ إِلَّا قَلِيلًا مِّنكُمْ وَأَنتُم مُّعْرِضُونَ ﴿٨٣﴾

Na pindi Tulipochukua ahadi ya nguvu ya wana wa Israaiyl (Tukawaambia): Msiabudu isipokuwa Allaah, na muwafanyie ihsaan wazazi wawili, na jamaa wa karibu, na mayatima, na masikini, na semeni na watu kwa uzuri na simamisheni Swalaah, na toeni Zakaah, kisha mkakengeuka ila wachache miongoni mwenu na huku nyinyi mnapuuza. [Al-Baqarah (2:83)]

9-Fanya Ihsaan Katika Kila Jambo Hata Kwa Wanyama:

Kumbuka, ee Mja wa Al-Muhsin, kwamba Al-Muhsin Ameandika ihsaan juu ya kila kitu, hata katika kuchinja mnyama: kunoa kisu na kumrahisishia mnyama (rejea juu: Hadiyth ya Shaddaad bin Aws (رضي الله عنه) [Muslim]). Basi fanya ihsaan katika ‘ibaadah yako, kazi yako, maneno yako na muamala wako na watu na viumbe vyote; na fanya kila kazi kwa umahiri na ukamilifu.

10-Lipa Uovu Kwa Wema Uwe Miongoni Mwa Wafanyao Ihsaan:

Tambua kwamba Al-Muhsin Anawafanyia Waja Wake ihsaan pamoja na kwamba wanamuasi; basi nawe usimlipe aliyekukosea kwa uovu, bali zuia uovu wake kwa wema, kwani wema huondosha uadui na hugeuza adui kuwa rafiki. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَلَا تَسْتَوِي الْحَسَنَةُ وَلَا السَّيِّئَةُ ۚ ادْفَعْ بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ فَإِذَا الَّذِي بَيْنَكَ وَبَيْنَهُ عَدَاوَةٌ كَأَنَّهُ وَلِيٌّ حَمِيمٌ﴿٣٤﴾

Na wala haulingani sawa wema na uovu. Zuia (uovu) kwa ambalo ni zuri zaidi. Hapo utamkuta yule ambaye baina yako na baina yake kuna uadui, kama ni rafiki mwandani. [Fusw-Swilat (41:34)]

11-Tambua Kwamba Al-Muhsin Yu Pamoja Na Wafanyao Ihsaan:

Tambua kwamba Al-Muhsin Yu Pamoja na wafanyao ihsaan kwa Ujuzi Wake, Nusra Yake, Hifadhi Yake na Taufiyq Yake, si kwa Dhati Yake; kwani Dhati Yake Iko juu ya ‘Arsh, na Ujuzi Wake Umeenea kila mahali na kila kitu. Basi kuwa miongoni mwa wafanyao ihsaan upate Ma’iyyah hii maalumu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

إِنَّ اللَّـهَ مَعَ الَّذِينَ اتَّقَوا وَّالَّذِينَ هُم مُّحْسِنُونَ﴿١٢٨﴾

Hakika Allaah Yu Pamoja na wenye taqwa, na wale ambao wao ni wenye kufanya ihsaan. [An-Nahl (16:128)]

12-Subiri Kwani Al-Muhsin Hapotezi Ujira Wa Wafanyao Ihsaan:

Kumbuka, ee Mja wa Al-Muhsin, kwamba hakuna wema unaoutenda, ukiwa mdogo au mkubwa, unaopotea Kwake; basi subiri juu ya kumtii Allaah na juu ya Qadar Yake, na usikate tamaa ukiona watu hawaithamini ihsaan yako, kwani malipo yako yapo kwa Al-Muhsin. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَاصْبِرْ فَإِنَّ اللَّـهَ لَا يُضِيعُ أَجْرَ الْمُحْسِنِينَ﴿١١٥﴾

Na vuta subira kwani hakika Allaah Hapotezi ujira wa wafanyao ihsaan. [Huwd (11:115)]

13-Mwombe Al-Muhsin Kwa Khofu Na Matumaini Ili Rehma Yake Ikukaribie:

Omba du’aa kwa Al-Muhsin kwa khofu na matumaini, na tambua kwamba Rehma Yake iko karibu na wafanyao ihsaan; basi kadiri unavyozidisha ihsaan katika ‘ibaadah na muamala wako, ndivyo unavyozidi kukaribia Rehma Yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَلَا تُفْسِدُوا فِي الْأَرْضِ بَعْدَ إِصْلَاحِهَا وَادْعُوهُ خَوْفًا وَطَمَعًا ۚ إِنَّ رَحْمَتَ اللَّـهِ قَرِيبٌ مِّنَ الْمُحْسِنِينَ ﴿٥٦﴾

Na wala msifanye ufisadi katika ardhi baada ya (Allaah) kuitengeneza sawa, na muombeni kwa khofu na matumaini. Hakika Rehma ya Allaah iko karibu na wafanyao ihsaan. [Al-A’raaf (7:56)]

14-Mwombe Al-Muhsin Akusaidie Kumdhukuru, Kumshukuru Na Kumwabudu Kwa Uzuri:

Omba du’aa, ee Mja wa Al-Muhsin, kwa du’aa aliyomuusia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Mu’aadh bin Jabal (رضي الله عنه) aiseme baada ya kila Swalaah, kwani huwezi kufikia ihsaan katika ‘ibaadah isipokuwa kwa Msaada wa Al-Muhsin:

عَنْ مُعَاذِ بْنِ جَبَلٍ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) أَخَذَ بِيَدِهِ وَقَالَ: ((يَا مُعَاذُ، وَاللَّهِ إِنِّي لأُحِبُّكَ ... أُوصِيكَ يَا مُعَاذُ لاَ تَدَعَنَّ فِي دُبُرِ كُلِّ صَلاَةٍ تَقُولُ: اللَّهُمَّ أَعِنِّي عَلَى ذِكْرِكَ وَشُكْرِكَ وَحُسْنِ عِبَادَتِكَ))

Amesimulia Mu’aadh bin Jabal (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) aliushika mkono wake akasema: “Ee Mu’aadh! Wa-Allaahi mimi nakupenda … Nakuusia ee Mu’aadh, usiache kusema mwishoni mwa kila Swalaah:

اللَّهُمَّ أَعِنِّي عَلَى ذِكْرِكَ وَشُكْرِكَ وَحُسْنِ عِبَادَتِكَ

Yaa Allaah! Nisaidie kukudhukuru, kukushukuru na kukuabudu kwa uzuri.” [Abuu Daawuwd (1522), na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh Abiy Daawuwd (1522)]

15-Mwombe Al-Muhsin Akufanyie Uzuri Tabia Yako Kama Alivyokufanyia Uzuri Umbo Lako:

Omba du’aa kwa Al-Muhsin Aliyekuumba kwa umbo zuri, Akufanyie pia tabia yako kuwa nzuri, kama alivyokuwa akiomba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):

عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ مَسْعُودٍ (رضي الله عنه) قَالَ: كَانَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) يَقُولُ: ((اللَّهُمَّ أَحْسَنْتَ خَلْقِي فَأَحْسِنْ خُلُقِي))

Amesimulia ‘Abdullaah bin Mas’uwd (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akisema:

اللَّهُمَّ أَحْسَنْتَ خَلْقِي فَأَحْسِنْ خُلُقِي

“Yaa Allaah! Umeufanya uzuri umbo langu, basi ifanye nzuri tabia yangu.” [Ahmad, na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Irwaa Al-Ghaliyl (1/115)]

16-Mwombe Al-Muhsin Mazuri Ya Dunia Na Aakhirah:

Omba du’aa kwa Al-Muhsin Akupe mazuri ya dunia na mazuri ya Aakhirah na Akukinge na adhabu ya Moto, kwani kheri zote ziko Mikononi Mwake, na Yeye Ndiye Mwenye kuwafanyia Waja Wake ihsaan juu ya ihsaan. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَمِنْهُم مَّن يَقُولُ رَبَّنَا آتِنَا فِي الدُّنْيَا حَسَنَةً وَفِي الْآخِرَةِ حَسَنَةً وَقِنَا عَذَابَ النَّارِ ﴿٢٠١﴾

Na miongoni mwao kuna wasemao: Rabb wetu Tupe katika dunia mazuri na katika Aakhirah mazuri na Tukinge na adhabu ya moto. [Al-Baqarah (2:201)]

Na Allaah Mjuzi zaidi

  • 1Imaam Ibn ‘Uthaymiyn, Fataawaa Nuwr ‘Alaa Ad-Darb (kanda 325), kama ilivyonukuliwa na islamqa.info (swali 155382). Na Imaam Ibn Baaz pia amesema: “عبد المحسن: فلا بأس به؛ لأن المحسن من أسماء الله” [Majmuw’ Fataawaa Ibn Baaz (5/358-359)].
  • 2Ad-Durar As-Saniyyah, Al-Mawsuw’ah Al-‘Aqadiyyah, mlango wa Sifa ya Al-Ihsaan (dorar.net/aqeeda/523).
  • 3Al-Qurtubiy, Al-Asnaa Fiy Sharh Asmaa-illaah Al-Husnaa, kama ilivyonukuliwa na kalemtayeb.com.
  • 4Al-Munaawiy, Faydhw Al-Qadiyr Sharh Al-Jaami’ Asw-Swaghiyr, katika kuisherehesha Hadiyth: «إن الله محسن يحب الإحسان», kama ilivyonukuliwa na kalemtayeb.com.