Skip to main content
Majina Mazuri Ya Allaah Jina 101 kati ya 103
At-Twayyib — Majina Mazuri ya Allaah

At-Twayyib: Mzuri, Msafi, Aliyetakasika na kila upungufu na aibu; Mzuri katika Dhati Yake, Majina Yake, Sifa Zake, Matendo Yake na Hukumu Zake, Asiyekubali isipokuwa kilicho kizuri.

Jina hili tukufu limethibiti katika Sunnah ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((أَيُّهَا النَّاسُ، إِنَّ اللَّهَ طَيِّبٌ لاَ يَقْبَلُ إِلاَّ طَيِّبًا، وَإِنَّ اللَّهَ أَمَرَ الْمُؤْمِنِينَ بِمَا أَمَرَ بِهِ الْمُرْسَلِينَ، فَقَالَ: ﴿يَا أَيُّهَا الرُّسُلُ كُلُوا مِنَ الطَّيِّبَاتِ وَاعْمَلُوا صَالِحًا إِنِّي بِمَا تَعْمَلُونَ عَلِيمٌ﴾، وَقَالَ: ﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُلُوا مِنْ طَيِّبَاتِ مَا رَزَقْنَاكُمْ﴾))، ثُمَّ ذَكَرَ الرَّجُلَ يُطِيلُ السَّفَرَ، أَشْعَثَ أَغْبَرَ، يَمُدُّ يَدَيْهِ إِلَى السَّمَاءِ: يَا رَبِّ، يَا رَبِّ، وَمَطْعَمُهُ حَرَامٌ، وَمَشْرَبُهُ حَرَامٌ، وَمَلْبَسُهُ حَرَامٌ، وَغُذِيَ بِالْحَرَامِ، فَأَنَّى يُسْتَجَابُ لِذَلِكَ؟

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Enyi watu! Hakika Allaah Ni Twayyib (Mzuri, Msafi), Hakubali isipokuwa kilicho kizuri. Na hakika Allaah Amewaamrisha Waumini yale Aliyowaamrisha Rusuli; Amesema: {Enyi Rusuli! Kuleni katika vizuri na tendeni mema, hakika Mimi kwa yale myatendayo Ni Mjuzi} [Al-Muuminuwn (23:51)]. Na Amesema: {Enyi walioamini! Kuleni vizuri Tulivyokuruzukuni} [Al-Baqarah (2:172)].” Kisha akamtaja mtu anayesafiri safari ndefu, nywele zake timtimu, amejaa vumbi, ananyoosha mikono yake mbinguni (akiomba): Yaa Rabb! Yaa Rabb! Ilhali chakula chake ni haraam, kinywaji chake ni haraam, mavazi yake ni haraam, na amelishwa kwa haraam; basi vipi ataitikiwa du’aa yake? [Muslim]

Na Jina hili halikutajwa katika Qur-aan kama Jina, bali limethibiti katika Sunnah; na miongoni mwa ‘Ulamaa waliolihesabu katika Majina ya Allaah ni Ibn Mandah, Ibn Al-‘Arabiy, Al-Haytamiy na Ibn ‘Uthaymiyn.1 Na ‘Ulamaa wametofautiana katika kulihesabu; wengi wao hawakulihesabu katika Majina ya Allaah, bali wameliona kuwa ni Sifa Yake (سبحانه وتعالى). Ama katika Qur-aan, Allaah (سبحانه وتعالى) Ametaja mara nyingi kwamba Anapenda kilicho kizuri (twayyib), Anaamrisha kula vizuri, kutoa vizuri na kusema neno zuri, na kwamba Kwake linapanda neno zuri.

Maana Ya At-Twayyib:

Asili ya neno twiyb katika lugha ni utakaso, usafi na kusalimika na ubaya (khubth). Na At-Twayyib katika Haki ya Allaah (سبحانه وتعالى) Ana maana zifuatazo:

1-Allaah (سبحانه وتعالى) Ni Msafi, Ametakasika na kila upungufu, kila aibu na kila kibaya; kwa maana hii Ni sawa na Al-Qudduws. Amesema Al-Qaadhwiy ‘Iyaadhw:

مَعنى تَسميةِ اللهِ بالطَّيِّبِ هنا -ولم يأتِ في حديثِ الأسماءِ- أي: المنَزَّهُ عن النَّقائصِ، بمعنى: القُدُّوسِ. وأصلُ الطيبِ: الزَّكاءُ والطَّهارةُ، والسَّلامةُ مِنَ الخُبثِ

“Maana ya kumwita Allaah kwa Jina la At-Twayyib hapa, na halikuja katika Hadiyth ya Majina, ni: Aliyetakasika na mapungufu, kwa maana ya Al-Qudduws. Na asili ya twiyb ni utakaso, usafi na kusalimika na ubaya.”2

Na Amesema Al-Qurtwubiy:

أي: مُنَزَّهٌ عن النَّقائِصِ والخبائِثِ، فيكونُ بمعنى: القُدُّوسِ

“Yaani: Ametakasika na mapungufu na mambo maovu; kwa hiyo linakuwa kwa maana ya Al-Qudduws.”3 Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

هُوَ اللَّـهُ الَّذِي لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْمَلِكُ الْقُدُّوسُ السَّلَامُ الْمُؤْمِنُ الْمُهَيْمِنُ الْعَزِيزُ الْجَبَّارُ الْمُتَكَبِّرُ ۚ سُبْحَانَ اللَّـهِ عَمَّا يُشْرِكُونَ﴿٢٣﴾

Yeye Ndiye Allaah Ambaye hakuna muabudiwa wa haki ila Yeye, Mfalme, Mtakatifu Ametakasika na sifa zote hasi, Mwenye Kusalimisha na Amesalimika na kasoro zote, Mwenye Kusadikisha ahadi na Kuaminisha, Mwenye Kudhibiti Kushuhudia Kuchunga na Kuhifadhi, Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Jabari Asiyeshindwa kufanya Atakalo, Mwenye Ukubwa na Uadhama, Utakasifu ni wa Allaah kutokana na ambayo wanamshirikisha. [Al-Hashr (59:23)]

2-Yeye Ni Mzuri katika Dhati Yake, Majina Yake, Sifa Zake, Matendo Yake na Hukumu Zake. Amesema Imaam Ibn ‘Uthaymiyn:

مِن أسماءِ اللهِ تعالى الطَّيِّبُ؛ لقَولِه: ((إنَّ اللهَ طَيِّبٌ))، وهذا يَشمَلُ طِيبَ ذاتِه، وأسمائِه، وصِفاتِه، وأفعالِه، وأحكامِه

“Miongoni mwa Majina ya Allaah (تعالى) ni At-Twayyib, kwa kauli yake (Nabiy): ((Hakika Allaah Ni Twayyib)); na hili linakusanya uzuri wa Dhati Yake, Majina Yake, Sifa Zake, Matendo Yake na Hukumu Zake.”4 Na Majina Yake yote ni mazuri kabisa. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

اللَّـهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۖ لَهُ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ ﴿٨﴾

Allaah, hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye. Anayo Majina Mazuri kabisa. [Twaahaa (20:8)]

3-Hakitoki Kwake isipokuwa kizuri, wala hakipandi Kwake isipokuwa kizuri, wala hakimkaribii isipokuwa kizuri. Amesema Imaam Ibn Al-Qayyim:

فهو طيِّبٌ، وأفعالُه طيِّبةٌ، وصِفاتُه أطيبُ شيءٍ، وأسماؤه أطيبُ الأسماءِ، واسمُه الطَّيِّبُ، لا يَصدُرُ عنه إِلَّا طيِّبٌ، ولا يَصْعَدُ إليه إلَّا طَيِّبٌ، ولا يَقرَبُ منه إِلَّا طيِّبٌ؛ فكلُّه طيِّبٌ، وإليه يَصعَدُ الكَلِمُ الطَّيِّبُ

“Basi Yeye Ni Mzuri, na Matendo Yake ni mazuri, na Sifa Zake ni kitu kizuri kuliko vyote, na Majina Yake ni mazuri kuliko majina yote, na Jina Lake Ni At-Twayyib; hakitoki Kwake isipokuwa kizuri, wala hakipandi Kwake isipokuwa kizuri, wala hakimkaribii isipokuwa kizuri; basi Yeye Ni Mzuri kwa ukamilifu, na Kwake linapanda neno zuri.”5 Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

مَن كَانَ يُرِيدُ الْعِزَّةَ فَلِلَّـهِ الْعِزَّةُ جَمِيعًا ۚ إِلَيْهِ يَصْعَدُ الْكَلِمُ الطَّيِّبُ وَالْعَمَلُ الصَّالِحُ يَرْفَعُهُ ۚ وَالَّذِينَ يَمْكُرُونَ السَّيِّئَاتِ لَهُمْ عَذَابٌ شَدِيدٌ ۖ وَمَكْرُ أُولَـٰئِكَ هُوَ يَبُورُ ﴿١٠﴾

Yeyote Anayetaka utukufu, basi utukufu wote uko kwa Allaah. Kwake Pekee linapanda Neno zuri na amali njema Huitukuza. Na wale wanaopanga njama za maovu watapata adhabu shadidi. Na njama za hao ni zenye kuangamia. [Faatwir (35:10)]

4-Hakubali isipokuwa kilicho kizuri: katika amali, mali, maneno na itikadi; kama ilivyo katika Hadiyth ya Jina hili (rejea juu). Na kizuri na kiovu haviwi sawa mbele Yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

قُل لَّا يَسْتَوِي الْخَبِيثُ وَالطَّيِّبُ وَلَوْ أَعْجَبَكَ كَثْرَةُ الْخَبِيثِ ۚ فَاتَّقُوا اللَّـهَ يَا أُولِي الْأَلْبَابِ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ﴿١٠٠﴾

Sema: Haviwi sawasawa viovu na vizuri japokuwa utakupendezea wingi wa viovu. Basi mcheni Allaah, enyi wenye akili ili mpate kufaulu. [Al-Maaidah (5:100)]

Taathira Ya Imaan, Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, At-Twayyib:

1-Mtakase At-Twayyib Na Kila Sifa Isiyolingana Naye:

Tambua kwamba At-Twayyib Ametakasika na kila upungufu na kila aibu; basi usimsifu isipokuwa kwa Sifa Alizojisifu Nazo Mwenyewe au Alizomsifu nazo Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم), na mtakase na kila wanalomvumishia wasiomjua. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

سُبْحَانَ رَبِّكَ رَبِّ الْعِزَّةِ عَمَّا يَصِفُونَ ﴿١٨٠﴾

Utakasifu ni wa Rabb wako; Rabb wa Enzi ya Nguvu Asiyeshindika kutokana na yale wanayoyavumisha. [Asw-Swaaffaat (37:180)]

2-Tambua Kwamba At-Twayyib Atapambanua Mbaya Na Mwema:

Kumbuka, ee Mja wa At-Twayyib, kwamba Allaah Huwapitisha Waja Wake katika mitihani ili Apambanue mbaya na mwema; basi jitahidi uwe miongoni mwa wema wanaotakasika katika mitihani hiyo. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

مَّا كَانَ اللَّـهُ لِيَذَرَ الْمُؤْمِنِينَ عَلَىٰ مَا أَنتُمْ عَلَيْهِ حَتَّىٰ يَمِيزَ الْخَبِيثَ مِنَ الطَّيِّبِ ۗ وَمَا كَانَ اللَّـهُ لِيُطْلِعَكُمْ عَلَى الْغَيْبِ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ يَجْتَبِي مِن رُّسُلِهِ مَن يَشَاءُ ۖ فَآمِنُوا بِاللَّـهِ وَرُسُلِهِ ۚ وَإِن تُؤْمِنُوا وَتَتَّقُوا فَلَكُمْ أَجْرٌ عَظِيمٌ ﴿١٧٩﴾

Haiwi kwa Allaah kuwaacha Waumini katika hali mliyo nayo mpaka Apambanue mbaya na mwema. Na haiwi kwa Allaah Akujulisheni ya ghaibu, lakini Allaah Humteua katika Rusuli Wake Amtakaye. Basi mwaminini Allaah na Rusuli Wake. Na mkiamini (imaan ya kweli) na mkawa na taqwa basi mtapata ujira mkuu kabisa. [Aal-‘Imraan (3:179)]

3-Twaharisha Moyo Wako Kwa Neno Zuri La Tawhiyd:

Tambua kwamba At-Twayyib Amepiga mfano wa neno zuri kwa mti mzuri wenye mizizi imara na matawi yanayofika mbinguni; na neno zuri lililo kuu kabisa ni neno la Tawhiyd. Basi lithibitishe moyoni mwako, kwani moyo mzuri ndio unaostahiki kumkaribia At-Twayyib. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

أَلَمْ تَرَ كَيْفَ ضَرَبَ اللَّـهُ مَثَلًا كَلِمَةً طَيِّبَةً كَشَجَرَةٍ طَيِّبَةٍ أَصْلُهَا ثَابِتٌ وَفَرْعُهَا فِي السَّمَاءِ ﴿٢٤﴾ تُؤْتِي أُكُلَهَا كُلَّ حِينٍ بِإِذْنِ رَبِّهَا ۗ وَيَضْرِبُ اللَّـهُ الْأَمْثَالَ لِلنَّاسِ لَعَلَّهُمْ يَتَذَكَّرُونَ ﴿٢٥﴾

Je, huoni vipi Allaah Amepiga mfano wa neno zuri? Ni kama mti mzuri, mizizi yake imethibitika imara na matawi yake yanafika mbinguni. Unatoa mazao yake kila wakati kwa Idhini ya Rabb wake. Na Allaah Anapiga mifano kwa watu ili wapate kukumbuka. [Ibraahiym (14:24-25)]

4-Kumbuka Kwamba Jannah Ni Nyumba Ya Waliotakasika:

Kumbuka kwamba At-Twayyib Hakubali katika Nyumba Yake ya Jannah isipokuwa waliotakasika; na walinzi wake watawaambia wanaoingia humo: “Mmekuwa wema (twibtum)”. Basi jitakase na madhambi kwa tawbah kabla ya kukutana Naye. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَسِيقَ الَّذِينَ اتَّقَوْا رَبَّهُمْ إِلَى الْجَنَّةِ زُمَرًا ۖ حَتَّىٰ إِذَا جَاءُوهَا وَفُتِحَتْ أَبْوَابُهَا وَقَالَ لَهُمْ خَزَنَتُهَا سَلَامٌ عَلَيْكُمْ طِبْتُمْ فَادْخُلُوهَا خَالِدِينَ﴿٧٣﴾

Na wataongozwa wale waliomcha Rabb wao kuelekea Jannah vikundi-vikundi, mpaka watakapoifikia na milango yake ishafunguliwa, na walinzi wake watawaambia: Salaamun ‘Alaykum! (Amani iwe juu yenu), furahini na iingieni, mdumu milele. [Az-Zumar (39:73)]

5-Ishi Ukiwa Mwema Ili Malaika Wakufishe Katika Hali Njema:

Tafakari, ee Mja wa At-Twayyib, jinsi Malaika wanavyowafisha watu wema katika hali njema na kuwapa bishara ya Jannah; basi ishi maisha yako katika utiifu wa At-Twayyib ili mwisho wako uwe mwema. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

الَّذِينَ تَتَوَفَّاهُمُ الْمَلَائِكَةُ طَيِّبِينَ ۙ يَقُولُونَ سَلَامٌ عَلَيْكُمُ ادْخُلُوا الْجَنَّةَ بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ﴿٣٢﴾

Wale ambao Malaika wanawafisha katika hali njema watawaambia: Salaamun ‘Alaykum (amani iwe juu yenu), ingieni Jannah kwa sababu ya yale mliyokuwa mkitenda. [An-Nahl (16:32)]

6-Tenda Mema Upate Uhai Mzuri Duniani:

Tambua kwamba At-Twayyib Amemuahidi kila Muumin anayetenda mema, mwanamume au mwanamke, uhai mzuri hapa duniani pamoja na ujira mzuri kabisa Aakhirah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

مَنْ عَمِلَ صَالِحًا مِّن ذَكَرٍ أَوْ أُنثَىٰ وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَلَنُحْيِيَنَّهُ حَيَاةً طَيِّبَةً ۖ وَلَنَجْزِيَنَّهُمْ أَجْرَهُم بِأَحْسَنِ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ﴿٩٧﴾

Mwenye kutenda mema miongoni mwa wanamume au wanawake naye ni Muumin, hakika Tutamhuisha uhai mzuri, na bila shaka Tutawalipa ujira wao kwa mazuri zaidi ya yale waliyokuwa wakitenda. [An-Nahl (16:97)]

7-Kula Cha Halali Kizuri, Kwani Haraam Huzuia Kuitikiwa Du’aa:

Kumbuka, ee Mja wa At-Twayyib, kwamba katika Hadiyth ya Jina hili Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amemtaja mtu anayeomba du’aa kwa unyenyekevu lakini haitikiwi kwa sababu chakula chake, kinywaji chake na mavazi yake ni vya haraam (rejea juu). Basi tafuta rizqi ya halali, na usile isipokuwa kizuri. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

يَا أَيُّهَا النَّاسُ كُلُوا مِمَّا فِي الْأَرْضِ حَلَالًا طَيِّبًا وَلَا تَتَّبِعُوا خُطُوَاتِ الشَّيْطَانِ ۚ إِنَّهُ لَكُمْ عَدُوٌّ مُّبِينٌ ﴿١٦٨﴾

Enyi watu! Kuleni katika vilivyomo ardhini vya halali, vizuri na wala msifuate hatua za shaytwaan. Hakika yeye kwenu ni adui wa wazi. [Al-Baqarah (2:168)]

8-Toa Swadaqah Kutoka Katika Chumo Kizuri:

Tambua kwamba At-Twayyib Hapokei swadaqah isipokuwa iliyotoka katika chumo kizuri cha halali, na Huikuza hata ikiwa ndogo kiasi gani. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((مَنْ تَصَدَّقَ بِعَدْلِ تَمْرَةٍ مِنْ كَسْبٍ طَيِّبٍ، وَلاَ يَقْبَلُ اللَّهُ إِلاَّ الطَّيِّبَ، وَإِنَّ اللَّهَ يَتَقَبَّلُهَا بِيَمِينِهِ، ثُمَّ يُرَبِّيهَا لِصَاحِبِهِ كَمَا يُرَبِّي أَحَدُكُمْ فَلُوَّهُ، حَتَّى تَكُونَ مِثْلَ الْجَبَلِ))

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Atakayetoa swadaqah kiasi cha tende moja kutoka katika chumo kizuri, na Allaah Hakubali isipokuwa kizuri, basi hakika Allaah Huipokea kwa Mkono Wake wa kulia, kisha Huikuza kwa ajili ya mwenyewe kama mmoja wenu anavyomkuza mwanafarasi wake, mpaka inakuwa mfano wa jabali.” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

9-Tahadhari Na Kumtolea At-Twayyib Kilicho Kibaya:

Tahadhari, ee Mja wa At-Twayyib, na kukusudia kutoa katika njia ya Allaah kilicho kibaya ambacho wewe mwenyewe usingekipokea; bali toa katika vizuri unavyovipenda, kwani At-Twayyib Hakubali isipokuwa kizuri. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَنفِقُوا مِن طَيِّبَاتِ مَا كَسَبْتُمْ وَمِمَّا أَخْرَجْنَا لَكُم مِّنَ الْأَرْضِ ۖ وَلَا تَيَمَّمُوا الْخَبِيثَ مِنْهُ تُنفِقُونَ وَلَسْتُم بِآخِذِيهِ إِلَّا أَن تُغْمِضُوا فِيهِ ۚ وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ غَنِيٌّ حَمِيدٌ ﴿٢٦٧﴾

Enyi walioamini! Toeni katika vizuri mlivyochuma na katika ambavyo Tumekutoleeni kutoka katika ardhi. Na wala msikusudie kutoa vibaya humo, mkavitoa ilhali nyinyi wenyewe msingevipokea isipokuwa kwa kuvifumbia macho. Na jueni kwamba hakika Allaah Ni Mkwasi, Mwenye Kustahiki Kuhimidiwa. [Al-Baqarah (2:267)]

10-Sema Neno Zuri, Kwani Ni Swadaqah:

Kumbuka kwamba At-Twayyib Anapenda neno zuri, na Kwake linapanda neno zuri (Rejea juu: Faatwir (35:10)); basi pamba ulimi wako kwa dhikr, kusoma Qur-aan, kuamrisha mema na kuwaambia watu maneno mazuri. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم): ((... وَالْكَلِمَةُ الطَّيِّبَةُ صَدَقَةٌ ...))

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “… Na neno zuri ni swadaqah …” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

11-Jiepushe Na Kauli Ovu Ili Uwe Miongoni Mwa Watu Wema:

Tahadhari na kauli ovu, kusengenya na kuwatuhumu watu; kwani kauli njema inaendana na watu wema, na kauli ovu inaendana na watu waovu, na At-Twayyib Anawapenda wema. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

الْخَبِيثَاتُ لِلْخَبِيثِينَ وَالْخَبِيثُونَ لِلْخَبِيثَاتِ ۖ وَالطَّيِّبَاتُ لِلطَّيِّبِينَ وَالطَّيِّبُونَ لِلطَّيِّبَاتِ ۚ أُولَـٰئِكَ مُبَرَّءُونَ مِمَّا يَقُولُونَ ۖ لَهُم مَّغْفِرَةٌ وَرِزْقٌ كَرِيمٌ ﴿٢٦﴾

Kauli ovu inaendana na watu waovu, na watu waovu wanaendana na kauli ovu. Na kauli njema inaendana na watu wema, na watu wema wanaendana na kauli njema. Hao wametakaswa na tuhuma za wanayoyasema, watapata Maghfirah na rizki karimu. [An-Nuwr (24:26)]

12-Mtukuze At-Twayyib Kwa Maneno Mazuri Katika Swalaah Yako:

Tambua kwamba katika kila Tashahhud unamtukuzia At-Twayyib maneno mazuri, kwani maneno na amali nzuri zote ni Zake Yeye; basi yasome ukiwa unaelewa maana yake. Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amefundisha:

عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ مَسْعُودٍ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ النَّبِيُّ (صلى الله عليه وسلم): ((... فَإِذَا صَلَّى أَحَدُكُمْ فَلْيَقُلِ: التَّحِيَّاتُ لِلَّهِ وَالصَّلَوَاتُ وَالطَّيِّبَاتُ، السَّلاَمُ عَلَيْكَ أَيُّهَا النَّبِيُّ وَرَحْمَةُ اللَّهِ وَبَرَكَاتُهُ، السَّلاَمُ عَلَيْنَا وَعَلَى عِبَادِ اللَّهِ الصَّالِحِينَ ...))

Amesimulia ‘Abdullaah bin Mas‘uwd (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “… Basi atakaposwali mmoja wenu aseme: Maamkizi yote ya kuadhimisha ni ya Allaah, na Swalaah zote, na maneno na amali nzuri zote (ni Zake). Amani iwe juu yako, Yaa Nabiy, na Rehma za Allaah na Baraka Zake. Amani iwe juu yetu na juu ya Waja wa Allaah walio wema …” [Al-Bukhaariy] [Muslim]

13-Omba Du’aa Ya Rizqi Nzuri:

Omba du’aa, ee Mja wa At-Twayyib, Akuruzuku rizqi nzuri ya halali, ilimu yenye manufaa na amali yenye kukubaliwa, kama alivyokuwa akiomba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) baada ya Swalaah ya Alfajiri:

عَنْ أُمِّ سَلَمَةَ (رضي الله عنها) أَنَّ النَّبِيَّ (صلى الله عليه وسلم) كَانَ يَقُولُ إِذَا صَلَّى الصُّبْحَ حِينَ يُسَلِّمُ: ((اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ عِلْمًا نَافِعًا، وَرِزْقًا طَيِّبًا، وَعَمَلًا مُتَقَبَّلًا))

Amesimulia Ummu Salamah (رضي الله عنها) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akisema anaposwali Swalaah ya Alfajiri anapotoa salaam: “Yaa Allaah! Hakika mimi nakuomba ilimu yenye manufaa, na rizqi nzuri, na amali yenye kukubaliwa.” [Ibn Maajah (925), na Imaam Al-Albaaniy ameisahihisha katika Swahiyh Ibn Maajah (762)]

14-Omba Du’aa Ya Kizazi Chema:

Omba du’aa kwa At-Twayyib Akutunukie kizazi chema, kama alivyoomba Nabiy Zakariyyaa (عليه السلام). Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

هُنَالِكَ دَعَا زَكَرِيَّا رَبَّهُ ۖ قَالَ رَبِّ هَبْ لِي مِن لَّدُنكَ ذُرِّيَّةً طَيِّبَةً ۖ إِنَّكَ سَمِيعُ الدُّعَاءِ ﴿٣٨﴾

Hapo hapo Zakariyyaa akamwomba Rabb wake, akasema: Rabb wangu! Nitunukie kutoka Kwako kizazi chema, hakika Wewe Ni Mwenye Kusikia duaa yangu. [Aal-‘Imraan (3:38)]

Na Allaah Mjuzi zaidi

  • 1Rejea: Ad-Durar As-Saniyyah, Al-Mawsuw‘ah Al-‘Aqadiyyah, Asmaa Allaah Al-Husnaa: At-Twayyib (https://dorar.net/aqeeda/727).
  • 2Ikmaal Al-Mu‘lim (3/535).
  • 3Al-Mufhim (3/58).
  • 4Sharh Al-Arba‘iyn An-Nawawiyyah (uk. 144).
  • 5Kitaab Asw-Swalaah Wa Hukmu Taarikihaa (uk. 182).