Mume Amenikimbia, Je, Niende Kwa Mganga Apate Kumrudisha?

 

Mume Amenikimbia, Je, Niende Kwa Mganga Apate Kumrudisha?

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Mume wangu amenikimbia yuko T.bara sipati huduma yeyote

jee si dhambi kwenda kwa mganga ili apate kurudi? kama dhambi munanishauri nifanye nini na nasikia mtu akidai Talaka pepo ya Mola haisikii hata harufu?  Mtihani mkubwa kwangu umekuwa naomba msaada wenu.

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Kutokana na umuhimu mkubwa wa kukuokoa kutoka katika shirki na kufru, tumeona haraka tukupe jibu ingawa kuna maswali mengi yaliyoingia kabla yako. Hivyo tunatumai pia kuwa juhudi zetu hizi na nasaha zetu utazipokea kwa moyo mkunjufu na utazitekeleza kwa manufaa yako.

 

Tambua na tahadhari kwamba kwenda kumkabili mganga ni kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika Majina Yake na Sifa Zake tukufu kwani unamkabili mganga kwa kuamini kwamba yeye atakuwa na uwezo wa kumrudisha mume wako na hali yeye ni kiumbe kama wewe dhaifu kabisa. Waganga hawana ila kutumia uchawi na kulaghai watu kwa kutaka mapato au chumo kutoka kwa watu wanaomwendea.

 

Mwenye kumwendea mganga ikiwa kwa ajili ya kumtegemea amtatulie matatizo yake au amtabirie jambo, hutoka nje ya Uislamu kutokana na kauli ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): 

((من أتى كاهناً فصدقه بما يقول فقد كفر بما أنزل على محمد صلى الله عليه وسلم))  رواه أبو داود   

"Atakayemwendea mchawi na kuamini aliyoambiwa, basi amekufuru yale aliyoteremshiwa Muhammad [Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam]" [Abu Daawud]

 

Hivyo pia ni kumshirkisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na ni dhambi ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Hamsamehe mja:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ ۚ وَمَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدِ افْتَرَىٰ إِثْمًا عَظِيمًا ﴿٤٨﴾

Hakika Allaah Haghufurii kushirikishwa; lakini Anaghufuria yasiyokuwa hayo kwa Amtakae. Na yeyote atakayemshirikisha Allaah basi kwa yakini amezua dhambi kuu. [An-Nisaa: 48]

 

Hatari nyingine ni kwamba mwenye kumshirkisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Hataingia Peponi:

..إِنَّهُ مَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدْ حَرَّمَ اللَّـهُ عَلَيْهِ الْجَنَّةَ وَمَأْوَاهُ النَّارُ ۖ وَمَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ أَنصَارٍ﴿٧٢﴾

Hakika mwenye kumshirikisha Allaah bila shaka Allaah Atamharamishia Jannah, na makazi yake yatakuwa ni motoni. Na madhalimu hawatopata yeyote mwenye kunusuru. [Al-Maaidah: 72]

 

Zingatia na fuata yafuatayo na InshaAllaah mumeo ikiwa ana kheri na wewe atarudi kwako, na ikiwa hakuna kheri, basi muombe Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Akupe mwenye kheri zaidi yake.

 

1) Kwanza, jiulize mwenyewe kwanini mumeo amekukimbia? Bila ya shaka kuna sababu fulani. Ikiwa ulikuwa na udhaifu fulani kwake, basi jambo la kwanza ni kujirekebisha huo udhaifu au tabia ambayo huenda ikawa ni sababu ya kukukimbia.

 

2) Pili, watafute watu katika jamaa zako au jamaa zake wakusaidie kuwasiliana naye na waseme naye wapate kujua tatizo lenu ili mpate kusuluhishwa. Ikiwa ni makosa kutoka kwako nawe unamtaka mumeo arudi, basi ujirekebishe na ukiri makosa yako na uombe radhi kwake na kumuahidi kwamba hutorudia tena na uko tayari kumridhisha. Salamu hizi hakikisha zinamfikia kwanza.

 

3) Kisha tambua kwamba Muislamu anapokutwa na mitihani ya aina yoyote anapaswa kuwa na subira na kumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa kuamini Qadhwaa na Qadar.

 

4) Kumbuka kwamba kupewa mitihani kuna maana ya kupandishwa daraja la mja anaposubiri.

 

5) Zidisha Taqwa na kumkabili Rabb wako Aliyekuumba na Mwenye uwezo wa kukuondolea kila mitihani, shida, dhiki na matatizo. 

 وَمَن يَتَّقِ اللَّهَ يَجْعَل لَّهُ مَخْرَجًا

Na yeyote anayemcha Allaah; Atamjaalia njia ya kutoka (shidani). [Atw-Twalaaq: 2]  

وَمَن يَتَّقِ اللَّهَ يَجْعَل لَّهُ مِنْ أَمْرِهِ يُسْرًا 

Na yeyote anayemcha Allaah Atamjaalia wepesi katika jambo lake. [Atw-Twalaaq: 4]

 

6) Amka usiku katika thuluthi ya mwisho ya usiku uswali Tahajjud na umuombe Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).

 

7) Jishughulishe na kumkumbuka Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kila mara asubuhi na jioni, kwa kusoma Qur-aan, kusikiliza mawaidha, kutafuta elimu ya dini yako, yote haya yatakupa faida ya dunia na Aakhirah na yatakuridhisha nafsi yako, na pia yatakupunguzia mawazo. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa): 

الَّذِينَ آمَنُوا وَتَطْمَئِنُّ قُلُوبُهُم بِذِكْرِ اللَّـهِ ۗ أَلَا بِذِكْرِ اللَّـهِ تَطْمَئِنُّ الْقُلُوبُ ﴿٢٨﴾

Wale walioamini na zikatua nyoyo zao kwa kumdhukuru Allaah. Tanabahi!  Kwa kumdhukuru Allaah nyoyo hutulia! [Ar-Ra'd: 28]

         

8) Kuwa na tawakkul (kumtegemea Allah) na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa mambo yako yote Naye Atakufungulia kila njia za kheri: 

 وَيَرْزُقْهُ مِنْ حَيْثُ لَا يَحْتَسِبُ ۚ وَمَن يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ فَهُوَ حَسْبُهُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ بَالِغُ أَمْرِهِ ۚ قَدْ جَعَلَ اللَّـهُ لِكُلِّ شَيْءٍ قَدْرًا﴿٣﴾

Na Atamruzuku kutoka njia ambayo hatizamii. Na yeyote anayetawakali kwa Allaah, basi Yeye Humtosheleza. Hakika Allaah Anatimiza kusudio Lake. Allaah Amejaalia kwa kila kitu makadirio. [At-Twalaaq: 3]

 

Baada ya kufuata yote hayo, tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akufanyie wepesi mtihani wako na Akufungulie lililo na kheri nawe.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

Share